Kanuni za Matumizi ya Madini ya Risasi za Mwaka 2023

Government Notice 287 of 2023

Kanuni za Matumizi ya Madini ya Risasi za Mwaka 2023

Tanzania
Factories Act

Kanuni za Matumizi ya Madini ya Risasi za Mwaka 2023

Tangazo la Serikali 287 ya 2023

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 109]

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Matumizi ya Madini ya Risasi za Mwaka 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—"madini ya risasi" maana yake ni madini ya risasi, mchanganyiko wa vitu na madini ya risasi na viambata vya madini ya risasi ambavyo vinaweza kufyonzwa kwa njia yeyote na binadamu;"Mamlaka ya Ukaguzi iliyoidhinishwa" maana yake ni Mamlaka ya Ukaguzi iliyoidhinishwa kwa ajili ya—
(a)ufuatiliaji wa viwango vya madini ya risasi katika hewa, au
(b)uchambuzi wa viwango vya madini ya risasi katika damu au mkojo;
"rangi yenye madini ya risasi" maana yake ni rangi yoyote yenye madini ya risasi inayoweza kupulizwa, kupakwa au kubandikwa;"Sheria" maana yake ni Sheria ya Afya na Usalama Mahali Pa Kazi;[Sura 297]mamlaka” maana yake ni Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi;tetra-alkyl” maana yake ni kiambata cha kemikali kwenye madini ya risasi;ufuatiliaji wa kibaiolojia” maana yake ni kupima kiwango cha madini ya risasi kwenye damu au mkojo;"vifaa kinga vya kupumulia" maana yake ni kifaa ambacho huvaliwa angalau mdomoni na puani ili kuzuia kuvuta hewa ambayo si salama, na ambacho kimeidhinishwa na Mamlaka; na"viwango vya afya na usalama" maana yake ni viwango vya afya na usalama kama vilivyoainishwa chini ya Kanuni hizi.

3. Matumizi

Kanuni hizi zitatumika kwa kila mwajiri na mtu aliyejiajiri ambapo madini ya risasi yanazalishwa, yanachakatwa, yanatumiwa, yanashikwa au kuhifadhiwa katika hali ambayo inaweza kuvutwa, kumezwa au kufyonzwa na mtu yeyote katika sehemu hiyo ya kazi.

4. Taarifa kuhusu mafunzo

(1)Mwajiri yoyote anayejihusisha na kazi zinazohusiana na madini ya risasi baada ya kushauriana na Kamati ya Afya na Usalama iliyoundwa, atatakiwa kuwapa wafanyakazi taarifa na mafunzo kuhusiana na—
(a)vyanzo vinavyoweza kusababisha kukumbwa na madini ya risasi;
(b)hatari ya kiafya inayoweza kusababishwa na kukumbwa na madini ya risasi, ikijumuisha hatari za kiafya kwa familia za wafanyakazi na wengine, ambao wanaweza kuathirika kutokana na vifaa au nguo zilizotumika kazini kupelekwa nyumbani;
(c)tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na mfanyakazi kumkinga dhidi ya hatari za kiafya zinazotokana na kukumbwa na madini ya risasi, ambazo zinajumuisha kuvaa na kutumia vifaa kinga;
(d)umuhimu, matumizi sahihi, matunzo na uwezo wa vifaa kinga, vifaa na hatua za udhibiti wa uhandisi zinazotolewa;
(e)tathmini ya kukumbwa na madini ya risasi, madhumuni ya kuchukua sampuli za hewa, umuhimu wa ufuatiliaji wa afya za wafanyakazi na faida za muda mrefu za kufanyiwa ufuatiliaji wa kiafya;
(f)muda wa kazi na kiwango cha ukomo wa kukumbwa na madini ya risasi;
(g)taratibu salama za ufanyaji kazi kuhusu utumiaji, utunzaji, usindikaji, uhifadhi na utupaji wa kitu au bidhaa yoyote iliyo na madini ya risasi, ili kupunguza uenezaji wa madini ya risasi nje ya eneo la kazi; na
(h)taratibu zinazopaswa kufuatwa katika tukio la kusambaa kwa madini ya risasi au dharura nyingine yoyote.
(2)Mafunzo ya rejea yatatolewa kuhusu masuala yanayokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) angalau kila mwaka au mkaguzi atakavyoelekeza.
(3)Mafunzo yatatolewa na mtu ambaye ana weledi na anayetambuliwa na Mamlaka kutoa mafunzo hayo.
(4)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba anatoa taarifa na maelekezo yanayohusiana na kukumbwa na madhara ya madini ya risasi kwa mtu yeyote atakayefika katika eneo lake la kazi.
(5)Mwajiri atatoa maelekezo kwa maandishi ya taratibu zinazokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1)(h) kwa madereva wa magari yanayobeba madini ya risasi ambayo yana uwezekano wa kusababisha uchafuzi wa mazingira au kuleta athari kwa watu.

