Kanuni za Hakimiliki na Hakishiriki (Kampuni za Ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha), 2023

Government Notice 215 of 2023

There are outstanding amendments that have not yet been applied. See the History tab for more information.
Kanuni za Hakimiliki na Hakishiriki (Kampuni za Ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha), 2023

Tanzania
Copyright and Neighbouring Rights Act, 1999

Kanuni za Hakimiliki na Hakishiriki (Kampuni za Ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha), 2023

Tangazo la Serikali 215 ya 2023

Sehemu ya kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina

Kanuni hizi zitaitwa Kanuni za Hakimiliki na Hakishiriki (Kampuni za Ukusanyaji na Ugawaji wa Mirabaha), 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—Sheria” maana yake ni Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki;Bodi” maana yake ni bodi ya wakurugenzi ya Ofisi iliyoanzishwa hivyo chini ya Sheria;haki za jumla” maana yake ni haki zote zinazotolewa kwenye Sheria;madaraja ya kazi” maana yake ni kazi kama zilivyotajwa katika kifungu cha 5(2) cha Sheria;kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha” ina maana iliyotajwa katika kifungu cha 4 cha Sheria;Msimamizi wa Hakimiliki” maana yake ni mkuu wa Ofisi aliyeteuliwa kwa mujibu wa Sheria;mkutano mkuu” maana yake ni mkutano mkuu wa mwaka au mkutano mkuu maalumu ambao wanachama wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha wanashiriki na kutumia haki zao za uanachama;Ofisi” maana yake ni Ofisi ya Hakimiliki ya Tanzania iliyoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria;ada ya usimamizi” maana yake ni kiasi kinachotozwa, kukatwa au kufidiwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kutokana na mapato yanayotokana na hakimiliki au kutokana na mapato yoyote ya uwekezaji wa mapato ya mauzo yanayozalishwa kutokana na hakimiliki ili kulipia gharama za usimamizi wa hakimiliki au haki zinazohusiana;Waziri” ina maana Waziri kwa wakati huo mwenye dhamana na haki miliki na haki shiriki;mwanachama” maana yake ni mmiliki wa hakimiliki au chombo kinachowawakilisha wenye hakimiliki, inajumuisha kampuni nyingine za kukusanya na kugawa mirabaha na chama cha wenye hakimiliki;makubaliano ya uwakilishi” maana yake ni makubaliano baina ya kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha ambapo kampuni moja inaipa kampuni nyingine madaraka ya kusimamia hakimiliki za wale inaowawakilisha;"mapato ya hakimiliki" maana yake ni mapato yanayokusanywa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wenye hakimiliki, iwe yanatokana na hakimiliki pekee, haki ya malipo au haki ya fidia;"mrabaha" maana yake ni malipo ya kiwango kilichokubalika kwa mwenye hakimiliki kwa kutumia kazi yenye hakimiliki; na"mtumiaji" maana yake ni mtu anayenufaika na kazi kutokana na idhini ya wenye hakimiliki, malipo ya wenye hakimiliki au malipo ya fidia kwa wenye hakimiliki.[Sura ya 218]

Sehemu ya pili – Utoaji wa leseni kwa kampuni ya kukusanya na kugawa miraba

3. Zuio la ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha

(1)Mtu hataendesha kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha isipokuwa kwa leseni inayotolewa kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(2)Kwa kuzingatia masharti yaliyotajwa katika kifungu cha 52C cha Sheria, kampuni haitaweza kuomba leseni isipokuwa kama—
(a)mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha siyo miongoni mwa mwanachama wa kampuni; na
(b)Bodi na menejimenti ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaundwa na raia wa Tanzania na kimsingi wawe wanaishi Tanzania.

4. Maombi ya leseni

(1)Kampuni inayokusudia kuendesha shughuli za ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha itaomba leseni kwenye Ofisi kupitia FOMU CM0 01 iliyoainishwa katika Jedwali la Kanuni hizi na kulipa ada ya maombi ya shilingi milioni tano.
(2)Kampuni inayoomba leseni ya kazi ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itawasilisha kwenye Ofisi:
(a)katiba ya kampuni;
(b)taarifa inayoonesha aina ya hakimiliki au daraja la wenye hakimiliki na madaraja ya kazi ambayo asasi inamiliki haki au inayotarajia kuwakilisha;
(c)orodha ya wanachama wenye hakimiliki wasiopungua thelathini wanaowakilisha daraja la hakimiliki ambapo kampuni au shirika linaomba leseni ya kufanya kazi kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ambayo itaonyesha saini za ridhaa za watu hao kuwa wako katika kampuni hiyo, au endapo kampuni imekuwapo, kwamba wao ni wanajamii;
(d)tamko la udhamini wa angalau wakurugenzi wawili au wawakilishi wa kampuni akiwemo mwenyekiti wa bodi ya kampuni kwamba kampuni itatii masharti ya Sheria na Kanuni hizi kuhusiana na uendeshaji wa kampuni;
(e)nakala iliyothibitishwa ya makubaliano ya uanachama inayotumiwa na kampuni;
(f)hati ya kuandikishwa;
(g)hati ya uthibitisho wa mlipa kodi;
(h)leseni ya biashara;
(i)kanuni za kampuni zinazoweka sharti la mwakilishi wa Ofisi kuhudhuria katika Bodi na mikutano mingine mikuu ya kampuni kama mwangalizi;
(j)uthibitisho wa uwepo wa tovuti inayofanya kazi; na
(k)nyaraka au taarifa nyingine zozote kama zitakavyohitajiwa na Ofisi.
(3)Katiba ya kampuni inapaswa kubainisha jukumu la kampuni la kukusanya na kugawa mirabaha kama jukumu la msingi la kampuni hiyo.

5. Uamuzi wa maombi

(1)Ofisi itakubali maombi endapo yanakidhi vigezo vilivyowekwa katika kanuni ya 4.
(2)Endapo Ofisi inakataa maombi ya leseni kwa mujibu wa Kanuni hizi, itampa mwombaji, kwa maandishi, sababu za uamuzi wake.

6. Utoaji wa leseni

(1)Kwa maombi yoyote yaliokubaliwa, Ofisi itampatia mwombaji leseni ya kufanya kazi kama kampuni ya kukusanya na kugawa miraba kupitia Fomu CMO 2 iliyoainishwa katika Jedwali la Kanuni hizi.
(2)Kwa kuzingatia vigezo vya leseni inayotolewa kwa mujibu wa Kanuni hizi, leseni itakuwa halali kwa muda wa mwaka mmoja na inaweza kuhuishwa kila mwaka kulingana na Kanuni hizi.

7. Hatua zinazochukuliwa iwapo hakuna kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha katika baadhi ya madaraja

(1)Endapo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haijaanzishwa kuhusiana na madaraja ya kazi, au leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha imebatilishwa, Ofisi, kwa taarifa itakayotoa katika gazeti linalosambazwa kwa wingi, itatangaza maombi mapya ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kuhusiana na daraja hilo.
(2)Endapo kampuni zaidi ya moja inaomba daraja moja la kazi, Ofisi itatathmini kila ombi kipekee na kutoa leseni kwa kampuni ambayo inawakilisha vizuri maslahi ya wenye hakimiliki kuhusiana na daraja hilo la kazi.

8. Kuondoa vigezo vya masharti ya leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

Endapo kuna mwombaji mmoja wa leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwa daraja la kazi na maombi hayakidhi vigezo vyovyote vya utoaji wa leseni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni hizi, Ofisi inaweza kuondoa vigezo hivyo kama itaona kwamba kuto tolewa kwa leseni kutaathiri utendaji kazi mzuri wa kampuni kuhusiana na daraja la kazi:Isipokuwa kwamba, Ofisi itaitaka kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kutimiza vigezo vya maombi ya leseni ndani ya muda wa leseni utakaoelekezwa.

