Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022

Act 6 of 2022

Uncommenced
This Act has not yet come into force.
Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022

Tanzania

Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022

Tenda 6 ya 2022

Sheria ya kuweka mfumo wa usimamizi na uratibu wa Maafa kwa ajili ya hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi Maafa yanapotokea pamoja na kuanzisha na kusimamia Mfuko wa Usimamizi wa Maafa na mambo yanayohusiana nayo.IMETUNGWA na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya Kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina fupi na kuanza kutumika

Sheria hii itajulikana kama Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022 na itaanza kutumika katika tarehe ambayo Waziri atatangaza katika Gazeti la Serikali.

2. Matumizi

Sheria hii itatumika Tanzania Bara.

3. Tafsiri

Katika Sheria hii, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo:afya moja” maana yake ni dhana inayotumika kuweka ushirikiano baina ya sekta zinazohusika na afya ya binadamu, wanyama na mazingira, ili kuimarisha uratibu na usimamizi katika utendaji na kupanga mikakati ya pamoja inayolenga kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea na mazao ikiwemo madhara ya majanga yanayovuka mipaka na yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi, usugu wa madawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza;Divisheni” maana yake ni Divisheni yenye jukumu la usimamizi na uratibu wa Maafa iliyoko ndani ya Wizara;eneo la Maafa” maana yake ni eneo lililotangazwa kwa mujibu wa Sheria hii kuwa eneo lenye madhara ya janga au lililopata madhara kutokana na Maafa;janga” maana yake ni balaa au baa linalotokana na nguvu za asili au shughuli za kibinadamu ambalo linaloweza kusababisha Maafa;Jukwaa” maana yake ni Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa lililoanzishwa chini ya Sheria hii;Katibu Mkuu” maana yake ni Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa Maafa;Kituo” maana yake ni Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 5;kukabiliana na Maafa” maana yake ni hatua yoyote inayochukuliwa mara tu baada ya Maafa kutokea ili kuokoa maisha, mali na mazingira, kupunguza madhara ya kiafya, kutoa huduma za kibinadamu, kuimarisha usalama wa umma au kushughulikia uharibifu unaotokana na Maafa;kupunguza madhara” maana yake ni hatua zinazoelekezwa katika kupunguza madhara ya Maafa yanayoweza kusababishwa na tukio la janga;kurejesha hali baada ya Maafa” maana yake ni hatua zinazosaidia kurejesha hali au kuboresha mifumo ya maisha iliyoathiriwa na Maafa kwa kujenga upya au kurejesha mifumo kwa ubora zaidi ili kuzuia au kupunguza madhara ya Maafa siku zijazo;kuzuia Maafa” maana yake ni hatua zinazochukuliwa kuzuia hatari mpya au kupunguza hatari zilizopo kutokana na shughuli na maamuzi ya kibinadamu au nguvu za asili yasisababishe kutokea kwa Maafa;Maafa” maana yake ni madhara yanayotokana na janga ambayo yanajumuisha uharibifu wa mfumo wa kawaida katika jamii ambao husababisha vifo, majeruhi, madhara ya kisaikolojia, upotevu au uharibifu wa mali, mifumo mbalimbali ya kiteknolojia na huduma za kiuchumi na kijamii au mazingira, ambapo jamii iliyoathirika haiwezi kukabili kwa kutumia rasilimali zake bila msaada kutoka nje ya jamii hiyo;Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa” maana yake ni mkakati ambao unaainisha hatua zitakazochukuliwa katika kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi Maafa yanapotokea;Sheria” maana yake ni Sheria ya Usimamizi wa Maafa;usimamizi wa Maafa” inajumuisha hatua zinazochukuliwa kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali endapo Maafa yanatokea kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo;Waziri” maana yake ni Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Maafa; naWizara” maana yake ni Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa Maafa.

