Kanuni za Egonomia za Mwaka 2023

Government Notice 288 of 2023

Kanuni za Egonomia za Mwaka 2023

Tanzania
Factories Act

Kanuni za Egonomia za Mwaka 2023

Government Notice 288 of 2023

(sura ya 297)(Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 109)

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Egonomia za Mwaka 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—"egonomia utambuzi" maana yake ni kuboresha uhusiano kati ya vipengele vya utambuzi na utendaji.majeraha na matatizo ya misuli na mifupa” maana yake ni madhara ya mwili ambayo yanaathiri misuli, viungo, mishipa na mishipa ya fahamu kwa kusababisha maumivu, kufa ganzi, uvimbe au kupoteza utendaji kazi wake.mbunifu” maana yake ni—(a)mtu aliyebobea ambaye—(i)anakagua na kupitisha kazi iliyosanifiwa;(ii)anampangia mtu aliye chini yake ikiwemo mfanyakazi kutayarisha sanifu; au(iii)kubuni kazi zinazofanyika kwa muda mfupi, ikiwa ni pamoja na vitu vinavyohusika.(b)msanifu majengo au mhandisi anayechangia au kuwa na jukumu la jumla la kufanya sanifu;(c)mhandisi wa miundombinu ya jengo anayeandaa michoro ya kiufundi inayoainisha namna ya ufungaji na upachikaji wa mitambo isiyohamishika; au(d)mkadiriaji majenzi anayebainisha viwango vya vitu vinavyotakiwa.mfumo wa misuli na mifupa” maana yake ni mfumo wa mifupa, misuli na tishu unganishi ambao hulinda mwili wa binadamu na viungo vyake, na ndio msingi wa viungo kusogea na kufanya kazi;"mbobezi kuhusiana na egonomia" maana yake ni mtu ambaye—(a)kuhusiana na kazi inayotakiwa kufanywa, ana ujuzi, mafunzo na uzoefu unaohitajika katika nyanja ya egonomia; na(b)anaifahamu sheria na kanuni zinazotumika zilizoundwa chini ya Sheria."programu ya egonomia" maana yake ni utaratibu wa kutarajia, kutambua, kuchambua na kudhibiti visababishi hatari vya egonomia ya mwili na utambuzi, ambayo itajumuisha angalau utambuzi wa vihatarishi vya egonomia na tathmini ya hatari, udhibiti wa hatari, ufuatiliaji wa tathmini ya taarifa na mafunzo na ufuatiliaji wa afya;[Sura ya 297]Sheria” maana yake ni Sheria ya Afya na Usalama Mahali Pa Kazi;"tathmini ya hatari ya egonomia" maana yake ni mpango unaofanywa ili kubaini hatari yoyote ya kukumbana na vihatarishi vya egonomia mahali pa kazi ili kutambua hatua zinazohitajika kuchukuliwa, kuondoa, kupunguza au kudhibiti hatari hiyo;"utambuzi" maana yake ni utafsiri wa vichocheo kutoka kwenye mazingira na ndani ya mwili wa mtu ambapo Vichocheo hivi hupitishwa na viungo vya hisia mpaka kwenye ubongo; na"visababishi vya hatari vya egonomia" maana yake ni vitendo vinavyofanyika mahali pa kazi, mazingira ya kazi, au mchanganyiko, ambavyo vinaweza kusababisha au kuzidisha matatizo ya misuli na mifupa yanayohusiana na kazi.

3. Matumizi

Kanuni hizi zitatumika kwa—
(a)mwajiri au mtu aliyejiajiri ambaye anafanya kazi mahali ambapo panaweza kumuweka mtu yeyote kwenye visababishi hatari vya egonomia za mwili au egonomia utambuzi; na
(b)watu wanaosanifu, wanaotengeneza, wanaosimika au kusambaza mashine au vifaa vya kutumika kazini.