5. Wajibu wa watu wanaoweza kukumbwa na madini ya risasi

Mtu yeyote ambaye amekumbwa au anayeweza kukumbwa na madini ya risasi mahali pa kazi, atatii maagizo yoyote halali yanayotolewa na mwajiri au mwakilishi wake au mtu aliyejiajiri, kuhusu—
(a)kuvaa na kutumia vifaa kinga;
(b)uvaaji wa vifaa vya ufuatiliaji ili kupima kiwango cha kukumbwa na madini ya risasi kilichopo katika hewa;
(c)mpangilio wa mazingira ya kazi, usafi binafsi na taratibu za utunzaji afya na mazingira; na
(d)mafunzo na maelekezo yaliyotolewa kama ilivyokusudiwa katika kanuni ya 4.

6. Tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na madini ya risasi

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na madini ya risasi katika eneo la kazi inafanywa na mamlaka iliyoidhinishwa, ili kubaini kama mtu yeyote anaweza kuwa katika hatari ya kukumbwa na madini ya risasi; na
(b)taarifa ya tathmini iliyotajwa katika kanuni ndogo ya 1(a) itawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu.
(2)Mwajiri kabla ya kufanya tathmini, atashauriana na Kamati ya Afya na Usalama ili kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na madini ya risasi.
(3)Wakati wa kufanya tathmini inayokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) mwajiri au mtu aliyejiajiri atazingatia—
(a)uwepo wa madini ya risasi ambayo mtu anaweza kukumbwa nayo;
(b)mahali yalipo, muundo wa madini ya risasi na kiwango ambacho mtu anaweza kukumbwa nacho;
(c)kazi zinazofanyika na uwezekano wa kushindwa kwa hatua za udhibiti; na
(d)maelezo ya kukumbwa yanayotarajiwa—
(i)kama madhara ni juu ya kikomo cha kukumbwa na madini ya risasi, ilikuweza kuchagua vifaa kinga sahihi vya kupumulia wakati hatua za udhibiti wa kihandisi ukisubiriwa;
(ii)endapo kukumbwa na madini ya risasi kama hayo ni ya nyakati tofauti, mzunguko wa kujirudia na muda wa kukumbwa;
(iii)idadi ya wafanyakazi waliopo katika mazingira ya kukumbwa na madini ya risasi na mtu mwingine yeyote ambaye anaweza kuwa katika mazingira hayo; na
(iv)pale inapohitajika, matokeo ya ufuatiliaji wa awali wa madini ya risasi uliofanyika mahali pa kazi yanapatikana.
(e)hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupunguza kukumbwa na madini ya risasi katika kiwango cha chini kabisa kinachowezekana na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupunguza viambata hewa vya madini ya risasi kwenda kwenye mazingira;
(f)taratibu za kushughulikia dharura; na
(g)taratibu za uondoaji wa taka zenye madini ya risasi kutoka mahali pa kazi.
(4)Pale ambapo tathmini au mapitio ya tathmini yaliyofanyika kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (1) na (5) yanaonesha kwamba, mtu yeyote anaweza kukumbwa na madini ya risasi, mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kukumbwa kunadhibitiwa kama inavyoelekezwa katika kanuni ya 11.
(5)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atapitia tathmini iliyowekwa katika kanuni ndogo ya (1) endapo—
(a)kuna sababu ya kuamini kwamba tathmini ya awali haifai tena;
(b)hatua za udhibiti hazina ufanisi tena;
(c)maendeleo ya kiteknolojia au kisayansi yanaruhusu mbinu bora zaidi za udhibiti; au
(d)kumekuwa na mabadiliko makubwa katika—
(i)taratibu za kufanya kazi;
(ii)aina ya kazi iliyofanywa; au
(iii)aina ya vifaa kinga vinavyotumika kudhibiti kukumbwa na kanuni ndogo za (2) na (3) zitatumika.

