Kanuni za Mazingira ya Kazi za Mwaka 2023

Government Notice 289 of 2023

Kanuni za Mazingira ya Kazi za Mwaka 2023

Tanzania
Factories Act

Kanuni za Mazingira ya Kazi za Mwaka 2023

Tangazo la Serikali 289 ya 2023

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 109]

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Mazingira ya Kazi za Mwaka 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—balaklava” maana yake ni vazi linalofunika kichwa na shingo isipokuwa sehemu ya uso;Kielezo cha Halijoto ya Balbu Mnyevu (WBGT)” maana yake ni namba inayobainisha kiwango cha hali ya joto katika mazingira ya kazi;kifaa kinga cha upumuaji” maana yake ni kifaa ambacho huvaliwa kufunika angalau mdomo na pua ili kuzuia kuvuta hewa ambayo si salama;kiharusi cha joto” maana yake ni hali ya kiafya inayotokana na kushindwa kwa mwili wa binadamu kudhibiti joto;kipimo cha sauti (dBA)” maana yake ni kipimo cha kiwango cha sauti hewani kama inavyotambuliwa na masikio ya binadamu;kikomo cha dozi mahali pa kazi” kiwango cha juu cha kukumbwa na mionzi ayonishi kinachoruhusiwa ambacho kinapimwa katika mSv/mwaka au mrem/mwaka;kishikizi cha taa” maana yake ni kifaa kinachoshikilia taa na kuiunganisha na umeme;kukumbwa na vihatarishi kila siku” maana yake ni hali ya mfanyakazi kukumbwa na vihatarishi kuanzia masaa nane ya kazi kwa siku na kuendelea;kiwango cha kikomo cha ukumbwaji” maana yake ni kiwango cha ukumbwaji wa kila siku kilichowekwa katika kanuni za kazi ambacho hakipaswi kuzidi;kiwango cha ukumbwaji cha kuchukua hatua” maana yake ni kiwango cha ukumbwaji wa kila siku kilichowekwa katika kanuni za kazi yoyote ambacho kikifikiwa au kikizidi inahitaji hatua maalum ili kupunguza hatari;kiwango sawa cha shinikizo la sauti” maana yake ni kiwango sawa cha sauti inayoendelea kutoa kiasi sawa cha nguvu ya sauti kama sauti halisi inayobadilika badilika, inayopimwa kwa muda sawa;kuzoea” maana yake ni kuzoea hali ya mabadiliko ya viambata vya mazingira ambavyo mfanyakazi anakumbana navyo;mitetemo ya kiganja-mkono” maana yake ni mitetemo inayosababishwa na mashine ambayo hupitishwa kwenye kiganja na mikono wakati wa kazi;mtetemo wa mwili mzima” maana yake ni mtetemo unaosababishwa na mashine ambao hupitishwa ndani ya mwili mzima wa mfanyakazi akiwa amekaa au kusimama wakati wa kufanya kazi;mwanga” maana yake ni kiwango cha mwangaza kinachofika katika eneo la kazi, ambacho husomwa kwa kizio cha lux;mwangaza elekezwa” maana yake ni mwangaza ambao mionzi ya mwanga huwekwa kwenye mwalo mwembamba uliobainishwa vyema;sehemu kwa milioni/trilioni (ppm/ppt)” maana yake ni kizio cha ujazo wa kiambata cha hewa ya mahali husika;[Sura ya 297]Sheria” maana yake ni Sheria ya Afya na Usalama Mahali Pa Kazi;shughuli za ujenzi” maana yake ni ujenzi, urekebishaji wa miundo, ukarabati au matengenezo ya jengo, inajumuisha kupaka rangi, kupamba upya na usafi wa nje wa jengo, ubomoaji wa jengo na maandalizi ya uwekaji wa msingi wa jengo lililokusudiwa, lakini haijumuishi operesheni yoyote ambayo ni kazi za majenzi ya kihandisi;ukanda wa kelele” maana yake ni eneo ambalo kiwango cha kelele ni sawa au kinazidi kiwango cha katazo;uwanda wa kufanyia kazi” maana yake ni eneo la mlalo ambapo kazi inafanywa;uwezo wa kupunguza” maana yake ni uwezo uliothibitishwa wa vilinda usikivu ili kupunguza kiwango cha kelele ambacho mvaaji anakumbana nacho;vilinda usikivu” maana yake ni mofu za masikio au vizibo vya masikio vya viwango vinavyotambulika; nawastani wa kipimo kwa nyakati tofauti” maana yake ni wastani wa idadi ya vipimo wakilishi ambavyo huchukuliwa kwa kipindi cha muda fulani.