9. Maombi ya kuhuisha leseni

(1)Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 52C cha Sheria, kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ndani ya miezi mitatu kabla ya leseni kuisha mda wake, itaomba kwa Ofisi kuhuisha leseni yake kupitia Fomu CMO 3 iliyoainishwa katika Jedwali la Kanuni hizi.
(2)Maombi katika kanuni hii yataambatishwa na—
(a)taarifa ya mabadiliko yaliyofanyika katika katiba na kanuni za kampuni katika mwaka uliotangulia maombi;
(b)nakala zilizothibitishwa za hesabu za kampuni zilizokaguliwa katika mwaka uliotangulia maombi;
(c)muundo wa taasisi wa kampuni na majina na sifa za viongozi wakuu;
(d)tamko la mabadiliko katika uongozi wa juu na sababu za mabadiliko hayo;
(e)ripoti ya kina ya shughuli za taasisi katika mwaka uliotangulia maombi;
(f)orodha iliyohuishwa ya wanachama wa taasisi;
(g)kazi mbalimbali zilizopo ambazo zinasimamiwa na kampuni zikionyesha jina la kila kazi na mwenye hakimiliki; na
(h)uthibitisho wa malipo ya ada ya uhuishaji ya shilingi milioni moja.

10. Uamuzi wa maombi ya kuhuisha leseni

(1)Ofisi itaamua kuhusu maombi ya kuhuisha leseni kwa kuzingatia mwenendo wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na uwezo wake wa kukusanya na kugawa mirabaha.
(2)Ofisi inaweza kukataa maombi ya kuhuisha leseni iwapo itaona kuwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haikidhi vigezo vya utoaji wa leseni.
(3)Katika kuamua kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inakidhi matakwa kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (1), Ofisi itazingatia mambo yafuatayo—
(a)iwapo taasisi imethibitisha kuwa na uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha;
(b)iwapo kampuni inazingatia kanuni za utawala bora;
(c)maelezo ya wakurugenzi na historia zao;
(d)iwapo uanachama wa kampuni ni uwakilishi halisi wa wamiliki wa madaraja ya kazi ambayo kampuni inadai kuwakilisha;
(e)iwapo gharama za uendeshaji wa kampuni inazidi asilimia thelathini ya mirabaha iliyokusanywa na kampuni;
(f)iwapo mirabaha inagawanywa kwa wakati na ipasavyo kwa kutumia kanuni za ugawaji zilizoidhinishwa;
(g)maelezo ya viongozi wa juu wa kampuni, elimu na taaluma zao;
(h)mikakati na mifumo ya kampuni ya kuhakikisha mirabaha inakusanywa na kugawanywa kwa ufanisi;
(i)hesabu zilizokaguliwa za kampuni;
(j)iwapo kampuni imewasilisha ripoti ya mwaka; na
(k)taarifa nyingine yoyote au ufafanuzi ambao unaweza kusaidia katika kuamua maombi ya uhuishaji wa leseni.
(4)Endapo taarifa zinazohitajika kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (1) hazipo, Bodi itamteua mkaguzi wa hesabu kufanya ukaguzi wa mifumo au ukaguzi wa fedha za kampuni kadri itakavyohitajika.

11. Utoaji wa leseni iliyohuishwa

Ofisi itampatia mwombaji aliyekubaliwa, leseni iliyohuishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kupitia Fomu CMO 4 iliyoainishwa katika Jedwali la Kanuni hizi.

12. Kusimamisha au kubatilisha leseni

(1)Endapo kampuni itashindwa kuchukua hatua yoyote ndani ya muda unaotakiwa kama ilivyoelekezwa kufanya na Ofisi, leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inaweza kusimamishwa kutokana na kutotekelezwa kwa hatua na kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itashindwa kutekeleza ndani ya miezi mitatu ya kusimamishwa huko, Ofisi inaweza kubatilisha leseni.
(2)Ofisi, kwa mamlaka yake au kwa maombi ya mtu yeyote mwingine mwenye maslahi, inaweza kufuta leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha endapo—
(a)kwa maoni ya Ofisi, kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inakiuka au inashindwa kufuata masharti yoyote ya Sheria na Kanuni hizi;
(b)kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haifanyi kazi tena, au haiwawakilishi wenye hakimiliki wa daraja lolote la kazi ambalo leseni ilitolewa;
(c)kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha imeshindwa kutoa taarifa ambazo, kama zingejulikana wakati wa kushughulikia maombi yake ya leseni, zingeweza kusababisha kukataliwa kwa maombi hayo;
(d)Ofisi imepata taarifa ambazo haikuwa inazijua wakati wa kutathmini maombi ya leseni, au matukio ya baadaye ambayo, iwapo Ofisi ingepata fursa ya kuyatathmini, ingekuwa ni kigezo cha kukataliwa kwa maombi ya kupatiwa leseni; au
(e)kwa jambo lingine lolote, Ofisi imejiridhisa uwepo wa sababu za msingi na za kutosheleza kukataa maombi ya leseni ya kutoa huduma ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha:
Isipokuwa kwamba, kabla ya kufuta leseni, Ofisi itaitaarifu kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwa maandishi kuhusu kusudio lake la kufuta leseni kwa sababu iliyopo katika kanuni ndogo ya (1), na kuitaka kampuni, ndani ya miezi mitata tangu tarehe ya kupewa taarifa, kuwasilisha maelezo au kusahihisha jambo husika.

13. Rejesta na tangazo kwa umma

(1)Ofisi, kwa namna itakavyoona inafaa, itaanzisha na kutunza rejesta ya kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha zitakazopata leseni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni hizi.
(2)Mara baada ya kutoa leseni, Ofisi itawezesha kuchapishwa kwa tangazo la kawaida kwa umma kupitia Gazeti la Serikali au Gazeti linalosambazwa kwa wingi, kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwa kila daraja la kazi linalohusika na leseni.

Sehemu ya tatu – Maadili ya kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha

14. Maadili ya kampuni kwa ujumla

(1)Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika Kanuni hizi, kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaonyesha kwa umma—
(a)hati ya usajili kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(b)nyaraka za msingi za utawala kama katiba ya kampuni, sheria na kanuni au hati ya idhini;
(c)orodha ya wajumbe wote wa menejimenti;
(d)jina na anwani ya mwenyekiti, wajumbe wengine wa menejimenti na maafisa wengine wa taasisi;
(e)haki au kundi la haki za hakimiliki katika kundi mahsusi la kazi ambalo leseni imetolewa kwaajili hiyo;
(f)kanuni zote zilizotengenezwa na kampuni;
(g)ripoti ya mwaka na hesabu zilizokaguliwa kama zilivyoidhinishwa na mkutano mkuu wa mwaka;
(h)muundo wa makubaliano ya leseni;
(i)maelezo yote ya leseni zilizopo isipokuwa maelezo ya leseni yenye taarifa za siri za kibiashara;
(j)kampuni za kigeni ambazo zina makubaliano ya kukusanya mirabaha na maelezo ya makubaliano tofauti na vifungu vyenye taarifa za siri za kibiashara; na
(k)maelezo ya malalamiko au migogoro iliyowasilishwa.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kuwa wanachama—
(a)wanahudumiwa bila ubaguzi na kwamba inawashughulikia kwa uwazi;
(b)wakati wanapojiunga na kampuni au wakati wowote wanapohitaji, wanapewa nakala ya nyaraka za utawala za kampuni zikiwemo katiba ya kampuni, kanuni za kampuni, hati idhini, kanuni za ushuru na kanuni za ugawaji wa mirabaha;
(c)wanapewa nakala ya waraka unaoainisha wajibu na majukumu ya kila mjumbe wa menejimenti ya kampuni; na
(d)wanafahamishwa au kujengewa uelewa kuhusu—
(i)vigezo vya kukokotoa mirabaha itakayolipwa kwa wanachama;
(ii)namna na idadi ya malipo kwa wanachama; na
(iii)hali ya jumla ya makato kutokana na jumla ya mapato kabla ya kugawa.
(3)Kila mfanyakazi wa kampuni—
(a)atatekeleza majukumu yake bila ya upendeleo, ubaguzi au chuki;
(b)hatofanya au kusababisha kufanyika kwa tendo lolote la ukosefu wa uaminifu, udanganyifu au tendo lolote lililokinyume cha sheria dhidi ya kampuni na wanachama wake;
(c)ataiwakilisha kampuni kwa uaminifu, kwa heshima na kwa kufuata sheria;
(d)ataonyesha na kuhimiza viwango vya juu vya utendaji wa kampuni ili kuongeza imani ya wananchi kwa kampuni;
(e)atashauri na kuhamasisha usuluhishi wa migogoro badala ya kufungua kesi mahakamani au kuendeleza kesi ikiwa kesi hiyo inaweza kutatuliwa kwa njia ya haraka, kwa usawa na kwa njia inayofaa.

