Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka, 2025

Act 3 of 2025

Uncommenced
This Act has not yet come into force.
Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka, 2025

Tanzania

Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka, 2025

Tenda 3 ya 2025

Sheria kwa ajili ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha Shirika la Utangazaji Tanzania; kubainisha wajibu, malengo, majukumu na mamlaka ya Shirika, kuweka masharti kuhusu ulinzi na usimamizi thabiti wa miundombinu ya utangazaji na kuainisha masuala mengine yanayohusiana na hayo.IMETUNGWA na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya Kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina na kuanza kutumika

Sheria hii itajulikana kama Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka 2025 na itaanza kutumika tarehe ambayo Waziri atateua kwa notisi itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali.

2. Tafsiri

Katika Sheria hii, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo:—Bodi” maana yake ni Bodi ya Wakurugenzi iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 6;chaneli maalumu” inajumuisha chaneli, idhaa, kituo au jukwaa lililoanzishwa na Serikali kwa madhumuni mahsusi, linalosimamiwa na kuendeshwa na Shirika;huduma ya utangazaji ya kulipia” maana yake ni huduma ya utangazaji ambayo inaweza kupatikana kwa mtu kwa malipo ya ada;huduma ya utangazaji wa umma” maana yake ni aina ya huduma ya utangazaji ambayo inatolewa kwa umma, inayofadhiliwa na umma na haina faida ya kibiashara;kipindi maalumu” maana yake ni kipindi chenye maslahi ya umma ambacho kinaweza kutangazwa wakati wowote katika kutimiza wajibu wa Shirika kwa umma na bila kujali kuwa kuna vipindi vingine katika ratiba;matukio ya kitaifa” maana yake ni ziara za Viongozi Wakuu wa Serikali, sherehe za kitaifa, maadhimisho, matukio au kumbukumbu mbalimbali za kitaifa;miundombinu ya utangazaji” maana yake ni miundombinu ya usambazaji wa maudhui ya utangazaji na inajumuisha mifumo ya utangazaji, studio, vifaa vya kurushia matangazo, mitambo, ardhi na majengo yanayotumika kuhifadhi miundombinu hiyo;mjumbe” maana yake ni mjumbe wa Bodi na inajumuisha Mwenyekiti;Mkurugenzi Mkuu” maana yake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika aliyeteuliwa chini ya kifungu cha 12;mtumishi” maana yake ni mtumishi yeyote wa Shirika na inajumuisha Mkurugenzi Mkuu;Shirika” maana yake ni Shirika la Utangazaji Tanzania ambalo limetambuliwa chini ya kifungu cha 3;tangazo la biashara” maana yake ni tangazo lolote kwa umma lenye madhumuni ya kukuza uuzaji, ununuzi au ukodishaji wa bidhaa au huduma, lililotengewa muda wa kutangazwa kwa malipo ya fedha au malipo mengine lenye madhumuni ya kuhamasisha kusudi au wazo au kuleta manufaa mengine anayotamani mtoa tangazo;udhamini” maana yake ni ushiriki wa mtu ambaye hajishughulishi katika shughuli za utangazaji au utayarishaji wa kazi za maudhui katika ufadhili wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja wa vipindi kwa nia ya kukuza jina, alama ya biashara au taswira ya mtu huyo;Viongozi Wakuu wa Serikali” maana yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Waziri Mkuu; naWaziri” maana yake ni Waziri mwenye dhamana ya huduma za utangazaji.

Sehemu ya Pili – Shirika la utangazaji Tanzania

3. Kuendelea kutambulika kwa Shirika

(1)Kutakuwepo na Shirika linalojulikana kama Shirika la Utangazaji Tanzania au “TBC” lililoanzishwa kwa mujibu wa Amri ya Uanzishwaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka 2007.
(2)Shirika litakuwa ni shirika hodhi lenye urithishaji endelevu na lakiri yake na kwa jina lake litakuwa na uwezo wa—
(a)kushtaki au kushtakiwa;
(b)kupata, kumiliki na kutoa mali zinazohamishika na zisizohamishika;
(c)kukopa kiasi cha fedha ambacho kinaweza kuhitajika kwa madhumuni yake;
(d)kuingia kwenye mikataba au taratibu nyingine; na
(e)kutumia mamlaka na kutekeleza majukumu chini ya Sheria hii.
(3)Shirika litakuwa chombo kikuu cha utangazaji cha umma kwa ajili ya kutoa habari, taarifa, elimu na burudani na kwa kuzingatia Sheria hii, litakuwa huru katika uendeshaji wa shughuli zake za kila siku.
[TS. Na. 186 la 2007]

