Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024

Act 2 of 2024

Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024

Tanzania

Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024

Tenda 2 ya 2024

Sheria kwa ajili ya kubainisha muundo, majukumu, utaratibu wa upatikanaji wa Wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na sifa za Mkurugenzi wa Uchaguzi, kuweka utaratibu wa uendeshaji wa vikao vya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuweka masuala mengine yanayohusiana na hayo.IMETUNGWA na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya Kwanza – Masharti ya utanguliz

1. Jina na tarehe ya kuanza kutumika

Sheria hii itajulikana kama Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024 na itaanza kutumika katika tarehe ambayo Waziri atateua kwa notisi katika Gazeti la Serikali.

2. Matumizi

Sheria hii itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, isipokuwa kwa masuala yanayohusu uchaguzi wa Madiwani, itatumika Tanzania Bara.

3. Tafsiri

Katika Sheria hii, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—"jimbo" maana yake ni jimbo la uchaguzi kwa madhumuni ya uchaguzi wa Wabunge;"Katiba" maana yake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;"Mjumbe" maana yake ni mtu aliyeteuliwa kuwa mjumbe wa Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba;"Mkurugenzi wa Uchaguzi" maana yake ni mtu aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 17 na itajumuisha mtu ambaye kwa kipindi hicho atakuwa anatekeleza majukumu yoyote ya ofisi hiyo;"Mwenyekiti" maana yake ni mtu aliyeteuliwa kuongoza Tume na inajumuisha Makamu Mwenyekiti;"Rais" maana yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;"Tume" maana yake ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba;"uchaguzi" maana yake ni uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na inajumuisha uchaguzi mdogo wa Mbunge au Diwani;"Waziri" maana yake ni Waziri mwenye dhamana na masuala ya uchaguzi.

Sehemu ya Pili – Kuanzishwa, muundo na majukumu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

4. Kuanzishwa kwa Tume

Kutakuwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano iliyoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba ambayo pia itajulikana kama “Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi”.

5. Muundo wa Tume

(1)Tume itakuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wengine watano watakaoteuliwa na Rais.
(2)Rais atateua wajumbe wa Tume kama ifuatavyo:
(a)Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume kutoka miongoni mwa majina yatakayopendekezwa na Kamati ya Usaili kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 74(1)(a) na (b) na (2) ya Katiba na kanuni zitakazotengenezwa chini ya Sheria hii; na
(b)Wajumbe wengine wa Tume kutoka miongoni mwa majina yatakayowasilishwa na Kamati ya Usaili baada ya kufanyiwa usaili.
(3)Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi watashika madaraka mara baada ya kuapishwa na Rais.
(4)Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume utafanywa kwa misingi kwamba, endapo Mwenyekiti atateuliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atateuliwa kutoka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano.
(5)Mkurugenzi wa Uchaguzi atakuwa Katibu na Mtendaji Mkuu wa Tume.

6. Hadhi ya Tume

(1)Tume itakuwa ni chombo huru na kinachojitegemea na uamuzi wake hautaingiliwa na chombo chochote au kulazimika kufuata maagizo ya mtu yeyote au Idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa.
(2)Tume itakuwa ni chombo chenye uwezo wa kumiliki mali na kuwa na nembo na lakiri yake, na kwa jina lake Tume inaweza—
(a)kujipatia na kumiliki mali zinazoweza kuhamishika na zisizoweza kuhamishika;
(b)kushtaki au kushtakiwa; na
(c)kufanya au kutekeleza masuala yoyote ambayo yanaweza kufanywa au kutekelezwa na chombo huru.
(3)Pale ambapo Tume itakuwa imeshtaki au kushtakiwa, itapaswa kumtaarifu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili awe sehemu ya shauri hilo kwa lengo la kukidhi masharti ya Sheria ya Uendeshaji wa Mashauri dhidi ya Serikali.[Sura ya 5]

7. Sifa za wajumbe wa Tume

(1)Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Tume atapaswa kuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani au kuwa na sifa ya kuwa Wakili na amekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano.
(2)Wajumbe wengine watano watakuwa na sifa zifuatazo:
(a)awe raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Tanzania;[Sura ya 357]
(b)awe mtu mwaminifu na mwadilifu;
(c)awe na uzoefu katika uongozi, utawala au masuala ya uchaguzi; na
(d)awe mtu anayeweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