Sehemu ya nne – Uanachama na usimamizi wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

15. Uanachama katika kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Uanachama wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha utawekwa wazi kwa wenye hakimiliki wote, wa ndani au nje ya nchi, kwa madaraja ya kazi au daraja la hakimiliki ambalo kampuni inaombea leseni au ina leseni ya kazi kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitaweka sharti la kumtaka mwanachama kuiunda kampuni kama wakala pekee wa ukusanyaji au wakala kwa madhumuni mengine yoyote tofauti na madhumuni ya kusimamia haki za wanachama kwa kuzingatia mipaka ya leseni ya kampuni kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(3)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitaweka sharti la lazima kwa mwanachama kukabidhi kwa kampuni haki ya kukusanya mirabaha kutoka kwa makampuni ya kukusanya mirabaha ya kigeni yanayojishughulisha na ukukusanyaji kama kampuni hiyo.
(4)Ofisi inaweza, endapo imeridhika kwamba kampuni inakiuka kanuni hii, kutoa onyo kwa maandishi au kuitaka kampuni au maafisa wake kusahihisha ukiukaji huo ndani ya muda utakaowekwa.

16. Kanuni za uanachama wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itawakubali kama wanachama wake—
(a)wenye haki miliki wa ndani na nje ya nchi, kwa kadri itakavyokuwa;
(b)vyombo vinavyowakilisha wenye hakimiliki ikijumuisha kampuni nyingine za kukusanya na kugawa mirabaha au vyama vya wenye hakimiliki, watakaotimiza masharti ya uanachama yaliyotajwa katika kanuni na katiba ya kampuni.
(2)Endapo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itakataa kukubali maombi ya uanachama, itatoa sababu za kukataa kwake kwa maandishi kwa mwenye hakimiliki.
(3)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba masharti yake ya uanachama—
(a)siyo ya upendeleo, ni ya uwazi na yasiyokuwa ya kibaguzi;
(b)yamejumuishwa katika kanuni na katiba ya kampuni; na
(c)yanafahamika kwa umma.
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inaweza kuweka ada ya uanachama kwa wanachama wake:Isipokuwa kwamba, ada ya uanachama itakuwa ni ile iliyokubaliwa katika mkutano mkuu wa wanachama na kuidhinishwa na Ofisi.

17. Uanachama na usimamizi wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

Mwanachama, baada ya kutoa taarifa ya nia yake ya kujitoa, atakuwa na haki ya kujivua uanachama wake kwenye kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au hakimiliki alizotoa kwa kampuni kuhusiana na kazi zake:Isipokuwa kwamba, Kampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha ambayo uanachama wake uko chini ya idadi ya wajumbe thelathini kutokana na wanachama kujitoa, itaitaarifu Ofisi ndani ya siku saba, na itasajili idadi ya wanachama inayohitajika ndani ya siku kumi na nne tangu siku ya taarifa kutolewa.

18. Ushiriki wa wanachama

Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha—
(a)itahakikisha kwamba kanuni na katiba ya kampuni inatoa taratibu zinazofaa na kuwezesha ushiriki wa wanachama wake katika kufanya uamuzi;
(b)itahakikisha kwamba uwakilishi wa makundi mbalimbali ya wanachama katika mchakato wa kufanya uamuzi ni wa haki na wenye uwiano;
(c)itawaruhusu wanachama wake, na wenye hakimiliki ambao sio wanachama ila wana uhusiano wa kisheria wa moja kwa moja na kampuni kwa mujibu wa sheria, leseni au utaratibu mwingine wa kimkataba kuwasiliana na wenye hakimiliki kwa madhumuni ya kutumia haki za wanachama; na
(d)itaweka na kutunza kumbukumbu za wanachama wake na kuzihuisha mara kwa mara.

19. Mikutano ya kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Kwa kuzingatia Kanuni hizi na sheria nyingine za usimamizi wa makampuni nchini, kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaitisha mkutano wa wanachama wake angalau mara mbili kwa mwaka.
(2)Mkutano mkuu wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha utaamua—
(a)kuhusu marekebisho yoyote katika kanuni na katiba ya kampuni, na masharti ya uanachama ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(b)kuhusu uteuzi na kufukuzwa kwa viongozi wa kampuni, kupitia utendaji wa viongozi na kuidhinisha malipo yao na marupurupu mengine;
(c)kuhusu kanuni za ugawaji wa kiasi wanachostahili wanachama na wenye hakimiliki;
(d)kuhusu kanuni za matumizi ya kiasi kisichogawanywa;
(e)kuhusu kanuni ya uwekezaji katika mapato ya hakimiliki na mapato yoyote yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki;
(f)kanuni kuhusu makato kutoka kwenye mapato ya hakimiliki na mapato yoyote yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki;
(g)kuhusu sera ya usimamizi na udhibiti wa hatari;
(h)kuhusu uidhinishaji wa umiliki wowote, uuzaji au utozaji wa mali zisizohamishika; na
(i)kuhusu kuidhinisha uunganishaji wa kampuni na ushirikiano na kampuni nyingine zinazofanana nazo.
(3)Mwenyekiti wa kampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha au, kwa kadri itakavyokuwa, angalau mbili ya tatu ya wanachama wa kampuni wanaweza kuitisha mkutano mkuu.

20. Haki ya kupiga kura

Mwanachama katika mkutano mkuu atakuwa na haki ya kupiga kura kwa kufuata vigezo vifuatavyo:
(a)idadi ya kazi zilizosajiliwa; au
(b)kiasi kilichopokelewa au kinachostahili kulipwa kwa mwanachama,
Isipokuwa kwamba, kigezo hicho kitaamuliwa na kutumika katika namna ambayo ni ya haki na inayolingana na thamani ya hakimiliki zao zinazosimamiwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha.

21. Ripoti za mikutano

Kila kampuni yenye leseni kwa mujibu wa Kanuni hizi ya kufanya kazi kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itatoa ripoti yenye kumbukumbu na uamuzi uliofanywa katika kila mkutano wa mkutano mkuu na Bodi ili ziingizwe kwenye daftari maalumu lililowekwa kwa madhumuni hayo, na nakala ya ripoti iliyothibitishwa itawasilishwa katika Ofisi pale Ofisi itakapoihitaji.

22. Hesabu, ripoti ya mwaka na ukaguzi

(1)Kila kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaweka hesabu sahihi kulingana na viwango vya kawaida vya uhasibu.
(2)Ofisi, itakapoona ni lazima, inaweza wakati wowote kumteua mkaguzi wa hesabu ili akague hesabu za kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, na gharama za ukaguzi huo zitalipwa na kampuni husika.
(3)Endapo kutokana na uchunguzi wa hesabu zozote au ukaguzi wa hesabu Ofisi itaona kwamba kosa lolote chini ya sheria yoyote limefanywa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au na yeyote kati ya maafisa wake, Ofisi inaweza kusababisha kufunguliwa kwa kesi ya jinai dhidi ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au maafisa wa kampuni waliobainika kufanya kosa hilo.
(4)Endapo afisa ametiwa hatiani kwa kosa kama ilivyoelezwa katika kifungu kidogo cha (3), Ofisi itaitaka kampuni kumsimamisha afisa huyo ili asiendelee kutekeleza majukumu aliyokuwa akitekeleza mara kabla ya kutiwa hatiani.