4. Majukumu na mamlaka ya Shirika

Majukumu na mamlaka ya Shirika yatakuwa—
(a)kutoa huduma za utangazaji wa umma zinazohabarisha, zinazoelimisha na zinazoburudisha kupitia redio, televisheni na majukwaa mengine ya mtandaoni au kielektroniki kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya usawa;
(b)kukuza ujuzi wa watumishi wa Shirika ili kuongeza ufanisi katika utendaji kupitia mafunzo, elimu na utafiti;
(c)kumiliki na kufunga vifaa kwa ajili ya kusafirishia mawimbi kwa kutumia waya au njia nyinginezo zinazotumika katika Jamhuri ya Muungano na kuvitumia kwa madhumuni yanayohusiana na malengo ya Shirika;
(d)kuendeleza, kuongeza na kuboresha huduma za utangazaji ndani na nje ya nchi kwa njia, mbinu na namna inayokubalika na mamlaka inayohusika na utoaji leseni;
(e)kutoa huduma za utangazaji, kuandaa, kujenga na kufunga au kusimamia uwekaji wa miundombinu ya utangazaji na vifaa vingine vya kurusha na kupokea maudhui nje ya Jamhuri ya Muungano;
(f)kushiriki katika matukio yote ya kitaifa yakiwemo yanayohusisha Viongozi Wakuu wa Serikali yenye maslahi ya umma ndani na nje ya nchi kwa madhumuni ya kukusanya, kuchakata, kutangaza na kuhifadhi kumbukumbu;
(g)kukusanya, kupokea au kutoa maudhui kwa vyombo vingine vya ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano na kujiunga katika mashirika ya habari;
(h)kukusanya, kuchakata, kuchapisha na kusambaza, kwa malipo au bila malipo, vipindi au taarifa zozote ambazo zinaweza kufaa kwa malengo ya Shirika;
(i)kuanzisha maktaba na kutunza kumbukumbu zenye maudhui yanayohusiana na malengo ya Shirika;
(j)kuandaa au kudhamini matamasha na burudani nyingine zinazohusiana na huduma za utangazaji au kwa madhumuni yoyote yanayohusiana na huduma za utangazaji;
(k)kuzalisha, kutengeneza, kununua, kupata, kutumia, kuuza, kukodisha au kutoa filamu, rekodi na vifaa vingine vyovyote vinavyoweza kutoa picha jongefu au sauti;
(l)kuomba na kupata, kununua au kutumia kibiashara kwa namna yoyote miliki ubunifu kuhusiana na uvumbuzi wowote wenye manufaa kwa madhumuni na majukumu ya Shirika;
(m)kuanzisha chaneli, vituo na majukwaa mengine ya utangazaji kama Bodi itakavyoidhinisha;
(n)kufanya tafiti zinazoendana na malengo ya Shirika;
(o)kutumia teknolojia mpya na zinazoibukia zinazoendana na malengo ya Shirika;
(p)kuanzisha au kuwezesha uanzishwaji wa kampuni kwa ajili ya uendelezaji wa malengo ya Shirika; na
(q)kutekeleza majukumu mengine kwa ajili ya kufikia malengo yake.