Sehemu ya Pili – Mfumo wa usimamizi na uratibu wa Maafa nchini

4. Uratibu na usimamizi wa Maafa

(1)Wizara itakuwa na jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za Maafa nchini.
(2)Katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya kifungu kidogo cha (1), Wizara kupitia Divisheni
(a)itatayarisha, kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni, mikakati na taratibu za utendaji kwenye shughuli zote zinazohusiana na usimamizi wa Maafa Tanzania Bara;
(b)itaratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za usimamizi wa Maafa kwa kushirikiana na wizara, sekta na kamati za kitaalam zenye dhamana ya usimamizi wa Maafa katika ngazi zote;
(c)itaratibu na kutoa mwongozo kuhusu ushirikiano wa kisekta katika usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, visumbufu vya mazao, usugu wa madawa dhidi ya vimelea vya magonjwa, usalama wa chakula na lishe, sumu kuvu, usalama na ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi vya magonjwa na magonjwa yasiyoambukiza;
(d)itaratibu wizara, idara, wakala, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi katika utekelezaji wa mikakati, mipango na miongozo ya usimamizi wa Maafa ikiwemo afya moja;
(e)itaratibu ushirikiano na nchi jirani kuhusu kuzuia, kujiandaa na kukabili dharura zinazovuka mipaka ikiwemo magonjwa ya mlipuko ya binadamu na wanyama na visumbufu vya mazao;
(f)itaratibu ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuhusu usimamizi wa masuala ya dharura na magonjwa ya mlipuko yanayovuka mipaka;
(g)itaratibu uandaaji na kusimamia utekelezaji wa miongozo ya tathmini ya hatari za Maafa katika miradi mikubwa ya maendeleo;
(h)itasimamia utendaji wa Kituo cha Mawasiliano ya Dharura na kukiunganisha na vituo vya kisekta;
(i)itaweka mfumo wa teknoloj ia ya habari na mawasiliano utakaowaunganisha wadau wa masuala ya Maafa, kufuatilia mwenendo wa majanga na hali ya Maafa kwa ajili ya kuchukua hatua za kuzuia na kukabiliana na Maafa kwa wakati;
(j)itaendeleza na kuanzisha kanzi data ya rasilimali, wadau, miundombinu muhimu, aina za majanga, misaada ya kibinadamu na takwimu za matukio ya Maafa kwa ajili usimamizi wa Maafa;
(k)itahamasisha matumizi ya teknolojia ya mawasiliano na habari katika kupunguza hatari za majanga na usimamizi wa Maafa;
(l)Itaunda mfumo wa tahadhali ya, mapema utakaojumuisha sekta zote na kuwa kiungo kati ya asasi mbalimbali zinazotoa huduma ya tahadhari;
(m)itakuza na kuendeleza mafunzo, utafiti, uvumbuzi, elimu kwa umma, mazoezi ya vitendo na nadharia, maarifa, mabadiliko ya tabia na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika usimamizi wa Maafa;
(n)itatafuta, kuhamasisha na kusimamia matumizi ya rasilimali kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa Maafa na kuweka miongozo ya ugawaji wa misaada ya huduma za kibinadamu;
(o)itapokea taarifa kutoka taasisi yoyote, idara, mamlaka, mtu au watu kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa Maafa;
(p)itaratibu na kusimamia tahadhari ya mapema inayozingatia athari na kuhuisha ujumbe wa onyo na hatua za kuchukua kwa majanga mbalimbali;
(q)itashirikiana na mamlaka za serikali za mitaa kuweka hatua za ulinzi wa raia dhidi ya Maafa;
(r)itahakikisha uwepo wa vifaa toshelevu kwa kushirikiana na wadau na sekta husika kwa ajili ya kukabiliana na Maafa na programu za kujenga uelewa kwa umma kuhusu kujiandaa kukabiliana na Maafa;
(s)itaratibu na kufanya utafiti, tathmini na kuandaa modeli za kisayansi na ramani kwa kuainisha aina za majanga, hatari zilizopo na uwezekano wa kutokea pamoja na kuainisha uwezo wa usimamizi wa janga;
(t)itatathmini na kufuatilia hatua za kukabiliana na Maafa ikiwemo huduma za kibinadamu kwa waathirika wa Maafa na kushauri ipasavyo;
(u)itaratibu na kusimamia tathmini ya haraka na kina ya uharibifu na mahitaji kwa ajili ya urejeshaji hali kutokana na madhara ya Maafa;
(v)itahamasisha ushiriki wa wanaojitolea, uendeshaji wa mafunzo na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa Maafa, huduma za dharura katika mikusanyiko mikubwa na huduma za kibinadamu; na
(w)itatekeleza majukumu mengine yoyote yanayohusiana na kupunguza hatari za Maafa na usimamizi wa Maafa.
(3)Wizara inaweza kutoa taarifa zilizotunzwa chini ya kifungu kidogo cha (2)(j) kwa mtu yeyote, idara au taasisi kwa kadri Katibu Mkuu atakavyoona inafaa.

5. Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura

Kutakuwa na Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura chini ya Divisheni ambacho kitaunganishwa na vituo vya kisekta kitakachokuwa na jukumu la kufuatilia mwenendo wa majanga, kupokea na kuchambua taarifa za tahadhari na dharura kwa ajili ya usimamizi wa Maafa.

6. Mamlaka ya Waziri

(1)Kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yake yanayohusiana na usimamizi wa Maafa, Waziri atakuwa na mamlaka ya—
(a)kuamuru watu kuondoka katika maeneo ya Maafa au maeneo hatarishi au kuamuru watu kubaki katika maeneo salama;
(b)kusimamisha au kuzuia uuzaji wa vileo, vinywaji, silaha, milipuko, au vitu vingine ambavyo vitaonekana havipaswi kuwa kwenye maeneo ya Maafa;
(c)kuamuru matumizi ya rasilimali za taasisi za umma kwa kadri itakavyoonekana ni muhimu kutumika kwa shughuli za dharura kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni;
(d)kuagiza mtu yeyote, idara au taasisi kuwasilisha taarifa kadri itakavyoonekana ni muhimu kwa ajili ya uratibu wa shughuli za Maafa; na
(e)kuwezesha upatikanaji wa rasilimali watu, fedha na vifaa kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa Maafa.
(2)Waziri atatumia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria hii kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo yake unazingatiwa na anaweza kuchukua au kuelekeza kuchukuliwa hatua dhidi ya atakayeshindwa kuzingatia maelekezo yake.
(3)Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa ya kusudio lake la kuchukua hatua zilizoainishwa katika kifungu hiki, kuelekeza taasisi, idara, mamlaka, mtu au watu, kutekeleza, ndani ya muda utakaopangwa na kwa namna atakavyoelekeza, kazi yoyote iliyoainishwa chini ya Sheria hii au Sheria nyingine yoyote kuhusiana na usimamizi na utekelezaji wa Sheria.
(4)Endapo taasisi, idara, mamlaka au mtu, atashindwa kutekeleza maelekezo chini ya kifungu hiki, Wizara itatekeleza kazi hizo au Waziri ataelekeza kazi hizo zitekelezwe na taasisi, idara, mamlaka au mtu mwingine na gharama zitakuwa deni la taasisi, idara, mamlaka au mtu aliyepaswa kutekeleza maelekezo hayo.
(5)Waziri anaweza kutengeneza kanuni zitakazoainisha utaratibu wa utekelezaji wa masharti ya kifungu kidogo cha (4).

7. Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kutakuwa na Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa ambayo itakuwa na jukumu la usimamizi wa Maafa katika ngazi ya Taifa.
(2)Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na wajumbe wafuatao—
(a)Waziri mwenye dhamana ya Maafa ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati;
(b)Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
(c)Waziri mwenye dhamana ya fedha na mipango;
(d)Waziri mwenye dhamana ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi;
(e)Waziri mwenye dhamana ya ulinzi;
(f)Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi;
(g)Waziri mwenye dhamana ya afya;
(h)Waziri mwenye dhamana ya kilimo na usalama wa chakula;
(i)Waziri mwenye dhamana ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari;
(j)Waziri mwenye dhamana ya ujenzi na usafirishaji;
(k)Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya jamii;
(l)Waziri mwenye dhamana ya tawala za mikoa na serikali za mitaa; na
(m)Waziri mwenye dhamana ya maji.
(3)Katibu Mkuu atakuwa Katibu wa Kamati.
(4)Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa inaweza kumualika mtu yeyote kwenye kikao chake kama itakavyoona inafaa, kutegemea na tishio au madhara ya tukio la Maafa.

8. Majukumu ya Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na majukumu yafuatayo—
(a)kusimamia, kutoa maelekezo na kuweka vipaumbele vya shughuli za usimamizi wa Maafa na huduma za kibinadamu;
(b)kuidhinisha Mpango wa Usimamizi wa Maafa na Mpango wa Mwendelezo wa Huduma wakati wa Dharura ya Kitaifa;
(c)kuhamasisha na kuwezesha utafutaji wa rasilimali ili kuimarisha uwezo wa kitaasisi na vifaa kwa ajili ya usimamizi wa Maafa na dharura katika ngazi ya Taifa; na
(d)kushauri mamlaka kuhusu kutangaza hali ya Maafa katika ngazi ya Taifa.
(2)Waziri mwenye dhamana na Maafa atakuwa msemaji wa Serikali wakati wa matukio ya Maafa katika ngazi ya Taifa.

9. Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kutakuwa na Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa.
(2)Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na wajumbe wafuatao—
(a)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa Maafa ambaye atakuwa Mwenyekiti;
(b)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa;
(c)Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
(d)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya mamlaka ya tawala za mikoa na serikali za mitaa;
(e)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya fedha;
(f)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya afya;
(g)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari;
(h)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi;
(i)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya kilimo na usalama wa chakula;
(j)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya maji;
(k)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi;
(l)Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya ujenzi na usafirishaji;
(m)Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania;
(n)Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji; na
(o)Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania.
(3)Mkurugenzi wa Divisheni ya Menejimenti ya Maafa atakuwa Katibu wa Kamati.
(4)Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa ya Taifa itakuwa na mamlaka ya kumualika mtu yeyote kwenye kikao chake kama itakavyoona inafaa, kutegemea na tishio au madhara ya tukio la Maafa.

10. Majukumu ya Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na majukumu yafuatayo—
(a)kuishauri Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa hatua za kuimarisha usimamizi wa Maafa nchini;
(b)kutekeleza maelekezo ya Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa;
(c)kuhakikisha afua za kupunguza hatari za Maafa zinajumuishwa katika Sera, Mipango, Mikakati na programu za maendeleo za taasisi husika za serikali;
(d)kutoa msaada katika utafutaji wa rasilimali za usimamizi wa Maafa ikiwemo kuimarisha uwezo wa kitaasisi na vifaa vya kutoa huduma za kibinadamu;
(e)kutoa mwelekeo wa makisio ya rasiiimali zitakazohitajika kwa mwaka wa fedha katika Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa;
(f)kuandaa Mpango wa Usimamizi wa Maafa na Mpango wa Mwendelezo wa Huduma wakati wa dharura ya Kitaifa; na
(g)kuhamasisha uandaaji na utekelezaji wa mikakati ya kitaifa ya utendaji na usimamizi wa Maafa kwa kuzingatia uvumbuzi na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
(2)Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa inaweza kuanzisha kamati ndogo kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji mzuri wa shughuli za uratibu na usimamizi wa Maafa kitaifa.

11. Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa.