23. Muundo na maudhui ya ripoti ya mwaka

(1)Kwa mujibu wa kifungu cha 53D cha Sheria, kila kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ndani ya miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, itawasilisha katika Ofisi, ripoti ya mwaka kwa mwaka huo ikiambatana na nakala ya hesabu za kampuni zilizokaguliwa za mwaka huo.
(2)Ripoti ya mwaka inayorejelewa katika kanuni ndogo ya (1) itakuwa na—
(a)ripoti ya kina ya shughuli za kampuni katika mwaka huo;
(b)orodha ya wanachama wa kampuni hadi mwishoni mwa mwaka wa fedha;
(c)jumla ya kiasi cha mirabaha kilichokusanywa na kampuni;
(d)kiasi cha mirabaha kilicholipwa na kampuni kwa kila mwanachama;
(e)kiasi cha fedha kilichotumiwa na kampuni katika utawala na uendeshaji;
(f)majina, anwani ya posta na ya makazi ya wakaguzi wa kampuni;
(g)kiasi cha fedha kilichotumika kwa shughuli za kijamii;
(h)mirabaha ambayo haikugawiwa na sababu za kutoigawa;
(i)majina, anwani na kazi za viongozi wa kampuni waliopo kwa wakati huo; na
(j)taarifa nyingine zozote muhimu kama ambavyo Ofisi itahitaji.

24. Akaunti ya akiba maalumu

(1)Kampuni ya ukusanyaji wa mirabaha itaanzisha akaunti ya akiba maalumu baada ya kufanya jitihada zote katika kubainisha wenye hakimiliki wa kazi zinazohusika ambazo zitatumika, pamoja na mambo mengine, kushikilia hisa yoyote ya kiasi kinachogawanywa, ambacho hakiwezi kutengwa au kugawanywa kwa sababu zifuatazo:
(a)kampuni imepoteza mawasiliano na mwanachama anayehusika;
(b)mtu mwenye sifa anayestahili sio mwanachama kwa wakati huo;
(c)endapo mwanachama au wakala wake hayupo au hapatikani kwa urahisi, mwenye hakimiliki anayehusika au wakala anayestahili kiasi hicho hapatikani;
(d)kuna mgogoro katika hakimiliki;
(e)sehemu ya fedha zilizokusanywa haziwezi kugawiwa mara moja kutokana na kutokuwepo kwa taarifa za kutosha kwa ajili ya mgawanyo.
(2)Endapo fedha katika akaunti ya akiba maalumu inabidi zigawanywe, Kampuni itagawa fedha kwa kuzingatia data bora zilizopo kabla ya kuisha muda kwa kipindi hicho maalumu.

25. Muda wa kuhifadhi fedha kwenye akaunti ya akiba maalumu

(1)Endapo kiasi chochote cha fedha kinabakia bila kugawanywa kwa kipindi cha miaka mitatu, kampuni itagawa fedha hizo kwa urari kwa pande zote zinazopokea mirabaha wakati wa mgao wa miaka mitatu iliyopita wa kampuni.
(2)Kiasi kinachobakia kwenye akaunti ya akiba maalumu wakati wa kipindi maalumu kumalizika kitaingia kwenye mapato ya jumla kwa ajili ya kugawanywa kuhusiana na kipindi kinachohusika cha kutoa taarifa ya fedha au kipindi kilichositishwa kama hilo linatokea ili kulingana na kumalizika kwa muda wa kipindi hicho maalumu.

26. Wajibu wa kuripoti wa kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ndani ya siku kumi na nne baada ya kuanzishwa, itaitaarifu Ofisi na kuikabidhi taarifa kuhusiana na—
(a)mabadiliko ya kanuni na katiba ya kampuni au kanuni zozote za ndani;
(b)kupitisha ushuru na mabadiliko mengine yoyote;
(c)makubaliano ya uwakilishi wa pande mbili na kampuni za ukusanyaji za kigeni;
(d)mabadiliko yoyote katika makubaliano ya kiwango cha uanachama;
(e)uamuzi wowote katika mahakama au mashauri rasmi ambapo kampuni inahusika, endapo Ofisi itahitaji; na
(f)nyaraka zozote, ripoti au taarifa ambazo Ofisi itahitaji.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itatarisha na kuwasilisha katika Ofisi nyaraka zifuatazo kuhusiana na uendeshaji wake kwa mwaka uliotangulia ifikapo tarehe 1 Julai ya kila mwaka—
(a)ripoti ya jumla ya shughuli zake; na
(b)ripoti ya mwaka ya fedha zilizokaguliwa ambayo, pamoja na mambo mengine, itaeleza—
(i)jumla ya mapato katika kipindi cha ripoti;
(ii)jumla ya fedha na aina ya matumizi kwa ujumla; na
(iii)malipo ya mirabaha kwa wanachama kulingana na sera ya ugawaji ya kampuni.

27. Wajibu wa kutoa taarifa kwa watumiaji wa hakimiliki

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itawapa watumiaji wa kazi za hakimiliki, au mwanachi yeyote, taarifa za msingi kuhusu huduma zao kwa maandishi pale watakapoziomba.
(2)Taarifa chini ya kanuni ndogo ya (1) itajumuisha—
(a)maelezo ya hakimiliki au aina ya hakimiliki inazozisimamia;
(b)utaratibu uliopo wa leseni ya kampuni ya usimamizi wa hakimiliki ikijumuisha ushuru, vigezo na masharti ya leseni kwa makundi yote ya watumiaji; na
(c)taarifa nyingine muhimu ambazo zinaweza kuhitajika.
(2)Endapo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inataka kubadilisha viwango vya ushuru kwa kundi lolote la watumiaji, itawataarifu watumiaji hao kupitia njia ambayo ni rahisi kwao kupata taarifa hiyo.
(3)Endapo Ofisi imeridhika kwamba kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inakiuka masharti yoyote ya kanuni ndogo ya (1) na (2), kampuni na maafisa wake wanaweza kustahili kupata onyo la maandishi na kutakiwa kurekebisha ukiukaji huo ndani ya muda utakaotajwa.
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itakayoshindwa kurekebisha ukiukaji ndani ya muda uliotajwa italipa faini ya shilingi milioni mbili zitakazotokana na gharama za uendeshaji wa kampuni.

28. Gharama za uendeshaji wa kampuni

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inaweza kuzuia makato ya lazima kutoka katika kiasi kilichokusanywa au ilichopokea ili kufidia gharama zozote ilizozitumia katika kutekeleza majukumu yake, na makato yatakayozuiwa yatakuwa ndani ya kikomo kitakachoamuliwa na bodi ya wakurugenzi ya kampuni kulingana na ukomo wa asilimia 30 ya jumla ya mirabaha na ada zilizokusanywa katika mwaka ambao makato yanafanyika.
(2)Bila ya kuathiri kanuni ndogo ya (1), Waziri, baada ya kupokea maombi ya maandishi kutoka kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, inaweza kuidhinisha makato ya zaidi ya asilimia 30 ya jumla ya mapato ya kampuni ili kufidia matumizi ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha.
(3)Endapo kampuni imezidisha ukomo wa matumizi yake yaliyoidhinishwa kama ilivyoelezwa katika kanuni ndogo ya (1) na (2), kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na afisa wake yeyote anayehusika na ukiukwaji huo atastahili karipio au onyo la maandishi na kutakiwa kurekebisha ukiukwaji huo ndani ya muda utakaotajwa na Ofisi.
(4)Ofisi inaweza kusitisha matumizi au kuifuta leseni ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha iwapo kampuni itashindwa kurekebisha ukiukaji kama inavyohitajika katika kanuni ndogo ya (3).

