Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka, 2023

Act 13 of 2023

There are outstanding amendments that have not yet been applied. See the History tab for more information.
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka, 2023
Collections
Related documents

Tanzania

Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka, 2023

Tenda 13 ya 2023

Sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kupitia bima ya afya, kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote, kuweka masharti ya kupanua wigo wa huduma mbalimbali za afya; na kuweka masharti mengineyo yanayohusiana na hayo.IMETUNGWA na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina na kuanza kutumika

(1)Sheria hii itajulikana kama Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2023 na itaanza kutumika kwa tarehe ambayo Waziri, kwa tangazo litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, atateua.
(2)Wakati wa utekelezaji wa masharti ya kifungu kidogo cha (1), Waziri anaweza kuteua tarehe tofauti ya kuanza kutumika kwa masharti ya Sehemu au vifungu vya Sheria hii kwa kadiri atakavyoona inafaa.

2. Matumizi

Sheria hii itatumika Tanzania Bara.

3. Definitions

Katika Sheria hii, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—Benki” maana yake ni Benki Kuu ya Tanzania iliyoanzishwa kwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania;[Sura ya 197]bima ya afya kwa wote” maana yake ni utaratibu ulioidhinishwa kwa mujibu wa Sheria hii unaowezesha kila mwananchi kupata huduma za afya kupitia bima ya afya bila kikwazo cha fedha pindi anapozihitaji huduma hizo;Divisheni” ina maana kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Hifadhi ya Jamii;[Sura ya 135]kitita cha bima ya afya cha jamii” maana yake ni kitita cha mafao kilichoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 15;kitita cha huduma za ziada” maana yake ni kitita cha huduma za afya zaidi ya kitita cha mafao ya huduma muhimu kinachotolewa na skimu ya bima ya afya;kitita cha mafao” maana yake ni huduma za afya zinazotolewa kwa mnufaika wa skimu ya bima ya afya;kitita cha mafao ya huduma muhimu” maana yake ni kitita cha mafao kilicho anzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 14;kitita maalum cha mafao” maana yake ni kitita cha mafao kitakachoanzishwa chini ya kifungu cha 8(2);kituo cha huduma za afya” inajumuisha kliniki, zahanati, kituo cha afya, hospitali, maabara, duka la dawa au kituo kingine chochote kinachotoa huduma za afya;kituo cha huduma za afya kilichoingia mkataba” maana yake kituo cha kutolea huduma za afya kilichoingia makubaliano na skimu kuwahudumia wanufaika kwa mujibu wa Sheria hii;kiwango cha mchango” maana yake ni kiwango kutoka katika mshahara au chanzo kingine chochote kitakacholipwa katika skimu ya bima ya afya na mwanachama au kwa niaba ya mwanachama;kiwango cha uchangiaji” maana yake ni kiasi cha fedha kinacholipwa kwa lengo la kuwa mwanachama kwa mujibu wa Sheria hii;Mamlaka” maana yake ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bima;[Sura ya 394]mkazi” ina maana kama ilivyotafsiriwa katika Sheria ya Uhamiaji;[Sura ya 54]mnufaika” maana yake ni mtu anayestahili kupata mafao ya matibabu chini ya Sheria hii;mshahara” kwa madhumuni ya:(a)mtumishi wa umma, maana yake ni mshahara usiojumuisha malipo ya ziada, stahiki, na posho;(b)mwajiriwa wa sekta binafsi, maana yake ni mshahara unaojumuisha stahiki zote za kisheria zinazolipwa kama sehemu ya mshahara wa mwajiriwa;mtegemezi” maana yake ni—(a)mzazi wa mwanachama au mzazi wa mwenza wa mwanachama;(b)mtoto wa mwanachama wa kuzaa, kuasili au wa kambo aliye na umri chini ya miaka ishirini na moja; au(c)ndugu wa damu wa mwanachama aliye na umri wa chini ya miaka ishirini na moja;mtoa huduma” inajumuisha kituo cha kutolea huduma za afya na skimu ya bima ya afya chini ya Sheria hii.mtu aliyejiajiri” maana yake ni mtu anayefanya kazi asiye katika uhusiano wa mwajiri na mwajiriwa;mtu asiye na uwezo” maana yake ni mtu anayeishi kwa kipato kilicho chini ya mstari unaopima kiwango cha umaskini kama inavyofafanuliwa na mamlaka husika;mwajiri” ina maana kama ilivyotafsiriwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini;[Sura ya 366]mwajiriwa” ina maana kama ilivyotafsiriwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini;[Sura ya 366]mwanachama” maana yake ni mtu yeyote aliyesajiliwa katika skimu chini ya Sheria hii na anachangia ama yeye mwenyewe au kupitia kwa Serikali;[Sura ya 366]ndugu wa damu” maana yake ni kaka au dada wa kuzaliwa wa mwanachama na aliye chini ya umri wa miaka ishirini na moja;raia” ina maana kama ilivyotafsiriwa katika Sheria ya Uraia;sekta isiyo rasmi” maana yake ni sekta inayojumuisha wafanyakazi wanaofanya kazi zisizo rasmi na ambao hawana mikataba ya ajira au mikataba mingine yoyote iliyoelezewa katika tafsiri ya neno “mwajiriwa” na inajumuisha mtu asiyejihusisha na aina yoyote ya uzalishaji;sekta rasmi” maana yake ni sekta inayojumuisha kazi zilizorasimishwa na kufanywa kwa mikataba ambapo mikataba hiyo imeainisha mishahara au ujira na muda maalum wa kazi;sekta rasmi binafsi” inajumuisha wafanyakazi katika mashirika au taasisi isipokuwa watumishi wa sekta ya umma;sekta ya umma” maana yake ni sekta inayojumuisha watumishi wa umma pamoja na wafanyakazi katika mashirika au taasisi binafsi ambayo Serikali inamiliki angalau asilimia thelathini ya hisa;skimu ya bima ya afya” maana yake ni bima ya afya ya umma au kampuni binafsi inayotoa huduma za bima ya afya chini ya Sheria hii;skimu ya bima ya afya binafsi” maana yake ni bima ya afya iliyoanzishwa au kutambuliwa chini ya Sheria hii;skimu ya bima ya afya ya umma” maana yake ni bima ya afya iliyoanzishwa au kutambuliwa chini ya Sheria hii;Waziri” maana yake ni Waziri mwenye dhamana na masuala ya afya; naWizara” maana yake ni Wizara yenye dhamana ya masuala ya afya.