(1)Kutakuwa na Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa ambalo litatoa nafasi ya wataalam kutoka Serikalini na nje ya Serikali kukutana na kujadili masuala yanayohusu usimamizi wa Maafa na kuishauri Kamati ya Taifa ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa.
(2)Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa litakuwa na wajumbe wafuatao—
(a)Mkurugenzi wa Divisheni ya Menejimenti ya Maafa ambaye atakuwa ni Mwenyekiti;
(b)wakuu wa idara zenye dhamana ya usimamizi wa Maafa kutoka:
(i)Wizara yenye dhamana ya kilimo na usalama wa chakula;
(ii)Wizara yenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi;
(iii)Wizara yenye dhamana ya fedha;
(iv)Wizara yenye dhamana ya serikali za mitaa;
(v)Wizara yenye dhamana ya afya;
(vi)Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii;
(vii)Wizara yenye dhamana ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi;
(viii)Wizara yenye dhamana ya mambo ya nje;
(ix)Wizara yenye dhamana ya viwanda;
(x)Wizara yenye dhamana ya maliasili;
(xi)Wizara yenye dhamana ya nishati;
(xii)Wizara yenye dhamana ya madini;
(xiii)Wizara yenye dhamana ya mawasiliano;
(xiv)Wizara yenye dhamana ya ardhi;
(xv)Wizara yenye dhamana ya uchukuzi;
(xvi)Wizara yenye dhamana ya maji;
(xvii)Wizara yenye dhamana ya elimu; na
(xviii)Wizara yenye dhamana ya habari na teknolojia ya mawasiliano;
(c)wakuu wa idara zinazohusika na huduma za masuala ya Maafa kutoka taasisi zifuatazo:
(i)Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania;
(ii)Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula;
(iii)Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania;
(iv)Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba;
(v)Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania;
(vi)Jeshi la Zima Moto na Uokoaji;
(vii)Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania;
(viii)Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania;
(ix)Jeshi la Wananchi Tanzania;
(x)Jeshi la Polisi Tanzania;
(xi)Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania;
(xii)Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali;
(xiii)Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania; na
(xiv)Wakala wa Nguvu za Atomiki Tanzania;
(d)wawakilishi wawili kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya kimataifa;
(e)mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
(f)wawakilishi wawili kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu;
(g)wawakilishi wawili kutoka Taasisi za Utafiti;
(h)mwakilishi kutoka jumuiya ya asasi za kiraia;
(i)wawakilishi wawili kutoka asasi za makundi ya watu wenye mahitaji maalum;
(j)mwakilishi kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania;
(k)mwakilishi kutoka Chama cha Skauti Tanzania;
(l)wawakilishi watatu kutoka taasisi za dini;
(m)mwakilishi kutoka Baraza la Vyombo vya Habari; na
(n)wawakilishi wawili kutoka Kamati za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazohusika na masuala ya usimamizi wa Maafa.
(3)Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa anayehusika na Mipango na Utafiti atakuwa Katibu wa Jukwaa.
(4)Jukwaa linaweza kumualika mtu yeyote kwenye kikao chake kama itakavyoona inafaa, kutegemea na tishio husika au madhara ya tukio la Maafa.
(5)Jukwaa litakutana angalau mara mbili kwa mwaka lakini linaweza kukutana wakati wowote kama kutakuwa na suala ambalo linahitaji kujadiliwa kwa dharura.
(6)Jukwaa linaweza kuunda kamati ndogo za wataalam ambazo wajumbe wake watateuliwa kutoka miongoni mwao ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.
(7)Jukwaa linaweza kujiwekea taratibu za uendeshaji.

12. Majukumu ya Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa

Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa litakuwa na jukumu la kuishauri Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa kwa kutekeleza majukumu yafuatayo—
(a)kushauri na kutekeleza hatua za kujumuisha upunguzaji wa madhara ya Maafa katika sera, sheria na mipango ya maendeleo ya taifa ili kushughulikia changamoto za Maafa zenye madhara ya kijamii, kiuchumi na mazingira na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha huduma za kibinadamu kwa ufanisi;
(b)kushauri na kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo na mabadiliko ya tabianchi yanayohusu kuzuia na kupunguza madhara ya majanga kwa kutoa mawazo ya mfumo thabiti unaozingatia vipaumbele katika sekta na nchi kwa ujumla;
(c)kuibua mijadala kutokana na tafiti na uzoefu wa kiutendaji ili kuwa kichocheo cha majadiliano ya kitaifa na kufikia makubaliano, pamoja na kuainisha vipaumbele vya usimamizi wa Maafa na uandaaji wa mipango na miongozo ya utekelezaji na ufuatiliaji;
(d)kuchangia na kushiriki katika maandalizi ya taarifa ya hali ya Maafa kwa mwaka na tathmini ya utekelezaji wa mikakati na mipango ya kupunguza madhara ya Maafa nchini;
(e)kushawishi upatikanaji wa rasilimali kutoka kwa wafadhili, mabenki ya maendeleo, na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kueleza umuhimu wa kuunga mkono na ushirikiano katika usimamizi wa Maafa na misaada ya kibinadamu; na
(f)kusaidia upatikanaji wa takwimu za msingi za usimamizi wa Maafa, ikiwa ni pamoja na maelezo ya vihatarishi vya majanga kwa ajili ya kuzingatia katika mipango ya maendeleo na bajeti za kisekta.

13. Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Usalama ya Mkoa iliyoundwa chini ya Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa itakuwa ndiyo Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa ambayo itakuwa na mamlaka ya kutoa maamuzi na maelekezo ya hatua za kuchukua katika usimamizi wa Maafa katika ngazi ya Mkoa.[Sura ya 61]
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), Wabunge wa Viti Maalum katika mkoa husika watakuwa wajumbe wa Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa.

14. Majukumu ya Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kupanga, kuratibu na kutoa maelekezo kuhusu kushughulikia masuala ya Maafa katika Mkoa;
(b)kusimamia majukumu ya Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa ya Mkoa;
(c)kuhamasisha na kuwezesha utafutaji wa rasilimali ili kuimarisha uwezo wa kitaasisi na vifaa kwa ajili ya usimamizi wa Maafa na dharura katika Mkoa;
(d)kuidhinisha mpango wa usimamizi wa Maafa na mpango wa mwendelezo wa huduma wakati wa dharura katika Mkoa kwa kuzingatia mipango ya Kitaifa wakati wa Maafa;
(e)kupendekeza kwa mamlaka husika kuhusu hatua za kupunguza madhara ya Maafa; na
(f)kuelekeza na kuweka vipaumbele vya usimamizi wa Maafa na dharura katika Mkoa.
(2)Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa atakuwa msemaji wa Serikali wakati wa matukio ya Maafa katika ngazi ya Mkoa.

15. Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kutakuwa na Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa ambayo itakuwa na wajibu wa kuratibu utekelezaji wa afua za usimamizi wa Maafa katika halmashauri zilizopo katika Mkoa husika.
(2)Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na wajumbe wafuatao—
(a)Katibu Tawala wa Mkoa ambaye atakuwa Mwenyekiti;
(b)Makatibu Tawala Wasaidizi wote;
(c)Mkurugenzi wa jiji, Wakurugenzi wa Manispaa, Miji na Wilaya kutoka Wilaya zote katika Mkoa;
(d)Makatibu Tawala wa Wilaya kutoka Wilaya zote katika Mkoa;
(e)Afisa Operesheni Mkoa wa Jeshi la Polisi Tanzania;
(f)Afisa Operesheni Mkoa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;
(g)Mshauri wa Mgambo Mkoa;
(h)Mkuu wa taasisi inayohusika na barabara za vijijini na mijini katika ngazi ya Mkoa;
(i)Mkuu wa taasisi inayohusika na barabara kuu na za mikoa katika Mkoa;
(j)Mkuu wa taasisi inayohusika na huduma za maji na usafi wa mazingira katika Mkoa;
(k)Mkuu wa taasisi inayohusika na usanifu na ubora wa majengo katika Mkoa; na
(l)Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika Mkoa.
(3)Katibu Tawala Msaidizi anayehusika na uratibu na mipango atakuwa Katibu wa Kamati.
(4)Kamati inaweza kumualika mtu yeyote kwenye kikao chake kama itakavyoona inafaa, kutegemea na tishio au madhara ya tukio la Maafa.

16. Majukumu ya Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kuishauri Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa kuhusu masuala ya usimamizi wa Maafa na mambo mengine yoyote yatakayoelekezwa na Mkuu wa Mkoa;
(b)kufuatilia na kuratibu shughuli za upunguzaji na usimamizi wa Maafa na huduma za dharura miongoni mwa taasisi za kisekta za Serikali, serikali za mitaa, jamii na wadau wengine wanaojihusisha na Maafa;
(c)kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa Maafa katika Mkoa;
(d)kuandaa Mkakati wa Mkoa wa Kupunguza Madhara ya Maafa na Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa;
(e)kufungamanisha mfumo wa tahadhari ya awali katika Mkoa na kuwezesha uanzishaji wa mfumo wa takwimu na taarifa za Maafa za Mkoa;
(f)kutoa mwelekeo wa makisio ya rasilimali zitakazohitajika kwa mwaka wa fedha katika Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa;
(g)kuratibu mipango ya Wilaya ya usimamizi wa Maafa iliyowasilishwa;
(h)kutunza kumbukumbu za taarifa na takwimu za awali za matukio ya Maafa na hatua za tahadhari katika Mkoa;
(i)kutafsiri taarifa za tahadhari ya mapema dhidi ya majanga na kupendekeza hatua za kuchukua katika Mkoa; na
(j)kuainisha, kufanya tathmini na kuandaa profaili ya majanga katika Mkoa.
(2)Kamati ya Wataalam ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa inaweza kuanzisha kamati ndogo kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji mzuri wa shughuli za usimamizi na uratibu wa Maafa katika Mkoa.

17. Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Usalama ya Wilaya iliyoundwa chini ya Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa itakuwa ndiyo Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa yenye mamlaka ya kutoa maamuzi na maelekezo ya hatua za kuimarisha na kushughulikia masuala ya Maafa katika Wilaya.[Sura ya 61]
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), mbunge wa jimbo lililopo katika wilaya husika, Meya wa Jiji na Manispaa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji na Wilaya watakuwa wajumbe wa Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa.

18. Majukumu ya Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kupanga, kuratibu na kutoa maelekezo kuhusu kushughulikia masuala ya Maafa katika Wilaya husika;
(b)kusimamia majukumu ya Kamati ya Wataalam ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa;
(c)kuhamasisha na kuwezesha utafutaji wa rasilimali ili kuimarisha uwezo wa kitaasisi na vifaa kwa ajili ya usimamizi wa Maafa na dharura katika Wilaya;
(d)kuelekeza na kuweka vipaumbele vya usimamizi wa Maafa na dharura katika Wilaya;
(e)kuidhinisha Mpango wa Usimamizi wa Maafa na Mpango wa Mwendelezo wa Huduma wakati wa Dharura katika Wilaya kwa kuzingatia mipango ya Kitaifa wakati wa Maafa; na
(f)kupendekeza kwa Kamati Elekezi ya Mkoa ya Usimamizi wa Maafa kuhusu hatua za kupunguza madhara ya Maafa.
(2)Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa atakuwa msemaji wa Serikali wakati wa matukio ya Maafa katika ngazi ya Wilaya.

19. Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kutakuwa na Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya ya Usimamizi wa Maafa itakayokuwa na jukumu la kuishauri Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa kuhusu hali ya Maafa katika maeneo yao na kuhakikisha mipango ya maendeleo inayoandaliwa inazingatia hatari za Maafa katika maeneo husika.
(2)Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na wajumbe wafuatao—
(a)Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti;
(b)Wakuu wa Idara na Vitengo vyote katika Halmashauri;
(c)Afisa Operesheni Wilaya wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;
(d)Mkuu wa Upelelezi Wilaya wa Jeshi la Polisi Tanzania;
(e)Mkuu wa taasisi inayohusika na barabara za mijini na vijijini katika Wilaya;
(f)Mkuu wa taasisi inayohusika na huduma za maji na usafi wa mazingira katika Wilaya;
(g)Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika Wilaya; na
(h)Kamishna wa Skauti Wilaya.
(3)Mkuu wa Idara inayohusika na Mipango katika Halmashauri husika atakuwa Katibu wa Kamati.
(4)Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya ya Usimamizi wa Maafa inaweza kumualika mtu yeyote kwenye kikao chake kama itakavyoona inafaa, kutegemea na tishio au madhara ya tukio la Maafa.