29. Usimamizi wa kazi na mgongano wa maslahi

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba mtu yeyote anayesimamia biashara zake anafanya hivyo katika namna ya uangalifu, kwa kutumia taratibu zinazokubalika za kiutawala, kihasibu na mifumo ya udhibiti wa ndani.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaandaa na kutumia taratibu—
(a)kwa ajili ya kuepuka migongano ya maslahi; na
(b)endapo migongano ya maslahi haiwezi kuepukika, kubainisha, kusimamia, kufuatilia na kufichua migongano ya maslahi iliyopo au inayoweza kutokea katika namna ya kuizuia isiathiri vibaya maslahi ya ukusanyaji wa wenye hakimiliki wanaowakilishwa na kampuni.
(3)Taratibu zinazorejelewa katika kanuni ndogo ya (2) zitajumuisha taarifa ya mwaka itakayotolewa katika mkutano mkuu na mtu aliyetajwa katika kanuni ndogo ya (1) ikieleza—
(a)maslahi yoyote katika kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(b)malipo yoyote yaliyopokelewa katika mwaka wa fedha uliotangulia kutoka kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ikijumuisha manufaa ya vitu na aina nyingine za manufaa;
(c)kiasi chochote kilichopokelewa katika mwaka wa fedha uliotangulia kama mwenye hakimiliki kutoka kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha; na
(d)tamko kuhusiana na mgogoro wowote uliopo au unaoweza kutokea kati ya-
(i)maslahi yoyote binafsi na yale ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha; na
(ii)madeni yoyote yanayodaiwa kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na ushuru unaodaiwa na mtu mwingine yeyote.
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba taratibu zake za mafunzo kwa wafanyakazi, mawakala na wawakilishi zinajumuisha mafunzo yanayofaa kuhusu mwenendo unaoendana na wajibu wake kwa mujibu wa Kanuni hizi.

Sehemu ya tano – Utoaji leseni, ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha

30. Haki ya wenye leseni na upangaji wa ada

(1)Kila kampuni itawatendea wenye leseni kwa haki, uaminifu, bila upendeleo na kwa heshima na kuhakikisha kwamba shughuli zake na wenye leseni ni za uwazi zaidi.
(2)Kila kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itazingatia yafuatayo wakati wa kuandaa mpango wa bei:
(a)ada ya leseni iwe ya haki na ya kuridhisha;
(b)kuzingatia thamani ya haki za kazi;
(c)madhmuni na namna ambayo haki zinapaswa kutumiwa; na
(d)uamuzi wowote muhimu wa mahakama na baraza.
(3)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na mtumiaji
(a)watajadiliana utoaji leseni kwa haki kwa nia njema; na
(b)watajadiliana kwa nia njema bei kwa hakimiliki za kipekee na hakimiliki za malipo kuhusiana na—
(i)thamani ya kiuchumi ya matumizi ya hakimiliki katika biashara kwa kuzingatia upeo wa matumizi ya kazi na jambo lingine lolote linalohusika;
(ii)thamani ya kiuchumi ya huduma inayotolewa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha; na
(iii)ongezeko la thamani linalotolewa na mtoa huduma yeyote na watu binafsi; na
(c)itamtaarifu mtumiaji kwa maandishi vigezo vinavyotumika kuweka bei zilizotajwa katika aya (b) ya kanuni ndogo ya (1).
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha—
(a)itajibu mara moja maombi kutoka kwa watumiaji ikionyesha, pamoja na mambo mengine, taarifa zinazotakiwa ili kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itoe leseni;
(b)baada ya kupokea taarifa zote zinazohusika—
(i)itatoa leseni; au
(ii)haitampa leseni mtumiaji na kumtaarifu kwa maandishi sababu za kutompa leseni;
(c)itawaruhusu watumiaji kuwasiliana nayo kwa njia yoyote, ikijumuisha madhumuni ya kutoa ripoti kuhusu matumizi ya leseni; na
(d)baada ya kumpa leseni mtumiaji, itamhudumia kwa uaminifu.
(5)Endapo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha zaidi ya moja inafanya shughuli katika sekta moja, kampuni hizo zitaingia katika mkataba wa umoja kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja ya utoaji leseni na ukusanyaji wa pamoja wa mirabaha.

31. Kukusanya na kutumia mapato ya hakimiliki

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba-
(a)inakuwa makini katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya hakimiliki;
(b)inatenganisha hesabu zake za—
(i)mapato ya hakimiliki na mapato mengine yoyote yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki;
(ii)mali zozote inazomiliki na mapato yanayotokana na mali hizo, kutokana na ada za usimamizi, ada za uanchama au kutokana na shughuli nyingine; na
(iii)kiasi cha utawala na ugawaji;
(c)kwamba haitumii mapato ya hakimiliki au mapato mengine yoyote yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki kwa madhumuni ambayo ni tofauti na kugawa kwa wenye hakimiliki, isipokuwa pale inaporuhusiwa—
(i)kukata au kufidia ada za usimamizi kwa mujibu wa Sheria au Kanuni hizi; au
(ii)kutumia mapato ya hakimiliki au mapato yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki kwa mujibu wa Sheria au Kanuni hizi; na
(d)kwamba pale inapowekeza mapato ya hakimiliki, au mapato yanayotokana na kuwekeza mapato ya hakimiliki, inafanya hivyo—
(i)kwa maslahi bora ya wenye hakimiliki ambao hakimiliki zao zinawakilishwa; na
(ii)kwa mujibu wa uwekezaji wa jumla na sera ya kampuni ya kusimamia na kudhibiti hatari.
(2)Bodi ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaomba kuidhinishwa kwa kanuni za ugawaji kutoka kwa mkutano mkuu wa wanachama wake.
(3)Mapato yoyote yanayohitajika kubakizwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itakuwa ni kwa idhini ya wanachama katika mkutano mkuu na yatatumika kwa madhumuni yaliyoamuliwa na wanachama.