5. Wajibu wa Shirika katika kuandaa vipindi

Katika kutekeleza majukumu yake, Shirika litaandaa vipindi—
(a)vinavyochangia kukuza demokrasia, uzalendo, maendeleo ya jamii, usawa wa kijinsia, ujenzi wa taifa, utoaji wa elimu na kuimarisha maadili ya jamii;
(b)vinavyolinda, kuimarisha na kudumisha uhuru, umoja na taswira ya Jamhuri ya Muungano;
(c)vinavyolinda na kuimarisha mfumo wa kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi;
(d)vinavyoakisi mitazamo, maoni, mawazo, maadili na ubunifu wa sanaa za Kitanzania;
(e)vinavyokuza vipaji vya Watanzania kupitia vipindi vya elimu na burudani;
(f)vinavyoweka anuai inayojitosheleza na inayotoa mizania ya habari, elimu na burudani ili kukidhi mahitaji ya utangazaji ya Watanzania wote;
(g)vinavyotoa maoni, taarifa, habari na uchambuzi wa masuala mbalimbali kwa mtazamo wa Kiafrika; na
(h)vinavyoendeleza na kulinda maslahi ya taifa na usalama ndani na nje ya nchi.

Sehemu ya Tatu – Utawala na usimamizi wa shirika

6. Bodi ya Shirika

(1)Kutakuwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika kwa ajili ya kusimamia utendaji wa Shirika.
(2)Bodi ya Shirika itakuwa na wajumbe wafuatao:
(a)Mwenyekiti ambaye atateuliwa na Rais; na
(b)wajumbe wengine nane watakaoteuliwa na Waziri wenye uzoefu wa zaidi ya miaka kumi katika tasnia ya habari, utangazaji, uhandisi, sheria, teknolojia ya habari, usimamizi, uchumi au fedha.
(3)Katika kuteua wajumbe chini ya kifungu kidogo cha (2)(b), Waziri atazingatia jinsia.
(4)Mkurugenzi Mkuu atakuwa Katibu wa Bodi.
(5)Masuala kuhusu muda wa kukaa madarakani, akidi, vikao vya Bodi na masuala mengine yatakuwa kama ilivyoainishwa katika Jedwali.
(6)Waziri anaweza, kwa amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, kurekebisha Jedwali.

7. Sifa za kuwa mjumbe

Mtu atakuwa na sifa za kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi iwapo mtu huyo—
(a)ni raia wa Tanzania;
(b)ni mkazi wa kudumu wa Tanzania;
(c)si mtumishi au mwajiriwa wa chama chochote cha siasa;
(d)hajatamkwa na mahakama kuwa amefilisika;
(e)ana akili timamu; na
(f)hajatiwa hatiani kwa kosa lolote na kuhukumiwa kifungo kisichopungua miezi sita, bila mbadala wa faini.

8. Majukumu na mamlaka ya Bodi

(1)Bila kuathiri masharti ya Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, majukumu na mamlaka ya Bodi yatakuwa—
(a)kutoa mwongozo wa kimkakati na kutengeneza sera za uendeshaji na usimamizi wa Shirika;
(b)kufanya usimamizi wa kiutawala na tathmini ya shughuli za Shirika na utendaji wa menejimenti ya Shirika;
(c)kupata na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali, ikijumuisha kuidhinisha mpango kazi wa mwaka, bajeti ya mwaka na bajeti ya nyongeza;
(d)kuidhinisha mipango na miongozo mbalimbali ya Shirika;
(e)kutathmini utendaji wa menejimenti na kuchukua hatua muhimu;
(f)kuidhinisha taarifa za utendaji wa Shirika;
(g)kuteua menejimenti katika Shirika na kusimamia nidhamu yao;
(h)kupitisha mabadiliko yoyote ya mishahara na masharti ya utumishi kwa watumishi;
(i)kuidhinisha na kusimamia kanuni za fedha na kanuni za utumishi;
(j)kuidhinisha uondoshaji wa mali za Shirika;
(k)kuidhinisha pendekezo la kukopa fedha kwa madhumuni ya Shirika;
(l)kuidhinisha uendelezaji wa miundombinu ya utangazaji na vifaa;
(m)kupitisha mpango mkakati, muundo wa Shirika na muundo wa kiutumishi;
(n)kuidhinisha sera na kanuni za ndani za utawala na uendeshaji;
(o)kuidhinisha miradi kwa kuzingatia sheria nyingine kwa madhumuni ya Shirika isiyojumuishwa ndani ya mpango au mpango kazi wa mwaka na bajeti;
(p)kuidhinisha uteuzi wa watumishi wa Shirika kwa idadi na vyeo kama itakavyoona inafaa kwa ajili ya uendeshaji bora na wa ufanisi wa shughuli za Shirika;
(q)kuishauri Serikali katika masuala yote yanayohusu Shirika; na
(r)kutekeleza majukumu mengine kadiri Bodi itakavyoona inafaa kwa ajili ya kufikia malengo ya Shirika.
(2)Waziri anaweza kutoa kwa Bodi maelekezo ya jumla au mahsusi kuhusu utendaji wa Shirika na majukumu yake chini ya Sheria hii.
[Sura ya 257 na 370]