4. Taarifa na mafunzo

(1)Mwajiri, baada ya kushauriana na Kamati ya Afya na Usalama iliyoundwa mahali pa kazi chini ya usimamizi wake au wawakilishi wa afya na usalama walioteuliwa kwenye sehemu hiyo ya kazi au vitengo tofauti tofauti vya kazi, ataweka kwa ajili ya wafanyakazi wote, au watu wengine mbali na wafanyakazi, ambao wanaweza kuathiriwa na hatari za egonomia, mpango wa mafunzo unaojumuisha—
(a)maudhui na wigo wa matumizi ya Kanuni hizi;
(b)vyanzo vya kukumbana na visababishi vya hatari za egonomia;
(c)asili ya visababishi vya hatari za egonomia;
(d)hatari ya afya inayohusiana na visababishi vya hatari za egonomia;
(e)kiwango ambacho wanaweza kuwa katika hatari;
(f)vidhibiti hatari vilivyopo katika eneo la kazi;
(g)utoaji taarifa mapema za kutojisikia vizuri au dalili zinazohusiana kwa mwakilishi wa afya na usalama au mwajiri;
(h)tahadhari za kuchukuliwa na mfanyakazi kujilinda dhidi ya hatari za kiafya zinazohusiana visababishi vya hatari za egonomia;
(i)tathmini ya kukumbwa na vihatarishi vya egonomia, madhumuni ya ufuatiliaji, ulazima wa ufuatiliaji wa afya na faida za muda mrefu za ufuatiliaji wa afya; na
(j)utaratibu wa kutoa taarifa za kasoro katika mitambo au vifaa ambavyo vinaweza kusababisha majeraha ya misuli na mifupa.
(2)Mafunzo yanayokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) yataendeshwa kwa wafanyakazi wote waliopo kazini.
(3)Mafunzo ya kukumbushana yatafanywa kila mwaka au kwa vipindi ambavyo vinaweza kupendekezwa na Kamati ya Afya na Usalama au wawakilishi wa afya na usalama au mkaguzi.
(4)Mafunzo yanayokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) yatatolewa na mtu ambaye ni mbobezi wa masuala ya afya na usalama mahali pa kazi na ameidhinishwa na Mkaguzi Mkuu.
(5)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kadiri inavyowezekana kwamba, wafanyakazi wake au watu wengine ambao siyo wafanyakazi wake ambao wanaweza kuathiriwa na visababishi vya hatari za egonomia mahali pa kazi wanapewa taarifa, maelekezo na mafunzo ya kutosha.
(6)Mwajiri atatunza kumbukumbu za mafunzo yoyote ambayo mfanyakazi amepewa kwa mujibu wa kanuni hii.

5. Wajibu wa wanaoweza kukumbwa na visababishi hatari za egonomia

Mtu yeyote ambaye anakumbwa au anayeweza kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia atatii maelekezo yoyote halali aliyopewa na mwajiri au mtu aliyejiajiri au na mtu yeyote aliyeidhinishwa na mwajiri au mtu aliyejiajiri, kuhusu—
(a)utekelezaji wa hatua zilizopitishwa kudhibiti visababishi vya hatari za egonomia;
(b)kushirikiana na mwajiri katika kazi ya kutambua namna mfanyakazi anaweza kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia;
(c)kutoa taarifa mapema za kutojisikia vizuri au dalili zinazohusiana kwa mwakilishi wa afya na usalama au mwajiri;
(d)kutoa taarifa mara moja ya kasoro katika mitambo au vifaa vinavyoweza kusababisha majeraha na matatizo ya misuli na mifupa kwa mwakilishi wa afya na usalama au mwajiri;
(e)taarifa na mafunzo yaliyotolewa kama ilivyoainishwa katika kanuni ndogo ya 4.