32. Ugawaji fedha kwa wenye hakimiliki

(1)Kila kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itawalipa wenye hakimiliki kulingana na kanuni zake za ukusanyaji na ugawaji.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itagawa, kwa kiwango chenye kuleta manufaa, mapato yaliyokusanywa kwa kukaribiana kadri iwezekanavyo na matumizi halisi ya kazi au rekodi za sauti chini ya usimamizi wao na kwamba watumiaji wana wajibu wa kutoa taarifa za matumizi kwa mujibu wa kanuni ya 31.
(3)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itagawa na kulipa mara moja kiasi kinachostahili kulipwa kwa wenye hakimiliki, lakini katika tukio lolote sio zaidi ya mwanzoni mwa kipindi kinachoanza miezi tisa kuanzia mwishoni mwa mwaka wa fedha ambao mapato ya hakimiliki yalikusanywa.
(4)Bila ya kuathiri kanuni ndogo ya (2), kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inaweza kugawa au kulipa kiasi kinachostahili kulipwa kwa wenye hakimiliki nje ya muda kama kuna sababu za msingi za kutogawa au kulipa kiasi hicho ikijumuisha sababu zinazohusiana na—
(a)watumiaji kuripoti;
(b)utambulisho wa hakimiliki au wenye hakimiliki; au
(c)kulinganisha taarifa na mambo mengine kuhusu kazi na mambo mengine pamoja na wenye hakimiliki.
(5)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba kiasi kinachostahili kulipwa kinawekwa katika akaunti tofauti za kampuni ambapo—
(a)kiasi hicho hakiwezi kugawanywa ndani ya muda uliopangwa; na
(b)kanuni ndogo ya (3) haitumiki.
(6)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itachukua hatua zote muhimu za kuwabainisha na kuwatafuta wenye hakimiliki kwa madhumuni ya ugawaji na malipo ya kiasi kinachostahili kulipwa kwa wenye hakimiliki ikiwa ni pamoja na—
(a)kutoa taarifa kuhusu kazi na mambo mengine ambapo mwenye hakimiliki bado hajatambuliwa au kujulikana aliko, katika kipindi kisichozidi miezi mitatu baada ya kuanza kwa kipindi kilichotajwa katika kanuni ndogo ya (2)—
(i)wenye hakimiliki wanaowakilishwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au vyombo ambavyo ni wanachama wao na ambavyo vinawakilisha wenye hakimiliki; na
(ii)kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo imekamilisha makubaliano ya uwakilishi;
(b)Kuthibitisha kumbukumbu husika zinazohusiana na mwenye hakimiliki kwa madhumuni ya kugawanya au kulipa kiasi kinachostahili kulipwa; na
(c)Endapo wenye hakimiliki hawafahamiki au hawajulikani walipo, kusambaza taarifa iliyotajwa katika aya (b) kwa wananchi kabla ya mwaka mmoja baada ya kipindi kilichotajwa katika aya (a).
(7)Taarifa iliyotajwa katika aya ya (5) itajumuisha, pale inapowezekana—
(a)jina la kazi na kitu kingine;
(b)jina la mwenye hakimiliki;
(c)Jina la mchapishaji au mtayarishaji wa kazi au kitu kingine; na
(d)Taarifa nyingine zozote muhimu ambazo zinaweza kusaidia katika kumtambua mwenye hakimiliki.
(8)Kiasi wanachostahili kulipwa wenye hakimiliki hakitagawanywa kwa madhumuni ya Kanuni hizi ambapo—
(a)hakiwezi kugawanywa kabla ya mwisho wa miaka mitatu kuanzia mwishoni mwa mwaka wa fedha ambao ukusanyaji wa mapato ya hakimiliki ulifanyika; na
(b)kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha imechukua hatua zote muhimu kubainisha na kujua walipo wenye hakimiliki.
(9)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itawapa wanachama wake taarifa za mirabaha iliyolipwa katika kipindi kilichobainishwa.

33. Malipo ya mirabaha kwenye makubaliano ya uwakilishi

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itagawa au kulipa mara kwa mara, kwa umakini na kwa usahihi kiasi kinachostahili kulipwa kwa kampuni nyingine za kukusanya na kugawa mirabaha.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itagawa au kulipa kiasi kinachostahili kulipwa chini ya kanuni ndogo ya (1), na kwa namna yoyote ile, si zaidi ya mwanzoni mwa kipindi kinachoanzia miezi tisa tangu kumalizika kwa mwaka wa fedha ambapo mapato ya hakimiliki yalikusanywa.
(3)Bila kujali kanuni ndogo ya (2), kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitagawa au kulipa kiasi kinachostahili kulipwa kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (2) iwapo kuna sababu za msingi za kutokufanya hivyo, zikiwemo sababu zinazohusiana na—
(a)watumiaji kuripoti;
(b)utambuzi wa hakimiliki na wenye hakimiliki; au
(c)kulinganisha taarifa za kazi na mambo mengine pamoja na wenye hakimiliki.
(4)Endapo kampuni nyingine ya kukusanya na kugawa mirabaha iliyotajwa katika kanuni ndogo ya (1) au, ikiwa kampuni hiyo ina mwanachama ambaye ni chombo kinachowawakilisha wenye hakimiliki, kampuuni hiyo au mwanachama huyo atahakikisha kwamba anagawanya na kulipa mara moja kiasi kinachostahili kulipwa kwa wenye hakimiliki, na kwa namna yoyote ile, sio zaidi ya mwanzoni mwa kipindi ambacho kinaanza miezi sita kuanzia siku ya kupokea kiasi hicho, isipokuwa kama mazingira yaliyotajwa katika kanuni ndogo ya (3) yatatokea.

34. Makato

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha yenye ruhusa ya wenye haki miliki ya kusimamia hakimiliki zao itahakikisha inampatia mwenye hakimiliki taarifa kuhusu—
(a)ada za usimamizi; na
(b)makato mengine yoyote kutoka katika mapato ya hakimiliki na mapato yoyote yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki kabla ya kupata ridhaa ya mwenye hakimiliki ya kusimamia hakimiliki zake.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kuwa—
(a)makato yanalingana na huduma inayotolewa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwa wenye hakimiliki;
(b)makato yamewekwa kwa kuzingatia vigezo visivyo na upendeleo;
(c)makato yanayoruhusiwa ni yale ya kulipia gharama halisi za uendeshaji, na kwa idhini ya wanachama wenye hakimiliki; na
(d)makato yoyote yanayoidhinishwa yafanyike kwa namna ya haki na kutobagua, na hayafanyiki kwenye mapato yanayokusanywa kwa wenye hakimiliki ambao sio wanachama.
(3)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itahakikisha kwamba ada ya usimamizi haizidi gharama halali zilizothibitika na zilizo katika kumbukumbu zilizotumiwa na kampuni.
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inayotoa huduma za kijamii, kiutamaduni au kielimu kutokana na mapato ya hakimiliki au mapato yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki itahakikisha inapotoa hizo kwa haki.
(5)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitafanya makato, yakiwemo makato ya ada ya usimamizi
(a)kutoka kwenye mapato ya hakimiliki yaliyotokana na hakimiliki inazozisimamia kwa misingi ya makubaliano ya uwakilishi; au
(b)kutoka kwenye mapato yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki, isipokuwa kama kampuni nyingine ambayo ni sehemu ya makubaliano ya uwakilishi inaridhia kufanyika kwa makato hayo.

35. Ushughulikiaji wa hakimiliki zinazosimamiwa chini ya makubaliano ya uwakilishi

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitabagua dhidi ya mwenye hakimiliki yeyote ambaye inasimamia hakimiliki zake chini ya makubaliano ya uwakilishi.
(2)Bila kuathiri kanuni ndogo ya (1), kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha haitabagua dhidi ya mwenye hakimiliki ambaye inasimamia haki zake chini ya makubaliano ya uwakilishi kuhusiana na—
(a)bei zinazotumika;
(b)ada ya usimamizi; na
(c)masharti ya—
(i)ukusanyaji wa mapato ya hakimiliki; na
(ii)ugawaji wa kiasi kinachostahili kwa wenye hakimiliki.

36. Wajibu wa mtumiaji

(1)Mtumiaji na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha wataingia katika makubaliano ya maandishi kuhusu taarifa ambazo mtumiaji atazitoa kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ndani ya muda uliokubaliwa au uliyowekwa mapema—
(a)ukusanyaji wa mapato ya hakimiliki; na
(b)ugawaji na malipo ya kiasi kinachostahili kwa wenye hakimiliki.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na mtumiaji watahakikisha kwamba wanazingatia, kwa kadri inavyowezekana, viwango vya vya hiari vya usalama kuhusu muundo kwa taarifa zinazotajwa katika kanuni ndogo ya (1).

37. Taarifa zinazotolewa kwa kampuni nyingine za kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itatoa taarifa zilizotajwa katika kanuni ndogo ya (2) angalau mara moja kila mwaka kwa kampuni nyingine za kukusanya na kugawa mirabaha ambayo kwa niaba yao inasimamia hakimiliki chini ya makubaliano ya uwakilishi kwa kipindi kinachohusiana na taarifa hizo.
(2)Taarifa zinazotakiwa kutolewa chini ya kanuni ndogo ya (1) zitajumuisha—
(a)mapato ya hakimiliki yanayohusishwa na hakimiliki zinazosimamiwa chini ya makubaliano ya uwakilishi;
(b)kiasi kinacholipwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha
(i)kwa kila kategoria ya hakimiliki inayosimamiwa chini ya makubaliano ya uwakilishi; na
(ii)kwa kila aina ya matumizi ya hakimiliki inayosimamiwa chini ya makubaliano ya uwakilishi;
(c)mapato ya hakimiliki yanayohusishwa ambayo hayajalipwa kwa kipindi chochote;
(d)makato yaliyofanywa kuhusiana na ada za usimamizi;
(e)makato yaliyofanywa kwa madhumuni tofauti na yale yanayohusiana na ada za usimamizi;
(f)leseni yoyote inayotolewa au kukataliwa kuhusiana na kazi na mambo mengine yaliyohusiana na makubaliano ya uwakilishi; na
(g)maazimio yaliyopitishwa na mkutano mkuu hadi wakati huo kwa kuwa maazimio ni muhimu katika usimamizi wa hakimiliki chini ya makubaliano ya uwakilishi.