4. Malengo

Malengo ya Sheria hii yatakuwa—
(a)kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote kupitia mfumo wa bima ya afya; na
(b)kuweka mfumo wa ushiriki katika skimu za bima ya afya kwa raia na wakazi wote.

Sehemu ya pili – Mfumo wa bima ya afya kwa wote

5. Ulazima wa bima ya afya

(1)Bima ya afya itakuwa ni ya lazima kwa watu wote.
(2)Kwa kuzingatia masharti ya Sheria hii, kila mtu anapaswa kujiunga na skimu ya bima ya afya ili kuhakikisha anapata huduma za afya.
(3)Kila mwajiri atatakiwa kumchangia mwajiriwa wake katika skimu ya bima ya afya kiwango cha uchangiaji kwa kuzingatia masharti ya Sheria hii.
(4)Wageni wote wenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi wanaoingia nchini na kukaa zaidi ya siku thelathini ambao hawana bima ya afya inayotambulika nchini watapaswa kujiunga na bima ya afya kwa mujibu wa Sheria hii.

6. Mfumo wa bima ya afya

Mfumo wa bima ya afya kwa wote utajumuisha—
(a)waajiri na waajiriwa katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi;
(b)watu walioko katika sekta isiyo rasmi;
(c)skimu za bima ya afya;
(d)watu wasio na uwezo;
(e)vituo vya kutolea huduma za afya; na
(f)Mamlaka.

7. Udhibiti wa mfumo wa bima ya afya

(1)Mamlaka ya Udhibiti wa bima iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Bima itakuwa ndiyo mamlaka ya udhibiti wa huduma za bima ya afya.
(2)Kwa madhumuni ya kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya kwa wote, Mamlaka itakuwa na wajibu wa—
(a)kusajili skimu za bima ya afya;
(b)kuhakikisha bima za afya zinatoa kitita cha mafao ya huduma muhimu kwa mujibu wa Sheria hii;
(c)kuhakikisha huduma za bima zinazotolewa zinaendana na viwango vya michango;
(d)kutoa miongozo ya malipo kwa watoa huduma;
(e)kutoa miongozo ya uendeshaji wenye ufanisi na tija katika usimamizi wa skimu za bima ya afya;
(f)kuhakikisha kuwa skimu ya bima ya afya ina ukwasi na akiba kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa;
(g)kutunza kanzidata ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoingia mikataba na skimu za bima ya afya;
(h)kufanya ukaguzi wa skimu za bima ya afya;
(i)kuweka miongozo kuhusu usajili wa wanachama katika skimu za bima ya afya;
(j)kuomba au kuitisha taarifa yoyote itakayoihitaji;
(k)kufanya tafiti na uvumbuzi kwa lengo la kuendeleza ufanisi na uendelevu wa mfumo wa bima ya afya kwa wote”; na
(l)kutekeleza jukumu lingine lolote kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa Sheria hii.
(3)Kila mwaka wa fedha au kwa kadiri itakavyohitajika, Mamlaka itawasilisha kwa Divisheni na nakala kwa Wizara, taarifa kuhusu udhibiti wa huduma za bima ya afya.

Sehemu ya tatu – Skimu za bima ya afya

8. Skimu ya bima ya afya ya umma

(1)Kwa madhumuni ya Sheria hii, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulioanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utatambulika kama skimu ya bima ya afya ya umma.
(2)Waziri kwa kushauriana na Mamlaka na kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni, anaweza kuboresha skimu ya bima ya afya ya umma ikiwemo kuanzisha kitita maalum cha mafao kulingana na uhitaji kwa lengo la kufikia bima ya afya kwa wote.
[Sura ya 395]

9. Skimu ya bima ya afya binafsi

(1)Mtu atakuwa na sifa ya kusajiliwa kuwa skimu ya bima ya afya ya binafsi baada ya kutimiza masharti kama yatakavyoainishwa katika kanuni chini ya Sheria hii.
(2)Bila kujali masharti ya kifungu kidogo cha (1), kampuni au chombo kilichoidhinishwa chini ya Sheria ya Bima kutoa bima ya afya, kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii, kitaendelea kutoa huduma kama skimu ya bima ya afya binafsi baada ya kutimiza masharti ya Sheria hii.[Sura ya 394]

10. Zuio la kuendesha skimu ya bima ya afya

(1)Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika Sheria hii, mtu hataendesha skimu ya bima ya afya isipokuwa kama amepewa cheti cha usajili na Mamlaka kwa mujibu wa Sheria hii.
(2)Kila skimu ya bima ya afya itatatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia masharti kama yalivyoainishwa katika Sheria hii.