6. Wajibu wa wasanifu, watengenezaji na wasambazaji

(1)Wasanifu wa mitambo, mashine, vifaa au vitu vya kutumika kazini watalazimika—
(a)kuondoa visababishi vya hatari za egonomia kwenye usanifu wa kifaa au endapo haiwezekani, kupunguza visababishi vya hatari za egonomia ambavyo wafanyakazi wanaweza kukumbwa navyo katika kutumia au mwingiliano na kifaa hicho wakati wa utendaji wa kazi;
(b)kutoa taarifa kuhusu visababishi vya hatari za egonomia zilizotambuliwa na udhibiti kwa mtengenezaji ili aweze kuchukua hatua wakati wa utengenezaji, na vyovyote vile inavyowezekana, kuondoa au kupunguza visababishi vya hatari za egonomia vilivyobakia wakati wa usanifu na kuhakikisha kuwa hakuna hatari mpya inayoletwa wakati wa mchakato wa utengenezaji; na
(c)kutoa taarifa kwa mtengenezaji au msambazaji, kama msanifu anatengeneza bidhaa kwa ajili ya watumiaji husika kuhusu visababishi vya hatari za egonomia ambavyo hajaweza kuondoa wakati wa usanifu na masharti yanayohitajika kwa matumizi salama.
(2)Watengenezaji wa mitambo, mashine, vifaa au vitu vya kutumika kazini watatakiwa—
(a)kutengeneza vitu au jengo au miundo mbinu ambayo ni salama;
(b)kutumia nyenzo ambazo hupunguza visababishi vya hatari za egonomia kuanzia wakati wa ujenzi, na wakati bidhaa zinatumiwa, na wakati wa kazi za mikono;
(c)kutumia na kupima hatua za usalama zilizoainishwa na msanifu katika utengenezaji; na
(d)kutoa taarifa kwa msambazaji, kwa watumiaji wanaohusika katika matumizi ya bidhaa kuhusu matumizi salama ya bidhaa na hatari ambazo hazijaondolewa katika hatua ya usanifu.
(3)Mtu yeyote anayesambaza au kuuza mitambo, mashine, vifaa au vitu kwa ajili ya matumizi ya kazini atatakiwa—
(a)kusambaza au kuuza bidhaa ambazo ni salama;
(b)kuuza bidhaa zinazoweza kusafirishwa, kupokelewa, kutunzwa na kushughulikiwa kwa usalama;
(c)kutoa maelezo na mafunzo kwa watumiaji watarajiwa wanaohusika katika kila matumizi yaliyotambuliwa ya bidhaa kuhusu masharti yanayohitajika kwa matumizi salama na visababishi vya hatari za egonomia ambayo havijaondolewa au kupunguzwa kadri inavyowezekana katika hatua za ubunifu, utengenezaji au uuzaji;
(d)kusimika vifaa au kujenga jengo kwa kutumia nyenzo salama na, kwa namna, na katika maeneo ambayo itahakikishwa kuwa nyenzo zinaendeshwa kwa usalama; na
(e)kuwasiliana na mtumiaji kuhusu matengenezo yanayohitajika ili kuhakikisha matumizi na uendeshaji.

7. Tathmini ya hatari za egonomia

(1)Mwajiri atatakiwa—
(a)kabla ya kuanza kwa kazi yoyote ambayo inaweza kuwaweka wafanyakazi katika visababishi vya hatari za egonomia, kuwepo tathmini ya hatari za egonomia inayofanywa na kuidhinishwa na Mamlaka; na
(b)kuweka matokeo ya tathmini ya hatari za egonomia kwenye kumbukumbu kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 11.
(2)Tathmini ya hatari inayotajwa katika kanuni ndogo ya (1) itajumuisha—
(a)utambuzi wa vihatarishi vya egonomia na visababishi vya hatari za egonomia ambavyo watu wanaweza kukumbana navyo;
(b)uchambuzi na tathmini ya visababishi vya hatari za egonomia na vihatarishi vilivyotambuliwa kupitia nyaraka mbalimbali;
(c)mpango na utaratibu salama wa kazi unaotumika ili kupunguza au kudhibiti visababishi vya hatari za egonomia na vihatarishi ambavyo vimetambuliwa;
(d)ufuatiliaji wa mpango kazi; na
(e)mapitio ya mipango.
(3)Mwajiri atahakikisha kwamba wafanyakazi wote walio chini ya usimamizi wake wanafahamishwa, wanaelekezwa na kufundishwa na mtaalamu kuhusu vihatarishi vyovyote na taratibu zinazohusiana na kazi na; au hatua za kudhibiti kabla ya kazi kuanza; na baada ya kazi kuanza kulingana na mpango wa ufuatiliaji wa tathmini ya hatari na mapitio.
(4)Mwajiri atapitia tathmini ya hatari za egonomia iliyofanywa kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (1) endapo—
(a)kuna sababu ya kuamini kwamba tathmini hiyo haikidhi mahitaji;
(b)hatua za udhibiti hazina ufanisi;
(c)maendeleo ya kiteknolojia au kisayansi yanaruhusu mbinu bora zaidi za udhibiti;
(d)kama mabadiliko yanaathiriwa kwa namna ambayo kazi inayofanywa inaweza kuleta mabadiliko ya visababishi vya hatari ya egonomia; au
(e)kama kuna tukio limetokea.