8. Muda wa utumishi wa wajumbe

(1)Mjumbe wa Tume atashika nafasi ya madaraka kwa kipindi cha miaka mitano.
(2)Mjumbe wa Tume atakoma kuwa Mjumbe endapo litatokea lolote kati ya mambo yafuatayo:
(a)ukimalizika muda wa miaka mitano tangu alipoteuliwa;
(b)ikiwa atafariki;
(c)endapo atajiuzulu;
(d)ikiwa litatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Mjumbe wa Tume, lingemfanya asiweze kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume; au
(e)ikiwa ataondolewa madarakani na Rais.
(3)Rais anaweza kumuondoa madarakani mjumbe wa Tume kutokana na—
(a)mjumbe kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya maradhi au sababu nyingine yoyote;
(b)tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi ya mjumbe wa Tume au inayokiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; au[Sura ya 398]
(c)kupoteza sifa ya kuteuliwa kuwa mjumbe.
(4)Endapo suala la kumuondoa Mjumbe wa Tume litajitokeza, Rais anaweza kuunda Kamati itakayofanya uchunguzi na kumshauri ipasavyo.
(5)Kamati iliyorejewa chini ya kifungu kidogo cha (4) itajumuisha wajumbe wafuatao:
(a)Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye atakuwa Mwenyekiti;
(b)Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
(c)Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(d)Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Zanzibar;
(e)wajumbe wawili wenye uzoefu wa masuala ya uchaguzi, mmoja kutoka Tanzania Bara na mwingine kutoka Tanzania Zanzibar; na
(f)Mjumbe mmoja kadri Rais atakavyoona inafaa kwa kuzingatia jinsia.
(6)Kwa kuzingatia kifungu kidogo cha (5), Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi atateua mtumishi wa umma mwandamizi kuwa Katibu wa Kamati.
(7)Katika kutekeleza majukumu yake, Kamati ya Uchunguzi itajiwekea utaratibu wa kujiendesha.

9. Kamati ya Usaili

(1)Wakati wowote inapobidi kuteuliwa mjumbe au wajumbe wa Tume, Rais ataitisha Kamati ya Usaili.
(2)Kamati itakayoitishwa chini ya kifungu kidogo cha (1) itakuwa na wajumbe wafuatao:
(a)Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa ni Mwenyekiti;
(b)Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti;
(c)Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; na
(d)mjumbe mmoja atakayeteuliwa na Rais kwa kuzingatia jinsia.
(3)Katibu wa Kamati ya Usaili atakuwa afisa mwandamizi katika utumishi wa umma atakayeteuliwa na Rais.
(4)Wajumbe wa Kamati ya Usaili wataapa mbele ya Rais kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao.
(5)Ndani ya siku kumi na nne baada ya kuundwa, Kamati ya Usaili itatoa tangazo kwa umma kupitia magazeti angalau mawili yenye wigo mpana wa usambazwaji nchini na vyombo vingine vya habari kuwaalika wananchi wenye nia ya kuomba kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume kuwasilisha maombi yao kwenye Kamati.
(6)Kamati ya Usaili mara baada ya kupokea na kuchambua maombi ya watu walioomba kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume, itafanya usaili na kupendekeza kwa Rais majina ya watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
(7)Kwa kuzingatia kifungu kidogo cha (6) na kifungu cha 5(2), utaratibu wa kusimamia—
(a)mchakato wa upatikanaji wa majina yatakayopendekezwa kwa ajili ya uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti; na
(b)mchakato wa usaili wa wajumbe wengine wa Tume,
utakuwa kama utakavyoainishwa katika kanuni.
(8)Kamati ya Usaili itawasilisha kwa Rais majina manne zaidi ya idadi ya nafasi zinazohitajika kujazwa.
(9)Muda wa Kamati ya Usaili utakoma mara baada ya Rais kuteua wajumbe wa Tume.

10. Majukumu ya Tume

(1)Kwa kuzingatia matakwa ya Ibara za 74(6), 75 na 78 za Katiba, Tume itakuwa na majukumu yafuatayo:
(a)kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara;
(b)kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge na uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara;
(c)kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge;
(d)kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge;
(e)kuteua na kuwatangaza Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu kwa Tanzania Bara;
(f)kuandaa na kusimamia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi;
(g)kutoa elimu ya mpiga kura nchini;
(h)kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura;
(i)kualika na kusajili waangalizi wa uchaguzi;
(j)kuajiri au kuteua watumishi na watendaji wa Tume kwa kadri itakavyohitajika kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Utumishi wa Umma na masharti mengine yatakayowekwa na Tume; na[Sura ya 298]
(k)kutekeleza majukumu mengine yoyote kama yalivyoainishwa kwenye Katiba au sheria nyingine yoyote.
(2)Tume inaweza kukasimu majukumu au sehemu ya majukumu yake kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, mtumishi au mtendaji mwingine wa Tume.