11. Utunzaji wa rejesta

Mamlaka itatunza rejesta ya skimu za bima ya afya zilizosajiliwa kwa mujibu wa Sheria hii na skimu nyingine za bima ya afya zilizokuwepo kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii.

12. Kufuta usajili wa skimu ya bima ya afya

(1)Mamlaka inaweza kufuta usajili wa skimu ya bima ya afya iwapo—
(a)Sheria iliyoanzisha skimu ya bima ya afya ya umma imefutwa;
(b)skimu ya bima ya afya imekiuka masharti ya Sheria hii, kanuni au miongozo chini ya Sheria hii;
(c)skimu ya bima ya afya imesitisha kutoa huduma za bima au imefilisika;
(d)skimu ya bima ya afya imeomba kufutiwa usajili na Mamlaka imeridhia maombi hayo; au
(e)skimu ya bima ya afya imepoteza sifa za kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria hii.
(2)Mamlaka, kabla ya kufuta usajili wa skimu ya bima ya afya, itatoa notisi ya angalau siku tisini ya kusudio lake la kufanya hivyo ikiitaka skimu ya bima ya afya kutoa sababu kwanini Mamlaka isifute usajili wa skimu hiyo.
(3)Skimu ya bima ya afya, baada ya kupokea notisi iliyotolewa chini ya kifungu kidogo cha (2)—
(a)itasitisha usajili wa wanachama wapya kuanzia tarehe ya kupokea notisi ya kufuta usajili hadi itakapoelekezwa vinginevyo na Mamlaka; na
(b)itaendelea, chini ya uangalizi wa Mamlaka, kutoa huduma kwa wanachama na kulipa vituo vilivyoingia mikataba na skimu hiyo.
(4)Mamlaka, kwa namna itakavyoainishwa katika kanuni, itaweka utaratibu utakaohakikisha kuwa wanachama hawaathiriki na kufutwa kwa skimu.

Sehemu ya nne – Vitita vya mafao

(a) – Kitita cha mafao ya huduma muhimu

13. Kitita cha mafao ya huduma muhimu

(1)Mwanachama au mnufaika wa skimu ya bima ya afya atakuwa na haki ya kupata kitita cha mafao ya huduma muhimu, kama hitaji la msingi, kama ambavyo itaainishwa chini ya Sheria hii.
(2)Kitita cha mafao ya huduma muhimu kitatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ambayo mwanachama atasajiliwa kujiunga na Bima ya Afya:Isipokuwa kwamba, kitita cha mafao ya huduma muhimu kwa mwanachama anayechangia kwa mujibu wa kifungu cha 23(1) kitaendelea kutumika hadi kufikia ukomo wake kwa kuzingatia masharti ya kifungu 28(2) cha Sheria hii.
(3)Bila kuathiri kifungu kidogo cha (1), mwanachama au mnufaika wa skimu ya bima ya afya, anaweza, kwa kutegemea mpango wa skimu husika, kupata kitita cha huduma za ziada.

14. Huduma za kitita cha mafao ya huduma muhimu

(1)Kitita cha mafao ya huduma muhimu kitajumuisha huduma za afya zitakazopatikana kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa.
(2)Kila skimu ya bima ya afya itatoa kitita cha mafao ya huduma muhimu kwa wanachama na wanufaika wake kama hitaji la msingi.
(3)Huduma zitakazotolewa katika kitita cha mafao ya huduma muhimu zitakuwa kama zilivyoorodheshwa katika Sehemu A ya Jedwali la Sheria hii.
(4)Waziri, kwa Amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, anaweza kurekebisha, kuboresha au kufuta Sehemu A ya Jedwali la Sheria hii:Isipokuwa kwamba, mabadiliko ya kitita cha mafao ya huduma muhimu yatazingatia matokeo ya tathmini ya uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya.

(b) – Kitita cha bima ya afya cha jamii

15. Kitita cha bima ya afya cha jamii

(1)Kwa madhumuni ya kufikia bima ya afya kwa wote, kutakuwa na kitita cha bima ya afya cha jamii chini ya skimu ya bima ya afya ya umma kitakachojumuisha huduma za afya zitakazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
(2)Mtu ambaye hatokuwa na bima ya afya yoyote chini ya Sheria hii, atapaswa kuwa na kitita cha bima ya afya ya Jamii.
(3)Huduma zitakazotolewa chini ya kifungu kidogo cha (1) zitakuwa kama ilivyoorodheshwa katika Sehemu B ya Jedwali la Sheria hii.
(4)Waziri, kwa Amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, anaweza kurekebisha, kuboresha au kufuta Sehemu B ya Jedwali la Sheria hii.

16. Akaunti ya kitita cha bima ya afya cha jamii

(1)Skimu ya bima ya afya ya umma itafungua akaunti maalumu ya kitita cha bima ya afya cha jamii ambapo fedha kutoka katika vyanzo vifuatavyo itawekwa:
(a)michango ya wanachama;
(b)fedha zitakazotengwa na Bunge;
(c)vyanzo vingine vitakavyotengwa na Serikali;
(d)misaada na zawadi kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi;
(e)fedha kutoka chanzo kingine chochote ambacho ni halali.
(2)Fedha katika akaunti maalumu chini ya kifungu hiki zitatumika kwa ajili ya huduma za bima ya afya kwa wanufaika wa kitita cha bima ya afya cha jamii pamoja na gharama za uendeshaji wake:Isipokuwa kwamba, gharama za uendeshaji wa akaunti maalumu hazitazidi asilimia 15 ya michango ya wanachama.

17. Usimamizi na uendeshaji wa kitita cha bima ya afya cha jamii

Waziri, kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana na masuala ya serikali za mitaa, anaweza kutunga kanuni kwa ajili ya kuweka utaratibu wa usimamizi na uendeshaji wa kitita cha bima ya afya cha jamii.