9. Mamlaka ya ukasimishaji

(1)Isipokuwa kama ilivyoelezwa katika kifungu kidogo cha (3), Bodi inaweza kwa maandishi, na kwa kuzingatia masharti kadiri itakavyoona inafaa, kukasimu kwa kamati au mtumishi majukumu au mamlaka yoyote chini ya Sheria hii au sheria nyingine yoyote.
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), Bodi inaweza kutekeleza majukumu iliyokasimisha.
(3)Bodi haitakasimu mamlaka ya—
(a)kukasimisha;
(b)kuteua wajumbe wa menejimenti;
(c)kuidhinisha ajira za watumishi wa Shirika;
(d)kuidhinisha taarifa za fedha za mwaka, bajeti ya mwaka au bajeti ya nyongeza;
(e)kuidhinisha taarifa za fedha za kila mwaka;
(f)kuanisha ada na tozo mbalimbali; na
(g)kukopa.

10. Ada au posho za wajumbe wa Bodi

Mjumbe atalipwa na Shirika ada au posho kama itakavyoamuliwa na Bodi na kuidhinishwa na mamlaka husika.

11. Kinga kwa wajumbe wa Bodi

Mjumbe wa Bodi hatachukuliwa hatua au kufunguliwa shauri kuhusiana na kitendo au jambo lolote alilotenda au kuacha kutenda kwa nia njema katika kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii.

12. Mkurugenzi Mkuu

(1)Kutakuwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ambaye atateuliwa na Rais.
(2)Mkurugenzi Mkuu atakuwa afisa mtendaji mkuu na afisa masuuli wa Shirika na atawajibika kwa Bodi katika usimamizi wa majukumu na shughuli za kila siku za Shirika.
(3)Mtu atakuwa na sifa za kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu ikiwa-
(a)ana angalau shahada ya uzamili kutoka chuo kikuu kinachotambulika katika fani ya mawasiliano kwa umma, uandishi wa habari, uzalishaji wa maudhui, sheria, uhandisi wa mawasiliano, uchumi, utawala au fani nyingine inayoendana na hizo;
(b)ana uzoefu wa angalau miaka kumi, miaka sita kati ya hiyo iwe katika nafasi ya uongozi; na
(c)amethibitika kuwa na ujuzi wa uchambuzi na maarifa katika sekta ya utangazaji.
(4)Mkurugenzi Mkuu atashika wadhifa kwa kipindi cha miaka mitano na anaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine kimoja.

13. Majukumu ya Mkurungenzi Mkuu

Pamoja na majukumu mengine aliyopewa kwa mujibu wa Sheria hii, Mkurugenzi Mkuu atakuwa na majukumu ya—
(a)kuanzisha na kudumisha mfumo wa mpango mkakati ambao unajumuisha dira na dhima ya Shirika pamoja na mpango wa utekelezaji;
(b)kusimamia uandaaji, udumishaji na utekelezaji wa sera na mifumo ya utendaji inayojumuisha nyanja zote za uendeshaji wa Shirika;
(c)kusimamia rasilimali za Shirika ili kukidhi mipango ya uendeshaji wa shughuli za Shirika;
(d)kuhakikisha uwepo wa watumishi wenye uwezo na ari katika utekelezaji wa majukumu yao;
(e)kufuatilia, kutathmini na kuchukua hatua za kurekebisha mipango kazi iliyokubaliwa katika miradi yote ya Shirika;
(f)kuidhinisha matumizi ya kawaida kama itakavyoamuliwa na Bodi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo; na
(g)kutekeleza majukumu mengine kama Bodi itakavyoelekeza.