3. Matumizi

Kanuni hizi zitatumika mahali pa kazi na kwa mtu aliyejiajiri ambaye anatakiwa kumlinda mtu yoyote anayefika katika eneo lake la kazi.

4. Mahitaji ya hali joto

(1)Kwa mujibu wa masharti ya kanuni ndogo ya (2), mwajiri hatamruhusu mfanyakazi kufanya kazi katika mazingira ambayo wastani wa hali joto ya balbu kavu iliyopimwa kwa kipindi cha muda wa masaa manne ni chini ya nyuzi joto 6, isipokuwa mwajiri atachukua hatua zinazofaa kumlinda mfanyakazi huyo dhidi ya baridi na kuchukua tahadhari zote muhimu kwa usalama wa mfanyakazi huyo, isipokuwa pale ambapo kazi ya nje inafanywa, mwajiri atachukua hatua hizo na tahadhari kama hizo katika mazingira ambayo halijoto ya balbu kavu ni chini ya nyuzi joto 6 wakati wote.
(2)Mwajiri hatamruhusu mfanyakazi kufanya kazi katika mazingira ya jokofu ambapo kipimo cha hali joto ya balbu kavu iko chini ya nyuzi joto 0 isipokuwa—
(a)muda wa juu wa mfanyakazi kukumbwa na hali joto hauzidi muda ulioainisha katika Jedwali la Nne la Kanuni hizi.
(b)mfanyakazi amepewa mavazi ya kinga yafuatayo—
(i)suti ya nailoni ya kujikinga na baridi kali, ambapo halijoto iliyopimwa iko chini ya nyuzi joto hasi thelathini na nne, vazi hilo litakuwa la safu mbili;
(ii)balaklava ya sufi;
(iii)glavu za ngozi zenye manyoya;
(iv)glavu zisizopitisha maji zenye sufi iliyosokotwa kwa ndani na aproni isiyopitisha maji ambapo vitu vyenye unyevu au kuyeyushwa hushughulikiwa;
(v)soksi za sufí; na
(vi)buti zisizopitisha maji,
Isipokuwa kwamba, mfanyakazi anayefanya kazi katika eneo lenye halijoto ya chini ambayo halijoto yake si chini ya nyuzi joto hasi kumi na nane kwa muda usiozidi dakika tano katika kila saa anahitaji tu kupewa viatu vinavyofunika mguu.
(c)mfanyakazi kabla ya kuanza kufanya kazi, na baada ya hapo kila mwaka awe amethibitishwa anaweza kufanya kazi katika mazingira hayo kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria; na
(d)nguo zote zinazovaliwa na mfanyakazi zinatakiwa ziwe kavu kabla ya kuingia katika eneo la joto la chini.
(3)Mwajiri atatakiwa kufuatilia uingiaji kwenye vyumba vya baridi ili kuhakikisha wafanyakazi hawakai muda mrefu ili kupunguza madhara na mfumo wa udhibiti wa uingiaji unafuatwa.
(4)Pale ambapo zana zinazoshikiliwa kwa mkono ambazo hutetema kwa kasi ya mtetemo wa chini ya 1000 Hz hutumika kwenye halijoto halisi ya balbu kavu chini ya nyuzi joto sita, mwajiri atampa mfanyakazi anayeendesha zana hizo glavu mahususi kwa kazi hiyo.
(5)Endapo wastani wa kielezo cha halijoto ya balbu mnyevu (WBGT), iliyopimwa kwa muda wa saa moja inazidi thelathini (WBGT) katika mazingira ambayo mfanyakazi anafanya kazi, mwajiri huyo atatakiwa—
(a)kuchukua hatua za kupunguza kielezo cha halijoto hadi chini ya 30 cha balbu mnyevu (WBGT); au
(b)ikiwa imeshindikana kupunguza hadi chini ya thelathini ya kielezo cha balbu mnyevu (WBGT) na pale ambapo kazi ngumu ya mikono inafanywa—
(i)kila mfanyakazi kabla ya kuanza kufanya kazi, na baada ya hapo kila mwaka awe amethibitishwa anaweza kufanya kazi katika mazingira hayo na daktari aliyeidhinishwa, iwapo atathibitika kuwa ana uwezo wa kufanya kazi katika mazingira hayo, apewe cheti cha uthibitisho;
(ii)kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi huyo amezoea mazingira hayo ya kazi kabla ya kuhitajika au kuruhusiwa kufanya kazi katika mazingira hayo;
(iii)kumuelimisha kila mfanyakazi uhitaji wa kunywa angalau mililita mia sita za maji kila saa;
(iv)utoa mafunzo kwa kila mfanyakazi juu ya tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepuka kiharusi cha joto; na
(v)isipokuwa pale ambapo kuna walakini wa kuwepo kazi ngumu za mikono, mapendekezo ya mkaguzi yataamua.