7. Ufuatiliaji wa afya

(1)Mwajiri atahakikisha kwamba mfanyakazi anakuwa chini ya ufuatiliaji wa afya wa mkaguzi wa afya mahali pa kazi ikiwa—
(a)mfanyakazi amekumbwa na viambata hewa vya madini ya risasi kwa kiwango zaidi ya kikomo cha kukumbwa na madini ya risasi kazini;
(b)mfanyakazi amekumbwa na madini ya risasi ya tetra-alkyl; na
(c)mkaguzi wa afya aliyeidhinishwa amethibitisha kwamba mfanyakazi husika anapaswa kuwa chini ya ufuatiliji wa afya.
(2)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (1), mwajiri atahakikisha kwamba—
(a)uchunguzi wa awali wa afya unafanyika mara tu, au ndani ya siku kumi na nne baada ya mtu kuanza kazi;
(b)kuzingatia kanuni ndogo ya (2)(a) pale ambapo madini ya risasi tofauti na madini ya risasi ya tetra-alkyl yanahusika, kipimo cha madini ya risasi ya damu ya mfanyakazi na kiwango cha hemoglobini kitafanyika kama ilivyoainishwa katika Sehemu A ya Jedwali;
(c)kipimo cha haraka cha mkusanyiko wa madini ya risasi kwenye mkojo kwa wafanyakazi waliokumbwa na madini ya risasi yenye tetra-alkyl na baada ya hapo kwa vipindi kama ilivyoainishwa katika Sehemu B ya Jedwali; na
(d)uchunguzi wa afya na vipimo vya kibaiolojia vya afya husika vitafanyika kwa kuzingatia maelekezo ya mkaguzi wa afya mahali pa kazi aliyeidhinishwa.
(3)Mwajiri atahakikisha kuwa hakuna mwajiriwa aliyethibitishwa na mkaguzi wa afya mahali pa kazi, kuwa hatakiwi kufanya kazi katika eneo analokumbwa na madini ya risasi anarejea kazini, hadi mkaguzi wa afya mahali pa kazi athibitishe kwa maandishi kwamba mfanyakazi anaweza kufanya kazi hiyo.
(4)Mwajiri atahakikisha kuwa—
(a)mfanyakazi wa kike ambaye ana uwezo wa kuzaa na anafanya kazi inayomuweka katika kukumbwa na madini ya risasi, anaondolewa kwenye kazi hiyo wakati mkusanyiko wake wa damu unazidi 40μg/100 mℓ au kiwango cha madini ya risasi kwenye mkojo unazidi 75μg/ℓ, au endapo ana ujauzito; na
(b)mfanyakazi anayetajwa katika kanuni ndogo ya (4)(a) haruhusiwi kurejea katika kazi ambayo itamweka katika kukumbwa na madini ya risasi, isipokuwa kama kiwango chake cha madini ya risasi katika damu ni chini ya 30μg/100 mℓ au kiwango cha madini ya risasi kwenye mkojo ni chini ya 65μg/ℓ, au endapo kuondolewa kulitokana na ujauzito, mfanyakazi hana ujauzito tena.