11. Maadili katika utendaji kwa wajumbe

Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu ya Tume, kila Mjumbe wa Tume atalazimika kuzingatia Sheria ya Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma na Kanuni za Maadili zitakazoandaliwa chini ya Sheria hii.[Sura ya 398]

12. Vikao vya Tume

(1)Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 74(7) ya Katiba, Tume itafanya uamuzi wake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao.
(2)Tume itakuwa na vikao vya kawaida visivyopungua vinne kwa mwaka.
(3)Bila kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (2), Tume inaweza kufanya vikao maalumu muda wowote itakapoonekana kuwa ni lazima kufanya hivyo.
(4)Tume itafanya vikao vyake katika sehemu na muda utakaopangwa na Tume.
(5)Mwenyekiti atahakikisha kuwa kila mjumbe wa Tume anapewa taarifa ya kikao mapema kabla ya kikao hicho kufanyika.
(6)Kwa kuzingatia masharti ya Sheria hii, Mwenyekiti ataongoza vikao vyote vya Tume na endapo Mwenyekiti hatakuwepo, Makamu Mwenyekiti ataongoza, au ikiwa wote wawili hawapo, wajumbe waliopo wanaweza kumchagua mjumbe mmoja miongoni mwao atakayekuwa mwenyekiti wa muda wa kikao husika.

13. Akidi katika vikao vya Tume

Akidi ya kikao chochote cha Tume itakuwa si chini ya wajumbe wanne.

14. Uamuzi wa Tume

(1)Uamuzi wa kikao chochote cha Tume utafikiwa kwa kuungwa mkono na Wajumbe walio wengi.
(2)Pale ambapo katika kikao chochote cha Tume italazimu uamuzi kufikiwa kwa kupigiwa kura, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au mwenyekiti wa muda atakayekuwa anaongoza kikao atakuwa na kura ya turufu zaidi ya kura yake ya kawaida inapotokea kulingana kwa kura zilizopigwa.

15. Posho na stahili za wajumbe wa Tume

(1)Wajumbe wa Tume watalipwa posho na stahili nyingine kwa mujibu wa Sheria, kanuni, taratibu na miongozo itakayotolewa na mamlaka husika.
(2)Wajumbe wa Tume watalipwa kiinua mgongo baada ya kumaliza muda wa ujumbe wa Tume.

16. Uhusiano kati ya Tume na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar

Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 74(13) ya Katiba, katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume itashauriana mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi ya Tanzania Zanzibar.

Sehemu ya Tatu – Sekretarieti ya Tume huru ya taifa ya uchaguzi

17. Mkurugenzi wa Uchaguzi

(1)Kutakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi atakayeteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.
(2)Mkurugenzi wa Uchaguzi atakuwa na sifa zifuatazo:
(a)awe ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Tanzania;[Sura ya 357]
(b)awe ni mtu mwaminifu na mwadilifu;
(c)awe na shahada ya chuo cha elimu ya juu kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria; na
(d)awe afisa mwandamizi katika utumishi wa umma.

18. Maadili ya utendaji kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi

Mkurugenzi wa Uchaguzi ataapa mbele ya Rais kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake na atalazimika kuzingatia Sheria ya Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma na Kanuni za Maadili zitakazoandaliwa chini ya Sheria hii.[Sura ya 398]