5. Mwanga

(1)Kila mwajiri atahakikisha katika sehemu yake ya kazi kuna mwanga kulingana na viwango vya mwangaza kama vilivyoainishwa kwenye Jedwali la Kwanza, isipokuwa pale ambapo mwanga maalum ni muhimu kwa ajili ya utendaji wa aina fulani ya kazi, bila kujali kama aina hiyo ya kazi imeorodheshwa kwenye Jedwali au la, mwajiri atahakikisha wafanyakazi wanaofanya kazi hiyo wanakuwa kwenye mazingira yenye mwanga unaohitajika.
(2)Kuhusiana na mwanga uliotajwa katika kanuni ndogo ya (1), waajiri watahakikisha kwamba—
(a)wastani wa mwanga ndani ya mita tano kutoka sehemu ambapo mfanyakazi anafanya kazi usiwe chini ya moja ya tano ya wastani wa mwanga unaohitajika kwa kazi hiyo;
(b)uakisi mwanga katika sehemu yoyote ya kazi umepunguzwa hadi kiwango ambacho hakiathiri uwezo wa kuona;
(c)mwanga kwenye mashine zinazozunguka zenye hatari ya athari za mwanga unaowaka na kuzimika ziondolewe; na
(d)vishikizi vya taa na taa viwekwe safi na, vinapokuwa na kasoro, vibadilishwe au kurekebishwa mara moja.
(3)Kwa hali ya dharura inayohitaji kuondoka haraka eneo la kazi la ndani ambalo halina mwanga asilia au ambalo watu wanafanya kazi kwa kawaida usiku, kila mwajiri atatakiwa, katika sehemu hizo za kazi, kutoa vyanzo vya dharura vya mwanga ambavyo pale vinapowashwa, vinatoa mwanga usiopungua lux1, ili kuwezesha wafanyakazi kuondoka kwa haraka mahali pa kazi,Isipokuwa kwamba, pale ambapo ni lazima kusimamisha mashine au kuzima mitambo au michakato kabla ya kuondoka kwa haraka mahali pa kazi, au ambapo vifaa hatari vipo au michakato hatari inafanywa, mwanga hautatakiwa kuwa chini ya lux 20.
(4)Mwajiri atahakikisha kwamba vyanzo vya dharura vya mwanga vilivyoainishwa katika kanuni ndogo ya (3)—
(a)zina uwezo wa kujiwashwa ndani ya sekunde 15 baada ya kushindwa kwa mwanga ulioainishwa na kanuni ndogo ya (1);
(b)itadumu kwa muda wa kutosha ili kuhakikisha kuondoka kwa haraka mahali pa kazi kwa usalama;
(c)zimewekwa katika mpangilio mzuri wa kufanya kazi na zinajaribiwa ufanisi wake katika kila kipindi kisochozidi miezi mitatu; na
(d)pale ambapo vishikizi mwelekeo vya taa vimewekwa, viwekwe kwenye urefu usiopungua mita mbili juu ya usawa wa sakafu na visielekezwe juu ya nyuzi kumi na chini ya nyuzi arobaini na tano ya mstari wa usawa ambao vishikizi hivyo vimewekwa.
(5)Mwajiri anayejishughulisha na shughuli za ujenzi katika eneo lake la kazi atahakikisha vyumba vyote, ngazi, njia za kupita, vyumba vya chini ya ardhi na sehemu nyinginezo ambazo hatari inaweza kuwepo kwa kukosa mwanga wa asili, kuweka mwanga ili kuwe salama.

6. Utofautishaji wa uoni

(1)Ili kutofautisha uoni wa mahali pa kazi na maeneo ya nje ya mahali pa kazi ambapo wafanyakazi wanafanya kazi sehemu kubwa ya zamu zao katika chumba ambacho eneo la sakafu ni chini ya mita za mraba mia moja, mwajiri atahakikisha kila chumba kinawekwa madirisha kwa njia ambayo—
(a)ukubwa wa madirisha hayo usiwe chini ya theluthi tatu ya kipeuo cha pili cha eneo la sakafu ya chumba, na maeneo yote mawili yawe yamepimwa kwa mita za mraba;
(b)ukomo wa dirisha hauko juu na vichwa vya dirisha haviko chini ya mita moja na nusu juu ya usawa wa sakafu ya chumba; na
(c)madirisha hayo yawekewe uzio unaopitisha mwanga.
(2)Isipokuwa, kama mkaguzi ataagiza vinginevyo, masharti ya kanuni ndogo ya (1) hayatatumika kwenye mazingira ambapo mwanga wa asili utakuwa na athari mbaya kwa mchakato wa kazi au nyenzo zinazotumika katika chumba, au pale ambapo mchakato katika chumba unapaswa kufanywa chini ya mazingira yaliyodhibitiwa ya hali ya mwanga, joto, unyevu au mzunguko wa hewa, au ambapo uamuzi wa muundo au rangi katika chumba unahitaji mazingira yenye kiwango cha mwanga chenye ubora, au kwa sababu za kiusalama, faragha au ulinzi, kufuata masharti yaliyokusudiwa inakuwa haiwezekani.
(3)Endapo kupenya kwa mwanga wa jua moja kwa moja katika sehemu yoyote ya kazi kunaweza kuleta tishio kwa usalama wa wafanyakazi katika sehemu hiyo ya kazi, mwajiri atahakikisha kuwa anaweka kizuizi katika sehemu hiyo ya kazi ili kuepuka kupenya huko, lakini afanye hivyo bila kuathiri mahitaji ya uoni katika chumba hicho.