38. Utoaji wa taarifa kwa umma

Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itatangaza na kuhuisha taarifa zifuatazo katika tovuti yake:
(a)kanuni na katiba ya kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(b)orodha ya viongozi wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(c)kanuni za ugawaji wa kiasi kinachostahili kwa wenye hakimiliki za kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(d)kanuni za kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha zinazohusu ada za usimamizi;
(e)kanuni za kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha zinazohusu makato, tofauti na yale yanayohusu ada za usimamizi, kutokana na-
(i)mapato ya hakimiliki;
(ii)mapato yanayotokana na uwekezaji wa mapato ya hakimiliki ikijumuisha makato kwa madhumuni ya huduma za kijamii, kiutamaduni na kielimu; na
(iii)ushughulikiaji wa malalamiko na taratibu za utatuzi wa migogoro zilizopo au kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha; na
(f)ripoti za kila mwaka za kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na hesabu zilizokaguliwa.

Sehemu ya nne – Utatuzi wa malalamiko na usuluhishi wa migogoro

[Tafadhali kumbuka: nambari imenakilliwa kama ilivyo katika hati asili.]

39. Utatuzi wa malalamiko

(1)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (3), wafuatao wanaweza kuwasilisha malamiko kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha-
(a)mwanachama wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha;
(b)mmiliki wa hakimiliki ambaye siyo mwanachama wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha lakini ambaye ana uhusiano nayo kisheria, kikazi, kwa mujibu wa leseni au utaratibu mwingine wa kimkataba;
(c)kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo inasimamia hakimiliki kwa niaba yake chini ya makubaliano ya uwakilishi; au
(d)mtumiaji.
(2)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itaweka utaratibu madhubuti wa ushughulikiaji wa malalamiko, na ambao utatuzi wake utakuwa wa muda mfupi.
(3)Malalamiko ambayo yanaweza kuwasilishwa na ambayo yatajumuishwa katika taratibu zitakazowekwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha yatahusu hasa—
(a)uidhinishaji wa kusimamia hakimiliki;
(b)kufutwa au kuondolewa kwa hakimiliki;
(c)masharti ya uanachama;
(d)ukusanyaji wa kiasi kinachostahili kulipwa cha wenye hakimiliki;
(e)makato na migawanyo;
(f)huduma inayotolewa; na
(g)mwenendo wa watumishi wa kampuni kwa wanachama wakati wa kutoa leseni.
(4)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha inayopokea malalamiko itamjibu malalamikaji kwa maandishi, na kutoa sababu endapo itayakataa malalamiko hayo.
(5)Kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ili kuwepo kwa haki ya kusikilizwa, itatathmini iwapo migogoro inayotajwa katika kanuni ndogo ya (2) inastahili kuwasilishwa kwa utaratibu huru na usio na upendeleo wa usuluhishi mbadala wa migogoro:Isipokuwa kwamba, chaguo la uwasilishaji kwa utaratibu huru na usio na upendeleo wa usuluhishi mbadala wa migogoro litakuwa ni kwa hiari ya wahusika katika mgogoro.

40. Usuluhishi

(1)Mtu asiyeridhishwa na uamuzi au tendo la kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ndani ya siku thelathini tangu tarehe ya uamuzi kutolewa au kitendo hicho kufanyika, anaweza kuwasilisha maombi ya usuluhishi kwa Ofisi kupitia Fomu CMO 05 iliyoainishwa katika Jedwali la Kanuni hizi, na baada ya malipo ya ada iliyowekwa.
(2)Notisi ya maombi ya usuluhishi iliyorejewa katika kanuni ndogo ya (1) itaambatishwa na—
(a)taarifa ya maelezo inayoainisha mazingira ambayo nafuu inaombwa, na maelezo ya utetezi yanayotegemwa na mwasilisha maombi;
(b)nakala ya uamuzi wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kama ipo;
(c)nakala za nyaraka yoyote inayotegemewa kutumika kama uthibitisho wakati wa usikilizwaji wa shauri.
(3)Baada ya kupokea notisi ya maombi ya usuluhishi, Ofisi itatoa au kusababisha kutolewa kwa taarifa ikiwataka wahusika wa mgogoro kufika katika Ofisi kwa ajili ya kusikilizwa katika tarehe iliyopangwa kwenye taarifa, ambayo haitazidi siku thelathini tokea tarehe ambayo notisi iliwasilishwa.

41. Kamati ya uamuzi

(1)Kutakuwa na kamati ya uamuzi ya Ofisi ambayo itakuwa na jukumu la kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa katikia Ofisi kwa mujibu wa kanuni ya 40.
(2)Kamati ya uamuzi itakuwa na mwenyekiti ambaye ni Msimamizi wa Hakimiliki au mtu atakayeteuliwa na Msimamizi wa Hakimiliki na wajumbe angalau wasiopungua watatu lakini wasiozidi watano wanaoteuliwa na Msimamizi wa Hakimiliki.
(3)Kikao cha kamati kitaongozwa na mwenyekiti au mjumbe aliyeteuliwa kwa madhumuni hayo.
(4)Akidi ya kikao cha kamati ya usuluhishi katika shauri lolote itakua imetimia ipasavyo iwapo kutakuwa na angalau nusu ya wajumbe.

42. Uamuzi wa kamati ya uamuzi

(1)Uamuzi wa kamati ya uamuzi ndiyo utakuwa uamuzi wa Ofisi na ambao utakuwa kwa maandishi, utakaoamuliwa na wajumbe walio wengi ndani ya siku thelathini kuanzia siku ya kufunga usikilizaji wa shauri, na kusomwa kwa watu wote.
(2)Uamuzi utajumuisha—
(a)aina ya malalamiko;
(b)majina ya pande zote mbili;
(c)agizo au uamuzi na sababu za kufanya hivyo; na
(d)nafuu au urekebishwaji ambao mdaawa anastahili kupata.
(3)Wajumbe wa jopo, ukiondoa mjumbe yeyote asiyekubaliana, watasaini uamuzi huo.

43. Rufaa dhidi ya uamuzi uliotokana na usuluhishi

(1)Mtu ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa Ofisi katika usuluhishi, anaweza kukata rufaa kwa Waziri, ndani ya siku thelathini tangu uamuzi kutolewa.
(2)Rufaa itawasilishwa kwa maandishi ikiainisha sababu za rufaa hiyo.
(3)Waziri baada ya kuzisikiliza pande zote mbili, yeye mwenyewe au kwa maandishi anaweza kuhakikisha jambo hili na kutoa uamuzi wake.

Sehemu ya sita – Kuzingatia masharti

44. Uhitaji wa taarifa

(1)Ofisi inaweza, kwa notisi ya maandishi—
(a)kuitaka kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au mwanachama;
(b)kumtaka mwenye hakimiliki au chombo kinachowakilisha maslahi ya wenye hakimiliki; au
(c)kumtaka mtumiaji wa chombo kinachowakilisha maslahi ya watumiaji,
kutoa taarifa au nyaraka ziazotakiwa katika notisi katika muda na mahali na katika muundo na namna iliyotajwa kwenye notisi.
(2)Hakuna chochote katika Kanuni hizi kinachoipa Ofisi mamlaka yoyote ya kumtaka mtu atoe taarifa zozote au nyaraka ambazo mtu angeweza kustahili kukataa kuzitoa—
(a)kwa sababu za kulinda mawasiliano ya siri kati ya wakili na mteja wake;
(b)taarifa ambazo ni za siri, mfano taarifa za siri za biashara; au
(c)taarifa zozote ambazo kutolewa kwake kunalindwa au vinginevyo kunazuiwa na sheria nyingine yoyote.