8. Udhibiti wa hatari

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba mtu kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia vinazuiwa au, ikiwa haiwezekani, vinadhibitiwa ipasavyo.
(2)Kwa madhumuni ya kutekeleza kanuni ndogo ya (1), mwajiri au mtu aliyejiajiri atatakiwa, kwa kadri inavyowezekana, kuondoa au kupunguza uwezekano wa kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia kwa kutekeleza hatua za udhibiti katika mpangilio ufuatao wa kipaumbele—
(a)hatua za udhibiti wa kihandisi ili kuondoa au kupunguza visababishi vya hatari; na
(b)hatua za udhibiti za kiutawala kupunguza idadi ya watu na muda wa kukumbwa na hatari.

9. Ufuatiliaji wa afya

(1)Mwajiri atahakikisha kuwa mfanyakazi anafanyiwa ufuatiliaji wa afya endapo—
(a)matokeo ya tathmini yanaonesha kwamba mfanyakazi amekumbwa na visababishi vya hatari za egonomia kwa kiasi kikubwa;
(b)kuathiriwa kwa wafanyakazi na visababishi vya hatari za egonomia ni kama vile—
(i)ugonjwa unatambulika au athari mbaya ya kiafya inaweza kuhusishwa na kukumbana na visababishi vya hatari za egonomia;
(ii)kuna uwezekano wa kutosha kwamba ugonjwa au athari za kiafya zinaweza kutokea katika hali fulani mahali pa kazi na kuna mbinu za kugundua dalili za ugonjwa au athari za kiafya kadiri inavyowezekana; au
(iii)mtaalamu wa afya ya mazingira ya kazi amependekeza kwamba wafanyakazi husika wanapaswa kuwa chini ya ufuatiliaji wa afya katika hali ambayo mwajiri anaweza kumwita mtaalamu wa afya wa magonjwa yanayotokana na kazi kuridhia usahihi wa mapendekezo hayo.
(2)Mwajiri atahakikisha kwamba ufuatiliaji wa afya unaokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) unajumuisha—
(a)tathmini ya awali ya afya kwa wafanyakazi wapya kabla ya kuanza ajira au ndani ya siku kumi na nne baada ya mtu kuanza ajira ya kazi hatarishi, au kwa wafanyakazi wengine wote katika ajira, ndani ya miezi ishirini na nne ya tarehe ya kuanza kwa kanuni hii, hii inajumuisha—
(i)tathmini ya historia ya afya na kazi aliyokuwa anafanya;
(ii)uchunguzi wa mwili; na
(iii)uchunguzi mwingine wowote muhimu ambao kwa maoni ya daktari wa magojwa yatokanayo na kazi ni muhimu kuwezesha tathimini ipasavyo;
(b)tathmini ya mara kwa mara ya afya;
(c)dodoso za kutambua dalili kwa wafanyakazi walio katika kazi hatarishi, katika vipindi visivyozidi miaka miwili, au kwa vipindi vilivyoainishwa na daktari wa magonjwa yanayotokana na kazi; Isipokuwa kwamba ikiwa dalili zimeonekana, tathmini zaidi inapaswa kufanywa kama inavyokusudiwa katika Kanuni ndogo ya 2 (a) (ii) na (iii); na
(d)uchunguzi wa misuli na mifupa baada ya ajira kukoma.
(3)Mwajiri hatamruhusu mfanyakazi ambaye amethibitishwa kuwa hafai kufanya kazi na daktari wa magonjwa yanayotokana na kazi, kufanya kazi mahali pa kazi ambapo anaweza kukumbwa na vihatarishi vya egonomia, isipokuwa mfanyakazi husika anaweza kuruhusiwa kurudi katika kazi ambayo anaweza kukumbwa na vihatarishi vya egonomia iwapo atathibitishwa kuwa imara kuweza kufanya kazi hiyo na daktari wa magonjwa yanayotokana na kazi.
(4)Mwajiri atachunguza na kuweka kumbukumbu za matukio yote ambayo yanapelekea mfanyakazi kupata matatizo ya misuli na mifupa yanayohusiana na kazi.