7. Hewa na uingizaji hewa

(1)Mwajiri atahakikisha kwamba kila sehemu ya mahali pa kazi inapitisha hewa kwa njia ya asili au ya kimakenika kwa namna ambayo—
(a)hewa inayovutwa na wafanyakazi haihatarishi usalama na afya zao;
(b)kiwango cha wastani cha ujazo wa kaboni dayoksaidi kilichopo katika hewa, na kilichopimwa kwa muda wa masaa nane, au muda mwingine wowote wa kazi hakizidi 1000 ppm;
(c)kiwango cha ukomo wa kukumbwa na viambata vya kwenye hewa hakizidi kama ilivyoainishwa katika Sehemu ya A ya Jedwali la Tano la Kanuni hizi;
(d)kiwango kilichopo cha gesi inayoweza kulipuka au kuwaka hakizidi kiwango cha chini cha kulipuka kama ilivyoainishwa katika Sehemu A ya Jedwali la Tano la Kanuni hizi; na
(e)maeneo ya kazi yenye ufinyu wa hewa ya asili yatakuwa na ufuatiliaji endelevu wa gesi wakati wote wa kazi.
(2)Pale ambapo hatua zilizowekwa chini ya kanuni ndogo ya (1) hazitekelezeki, au kuna hatari ya hewa isiyo salama katika usawa wa kupumulia wa mfanyakazi, mwajiri atampa kila mfanyakazi husika na kuhakikisha kwamba anatumia kwa usahihi vifaa kinga vya kupumulia vya aina ambayo hupunguza kukumbwa na vihatarishi vya kwenye hewa kwa kiwango salama, na mwajiri atamfahamisha mfanyakazi juu ya vihatarishi vilivyopo na hatua za tahadhari dhidi ya kukumbwa kupita kiasi na vihatarishi hivyo.

8. Mpangilio wa mazingira ya kazi

(1)Mtumiaji wa mashine atatoa na kuweka nafasi ya kutosha ya wazi na isiyozuiliwa katika kila mashine ili kuwezesha kazi kufanyika bila kuhatarisha usalama wa wafanyakazi.
(2)Mwajiri atatakiwa—
(a)bila kujumuisha sehemu za kazi ambazo shughuli za ujenzi zinafanyika, aweke angalau mita za mraba 2.25 za eneo la sakafu lililo wazi kwa kila mfanyakazi anayefanya kazi katika eneo la kazi la ndani;
(b)kuwepo na nafasi isiyo na kizuizi katika eneo la kazi kwa kila mfanyakazi;
(c)kuweka kila sehemu ya kazi ya ndani katika hali ya usafi, mpangilio mzuri, na kuondoa vifaa, zana na vitu ambavyo havihitajiki kwa kazi inayofanywa katika sehemu hiyo ya kazi;
(d)kuweka sakafu, njia, na ngazi zote katika hali ya usalama, kusiwepo vizuizi, utelezi, taka na zana; na
(e)kuweka paa na kuta za kila sehemu ya kazi ya ndani katika ubora bila kuvuja.
(3)Mwajiri hatamruhusu mtu yeyote kutupa kitu chochote kutoka mahali pa juu isipokuwa kwa kutumia kinyanyuzi, au kama kuna utaratibu umewekwa wa kuhakikisha usalama unakuwepo kwa vitu vinavyoanguka.