14. Watumishi wa Shirika

(1)Kwa kuzingatia sheria zinazosimamia utumishi wa umma, Shirika litaajiri watumishi kwa idadi itakayohitajika kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu ya Shirika.
(2)Shirika linaweza kuteua washauri na wataalamu katika taaluma mbalimbali kwa kuzingatia vigezo na masharti yatakayowekwa na Shirika.

Sehemu ya Nne – Miundombinu ya Shirika

15. Miundombinu ya utangajazi

(1)Shirika litasimamia miundombinu ya utangazaji iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za utangazaji na litakuwa na mamlaka ya—
(a)kupanga matumizi ya miundombinu hiyo;
(b)kuzuia mtu yeyote kuingia au kuendeleza miundombinu ya utangazaji; na
(c)kuidhinisha uwekaji wa miundombinu kwenye ardhi ya Shirika.
(2)Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (1), Shirika linaweza kutoa maelekezo na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kuhakikisha usimamizi bora wa miundombinu ya utangazaji.
(3)Maelekezo ya Shirika katika kifungu hiki yanaweza kujumuisha matengenezo ya vifaa, malipo ya ada au tozo, uendeshaji wa shughuli za biashara na masuala mengine ya usimamizi wa miundombinu ya utangazaji.

16. Ulinzi na usimamizi wa miundombinu ya utangajazi

Shirika litasimamia miundombinu katika namna inayohakikisha manufaa ya kiusalama, kiuchumi na kibiashara katika miundombinu ya utangazaji.

Sehemu ya Tano – Makatazo

17. Uharibifu wa mali za Shirika

(1)Mtu hataingilia au kutumia kwa madhumuni yoyote au kushiriki katika kitendo kinachosababisha au kinachoweza kusababisha mabadiliko, uharibifu au kusababisha kuondolewa kwa au uharibifu wowote wa miundombinu ya utangazaji inayomilikiwa na Shirika.
(2)Mtu anayekiuka masharti ya kifungu kidogo cha (1) anatenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyozidi mara kumi ya thamani ya pato la uharibifu wowote wa miundombinu ya utangazaji, mfumo wa utangazaji au mtambo au kifaa au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote.

18. Kuingia kwenye eneo la Shirika

Mtu ambaye—
(a)bila ruhusa au kibali anakutwa katika eneo lolote lililozuiliwa na linalomilikiwa na Shirika;
(b)anakataa kuondoka katika eneo la Shirika baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Shirika;
(c)akiwa kwenye maeneo ya Shirika, anapohitajika na mtumishi kutaja jina na taarifa zake, anakataa au anatoa jina au taarifa za uongo; au
(d)anamzuia mtumishi au wakala wa Shirika kutekeleza majukumu yake,
anatenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu au vyote.

19. Matumizi ya maudhui

(1)Mtu hatatumia maudhui ya matangazo ya Shirika kwa njia yoyote au kupitia katika chanzo chochote bila idhini ya Shirika.
(2)Mtu anayekiuka masharti ya kifungu hiki anatenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi na isiyozidi shilingi milioni ishirini au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote.

Sehemu ya Sita – Masharti ya fedha

20. Vyanzo vya fedha vya Shirika

(1)Vyanzo vya fedha vya Shirika vitakuwa ni—
(a)kiasi cha fedha ambacho kitatengwa na Bunge;
(b)ada na tozo zitakazotozwa kwa bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika;
(c)ada na tozo kwenye bidhaa au huduma ambazo Serikali itaelekeza kwa ajili ya utangazaji wa umma;
(d)mapato yatakayotokana na uwekezaji;
(e)fedha zitakazopatikana kupitia mikopo, michango, zawadi au ruzuku kwa ajili ya Shirika;
(f)fedha kutoka kwenye mfuko kama ambavyo Serikali inaweza kuanzisha kwa madhumuni ya majukumu ya Shirika;
(g)fedha kutoka katika—
(i)shughuli za kibiashara kama vile ushauri elekezi au kukodisha mali yoyote ya Shirika;
(ii)ukodishaji wa vifaa vingine ambavyo picha jongefu au sauti inaweza kutengenezwa; na
(h)mapato mengine yanayotokana na utendaji wa shughuli za Shirika chini ya Sheria hii.
(2)Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (1)(b), huduma zinazotolewa na Shirika zitajumuisha—
(a)huduma za chaneli maalumu chini ya Sheria hii;
(b)huduma za utangazaji za kulipia; na
(c)matangazo ya biashara na udhamini wa vipindi.