8. Ukanda wa kuvaa kifaa kinga cha kupumulia

Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)mahali pa kazi au sehemu ya mahali pa kazi ambapo kiwango cha madini ya risasi katika hewa kipo au kinaweza kuwa kikubwa zaidi ya kikomo cha kukumbwa na madini hayo endapo mtu hajavaa kifaa kinga cha kupumulia, itengwe kama ukanda wa kuvaa kifaa kinga cha kupumulia;
(b)eneo lililotengwa la ukanda wa kuvaa vifaa kinga vya kupumulia linawekwa ishara za usalama zinazoonesha kwamba eneo husika ni ukanda wa kuvaa kifaa kinga cha kupumulia kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 12;
(c)hakuna mtu anaingia au kufanya kazi katika ukanda wa kuvaa vifaa kinga vya kupumulia bila kuwa amevaa vifaa kinga husika; na
(d)sababu ya kuongezeka kwa kiwango cha madini ya risasi katika hewa inatambuliwa na hatua za haraka zinachukuliwa mbali na kuvaa vifaa kinga vya kupumulia ili kupunguza kiwango cha madini ya risasi chini ya kikomo.

9. Kumbukumbu

Mwajiri atatakiwa—
(a)kuweka kumbukumbu za matokeo ya tathmini zote, ufuatiliaji wa hewa, taarifa za uchunguzi wa afya na maboresho ya hatua za udhibiti zinazohitajika na kanuni za 6, 7 na 8 kwa muda usiopungua miaka thelathini:Isipokuwa kwamba, kumbukumbu binafsi za matibabu atapatiwa mkaguzi wa afya tu au endapo mfanyakazi ataruhusu kwa maandishi apatiwe mtu mwingine;
(b)kumpatia mkaguzi taarifa za tathmini zote na ufuatiliaji wa hewa ili kubaini kiwango cha kukumbwa na madini ya risasi;
(c)kutunza kumbukumbu zote za ufuatiliaji wa afya kwa muda usiopungua miaka thelathini na ikiwa mwajiri atasitisha shughuli anazofanya, akabidhi au awasilishe kumbukumbu zote kwa Mkaguzi Mkuu, kwa kuzingatia kwamba kumbukumbu hizo zitakuwa angalau na—
(i)jina la ukoo la mfanyakazi, majina ya awali, jinsia, tarehe ya kuzaliwa, jina la mwenzi wa ndoa au ndugu wa karibu zaidi na anwani ya kudumu;
(ii)kumbukumbu ya aina ya kazi iliyofanywa ambayo ilisababisha mfanyakazi kukumbwa na madini ya risasi, eneo ambalo wafanyakazi wamekumbwa, tarehe ya kuanza na kumaliza kazi husika, na muda wa kukumbwa na madini ya risasi katika masaa kwa wiki;
(iii)kumbukumbu ya kukumbwa na madini ya risasi inayohusiana na kazi ya awali kabla ya ajira ya sasa ya mfanyakazi; na
(iv)tarehe za ufuatiliaji wa afya na matokeo yake.
(d)kutunza kumbukumbu za mafunzo ya kinadharia na vitendo aliyopewa mfanyakazi kwa mujibu wa kanuni ya 4 kwa muda wote mfanyakazi atakapokuwa kwenye ajira.