(c) – Kitita cha huduma za ziada

18. Kitita cha huduma za ziada

(1)Skimu ya bima ya afya inaweza kutoa huduma ya ziada ya kitita cha mafao ya huduma muhimu kwa wanufaika wake na michango kuhusiana na kitita cha huduma za ziada itakuwa kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa na Mamlaka.
(2)Mamlaka itasimamia ushindani katika utoaji wa vitita vya huduma za ziada wa skimu za bima ya afya kwa madhumuni ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora.

Sehemu ya tano – Uanachama na uchangiaji katika skimu ya bima ya afya

19. Uanachama

(1)Uanachama katika skimu ya bima ya afya utajumuisha watu wafuatao:
(a)watu wote ambao kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii walikuwa wanachama wa skimu ya bima ya afya kama ilivyoainishwa katika Sheria zinazosimamia skimu husika;
(b)watu wote ambao katika tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria hii watakuwa wametimiza umri wa miaka ishirini na moja;
(c)watu wote ambao, kwa tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria hii, watakuwa chini ya umri wa miaka ishirini na moja lakini wanasifa za kusajiliwa kuwa wanachama kwa mujibu wa Sheria hii au Sheria nyingine yoyote;
(d)watu wote walioaj iriwa katika sekta binafsi au ya umma;
(e)watu wote waliojiajiri;
(f)watu wasio na uwezo; na
(g)makundi mengine ya watu kadri itakavyoainishwa na Waziri katika kanuni.
(2)Mtu kutoka sekta rasmi binafsi au sekta isiyo rasmi atajiunga na skimu ya bima ya afya yoyote.

20. Wanufaika

Mwanachama anaweza kusajili watu wafuatao kama wanufaika:
(a)mwenza wa mwanachama; na
(b)wategemezi wasiozidi wanne.

21. Wigo wa upatikanaji wa huduma za afya

Mwanachama au mnufaika anaweza kupata huduma za afya mahala popote katika kituo cha kutolea huduma za afya kilichoingia mkataba na skimu ya bima ya afya kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ikiwemo miongozo ya rufaa.

22. Usajili wa wanachama katika skimu ya bima ya afya

(1)Kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni, mwajiri katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi atapaswa kumsajili mwajiriwa katika skimu ya bima ya afya ndani ya siku thelathini kutoka tarehe ya kuanza kwa mkataba wa ajira.
(2)Kila raia au mkazi aliye katika sekta rasmi na isiyo rasmi atasajiliwa katika skimu ya bima ya afya kwa utaratibu utakaoanishwa katika kanuni.

23. Viwango vya uchangiaji

(1)Kwa madhumuni ya upatikanaji wa kitita cha mafao ya huduma muhimu katika skimu ya bima ya afya ya umma, kila mwajiri katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi atawasilisha katika skimu hiyo kiwango cha mchango kwa kuzingatia Sheria inayosimamia skimu ya bima ya afya ya umma.
(2)Bila kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (1), mwajiri katika sekta rasmi binafsi anaweza kumsajili mwajiriwa wake katika skimu ya bima ya afya ya binafsi na kuwasilisha kiwango cha uchangiaji kitakachopangwa na skimu hiyo baada ya kuidhinishwa na Mamlaka.
(3)Waziri kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, ataainisha viwango vya uchangiaji kwa ajili ya sekta isiyo rasmi, kama itakavyoainishwa katika kanuni, kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya katika utoaji wa kitita cha mafao ya huduma muhimu.

24. Utambuzi na upatikanaji wa huduma kwa watu wasio na uwezo

(1)Waziri, kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika, na kwa kupitia kanuni, ataweka utaratibu na namna ya utambuzi wa watu wasio na uwezo.
(2)Watu watakaotambuliwa kama watu wasio na uwezo chini ya kifungu kidogo cha (1) watakuwa na haki ya kujumuishwa chini ya skimu ya bima ya afya kwa namna itakayoainishwa kwenye kanuni.
(3)Waziri, kwa madhumuni ya Sheria hii, atatunza na kuhuisha kanzidata ya watu waliotambuliwa chini ya kifungu kidogo cha (1).

25. Mfuko wa kugharamia wasio na uwezo, nk.

(1)Kunaanzishwa mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.
(2)Bila kuathiri kifungu kidogo cha (1), Mfuko unaweza kutumika kugharamia—
(a)huduma za matibabu ya magonjwa sugu na ya muda mrefu; na
(b)huduma za afya za dharura zitokanazo na ajali, kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa na Wizara.
(3)Kwa kuzingatia masharti ya sheria za fedha, fedha zinazolipwa katika Mfuko wa kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo zitatatokana na vyanzo vifuatavyo—
(a)mapato yatokanayo na miamala ya kielektroniki kwa kiwango kitakachoainishwa katika Sheria za fedha;
(b)kwa namna itakavyopendekezwa na Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha—
(i)mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa za vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vyenye vileo na bidhaa za vipodozi;
(ii)kodi kwenye michezo ya kubahatisha; na
(iii)ada ya bima ya vyombo vya moto.
(c)fedha zitakazotengwa na Bunge;
(d)mapato yatakayotokana na uwekezaji wa Mfuko; na
(e)zawadi na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali;
(4)Waziri kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha ataweka utaratibu wa usimamizi bora wa Mfuko.