9. Kelele na kuhifadhi usikivu

(1)Kanuni hii itatumika mahali pa kazi ambapo mfanyakazi katika sehemu hiyo ya kazi anakumbwa na kiwango sawa cha kelele cha 85 dB(A) au zaidi.
(2)Kwa kuzingatia masharti ya kanuni ndogo ya (3) na (4), mwajiri hatamruhusu mfanyakazi kufanya kazi katika mazingira ambayo anakumbwa na kiwango sawa cha kelele cha 85 dB(A) au zaidi.
(3)Mwajiri atapunguza kiwango sawa cha kelele hadi chini ya 85 dB(A) au, ikiwa hii haiwezekani, atapunguza kiwango hicho kadri inavyowezekana na kuchukua hatua zote zinazofaa kuzuia kelele kutoka kwenye chanzo.
(4)Ikiwa kiwango sawa cha kelele katika sehemu yoyote ya kazi hakiwezi kupunguzwa hadi chini ya 85 dB(A), kama ilivyokusudiwa katika kanuni ndogo ya (3), mwajiri atatakiwa—
(a)kuweka ishara inayoashiria kelele kwenye ukanda wenye kelele katika eneo hilo la kazi na katika milango ya kuingia na kutoka kwenye chumba ambacho kina kelele; na
(b)kumkataza mtu yeyote kuingia katika eneo la kelele isipokuwa kama mtu huyo amevaa vilinda usikivu.
(5)Katika shughuli za ujenzi ambapo haiwezekani kufuata masharti ya kanuni ndogo ya (4)(a) kutokana na asili au ukubwa wa eneo, mwajiri ataweka ishara hizo katika eneo la kuingia na kutoka, au ataweka ishara kama hizo mahali pa wazi karibu iwezekanavyo na mahali pa kazi husika au mahali ambapo mkaguzi anaweza kuelekeza.
(6)Pale ambapo kwa maoni ya mkaguzi, mwajiri ameacha au ameshindwa kupunguza kiwango sawa cha kelele katika eneo la kelele hadi chini ya 85 dB(A) au kutenga chanzo cha kelele anaweza kumuamuru mwajiri huyo kwa notisi ya maandishi, kuchukua hatua zaidi kwa kadri ambayo mkaguzi ataona kuwa ni za busara na zinazotekelezeka kwa madhumuni ya kuhifadhi usikivu wa wafanyakazi wanaoingia au kufanya kazi katika eneo hilo la kelele.
(7)Mwajiri atatakiwa atoe bila malipo, vilinda usikivu kwa kila mfanyakazi anayefanya kazi ndani au, kwa mtu yeyote anayehitajika au kuruhusiwa kuingia eneo la kelele, na mwajiri hataruhusu mtu yeyote kufanya kazi au kuingia eneo la kelele isipokuwa kama amevaa vilinda usikivu kwa njia sahihi.
(8)Vilinda usikivu ambavyo mwajiri atatoa kwa mujibu wa kanuni ndogo ya (7) vitakuwa—
(a)vimeridhiwa na mkaguzi kwamba, mwajiri amechukua hatua za kutosha za tahadhari ili kuhakikisha kwamba matumizi ya kawaida ya vilinda usikivu hayatasababisha kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, na ameidhinisha matumizi ya kawaida ya vilinda usikivu hivyo;
(b)vinatunzwa na mwajiri katika hali bora na ya usafi wakati wote; na
(c)vinahifadhiwa kwenye chombo safi kisicho na vumbi kilichotolewa na mwajiri wakati havitumiki.
(9)Mwajiri atatakiwa kutoa maelezo kwa mtu yeyote anayetakiwa kuvaa vilinda usikivu matumizi ya vilinda usikivu hivyo, na kumtaarifu kuhusu ukanda wenye kelele ambapo uvaaji ni walazima.
(10)Mwajiri atatakiwa—
(a)kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi aliyeajiriwa katika ukanda wenye kelele anafanyiwa uchunguzi wa usikivu unaofanywa kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria, na mkaguzi wa afya aliyeidhinishwa na Mkaguzi Mkuu;
(b)kutunza kumbukumbu za uchunguzi wa usikivu na kuhakikisha anapatiwa mkaguzi iwapo atazihitaji; na
(c)kutunza kumbukumbu hizo kwa muda usiopungua miaka thelathini baada ya kukoma kwa ajira, isipokuwa pale ambapo mwajiri atasitisha kazi, atoe taarifa kwa Mkaguzi Mkuu.
(11)Katika kutekeleza masharti ya kanuni ndogo ya (4)(a), mwajiri atapokea maelekezo kutoka Mamlaka ya ukaguzi iliyoidhinishwa.
(12)Kwa kuzingatia masharti ya kanuni hii, wastani wa viwango vya kelele vinavyoruhusiwa mahali pa kazi, ni kama vilivyoainishwa katika Jedwali la Pili la Kanuni hizi.