10. Udhibiti wa kukumbwa na madini ya risasi

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kukumbwa na madini ya risasi katika mahali pa kazi kunazuiwa au kudhibitiwa vya kutosha, udhibiti huo utachukuliwa kuwa wa kutosha endapo—
(a)kiwango cha madini ya risasi katika hewa kipo chini ya kikomo cha kukumbwa na madini ya risasi kazini, au kama kipo juu ya kikomo, sababu imetambuliwa na hatua ya haraka tofauti na kugawa vifaa kinga vya kupumulia imechukuliwa ili kupunguza kiwango hicho; na
(b)ikiwa kuna hali ya kukumbwa na—
(i)madini ya risasi yanayoweza kumezwa, kiwango cha madini ya risasi ni chini ya 20μg/100 mℓ kwenye damu; au
(ii)madini ya risasi ya tetra-alkyl, kiwango cha madini ya risasi ni chini ya 120μg/ℓ kwenye mkojo.
(2)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atadhibiti uwezekano wa mtu kukumbwa na madini ya risasi kwa—
(a)kutumia mbadala wa madini ya risasi au bidhaa zenye mchanganyiko wa madini ya risasi;
(b)kupunguza au kudhibiti idadi ya watu wanaoweza kukumbwa na madini ya risasi;
(c)kupunguza muda ambao mtu atakumbwa au anaweza kukumbwa na madini ya risasi;
(d)kupunguza kiwango cha madini ya risasi ambacho kinaweza kuingia katika mazingira ya kazi;
(e)kuanzisha hatua za udhibiti wa kihandisi ili kupunguza kukumbwa na madini ya risasi kama—
(i)kutenganisha mchakato wa uzalishaji, kutumia mitambo peke yake au kufungia;
(ii)ufungaji wa mifumo ya kutoa hewa chafu karibu na chanzo ili kudhibiti uzalishaji wa madini ya risasi katika hewa;
(iii)kumwagia maji ili kupunguza vumbi lenye madini ya risasi;
(iv)kutenganisha maeneo ya kazi yenye uzalishaji tofauti; na
(v)utambuzi wa hatua za haraka za urekebishaji zinazopaswa kuchukuliwa.
(f)kuanzisha taratibu salama za maandishi za ufanyaji kazi ambazo mfanyakazi lazima azingatie ili kuhakikisha kuwa—
(i)madini ya risasi yanatumika na yanaondolewa mahali pa kazi kwa usalama;
(ii)mitambo ya uzalishaji, vifaa, zana, uchimbaji, na mifumo ya kutoa hewa chafu katika chanzo inatumiwa kwa usalama na kutunzwa; na
(iii)hatua sahihi za awali za kurekebisha udhibiti wa kukumbwa na madini ya risasi zinachukuliwa.

11. Vifaa kinga

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atatakiwa—
(a)Kuwapatia wafanyakazi na watu ambao wanaweza kukumbwa na madini ya risasi katika hewa katika kiwango kinachozidi nusu ya kikomo cha kukumbwa na madini ya risasi kazini, mavazi ya kazi ambayo hayana mifuko ili kupunguza uwezekano wa kubeba vumbi lenye madini ya risasi;
(b)kuhusiana na madini ya risasi ya tetra-alkyl ambayo yanaweza kufyonzwa kupitia ngozi, kumpa mtu vifaa kinga ambavyo havipitishi madini ya risasi kwenye ngozi; na
(c)kumpa vifaa kinga vya kupumulia ili kuhakikisha kuwa kukumbwa na madini ya risasi katika hewa kunadhibitiwa.
(2)Pale ambapo kifaa kinga cha kupumulia kimetolewa, mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)kifaa husika kinauwezo wa kuweka kiwango cha kukumbwa na madini ya risasi chini ya kikomo cha kukumbwa kazini kulingana na aina ya madini ya risasi;
(b)kifaa kinga sahihi kimechaguliwa kwa usahihi na kutumika ipasavyo;
(c)taarifa, maelekezo, mafunzo na usimamizi wa matumizi ya vifaa kinga inafahamika kwa watu; na
(d)vifaa vinawekwa katika hali nzuri na utaratibu mzuri wa kufanya kazi.
(3)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha—
(a)kutowapatia watu vifaa kinga ambavyo tayari vimetumika, isipokuwa kama vifaa hivyo vimesafishwa na kutakaswa kwa namna ambayo haitaruhusu madini ya risasi kuingia katika mazingira ya kazi; na
(b)kuwa sehemu ya kuhifadhia vifaa kinga wakati ambapo havitumiki.