21. Usimamizi wa fedha

Fedha za Shirika zitasimamiwa na Bodi kwa mujibu wa sheria na kanuni za fedha na zitatumika kulipia gharama zinazohusiana na utendaji wa majukumu ya Shirika chini ya Sheria hii.

22. Makadirio ya mapato na matumizi

(1)Kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Mkurugenzi Mkuu ataandaa makadirio ya bajeti inayojumuisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka unaofuata na kuwasilisha kwa Bodi kwa ajili ya idhini na anaweza, wakati wowote kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha kuandaa na kuwasilisha kwa Bodi kwa ajili ya idhini makadirio yoyote ya nyongeza.
(2)Bodi inaweza kulitaka Shirika kufanya marekebisho ya bajeti ikiwa kwa maoni yake bajeti haiakisi makadirio sahihi na ya kuridhisha ya mapato na matumizi.
[Sura ya 439]

23. Matumizi ya fedha

(1)Matumizi yote ya fedha katika Shirika yataidhinishwa na Bodi katika mwaka wa fedha husika.
(2)Mkurugenzi Mkuu atahakikisha kwamba malipo yote kutoka kwenye fedha za Shirika yanafanywa kwa usahihi na kuidhinishwa ipasavyo.
(3)Bila kuathiri kifungu kidogo cha (2), Mkurugenzi Mkuu anaweza, pale inapotokea dharura katika utendaji wa majukumu ya Shirika, kufanya matumizi ambayo hayajaidhinishwa na Bodi na Mkurugenzi Mkuu atalazimika kuomba idhini ya Bodi ndani ya miezi mitatu baada ya matumizi hayo.

24. Hesabu na ukaguzi

(1)Shirika litatunza na kuhifadhi vitabu vya hesabu na kumbukumbu nyingine zinazohusiana na shughuli zake na kuandaa taarifa ya hesabu ya mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma.[Sura ya 348]
(2)Hesabu za Shirika zitakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali au mtu mwingine yeyote aliyeidhinishwa kwa ajili hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

25. Taarifa ya mwaka

(1)Ndani ya miezi miwili baada ya kupokea hesabu za Shirika zilizokaguliwa, Mkurugenzi Mkuu atawasilisha kwa Waziri taarifa ya mwaka husika ikijumuisha—
(a)nakala ya hesabu zilizokaguliwa za Shirika, pamoja na taarifa ya mkaguzi wa hesabu hizo;
(b)taarifa ya utekelezaji wa malengo muhimu na taarifa nyingine yoyote inayohusiana na utekelezaji wa malengo hayo;
(c)taarifa ya uendeshaji wa Shirika katika mwaka wa fedha husika; na
(d)taarifa nyingine kadiri Waziri anavyoweza kuhitaji.
(2)Waziri atawasilisha Bungeni nakala ya taarifa ya mwaka ya Shirika ndani ya miezi miwili au katika mkutano wa Bunge unaofuata.

Sehemu ya Saba – Masharti ya jumla

26. Udhamini wa vipindi

Kipindi chochote au kipindi maalumu kinachotangazwa na Shirika au kwa niaba ya Shirika kinaweza kudhaminiwa na kujumuisha matangazo ya biashara.

27. Matengenezo au mabadiliko yanayoweza kuharibu mfumo wa matangazo

(1)Endapo taasisi ya Serikali, mamlaka ya serikali za mitaa au mtu yeyote atafanya matengenezo au mabadiliko yoyote katika miundombinu yake yatakayohusisha kuondolewa au kuharibiwa kwa mfumo wa matangazo, kifaa au mtambo wa Shirika, atapaswa kufanya matengenezo ili kurejesha huduma za Shirika katika hali ya awali.
(2)Taasisi ya Serikali, mamlaka ya serikali za mitaa au mtu yeyote anayekusudia kufanya matengenezo au mabadiliko yoyote katika miundombinu yake yatakayohusisha kuondolewa au kuharibiwa kwa mfumo wa matangazo, kifaa au mtambo wa Shirika, atapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa Shirika kabla ya kufanya matengenezo au maboresho hayo.