19. Majukumu ya Mkurugenzi wa Uchaguzi

(1)Mkurugenzi wa Uchaguzi atakuwa Mtendaji Mkuu na msimamizi mkuu wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Tume.
(2)Mkurugenzi wa Uchaguzi atakuwa Afisa Masuuli wa Tume na atatekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu za fedha.
(3)Bila kuathiri kifungu kidogo cha (1), Mkurugenzi wa Uchaguzi atatekeleza majukumu yafuatayo:
(a)kuandaa na kuratibu vikao vya Tume;
(b)kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura;
(c)kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi;
(d)kutoa ushauri wa kitaalamu ~kwa Tume katika kutekeleza majukumu yake;
(e)kuandaa bajeti na kalenda ya shughuli za Tume;
(f)kuweka kumbukumbu za vikao vya Tume;
(g)kutayarisha nyaraka mbalimbali za Tume;
(h)kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zinafanya kazi zinazohusu uchaguzi, demokrasia na utawala bora;
(i)kusimamia miongozo kwa watendaji wa uchaguzi katika kutekeleza majukumu yao kama itakavyoagizwa na Tume;
(j)kusimamia rasilimali watu na mali za Tume;
(k)kufanya tafiti zinazohusiana na uchaguzi; na
(l)kutekeleza majukumu mengine yoyote kama atakavyoagizwa na Tume kwa mujibu wa Sheria hii.
(4)Mkurugenzi wa Uchaguzi atatekeleza majukumu yake kwa kusaidiwa na watendaji ambao ni watumishi wa umma au watu wengine wenye sifa kwa kadri itakavyohitajika.

20. Watumishi na watendaji wa Tume

(1)Kwa madhumuni ya Sheria hii, mtumishi aliyeajiriwa, aliyeteuliwa au aliyeazimwa na Tume, kwa kipindi chote atakachokuwa anatekeleza majukumu ya Tume, atachukuliwa kuwa ni mtumishi wa Tume na atatakiwa kuzingatia Katiba, Sheria hii, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na sheria nyingine yoyote inayohusu utekelezaji wa majukumu ya Tume.[Sheria Na.1 ya 2024]
(2)Mtu yeyote aliyeajiriwa kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu ya Tume, ikiwa hajaajiriwa katika utumishi wa umma, atapokea malipo yanayostahili kwa kazi hiyo kadri Tume itakavyoona inafaa kuidhinisha.

Sehemu ya Nne – Masharti ya fedha

21. Fedha za uendeshaji wa Tume

Fedha za "uendeshaji wa shughuli za Tume zitatoka katika bajeti ya Serikali.

22. Gharama kulipwa kutoka mfuko mkuu wa hazina ya serikali

Gharama zote—
(a)zilizotumika katika kuandaa daftari, kutoa kadi ya mpiga kura na kufanya mambo mengine au vitu vingine vinavyohitajika kufanywa kwa madhumuni ya kutekeleza masharti ya Sheria hii;
(b)zilizotumiwa na Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na mtu mwingine yeyote aliyeajiriwa kutekeleza majukumu ya uchaguzi;
(c)zilizotumika kwa ajili ya malipo ya maafisa walioainishwa katika kifungu cha 20(2); na
(d)zilizotumika kwa ajili ya malipo kwa afisa yeyote wa umma kuhusu shughuli rasmi zinazohusu au zinazotokana na uchaguzi,
zitatozwa na kulipwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.

23. Hesabu na ukaguzi

(1)Mkurugenzi wa Uchaguzi atatunza vitabu vya hesabu na kumbukumbu nyingine zinazohusu shughuli za Tume na kuandaa taarifa ya hesabu ya mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma.[Sura ya 348]
(2)Hesabu za Tume zitakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

24. Taarifa ya mwaka

(1)Ndani ya miezi mitatu baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha, Tume itaandaa taarifa ya mwaka kuhusiana na mwaka wa fedha uliopita na kuwasilisha taarifa hiyo kwa Waziri ambaye ataiwasilisha Bungeni.
(2)Taarifa ya mwaka itajumuisha—
(a)maelezo ya kina kuhusu utendaji wa Tume kwa mwaka husika;
(b)nakala ya hesabu za Tume zilizokaguliwa pamoja na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; na
(c)taarifa nyingine yoyote ambayo Tume itahitajika kutoa chini ya Sheria hii.

Sehemu ya Tano – Masharti mengineyo

25. Muundo wa utumishi wa Sekretarieti ya Tume

Tume kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi, itaandaa Muundo wa Utumishi wa Sekretarieti ya Tume.

26. Kanuni na miongozo

Tume inaweza kutengeneza kanuni na miongozo na kutoa maelekezo kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu yake.

27. Masharti ya mpito

Mara baada ya kuanza kutumika kwa Sheria hii, mtu yeyote ambaye ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Mjumbe wa Tume ataendelea kushika madaraka hayo hadi pale ujumbe wake utakapokoma.
▲ To the top

History of this document

Subsidiary legislation

Title
Legislation
Government Notice 390 of 2024