20. Majukumu ya Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji au Wilaya ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa Maafa na huduma za dharura katika eneo husika kama itakavyoelekezwa na Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa;
(b)kusaidia, kuhamasisha upatikanaji na kutenga rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa Maafa na huduma za dharura katika eneo husika;
(c)kuwezesha na kufuatilia ujumuishaji wa masuala ya kupunguza madhara ya majanga katika mpango wa maendeleo, miradi, programu na bajeti katika eneo husika;
(d)kusaidia na kushiriki kufanya tathmini ya hatari za majanga, madhara ya uharibifu na mahitaji ya kibinadamu na kurejesha hali baada ya Maafa katika eneo husika;
(e)kuandaa na kutekeleza mkakati wa kupunguza madhara ya Maafa na mpango wa kujiandaa na kukabiliana na dharura, kuendesha mafunzo, mazoezi ya nadharia na mfumo wa kurejesha hali katika eneo husika;
(f)kutoa mwelekeo wa makisio ya rasilimali zitakazohitajika kwa mwaka wa fedha katika Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa;
(g)kuandaa mfumo wa teknolojia na mawasiliano ya habari kwa ajili ya tahadhari ya mapema, operesheni na takwimu kwa ajili ya usimamizi wa Maafa katika eneo husika;
(h)kutunza kumbukumbu za taarifa na takwimu za awali za matukio ya Maafa na hatua za tahadhari katika Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya;
(i)kutafsiri taarifa za tahadhari ya mapema dhidi ya majanga na kupendekeza hatua za kuchukua katika Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya; na
(j)kuainisha, kufanya tathmini na kuandaa profaili ya majanga katika Jiji, Manispaa, Mji au Wilaya.
(2)Kamati ya Wataalam ya Jiji, Manispaa, Mji au Wilaya ya Usimamizi wa Maafa inaweza kuanzisha kamati ndogo kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji bora wa shughuli za usimamizi na uratibu wa Maafa katika Jiji, Manispaa, Mji au Wilaya.

21. Mamlaka ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya kwa kuzingatia maamuzi ya Kamati Elekezi ya Mkoa au Wilaya ya Usimamizi wa Maafa, atakuwa na mamlaka ya—
(a)kuelekeza taasisi yoyote katika Mkoa au Wilaya kuzuia au kupunguza madhara ya janga na kujiandaa kukabili na kurejesha hali baada ya Maafa;
(b)kuamuru watu kuondoka katika maeneo hatarishi au yaliyoathirika na Maafa na kuwahamishia maeneo salama katika Mkoa au Wilaya au kuamuru watu kubaki katika maeneo salama;
(c)kutumia rasilimali za umma kama vile usafiri, jengo lolote, vifaa, bidhaa muhimu na vitu vingine kwa ajili ya kusaidia jitihada za usimamizi wa Maafa; na
(d)kufanya jambo lolote ambalo ni la lazima kufanywa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi zake chini ya Sheria hii kwa mujibu wa sera, mipango na taratibu katika Mkoa au Wilaya.

22. Kamati ya Kata ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Maendeleo ya Kata iliyoundwa chini ya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) itakuwa ndiyo Kamati ya Kata ya Usimamizi wa Maafa itakayokuwa na jukumu la kuhakikisha ushiriki wa wadau wote katika hatua za kuzuia au kupunguza madhara ya majanga pamoja na kutoa huduma za kibinadamu wakati wa dharura.[Sura ya 287]
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), Diwani wa viti maalumu katika Kata, maafisa wa Serikali waliopo katika Kata, mwakilishi kutoka kituo cha afya au zahanati katika Kata, mwakilishi kutoka kituo kidogo cha polisi katika Kata na mwakilishi kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika Kata watakuwa wajumbe wa Kamati ya Kata ya Usimamizi wa Maafa.

23. Majukumu ya Kamati ya Kata ya Usimamizi wa Maafa

Kamati ya Kata ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kufuatilia na kuratibu usimamizi wa Maafa na operesheni za dharura katika ngazi ya Kata;
(b)kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa Maafa kwa kushirikisha wadau katika Kata;
(c)kusaidia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa Maafa ya Kata;
(d)kusambaza taarifa za tahadhari ya mapema na maelekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya hatari ya Maafa katika Kata;
(e)kuainisha majanga yanayoweza kutokea na kuandaa ramani ya maeneo hatarishi pamoja na kuchukua hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga kwa kutumia rasilimali zilizopo kwenye Kata; na
(f)kutayarisha mkakati wa kupunguza madhara ya Maafa na mpango wa kukabiliana na dharura wa Kata.

24. Kamati ya Kijiji ya Usimamizi wa Maafa

(1)Halmashauri ya Kijiji iliyoundwa chini ya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) itakuwa ndiyo Kamati ya Kijiji ya Usimamizi wa Maafa itakayokuwa na wajibu wa awali wa kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya majanga pamoja na kushirikisha jamii katika kupata ufumbuzi wa haraka wa huduma za kibinadamu kwa waathirika wa Maafa.[Sura ya 287]
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), mwakilishi kutoka zahanati ya Kijiji, mwakilishi kutoka katika kituo kidogo cha polisi katika Kijiji na mwakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika Kijiji watakuwa wajumbe wa Kamati ya Kijiji ya Usimamizi wa Maafa.

25. Kamati ya Mtaa ya Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati ya Mtaa iliyoundwa chini ya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) itakuwa ndiyo Kamati ya Mtaa ya Usimamizi wa Maafa itakayokuwa na wajibu wa awali wa kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya majanga pamoja na kushirikisha jamii katika kupata ufumbuzi wa haraka wa huduma za kibinadamu kwa waathirika wa Maafa.[Sura ya 288]
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), mwakilishi kutoka zahanati ya Mtaa, mwakilishi kutoka katika kituo kidogo cha polisi katika Mtaa na mwakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika Mtaa watakuwa wajumbe wa Kamati ya Mtaa ya Usimamizi wa Maafa.