28. Uanzishwaji wa chaneli maalumu

(1)Waziri anaweza, kwa amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, kuanzisha chaneli maalumu kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya umma.
(2)Vigezo vya uanzishaji na uendeshaji wa chaneli maalumu vitaainishwa kwenye kanuni.

29. Adhabu ya jumla

Mtu anayetenda kosa chini ya Sheria hii na hakuna adhabu mahsusi iliyoainishwa, akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tano na isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote.

30. Mamlaka ya Waziri kutengeneza kanuni

(1)Waziri anaweza kutengeneza kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya Sheria hii.
(2)Bila kuathiri ujumla wa kifungu kidogo cha (1), kanuni zitakazotengenezwa chini ya kifungu hiki zinaweza kuainisha—
(a)vigezo vya uanzishaji na uendeshaji wa chaneli maalumu;
(b)ada na tozo za bidhaa na huduma zinazotolewa na Shirika;
(c)utaratibu wa uendeshaji wa kipindi au kipindi maalumu; na
(d)utaratibu wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za maudhui ya matukio yenye maslahi ya kitaifa.

31. Masharti ya mwendelezo

Mambo yote yaliyofanyika kwa mujibu wa Amri ya Uanzishwaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania ya Mwaka 2007, yataendelea kuwa halali na yatatafsiriwa kuwa yalifanyika chini ya Sheria hii.[TS. Na. 186 la 2007]

Jedwali (Limetengenecwa chiniya kifungu cha 6(5))