10. Utunzaji wa vidhibiti

Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kitu chochote anachotoa kwa manufaa ya wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yake chini ya kanuni hizi—
(a)kinatumika kikamilifu na ipasavyo; na
(b)kinatunzwa katika hali ya ufanisi na katika utaratibu mzuri wa kufanya kazi.

11. Utunzaji wa kumbukumbu

Mwajiri au mtu aliyejiajiri atatakiwa—
(a)kutunza kumbukumbu za matokeo ya taarifa zote za tathmini na ufuatiliaji wa afya na utunzaji wa vidhibiti unaohitajika na kanuni hizi;
(b)kwa kuzingatia masharti Kanuni ndogo 1(c), kuweka kumbukumbu za taarifa za afya zinazokusudiwa katika Kanuni ndogo 1 (a) apatiwe mkaguzi wakati wa ukaguzi;
(c)kwa kuzingatia kibali rasmi cha maandishi cha mfanyakazi, kuruhusu mtu yeyote kusoma taarifa za afya kuhusiana na mfanyakazi husika;
(d)kuweka kumbukumbu za tathmini zote zipatikane kwa ajili ya kusomwa na mwakilishi husika wa afya na usalama au kamati husika ya afya na usalama;
(e)kutunza kumbukumbu zote za tathmini kwa muda usiopungua miaka thelathini;
(f)kutunza kumbukumbu zote za ufuatiliaji wa afya kwa muda usiopungua miaka thelathini, na ikiwa mwajiri atasitisha shughuli anazofanya, akabidhi au awasilishe kumbukumbu zote kwa Mkaguzi Mkuu; kwa kuzingatia kwamba kumbukumbu hizo zitakuwa na angalau taarifa zifuatazo:
(i)jina la ukoo la mfanyakazi, majina ya awali, jinsia, tarehe ya kuzaliwa, jina la mwenzi wa ndoa au ndugu wa karibu zaidi na anwani ya kudumu;
(ii)kumbukumbu ya aina ya kazi iliyofanywa ambayo ilisababisha mfanyakazi kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia, eneo ambalo wafanyakazi wamekumbwa na vihatarishi, tarehe ya kuanza na kumaliza kazi husika, na muda wa kukumbwa na hatari katika masaa kwa wiki;
(iii)kumbukumbu ya kukumbwa na visababishi vya hatari za egonomia vinavyohusiana na kazi ya awali kabla ya ajira ya sasa ya mfanyakazi; na
(iv)tarehe za ufuatiliaji wa afya na matokeo yake kuweka kumbukumbu ya mafunzo aliyopewa mfanyakazi kwa muda wote ambao yupo kwenye ajira ambapo anakumbwa na visababishi vya hatari za egonomia.
▲ To the top

History of this document

07 April 2023 this version