10. Udhibiti wa vumbi

(1)Mwajiri atahakikisha kwamba kikomo cha vumbi hakizidi kiwango kilichoainishwa katika Jedwali la Tano.
(2)Mwajiri atahakikisha kazi zozote zinazofanyika katika mahali pa kazi, zana au bidhaa anazotumia hazizalishi vumbi, au apunguze uzalishaji wa vumbi.
(3)Pale ambapo mwajiri atashindwa kutekeleza masharti ya kanuni ndogo ya (2) atatakiwa kufanya yafuatayo—
(a)ufuatiliaji wa kiwango cha vumbi kinachozalishwa katika eneo lake la kazi na kiwango cha vumbi ambacho mfanyakazi husika anakumbwa; na
(b)anaweka miundo mbinu ya za kuweza kudhibiti vumbi katika mahali pa kazi ili kiwango cha kukumbwa na vumbi kiwe chini ya kikomo kwa kufanya yafuatayo—
kuweka kizuizi kati ya mfanyakazi na chanzo cha vumbi, au kutenga kazi zinazozalisha vumbi na kazi zingine katika mahali pa kazi;
(i)kuweka kifaa karibu na chanzo cha vumbi au miundo mbinu inayovuta na kutoa vumbi nje ya eneo la kazi;
(ii)kufanya usafi wa mara kwa mara wa mitambo, mashine, nyaraka, vifaa, samani, paa za nyumba, madirisha, sakafu, kuta, maeneo yaliyojificha na yasiyotumika kwa namna ambayo haisababishi vumbi kusambaa,
(iii)kusafisha maeneo ya kazi kwa kutumia kifaa cha kuvuta uchafu badala ya fagio kwa maeneo ambayo italazimika kufanya hivyo ili kuondoa vumbi; na
(iv)kumwagia maji eneo lenye vumbi ili kuondoa vumbi linalosambaa hewani;
(4)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (3), mwajiri atapunguza muda wa kukumbwa kwa wafanyakazi katika maeneo yenye vumbi, au kubadilisha wafanyakazi wanaofanya katika maeneo yenye vumbi au kufanya kazi zinazozalisha vumbi katika sehemu ya kazi ili kupunguza athari za kukumbwa na vumbi kwa wafanyakazi husika.
(5)Mwajiri atawapatia wafanyakazi wanaofanya kazi katika maeneo yenye vumbi, au wanaofanya kazi zinazozalisha vumbi au watu wowote wanaofika katika maeneo yenye vumbi katika sehemu ya kazi vifaa kinga vya kupumulia sahihi, kwa kuzingatia kiwango cha vumbi, muda wa kukumbwa, na aina ya vumbi linalozalishwa katika eneo la kazi kama itavyoelekezwa na mkaguzi.
(6)Mwajiri au mtu aliyejiajiri lazima atoe taarifa, maelekezo na mafunzo kwa watu kuhusu—
(a)chanzo cha kukumbwa na vumbi;
(b)athari za kiafya na usalama zinazoambatana na kukumbwa kwa vumbi;
(c)tahadhari muhimu za kuchukua ili kupunguza kukumbwa na vumbi;
(d)matumizi sahihi ya vifaa kinga vya kupumulia; na
(e)njia salama za kufanya kazi ili kuzuia au kupunguza uzalishaji wa vumbi.
(7)Mwajiri atahakikisha—
(a)kila mfanyakazi aliyeajiriwa katika maeneo yenye vumbi au anafanya kazi zinazozalisha vumbi anafanyiwa uchunguzi wa mapafu unaofanywa kwa mujibu wa Sheria, na mkaguzi wa afya aliyeidhinishwa na Mkaguzi Mkuu;
(b)anatunza kumbukumbu za uchunguzi wa mapafu na kuhakikisha anapatiwa mkaguzi iwapo atazihitaji; na
(c)anatunza kumbukumbu hizo kwa muda usiopungua miaka thelathini baada ya kukoma kwa ajira, isipokuwa pale ambapo mwajiri atasitisha kazi, atoe taarifa kwa Mkaguzi Mkuu.