26. Uwekaji wa amana

(1)Mtu anayeendesha skimu ya bima ya afya binafsi, kama sharti la usajili, ataweka Benki kiwango cha fedha kilichoainishwa kwenye Sheria ya Bima.
(2)Skimu ya bima ya afya itatunza akiba ya kiasi cha fedha kitakachotosheleza utolewaji wa huduma kwa wanachama wake kwa kipindi cha angalau miaka miwili, kwa namna itakavyoainishwa katika kanuni.
(3)Amana inayorejewa katika kifungu kidogo cha (1) itadumu kwa kipindi chote cha uendeshaji wa skimu ya bima ya afya binafsi.

27. Utambuzi wa uanachama

Skimu ya bima ya afya itaweka utaratibu kwa ajili ya—
(a)upatikanaji wa utambulisho kwa mwanachama na wanufaika wake; na
(b)uhakiki wa utambulisho uliotolewa na huduma zinazotolewa na kituo cha kutolea huduma za afya.

28. Ukomo wa uanachama

(1)Uanachama katika skimu ya bima ya afya utakoma baada ya kutokea kwa kifo cha mwanachama au pale ambapo mwanachama ataacha kuchangia kwenye skimu ya bima ya afya kwa kipindi kitakachoainishwa kwenye kanuni.
(2)Iwapo mwanachama anayechangia kupitia makato ya mshahara wake atafariki, atapata ulemavu wa kudumu au ataachishwa kazi, wategemezi wake wataendelea kunufaika na huduma kwa kipindi kitakachoinishwa katika kanuni.
(3)Iwapo mwanachama anayechangia kwa utaratibu wa michango kwa mwaka atafariki, wategemezi wake wataendelea kunufaika na huduma kwa kipindi kilichosalia cha mkataba wa uanachama.

Sehemu ya sita – Udhibiti ubora

29. Viwango vya udhibiti ubora vya skimu ya bima ya afya

Skimu ya bima ya afya itatekeleza viwango vya ubora vitakavyoainishwa na Mamlaka.

30. Udhibiti ubora wa watoa huduma za afya

Wizara itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa vituo vya kutolea huduma vilivyoingia mikataba na skimu za bima ya afya vinatekeleza viwango vya ubora vilivyotolewa na Wizara au kwa mujibu wa Sheria.

Sehemu ya saba – Masharti mengineyo

31. Ukwasi na uendelevu wa bima ya afya

(1)Skimu ya bima ya afya itatakiwa kufanya tathmini ya uhai na uendelevu kila baada ya miaka mitatu au wakati wowote kadiri itakavyokuwa imeelekezwa na Mamlaka kwa kumtumia mtathmini.
(2)Taarifa ya tathmini itakayofanywa kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (1) itawasilishwa kwa Mamlaka na nakala kupelekwa kwa Waziri.
(3)Mamlaka inaweza kuelekeza skimu ya bima ya afya kuchukua hatua kama itakavyohitajika kurekebisha upungufu ulioonekana katika taarifa ya tathmini ya uhai na uendelevu.

32. Uwekezaji wa skimu za bima ya afya

(1)Uwekezaji wa skimu za bima ya afya utazingatia miongozo itakayotolewa na Benki kwa kushauriana na Mamlaka.
(2)Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (1), Benki, kwa kushirikiana na Mamlaka, itakuwa na mamlaka ya—
(a)kutoa miongozo ya uwekezaji wa skimu za bima ya afya;
(b)kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa skimu za bima ya afya kwa wahusika wote chini ya Sheria hii; au
(c)kuchunguza na kukagua masuala yote yanayohusiana na usimamizi wa fedha wa skimu za bima ya afya.

33. Gharama za usimamizi na uendeshaji

Mamlaka itatoa miongozo kuhusu ukomo wa juu wa gharama za uendeshaji wa skimu ya bima ya afya.

34. Malalamiko na usuluhishi wa migogoro

Utaratibu wa kushughulikia malalamiko na utatuzi wa migogoro baina ya au dhidi ya skimu ya bima ya afya, kituo cha huduma za afya kilichoingia mkataba, mnufaika, mwajiri na mtu yeyote anayehusika utakua kama ulivyoainishwa kwenye Sheria ya Bima.[Sura ya 394]

35. Mamlaka ya kutunga kanuni

Waziri anaweza kutengeneza kanuni zitakazoainisha—
(a)utaratibu wa usajili wa skimu za bima ya afya;
(b)kitita cha mafao, muda, masharti au wigo wa kitita cha mafao kwa kushirikiana na Mamlaka;
(c)utaratibu wa kuboresha skimu ya bima ya afya ya umma ikiwemo kuanzisha kitita cha mafao maalum;
(d)muda wa kuahirishwa kwa malipo yoyote ya madai wakati uchunguzi unaendelea;
(e)utaratibu wa kusajiliwa kwenye skimu ya bima ya afya kwa watu wenye umri chini ya miaka ishirini na moja;
(f)utaratibu wa ulipaji wa faini zote au sehemu ya faini kwa kuzingatia masharti kama yatakavyoainishwa;
(g)utaratibu wa utambuzi wa watu walio katika sekta isiyo rasmi na namna ya kuwasajilii katika skimu;
(h)maelezo, taarifa, uthibitisho au ushahidi utakaotolewa kwa suala lolote au jambo linalojitokeza chini ya Sheria hii, ikiwemo suala lolote au jambo muhimu kuhusiana na malipo ya michango aliyolipa mwanachama au kuhusiana na mtu yeyote au uandaaji au uhalalishaji wa madai yoyote au maombi kwa ajili ya malipo ya mafao yoyote yanayotolewa chini ya Sheria hii;
(i)utaratibu wa malipo kwa vituo vya kutolea huduma za afya;
(j)hatua yoyote inayohitajika au kuruhusiwa kuchukuliwa chini ya Sheria hii, muda na namna ya kuchukua hatua hiyo, utaratibu utakaofuatwa na fomu zitakazotumika;
(k)utambuzi na usajili wa watu wasio na uwezo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine;
(l)namna ya upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wasio na uwezo;
(m)utaratibu wa kuboresha kitita cha mafao katika skimu ya bima ya afya ya umma; na
(n)suala lingine lolote kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya Sheria hii.