26. Majukumu ya Kamati ya Kijiji au Mtaa ya Usimamizi wa Maafa

Kamati ya Kijiji au Mtaa ya Usimamizi wa Maafa itakuwa na jukumu la—
(a)kufuatilia na kuratibu shughuli za usimamizi wa Maafa na operesheni za dharura katika ngazi ya Kijiji au Mtaa;
(b)kusambaza taarifa za tahadhari ya mapema na maelekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya hatari ya Maafa katika Kijiji au Mtaa;
(c)kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za Maafa katika Kijiji au Mtaa;
(d)kuelimisha jamii kuhusu hatua za kuchukua kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa na kukabiliana na majanga katika Kijiji au Mtaa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam na mbinu za asili katika eneo husika;
(e)kuainisha majanga yanayoweza kutokea na kuandaa ramani ya maeneo hatarishi pamoja na kuchukua hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga kwa kutumia rasilimali zilizopo katika Kijiji au Mtaa; na
(f)kutayarisha mkakati wa kupunguza madhara ya majanga na Mpango wa Kukabiliana na Dharura katika Kijiji au Mtaa.

27. Utoaji taarifa za Usimamizi wa Maafa

(1)Kamati za Wataalam za Mikoa za Usimamizi wa Maafa, Kamati za Wataalam za Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya za Usimamizi wa Maafa, Kamati za Kata za Usimamizi wa Maafa na Kamati za Vijiji au Mitaa za Usimamizi wa Maafa zilizoanzishwa chini ya Sheria hii, katika kila robo mwaka au kwa kadri zitakavyoelekezwa, zitaandaa na kuwasilisha katika Wizara taarifa za kina kuhusu utekelezaji wa usimamizi wa Maafa katika mamlaka zake.
(2)Waziri anaweza kutengeneza kanuni zitakazoainisha namna ambavyo Kamati zilizotajwa katika kifungu hiki, zitaandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa usimamizi wa Maafa.

28. Miongozo ya Kamati za Maafa

(1)Waziri anaweza kuandaa miongozo kwa ajili ya usimamizi wa Kamati zilizoanzishwa chini ya Sheria hii.
(2)Miongozo iliyoandaliwa chini ya kifungu hiki itaainisha kuhusu—
(a)utayarishaji na utekelezaji wa mikakati, mipango na taratibu za utendaji katika ngazi mbalimbali za Kamati;
(b)njia za mawasiliano na usambazaji wa taarifa zinazohusu usimamizi wa Maafa;
(c)uandaaji na usambazaji wa taarifa zinazohusu tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua kwa umma na wadau;
(d)uendeshaji wa shughuli za Kamati; na
(e)suala lingine lolote kadri itakavyoonekana ni muhimu.

29. Kanuni za Kamati

Kamati zilizoanzishwa chini ya Sheria hii zitaandaa taratibu za uendeshaji wa shughuli zake katika mamlaka husika.

Sehemu ya Tatu – Mkakati wa taifa wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa na operesheni wakati wa Maafa

30. Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa

(1)Wizara itaandaa, kuratibu na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa.
(2)Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa utajumuisha hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya Maafa kutokea kwa kuainisha kazi zinazopaswa kutekelezwa katika sekta kwa kuzingatia wajibu wa kisheria, vyanzo au sababu za kutokea kwa majanga na madhara ya Maafa yaliyosababishwa.
(3)Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa utawezesha masuala ya kuzuia na kupunguza madhara ya Maafa kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya kisekta na utatumiwa na wizara, idara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa na Kamati zilizoanzishwa chini ya Sheria hii, na asasi mbalimbali katika usimamizi wa Maafa.

31. Wajibu wa jumla

(1)Wizara itaandaa programu za kujenga uwezo kwa Kamati zilizoanzishwa chini ya Sheria hii, taasisi za serikali na taasisi za sekta mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma za lazima na taratibu za kuzingatiwa katika usimamizi wa Maafa.
(2)Kila Wizara, Idara, taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa, na mamlaka za Serikali za mitaa zitakuwa na wajibu wa—
(a)kujumuisha katika mipango na bajeti zao hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na Maafa;
(b)kuainisha hatari za majanga yanayoweza kutokea katika maeneo yao na kuandaa mikakati ya usimamizi wa Maafa; na
(c)kushirikiana na sekta nyingine na wadau mbalimbali katika shughuli za usimamizi wa Maafa.
(3)Kila mtu ana wajibu wa—
(a)kudumisha amani na utulivu wakati wa Maafa;
(b)kuzingatia ushauri wa kitaalamu na maelekezo ya viongozi kuhusu hatua za usimamizi wa Maafa;
(c)kuwa na mwenendo wa maisha utakaowezesha kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali baada ya Maafa; na
(d)kuwa na utayari wa kushiriki katika shughuli za usimamizi wa Maafa.

32. Kutangaza eneo la Maafa

(1)Endapo Waziri ataridhika kwamba mwenendo wa janga unaelekea kuwa Maafa, kwa tangazo katika Gazeti la Serikali, atatangaza kuwa eneo husika ni eneo la Maafa na ataelekeza Mpango wa Taifa wa Kujiandaa Kukabiliana na Maafa kutekelezwa katika eneo hilo kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu au kwa muda mwingine wa nyongeza kwa kadri Waziri atakavyoona inafaa.
(2)Endapo Mpango wa Taifa wa Kujiandaa Kukabiliana na Maafa unatekelezwa katika eneo husika, kila sekta itatekeleza jukumu katika eneo lake kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa kushirikiana na wadau wengine kupitia uratibu wa Wizara.