11. Kuondoa au kudhibiti kukumbwa na mitetemo

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa—
(a)katika sehemu yake ya kazi anatumia mitambo, mashine, vifaa au zana ambazo hazizalishi mitetemo; au
(b)anatumia mitambo, mashine, vifaa na zana ambazo zinazalisha mitetemo katika kiwango salama.
(2)Pale ambapo haiwezekani kutekeleza masharti ya kanuni ndogo ya (1), mwajiri atapunguza muda wa mfanyakazi kukumbwa na mitetemo kwa—
(a)kupunguza muda wa mfanyakazi kukumbwa na mitetemo ya mwili au mkono; na
(b)kufanya kazi kwa awamu kwa wafanyakazi wanaokumbwa na mitetemo ya mwili na mkono.
(3)Ili kuzuia mitetemo ya mwili mzima mwajiri atatakiwa—
(a)kuweka kikomo cha muda unaotumiwa na wafanyakazi kwenye sehemu au mtambo yenye mitetemo kama ilivyoainishwa katika Sehemu A ya Jedwali la Sita la Kanuni hizi;
(b)kuhakikisha kuwa kifaa au mashine inatunzwa, kuboreshwa au kurekebishwa pale inapohitajika ili kupunguza mitetemo; na
(c)anaweka kifaa kinachosaidia kupunguza mitetemo katika viti;
(4)Ili kuzuia mitetemo ya kwenye mikono, mwajiri atatoa glavu maalum za kuzuia mitetemo, pamoja na kufanya yafuatayo—
(a)kutoa zana zenye vishikio vinavyohitaji nguvu ndogo ya mikono ambayo bado itaruhusu utumiaji salama wa zana na mchakato husika,
(b)kusimamia uvaaji wa glavu ili kuzuia mitetemo
(c)kutoa vipindi vya kupumzika katika muda wa kazi ili kupunguza muda wa wafanyakazi kukumbwa na mitetemo
(d)kuweka ukomo wa muda wa kuvumilia mtetemo wa mkono kama ilivyoainishwa katika Sehemu B ya Jedwali la Sita ya Kanuni hizi;
(e)kukataza matumizi ya zana zenye kasoro; na
(f)kuboresha, kurekebisha, au kubadilisha zana ambazo zimechakaa, butu au zisizo na mpangilio.
(5)Mwajiri atafanya ufuatiliaji wa mitetemo kwa wafanyakazi, kwa kutumia vifaa husika vya kupima mitetemo ya mikono na mwili kwa wafanyakazi wote wanaotumia zana, vifaa au kuendesha mashine zinazozalisha mitetemo.
(6)Mwajiri atatoa mafunzo kwa wafanyakazi ya namna sahihi ya kutumia zana na vifaa vinavyotetema na kuzitunza ili kupunguza kukumbwa na mitetemo kwa kiwango kikubwa.
(7)Mwajiri atahakikisha—
(a)kila mfanyakazi anayefanya kazi katika maeneo, mashine, mitambo au anatumia zana na vifaa vyenye mitetemo anafanyiwa uchunguzi wa afya, unaofanywa kwa mujibu wa Sheria, na mkaguzi wa afya aliyeidhinishwa na Mkaguzi Mkuu;
(b)anatunza kumbukumbu za uchunguzi wa afya na kuhakikisha anapatiwa mkaguzi iwapo atazihitaji; na
(c)anatunza kumbukumbu hizo kwa muda usiopungua miaka thelathini baada ya kukoma kwa ajira, isipokuwa pale ambapo mwajiri atasitisha kazi, lazima atoe taarifa kwa Mkaguzi Mkuu.

12. Kinga dhidi ya kukumbwa na mionzi ayonishi

(1)Mwajiri anayetumia vifaa vya mionzi au chanzo cha mionzi ayonishi au kushiriki katika shughuli zinazohusisha kukumbwa na mionzi ayonishi atahakikisha kwamba—
(a)wafanyakazi wanakingwa dhidi ya kukumbwa na mionzi ayonishi;
(b)mtu yeyote asikumbwe na mionzi ayonishi inayozidi kiwango kilichoainishwa katika Jedwali la Tatu;
(c)mfanyakazi au mtu yeyote anayeingia katika maeneo yenye mionzi ya kuchaji anapatiwa kifaa stahiki au beji inayovaliwa ili kufuatilia kikomo cha kuathiriwa na mionzi;
(d)anatoa vifaa kinga stahiki na vya kutosha ili kulinda usalama na afya za wafanyakazi;
(e)kunakuwepo na wakufunzi wenye sifa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mara kwa mara yanayohusiana na mionzi ayonishi, mafunzo yatolewe kwa kuzingatia majadiliano kati ya mwajiri na wafanyakazi au wawakilishi wa usalama na afya mahali pa kazi.
(2)Mfanyakazi wa kike anayefanya kazi katika maeneo yenye mionzi ayonishi baada ya kufahamu kuwa ni mjamzito atamjulisha mwajiri ili mazingira yake ya kazi yaweze kuboreshwa, mwajiri ataboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia kiwango cha madhara husika, ili kuhakikisha kuwa mtoto aliyeko tumboni pia anapewa kiwango sawa cha ulinzi kama ilivyoanishwa katika Jedwali la Tatu.
(3)Mfanyakazi hataruhusiwa na kukumbwa zaidi ya kiwango cha juu cha kipimo cha mionzi ayonishi kwa mwaka mmoja kama ilivyoainishwa katika Jedwali la Tatu, isipokuwa—
(a)kwa madhumuni ya kuokoa maisha au kuzuia majeraha makubwa;
(b)ikiwa anachukua hatua zinazolenga kuzuia kiwango kikubwa cha mionzi;
(c)ikiwa anachukua hatua za kudhibiti hali ya janga kuendelea.
(4)Chombo kinachohifadhi kiambata chenye mionzi ambacho hakijafungwa kitawekwa alama za kudumu zifuatazo:
(a)jina au alama ya mtengenezaji;
(b)alama ya kemikali, kiwango cha kemikali inayozalisha mionzi, na ikiwezekana jina la maandalizi ya kemikali; na
(c)kiwe na neno “RADIOACTIVE”.