36. Taarifa za uongo

(1)Mtu yeyote ambaye—
(a)kwa madhumuni ya kukwepa kulipa mchango wake au wa mtu yeyote mwingine kwa niaba yake, kwa kufahamu, akitoa taarifa zozote za uongo au kusababisha kutolewa kwa nyaraka au taarifa ambazo anaamini kuwa ni za uongo;
(b)kwa madhumuni ya kunufaika au kufidiwa yeye binafsi au mtu yeyote mwingine, kwa kufahamu, akitoa taarifa zozote za uongo au kusababisha kutolewa kwa nyaraka au taarifa ambazo anaamini kuwa ni za uongo;
(c)anashindwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika chini ya Sheria hii pasipokuwa na sababu za msingi,
natenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika—
(i)kwa kosa lililotendwa na mwanachama au mnufaika, kulipa faini isiyopungua shilingi laki tano na isiyozidi shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi kumi na mbili au vyote;
(ii)kwa kosa lililotendwa na skimu ya bima ya afya, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi na isiyozidi shilingi milioni mia moja, na mahakama inaweza ikaamuru kulipwa kwa fidia ya hasara iliyosababishwa; na
(iii)kwa kosa liliotendwa na kituo cha kutolea huduma za afya, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tano na isiyozidi shilingi milioni hamsini na mahakama inaweza ikaamuru kulipwa kwa fidia ya hasara iliyosababishwa;
(2)Bila kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (1), Mamlaka
(a)inaweza kuifungia skimu ya bima ya afya au kituo cha kutolea huduma za afya kitakachobainika kutenda kosa chini ya kifungu hiki kwa kipindi kisichozidi miaka miwili; au
(b)itaitaarifu mamlaka husika ya kitaaluma kuchukua hatua stahiki dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa kukiuka masharti ya kifungu hiki.

37. Kutojiunga na skimu ya bima ya afya

(1)Isipokuwa kwa wageni wanaoingia nchini ambao masharti mengine kuhusu adhabu katika Sheria hii yatatumika, mtu yeyote ambaye bila sababu za msingi atashindwa kujiunga na skimu ya bima ya afya ndani ya miaka mitatu tangu kuanza kutumika kwa Sheria, atakapojiunga na bima ya afya, atalazimika kulipa riba ya asilimia 10 ya kiwango cha uchangiaji kwa kila mwaka wa uchangiaji.
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), Waziri, kwa notisi itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali na kwa kuzingatia maslahi ya umma au kwasababu yoyote nyingine atakayoainisha katika notisi, anaweza kutoa msamaha wa ulipwaji wa riba kwa watu au kundi lolote lenye wajibu wa kujiunga na skimu ya bima ya afya chini ya Sheria hii.

38. Utaratibu wa madai ya skimu ya bima ya afya

(1)Mahakama inayosikiliza shauri dhidi ya mtu yoyote aliyeshtakiwa kwa kosa chini ya Sheria hii, bila kujali uwepo wa shauri lolote la madai, inaweza kuamuru mshtakiwa kuilipa skimu ya bima ya afya kiasi cha mchango kinachodaiwa pamoja na faini itakayotozwa au gharama nyingine yoyote, na kiasi kitakachoamriwa kinaweza kudaiwa na kulipwa kwa skimu.
(2)Kiasi chochote kinachodaiwa na skimu ya bima ya afya kitakuwa ni deni kwa skimu na, bila kuathiri namna nyingine ya kudai, kiasi hicho kinaweza kudaiwa kwa njia ya madai ya haraka kwa mujibu wa kanuni ya XXXV ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.[Sura ya 33]

39. Makosa ya jumla

Mtu anayekiuka masharti yoyote ya Sheria hii pale ambapo hakuna adhabu mahususi iliyowekwa, anatenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika—
(a)iwapo ni mtu binafsi, kulipa faini isiyopungua shilingi laki tano na isiyozidi shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote; na
(b)iwapo ni kampuni au taasisi, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi na iziyozidi shilingi milioni mia moja.

40. Makosa yatendwayo na taasisi

Endapo kosa limetendwa na kampuni au taasisi chini ya Sheria hii, mkurugenzi, meneja au mbia wa kampuni au taasisi hiyo atawajibika, ikiwa atatiwa hatiani, kwa adhabu iliyoainishwa kuhusiana na kosa hilo, isipokuwa kama mkurugenzi, meneja au mbia huyo ataithibitishia mahakama kwa kiasi cha kuiridhisha kwamba kitendo kilichosababisha kosa hilo kufanyika kilifanyika pasipo yeye kuwa na uelewa, kutoa idhini au kuchukua hatua za makusudi kuzuia kosa hilo kutendeka.

41. Mkinzano na sheria nyingine

Endapo kutakuwa na mkinzano baina ya masharti ya Sheria hii na masharti ya sheria nyingine yoyote kuhusiana na masuala ya bima ya afya, masharti ya Sheria hii yatapewa kipaumbele.