33. Maafa yanayoashiria hali ya hatari

(1)Endapo dharura ya Maafa inaashiria hali ya hatari ambayo inahitaji kuchukuliwa hatua za kipekee na za haraka na Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa itaridhika kwamba hali ya Maafa inalazimu kutolewa kwa tamko la hali ya hatari, Kamati Elekezi, kwa kuzingatia utaratibu ulioainishwa katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Mamlaka ya Kutangaza Hali ya Hatari, itamtaarifu Rais juu ya matukio yanayolazimu kutolewa kwa tamko la hali ya hatari kwa eneo husika au Tanzania Bara yote.[Sura ya 221]
(2)Tamko la hali ya hatari litaeleza hatua za haraka ambazo zinaweza kuchukuliwa, ikijumuisha—
(a)kuondoa au kutenga watu pamoja na mali zao;
(b)kutumia msaada wa kijeshi;
(c)kuomba msaada kutoka mataifa mengine; au
(d)hatua nyingine yoyote itakayofaa kulingana na hali halisi.

Sehemu ya Nne – Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa

34. Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa

(1)Kutakuwa na Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa.
(2)Vyanzo vya fedha vya Mfuko vitakuwa—
(a)fedha ambayo itaidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya usimamizi wa Maafa;
(b)michango ya hiari kutoka kwa mtu au taasisi yoyote;
(c)fedha yoyote itakayopatikana kwa njia ya msaada au mkopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano;
(d)fedha yoyote itakayopatikana kutokana na mauzo ya vitu vilivyotolewa kama msaada; na
(e)fedha itakayopatikana kupitia michango.
(3)Mfuko utasimamiwa na Wizara na Katibu Mkuu atakuwa afisa masuuli.
(4)Mfuko utatumika kutoa fedha kwa ajili ya—
(a)kuzuia na kupunguza madhara ya majanga;
(b)kujiandaa kwa ajili ya Maafa yanayoweza kutokea;
(c)kukabiliana na Maafa yanapotokea; na
(d)kurejesha hali baada ya Maafa.

35. Usimamizi wa makusanyo na misaada

(1)Wizara inaweza kutoa ombi maalum au la jumla la wataalam, vifaa au fedha kutoka kwa umma kwa madhumuni ya kuokoa maisha, mali, kuzuia au kupunguza uharibifu au kurejesha mfumo wa maisha ya jamii iliyoathirika na Maafa.
(2)Mtu au taasisi inayokusanya vifaa au fedha itatakiwa kuwasilisha kwa kamati za Taifa, Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji au Mtaa au Viongozi wa Kitaifa.
(3)Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (2), misaada kwa ajili ya jamii iliyoathirika na Maafa itapelekwa kwa jamii husika kupitia kamati za Taifa, Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji au Mtaa au Viongozi wa Kitaifa.

Sehemu ya Tano – Masharti ya jumla

36. Makosa na adhabu

(1)Mtu ambaye—
(a)atachelewesha au kumzuia afisa yeyote kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii;
(b)atakataa kutoa ushirikiano kwa afisa yeyote kama atakavyoombwa na afisa kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii;
(c)kwa makusudi atatoa taarifa za uongo au za kupotosha wakati akijibu maswali anayoulizwa na afisa kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii;
atakuwa anatenda kosa na akitiwa hatiani atalipa faini isiyopungua shilingi laki tatu na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua mwezi mmoja na kisichozidi mwaka mmoja.
(2)Mtu ambaye atakusanya michango au misaada kwa ajili ya jamii iliyoathirika na Maafa na kutoiwasilisha katika kamati husika ya Maafa atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atalipa faini sawa na mara mbili ya thamani ya fedha au vitu alivyokusanya au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitano au vyote.

37. Makosa yanayosababishwa na taasisi

Endapo kosa limetendwa chini ya sheria hii na taasisi au kampuni, mtu yeyote ambaye wakati kosa hilo linatendwa alihusika na usimamizi wa taasisi au kampuni hiyo atachukuliwa kuwa yeye ndiye aliyetenda kosa hilo, isipokuwa kama ataithibitishia mahakama kuwa hakufahamu na katika mazingira ya kawaida asingeweza kufahamu kuhusu kutendeka kwa kosa hilo.

38. Adhabu ya jumla

Mtu yeyote anayekiuka masharti yoyote ya Sheria hii, na iwapo hakuna adhabu mahsusi iliyotamkwa, atakuwa anatenda kosa, na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi laki tatu na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua mwezi mmoja na kisichozidi mwaka mmoja au vyote.

39. Kinga dhidi ya mashtaka

Mtu yeyote ambaye kwa mujibu wa Sheria hii au kanuni ameruhusiwa kushiriki katika utekelezaji wa masharti ya Sheria hii hatashtakiwa binafsi kwa jambo lolote alilolitenda au kuacha kutenda kwa nia njema wakati akitekeleza shughuli yoyote ya usimamizi wa Maafa.

40. Kanuni

Waziri atatengeneza Kanuni kuhusu suala lolote ambalo ni la lazima kwa madhumuni ya utekelezaji wa Sheria hii.

41. Kufutwa na masharti ya mwendelezo

(1)Sheria ya Usimamizi wa Maafa inafutwa.
(2)Bila kujali kufutwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, kanuni, amri au matangazo yoyote ya Serikali yaliyotolewa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Maafa na ambayo bado yatakuwa na nguvu kabla ya Sheria hii kuanza kutumika, yataendelea kutumika kama yametolewa chini ya Sheria hii.[Sura 242]
▲ To the top

History of this document

07 October 2022 this version
30 September 2022
Assented to

Subsidiary legislation

Title
Government Notice 658A of 2022