Masuala kuhusu Bodi

1.Muda wa kuwa madarakaniMjumbe wa Bodi, isipokuwa kama uteuzi wake utatenguliwa au atakoma kuwa mjumbe kwa namna nyingine yoyote, atakuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu na anaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine kimoja.
2.Makamu MwenyekitiWajumbe watachagua kutoka miongoni mwao Makamu Mwenyekiti.
3.Kujaza nafasi iliyo waziEndapo mjumbe yeyote atakoma kuwa mjumbe kabla ya kumaliza kipindi cha ujumbe, mamlaka ya uteuzi inaweza kumteua mtu mwingine kushika nafasi hiyo mpaka muda wa kuhudumu kipindi hicho utakapokwisha.
4.Vikao vya Bodi
(1)Bodi itakutana kwa kawaida kila robo ya mwaka kwa ajili ya kuendesha shughuli zake wakati na mahali kama itakavyoamuliwa.
(2)Bila kujali aya ndogo ya (1), Bodi inaweza wakati wowote kuitisha kikao maalumu endapo kuna suala la dharura linalohitaji uamuzi wa Bodi.
(3)Mwenyekiti ataongoza kila kikao cha Bodi au ikiwa hayupo Makamu Mwenyekiti.
(4)Endapo katika kikao chochote cha Bodi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hawapo, wajumbe waliohudhuria watamchagua mjumbe mmoja kutoka miongoni mwao kuongoza kikao hicho.
(5)Bodi inaweza kumwalika mtu yeyote ambaye si mjumbe kuhudhuria na kushiriki katika majadiliano katika kikao chochote cha Bodi isipokuwa mtu huyo hatakuwa na haki ya kupiga kura.
5.Kamati za Bodi
(1)Bodi inaweza kuunda na kuteua kamati kadiri itakavyoona inafaa kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu yake.
(2)Kamati itakayoundwa chini ya aya ndogo ya (1)—
(a)itajumuisha wajumbe Bodi au watu wengine watakaoteuliwa na Bodi kadiri Bodi itakavyoona inafaa; na
(b)itakutana kwa nyakati na mahali kama itakavyoamuliwa na Bodi.
(3)Mjumbe wa kamati ambaye si mjumbe wa Bodi au mtumishi wa Shirika atalipwa na Shirika ada au posho kwa kiwango kitakachoidhinishwa na Bodi.
7.LakiriLakiri ya Shirika itawekwa ipasavyo katika nyaraka ikiwa imeshuhudiwa kwa saini ya Mkurugenzi Mkuu au mjumbe mwingine yeyote wa Bodi atakayeteuliwa kwa madhumuni hayo, na uwekwaji huo wa lakiri iliyosainiwa na kuthibitishwa utatambulika kisheria.[Tafadhali kumbuka: Nambari kama ilivyo kwenye asili.]
8.Amri na maelekezo ya BodiAmri, maelekezo, notisi au nyaraka nyingine zozote zinazotolewa na Bodi au kwa niaba ya Bodi zitasainiwa na—
(a)Mwenyekiti; au
(b)Katibu au afisa yeyote wa Shirika aliyeidhinishwa kwa maandishi na Bodi.
9.Mgongano wa maslahi
(1)Mjumbe wa Bodi atachukuliwa kuwa na mgongano wa maslahi ikiwa anapata maslahi ya kifedha au maslahi mengine yoyote kwa madhumuni ambayo yanakinzana na utendaji bora wa majukumu au mamlaka yake kama mjumbe wa Bodi.
(2)Endapo mjumbe wa Bodi ana mgongano wa maslahi kuhusiana na—
(a)jambo lolote lililo mbele ya Bodi kwa ajili ya kujadiliwa au kuamuliwa; au
(b)jambo lolote ambalo Bodi ingelitarajia kuja mbele yake kwa ajili ya kujadiliwa au kuamuliwa,
mjumbe huyo ataweka wazi maslahi aliyo nayo na kujiepusha kushiriki au kuendelea kushiriki katika majadiliano au uamuzi wa jambo husika.
10.Kujiuzulu au kutenguliwa kwa mjumbe
(1)Mjumbe wa Bodi anaweza kujiuzulu nafasi yake wakati wowote kwa kutoa taarifa kwa mamlaka ya uteuzi kwa maandishi.
(2)Mjumbe wa Bodi anaweza kuondolewa madarakani na mamlaka ya uteuzi kwa maandishi iwapo—
(a)hatahudhuria vikao vitatu mfululizo vya Bodi bila kibali cha Bodi;
(b)atapoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake kutokana na ugonjwa wa muda mrefu wa kimwili au kiakili;
(c)hafai kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosa uwezo na ukosefu wa maadili;
(d)atapoteza sifa ya kuteuliwa kuwa mjumbe; au
(e)kwa sababu nyingine yoyote ambayo mamlaka ya uteuzi itaona inafaa.
11.AkidiAkidi katika kikao chochote cha Bodi itakua zaidi ya nusu ya wajumbe wa Bodi.
12.Uamuzi wa Bodi
(1)Uamuzi wa Bodi katika suala lolote utafikiwa kwa wingi wa kura za wajumbe waliopo na pale ambapo kura hizo zitalingana, Mwenyekiti atakuwa na kura ya uamuzi.
(2)Bodi inaweza kufanya uamuzi bila kikao kwa kusambaza miongoni mwa wajumbe nyaraka zinazohusika na mawasilisho ya wajumbe kwa maandishi yatakuwa uamuzi wa Bodi, isipokuwa mjumbe yeyote anaweza kuomba uamuzi husika uahirishwe na suala hilo lijadiliwe katika kikao cha Bodi kitakachofuata.
13.Muhtasari wa vikaoMuhtasari wa kila kikao cha Bodi utahifadhiwa na kuthibitishwa na Bodi katika kikao kitakachofuata na kusainiwa na Mwenyekiti au mjumbe aliyeongoza kikao kinachohusika na muhtasari huo pamoja na Katibu.
14.Uhalali wa shughuli za BodiShughuli za Bodi hazitakuwa batili kwa sababu ya kasoro yoyote katika uteuzi wa mjumbe yeyote au kwa kigezo kuwa mjumbe yeyote wakati wa uteuzi hakuwa na sifa au hakustahili kuteuliwa.
15.Bodi kuweka taratibu za kujiendeshaKwa kuzingatia masharti ya Jedwali hili, Bodi itajiwekea utaratibu wa kujiendesha.
▲ To the top

History of this document

04 March 2024
Assented to