Sehemu ya nane – Kufutwa kwa sheria na masharti ya mpito

42. Kufutwa kwa sheria na masharti yanayoendelea

(1)Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii inafutwa.
(2)Bila kujali kufutwa kwa Sheria chini ya kifungu kidogo cha (1)—
(a)kanuni, amri, miongozo na sheria ndogo nyingine zilizotungwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii na ambazo zilikuwa zinatumika kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii, zitaendelea kutumika hadi zitakapofutwa;
(b)maelekezo yote yaliyotolewa chini ya masharti ya Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii yataendelea kuwa halali hadi hapo yatakapofutwa, kusitishwa au kukoma kutokana na sababu ya kuisha kwa muda wake;
(c)mtu ambaye wakati wa kuanza kutumika kwa Sheria hii alikuwa akinufaika na mafao ya Mfuko wa Afya ya Jamii ataendelea kunufaika na mafao hayo hadi Waziri atakapoweka utaratibu wa kujiunga na kitita cha bima ya afya cha jamii kilichowekwa kwa mujibu wa Sheria hii; na
(d)haki na afua ambazo, kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii zilitolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii, zitaendelea kuwepo kana kwamba zilitolewa chini ya Sheria hii hadi hapo zitakapofutwa kwa mujibu wa Sheria hii.
[Sura ya 409]

43. Masharti ya mpito

(1)Kutakuwa na kipindi cha mpito kisichozidi miezi kumi na mbili, kitakachoanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria hii.
(2)Kwa kuzingatia Sheria hii na kabla kuisha kwa kipindi cha mpito, Wizara kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana na mamlaka za serikali za mitaa na mamlaka nyingine husika, itaratibu uhitimishwaji wa shughuli za Mfuko wa Afya ya Jamii ikiwa ni pamoja na utambuzi wa mali, madeni, madai, hatma ya mikataba iliyopo, mashauri yaliyopo na masuala mengine yanayohusiana na Mfuko wa Afya ya Jamii kwa namna itakavyoainishwa katika kanuni.
(3)Bila kujali masharti ya kifungu kidogo cha (1), Waziri anaweza kuongeza muda wa kipindi cha mpito kwa kipindi kingine cha ziada kisichozidi miezi sita.

Sehemu ya tisa – Marekebisho ya sheria mbalimbali

(a) – Sheria ya fuko wa ta.fa wa bima ya afya

[Sura ya 395]

44. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 395]

45. Marekebisho ya kifungu cha 2

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 2(1) kwa kuongeza maneno “persons under formal private sector, students” kati ya maneno “Councillors,” na “retirees”.

46. Marekebisho ya kifungu cha 3

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 3 kwa kufuta tafsiri ya neno “Authority” na badala yake kuweka tafsiri ifuatayo:“Authority” has the meaning ascribed to it under the Universal Health Insurance Act;”.

47. Marekebisho ya kifungu cha 11

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu 11(1) kwa kuongeza maneno “persons under formal private sector, student and children” baada ya neno “Councilors” lililopo katika aya (e).

48. kufutwa na kuandikwa upya kwa kifungu cha 16

Sheria Kuu inarekebishwa kwa kufuta kifungu cha 16 na badala yake kuweka kifungu kifuatacho:

16. Benefit package

(1)The Fund shall provide the standard benefit package in accordance with the Universal Health Insurance Act.
(2)Without prejudice to the provisions of subsection (1), the Fund may provide supplementary benefit packages in accordance with the Universal Health Insurance Act.”.

49. Kufutwa na kuandikwa upya kwa kifungu cha 40

Sheria Kuu inarekebishwa kwa kufuta kifungu cha 40 na badala yake kuweka kifungu kifuatacho:

40. Appeal

A member or health care provider who is aggrieved by any decision of an officer of a scheme may appeal to the Ombudsman through the Authority in accordance with section 1 24(5) of the Insurance Act.[Cap. 394]”.

50. Kufutwa kwa vifungu vya 41 na 42

Sheria ya Kuu inarekebishwa kwa kufuta vifungu vya 41 na 42

(b) – Sheria ya hfadhi ya jamii

[Sura ya 135]

51. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Hifadhi ya Jamii ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 135]

52. Marekebisho ya kifungu cha 61

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 61(b)(ii) kwa kufuta maneno “Ministry responsible for health matters” na badala yake kuweka maneno “Tanzania Insurance Regulatory Authority pursuant to the Universal Health Insurance Act.”

(c) – Sheria ya bima

[Sura ya 394]

53. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Bima ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 394]

54. Marekebisho ya kifungu cha 6

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 6—
(a)katika kifungu kidogo cha (1), kwa kuongeza maneno “health insurance scheme members, employers, health service providers and health insurance schemes” baada ya neno “policy-holders”;
(b)katika kifungu kidogo cha (2) kwa—
(i)kuongeza maneno “health insurance scheme members, employers, health service providers and health insurance schemes” baada ya neno “policyholder” lililopo mwishoni mwa aya (j);
(ii)kuongeza aya mpya mara baada ya aya (k) kama ifuatavyo:
(l)oversee and ensure quality assurance of the primary benefit package and contribution rates in collaboration with the Ministry responsible for health matters;
(m)supervise and regulate funds, insurance companies and health care providers;
(n)supervise the compliance of laws related with insurance;” na
(iii)kubadilisha mpangalio wa aya (l) na (m) kuwa aya (o) na (p), mtawalia.

55. Marekebisho ya kifungu cha 123

Sheria Kuu inarekebishwa kwa—
(a)kukifanya kifungu cha 123 kuwa kifungu cha 123(1); na
(b)kuongeza mara baada ya kifungu kidogo cha (1) kifungu kidogo cha (2) kama ifuatavyo:
(2)Notwithstanding subsection (1)—
(a)health insurance schemes may file to the Ombudsman complaints against a member of a health insurance scheme or a health service provider; and
(b)a member of a health insurance scheme and health service provider may file to the ombudsman applications for review against the decision of a health insurance scheme.”.