45. Notisi ya kutozingatiwa kwa masharti

(1)Ofisi inaweza kutoa notisi ya kutozingatiwa kwa masharti kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo imeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni hizi.
(2)Notisi ya kutozingatia masharti itakuwa kwa maandishi na—
(a)itaeleza kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo haijazingatia masharti ya Kanuni hizi;
(b)itataja masharti husika na kueleza vitendo au kutotenda ambako ni ukiukwaji wa masharti husika; na
(c)itaitaka kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, kutekeleza masharti inayokiuka ndani ya muda kama ambavyo notisi itataja, na kuitaka kampuni kutoa ushahidi kwamba imetii na haiendelei na ukiukwaji.
(3)Ofisi, itakapoona inafaa, inaweza—
(a)kuitaka kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kutoa maelezo ya maandishi kwamba kutozingatia masharti hakutarudiwa; na
(b)kuipa onyo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha kwamba iwapo kampuni haitazingatia notisi, au iwapo kampuni inashindwa kutekeleza maelezo yake katika maandishi yaliyotolewa kuhusiana na notisi ya kuzingatia masharti, hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa Sheria au Kanuni hizi.
(4)Ofisi inaweza kuondoa taarifa ya uzingatiaji wa masharti na kwa kufanya hivyo itaipa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha taarifa ya kuiondoa.
(5)Endapo taarifa ya kutofuata uzingatiaji imetolewa, hakuna hatua ya kutoa adhabu chini ya Kanuni hizi itakayochukuliwa kuhusiana na kushindwa huko isipokuwa kama kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo imepewa—
(a)imeshindwa kufuata taarifa ya uzingatiaji wa masharti; au
(b)kuzingatia kwa maelezo ya maandishi yaliyotolewa kuhusiana na taarifa ya uzingatiaji.

46. Adhabu kulipa fedha kutokana na ukiukwaji

(1)Kwa kuzingatia kanuni ya 45(5), Ofisi inaweza kutoa adhabu ya kulipa fedha kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ambayo Ofisi inaridhika kwamba kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha imeshindwa kuzingatia majukumu yake kwa mujibu wa Sheria au Kanuni hizi.
(2)Adhabu chini ya kanuni ndogo ya (1) inaweza pia kuwekwa kwa mkurugenzi, meneja au afisa wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha.
(3)Kiasi cha adhabu ya kulipa fedha kitakuwa ni kiasi ambacho Ofisi itaona kinafaa.
(4)Katika kuamua ni kiasi gani kinafaa, Ofisi itazingatia aina ya ukiukwaji wa masharti.
(5)Adhabu ya fedha inaweza kujumuisha ama—
(a)jumla ya kiasi kisichopungua shilingi milioni mbili; au
(b)jumla ya kiasi kisichopungua shilingi milioni mbili kwa pamoja na kiasi kisichozidi shilingi laki moja kwa kila siku ambayo mtu alitetajwa katika kanuni ndogo ya (2) anaendelea kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(6)Adhabu ya fedha italipwa kwa Ofisi.

47. Taratibu za utoaji wa adhabu ya fedha

(1)Adhabu ya fedha chini ya kanuni ya 45 itatolewa kwa notisi na Ofisi kwa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ikieleza—
(a)kwamba Ofisi imetoa adhabu;
(b)kiasi cha adhabu;
(c)vitendo au kutotenda ambako Ofisi inaona kunakiuka Sheria na Kanuni hizi;
(d)masharti ya Sheria au Kanuni hizi ambazo Ofisi inaona zikakiukwa;
(e)maelezo mengine yoyote ambayo Ofisi inaona yanathibitisha utoaji wa adhabu; na
(f)kipindi ambacho kitakuwa sio chini ya siku ishiriki na nane kuanzia tarehe ambayo mtu alipokea taarifa hiyo, ambapo adhabu inatakiwa kulipwa.
(2)Bodi inaweza kufuta adhabu ambayo imetolewa katika kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha na kuipa kampuni hiyo taarifa ya maandishi ya kufutwa huko.

48. Rufaa dhidi ya utozwaji wa adhabu ya fedha

(1)Endapo kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha au mtu ambaye amepewa adhabu hakuridhika na utolewaji wa adhabu au kiasi cha adhabu, kampuni inaweza kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana na Hakimiliki ndani ya siku ishirini na nane baada ya kupewa adhabu.
(2)Rufaa iwe katika maandishi ikijumuisha sababu za rufaa.
(3)Waziri, baada ya kuzisikiliza pande zote mbili, iwe ana kwa ana au kwa maandishi, anaweza kuamua jambo hilo na kutoa uamuzi wake.

49. Kutolipa adhabu wakati wa kusubiri rufaa

Endapo rufaa au hatua ya mahakama inatolewa dhidi ya uamuzi wa ofisi, upande unaowasilisha rufaa haulazimiki kulipa adhabu wakati wa kusubiri mashauri na uamuzi wa rufaa na adhabu hiyo ya kulipa haitatekelezwa wakati wa kusubiri rufaa.

Sehemu ya saba – Masharti mengineyo

50. Fidia ya kutotumia leseni

Kila kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha itatoa fidia au utaratibu ambao utatumika ikitokea mtumiaji hawezi kutumia leseni aliyopewa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha, ambapo tukio hilo litakuwa limetokana na uzembe, uwasilishaji usio sahihi au kasoro nyingine zinazotokana na hilo au kusababishwa na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha.

51. Hatua dhidi ya maafisa wa kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha

(1)Endapo kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha zimebainika kukiuka sehemu yoyote ya Kanuni hizi au Sheria au imeelekezwa kuchukua hatua yoyote au endapo vikwazo vimewekwa kwao na Ofisi, na kampuni ya kukusanya na kugawa mirabaha ikashindwa kutekeleza au kuondoa kikwazo ndani ya muda maalumu uliobainishwa na Ofisi, maafisa wa usimamizi wa kampuni wanaweza kuwajibika kwa kupewa onyo la maandishi.
(2)Afisa yeyote wa kampuni ambaye amepewa onyo zaidi ya mara moja anaweza kufutiwa sifa ya kufanya shughuli zozote za usimamizi na Ofisi katika kampuni yoyote ya kukusanya na kugawa mirabaha isipokuwa kama atairidhisha Ofisi kwa kutoa sababu za msingi za kutofutiwa sifa ya usimamizi au hatua ya uondoaji wa sifa ifutwe.

52. Kanuni za kampuni

Kampuni inaweza kutengeneza kanuni za ustawi wa wanachama wake na kutenga si zaidi ya asilimia tano ya mirabaha yake yote iliyokusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa kanuni kwa ufanisi, na kiasi hicho hakipaswi kugawanywa kwa watu wasiohusika kwa mujibu wa kanuni ya 30.

53. Kufutwa kwa kanuni na masharti ya mpito

(1)Kanuni za Hakimiliki na Hakishiriki (Leseni za Maonyesho ya Umma na Unufaikaji wa Mauzo Endelevu) za Mwaka 2022 zimefutwa.
(2)Bila kujali kifungu kidogo cha (1), masharti kuhusu haki za maonyesho ya umma na unufaikaji wa mauzo endelevu chini ya kanuni zilizofutwa yataendelea kutumika hadi tangazo kwa umma litakapochapishwa kwa mujibu wa kanuni ya 13(2) ya Kanuni hizi.
[TS. Na. 137 la 2022]

Jedwali

Fomu

[Angalizo la mhariri: Fomu hazijatolewa tena.]
▲ To the top

History of this document

24 March 2023 this version
06 March 2023
Assented to