12. Usafi wa majengo na mitambo

Kila mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha—
(a)sehemu zote za kazi zinawekwa katika hali ya usafi bila taka zenye madini ya risasi, na pale ambapo madini ya risasi yanapomwagika au kupeperushwa na upepo mahali pa kazi, hatua za kurekebisha zichukuliwe mara moja, kabla ya kazi yoyote kuendelea;
(b)usafi unafanyika na kifaa kinachoweza kuvuta uchafu chenye ufanisi wa kuchuja angalau asilimia 99 ya chembe zenye ukubwa wa maikromita moja, ili vumbi lenye madini ya risasi lisiingie hewani kuchafua mahali pa kazi au mazingira;
(c)vifaa vya kuvuta uchafu vinakarabatiwa na kusafishwa kwa wakati ili kuondoa vumbi la madini ya risasi; na
(d)pale ambapo matumizi ya vifaa vya kuvuta uchafu haiwezekani, sehemu zinazopaswa kusafishwa zinawekwa maji na watu wanaofanya usafi huo wanavaa mavazi sahihi na vifaa kinga vya kupumulia.

13. Kudumisha hatua za udhibiti

Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)vifaa vyote vya udhibiti vinatunzwa katika hali na mpangilio mzuri wa kufanya kazi; na
(b)hatua za udhibiti wa kihandisi zipimwe na zijaribiwe kila baada ya miezi kumi na mbili au itakavyoelekezwa na mkaguzi.

14. Kuweka lebo, ufungaji, usafiri na uhifadhi

Mwajiri au mtu aliyejiajiri, ili kuzuia usambaaji wa madini ya risasi atahakikisha kwamba—
(a)madini ya risasi yaliyohifadhiwa au kusambazwa yanatambulika ipasavyo, yanainishwa na kutumika kwa mujibu wa taratibu za afya na usalama; na
(b)kontena au gari ambalo madini ya risasi yanasafirishwa, limebainishwa bayana na kupakiwa kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.[Sura ya 177]

15. Mazuio

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri hataruhusu mtu yeyote kufanya kazi katika mazingira ambayo kiwango cha madini ya risasi kitazidi kiwango cha kikomo cha kukumbwa.
(2)Mtu yeyote hataruhusiwa—
(a)kutumia hewa iliyo katika mgandamizo kupuliza chembe chembe za madini ya risasi kutoka kwenye sehemu yoyote;
(b)kuvuta sigara, kula, kunywa au kuweka chakula au vinywaji ndani ya eneo ambalo halijatengwa mahususi kwa ajili hiyo; na
(c)kupaka rangi yenye madini ya risasi ndani ya majengo au samani, kufuta au kusugua rangi yenye madini ya risasi katika sehemu kavu au kuondoa rangi yenye madini ya risasi kwa kuchoma.

Jedwali (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 7(2)(b) na (c))

Sehemu ya A – Vipindi vya kuchukua vipimo vya kiwango cha madini ya risasi kwenye damu

Damu yenye madini ya risasi μg/100 mℓUkomo wa vipindi vya kuchukua vipimo vya madini ya risasi kwenye damu
chini ya 20miezi 12
20 - 39miezi 6
40 - 59miezi 3
60 na zaidiKwa maelekezo ya mkaguzi wa afya mahali pa kazi.

Sehemu ya B – Vipindi vya kuchukua vipimo vya kiwango cha madini ya risasi kwenye mkojo

Mkojo wenye madini ya risasi μg/ℓitaUkomo wa vipindi vya kuchukua vipimo vya madini ya risasi kwenye mkojo
chini ya 120wiki 6
120 - 149wiki 1
150 na zaidiKwa maelekezo ya mkaguzi wa afya mahali pa kazi.
▲ To the top

History of this document

07 April 2023 this version
03 April 2023
Assented to