56. Marekebisho ya kifungu cha 124

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 124 kwa kuongeza mara baada ya kifungu kidogo cha (4), kifungu kidogo cha (5) kama ifuatavyo:
(5)Notwithstanding subsection (1), the Ombudsman shall have unlimited jurisdiction to determine health insurance related complaints from a member of a health insurance scheme or a health service provider referred to it by the Authority.”.

57. Marekebisho ya kifungu cha 126

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 126 kwa kufuta na kuandika upya kifungu kidogo cha (2) kama ifuatavyo—
(2)The Tribunal shall be an adhoc forum consisting of five persons as follows:
(a)three persons appointed by the Minister with adequate experience in insurance matters, provided that, one of the members shall be a law officer from the Office of the Attomey General;
(b)two persons appointed by the Minister in consultation with the Minister responsible for health matters who shall be persons with adequate experience in health matters, provided that, consultation with the Minister responsible for health shall only be sought where a Tribunal is constituted to handle health insurance matters.”.

(d) – Sheria ya fuko wa ta.fawahfadhi ya jamii

[Sura ya 50]

58. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 50]

59. Marekebisho ya kifungu cha 21

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 21(1) kwa kufuta neno “insurance” lililopo katika aya (g).

60. Kufutwa na kuandikwa upya kifungu cha 41

Sheria Kuu inarekebishwa kwa kufuta kifungu cha 41 na kukiandika upya kama ifuatavyo:

41. Condition for medical benefit

Medical benefit shall be paid to a member, the spouse and four children of the member if the member has contributed to the Fund for a minimum of three months, of which three months of contributions were paid to the Fund in thethree months immediately preceding the medical contingency.”

61. Marekebisho ya kifungu cha 42

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 42(1) kwa kufuta maneno “based on health insurance”.

(e) – Sheria ya mtoto

[Sura ya 13]

62. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Mtoto ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 13]

63. Marekebisho ya kifungu cha 8

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 8 kwa kuongeza kifungu kidogo cha (7) kama ifuatavyo:
(7)For the purpose of ensuring attainment of the right of a child to medical care, a parent, guardian or any other person having custody of a child shall enroll the child with a health insurance scheme.”.

(f) – Sheria ya ajira na mahusiano kazini

[Sura ya 366]

64. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 366]

65. Kuongezwa kwa sehemu ndogo E

Sheria Kuu inarekebishwa kwa kuongeza mara baada ya kifungu cha 11 Sehemu Ndogo ya E kama ifuatavyo—

E – Access to health insurance

11A. Access to health insurance

(1)Subject to the provisions of the Universal Health Insurance Act, the employer shall register his employee with a health insurance scheme.
(2)A person who contravenes the provisons of this section commits an offence.”.

(g) – Sheriaya udhibiti wa hospitali bincfsi

[Sura ya 151]

66. Ufafanuzi

Sehemu Ndogo hii itasomwa pamoja na Sheria ya Udhibiti wa Hospitali Binafsi ambayo hapa itarejewa kama “Sheria Kuu”.[Sura ya 151]

67. Marekebisho ya kifungu cha 7

Sheria Kuu inarekebishwa katika kifungu cha 7(2)—(a) kwa kuongeza mara baada ya aya (b), aya ifuatayo—
(c)the Commissioner of Insurance or a person nominated on his behalf from the Tanzania Insurance Regulatory Authority;”;
(b) kwa kubadilisha mpangilio wa aya (c) kuwa aya (d); na(c) katika aya (d) kama ilivyobadilishwa, kwa kufuta neno “five” na badala yake kuweka neno “four”.

Jedwali

Sehemu A (chini ya kifungu cha 14(3))

Huduma zitakazotolewa katika kitita cha huduma muhimu zitakuwa kama ifuatavyo—
(a)uandikishaji na kumuona daktari;
(b)vipimo vya uchunguzi tiba vya maabara, radiolojia na mionzi kwa ngazi husika;
(c)huduma za kulazwa;
(d)matibabu ikiwemo—
(i)huduma za dawa zilizo katika orodha ya dawa muhimu ya Taifa inayotolewa na Wizara;
(ii)huduma za matibabu ya macho, kinywa na meno;
(iii)huduma za kujifungua; na
(iv)huduma za upasuaji;
(e)huduma za kibingwa na ubingwa bobezi; na
(f)huduma nyinginezo kwa kadri zitakavyoainishwa na Waziri katika kanuni chini ya Sheria hii.”

Sehemu B (chini ya kifungu cha 15(3))

Huduma za kitita cha bima ya afya ya jamii zitakuwa kama ifuatavyo—
(a)uandikishaji na kumuona daktari;
(b)vipimo vya uchunguzi tiba vya maabara, radiolojia na mionzi kwa ngazi husika;
(c)huduma za kulazwa; na
(d)matibabu ikiwemo—
(i)huduma za dawa zilizo katika orodha ya dawa muhimu ya Taifa inayotolewa na Wizara;
(ii)huduma za matibabu ya macho, kinywa na meno;
(iii)huduma za kujifungua; na
(iv)huduma za upasuaji;
(e)huduma nyinginezo kwa kadri zitakavyoainishwa na Waziri katika kanuni chini ya Sheria hii.”
▲ To the top

History of this document

01 July 2024 amendment not yet applied
Amended by Finance Act, 2024
01 December 2023 this version
19 November 2023
Assented to