Jedwali la kwanza (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 5(1))

Wastani wa viwango vya mwanga vinavyotakiwa katika eneo la kazi

Eneo la kaziKiwango cha chini (lux)Kiwango cha juu (lux)
Ofisi200750
Varanda100750
Stoo100750
Jikoni100750
Kiwandani100750
Kazi za ufinyanzi100750
Vyooni100750
Maabara200750
Chumba cha mkutano200750
Ukumbi wa mikutano150750
Kazi za kuchora500750
Chumba cha kusanifu200750
Kazi inayohitaji umakini mkubwa5001000
Uchimbaji wa chini ya ardhi100300

Jedwali la pili (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 9(12))

Wastani wa viwango vya kelele vinavyoruhusiwa katika eneo la kazi

Leq dB (A)Muda (Kila siku)Muda (Kila wiki)
85saa 8.00saa 40.00
88saa 4.00saa 20.00
91saa 2.00saa 10.00
94saa 1.00saa 5.00
97dakika 30.00saa 2.50
100dakika 15.00saa 1.25
103dakika 7.50dakika 37.5
106dakika 3.75dakika 18.75
109dakika 1.87dakika 9.37

Jedwali la tatu (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 12(1)(b))

Ukomo wa kukumbwa na mionzi ayonishi katika eneo la kazi

Eneo katika mwiliKikomo cha dozi ya kukumbwa
mrem/mwakamSv/mwaka
mwili mzima500050
sehemu ya mwili50000500
ngozi50000500
kwenye lenzi ya jicho15000150
mtoto aliyeko tumboni5005

Jedwali la nne (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 4(2)(a))

Kiwango cha shinikizo la joto

Aina ya mavaziWBGT (°C)
Mavazi ya kazi (Shati la mikono mirefu na Suruali)0
Vazi yaliyotengenezwa kwa malighafi iliyosokotwa0
Ovaroli ya plastic+ 0.5
Ovaroli ya plastic isiyopitisha maji+ 1
Mavazi ya tabaka mbili+ 3
Ovaroli ya kuzuia mvuke+ 11
Kukumbwa na Shinikizo la joto (WBGT katika °C)kwa masaa 8 ya kazi kwa siku juma moja
Mpangilio wa KaziKuzoeaKiwango cha kuchua hatua (kutokuzoea)
Kazi NyepesiKazi ya KawaidaKazi NzitoKangi nzito SanaKazi NyepesiKazi ya KawaidaKazi NnzitoKangi nzito Sana
75-100%31.028.0----28.025.0----
50-75%31.029.027.5--28.526.024.0--
25-50%32.030.029.028.029.527.025.524.5
0-25%32.531.530.530.030.029.028.027.0
Mifano ya uzito wa kazi:kupumzika - kukaa, kwa harakati za wastani za mkonokazi nyepesi - kukaa au kusimama ili kudhibiti mashine, kufanya kazi nyepesi ya mkono au kiganja kwa mfano kutumia msumeno wa meza, kutembea mara kwa mara, kuendesha garikazi ya wastani - kutembea na kuinua kwa wastani na kusukuma au kuvuta; kutembea kwa kasi ya wastani, kusugua sehemu kwa kusimamakazi nzito - kazi ya kuchukua na koleo, kuchimba, kubeba, kusukuma / kuvuta mizigo mizito kutembea kwa kasi, k.m. seremala akishona kwa mkononzito sana - shughuli kali sana kwa kasi ya juu, k.m. kusukuma mchanga wenye unyevu

Jedwali la tano (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 7(1)(c)(d) na 10(1))

Kiwango cha ubora wa hewa

Viambata vya hewaKiwango cha ukomo wa kukumbwaMuda (masaa)
Kaboni monoksaidi35ppm8
Kiwango cha chini cha mlipukokisizidi 5%Muda wowote
Kaboni dayoksaidikisizidi 1000ppm ikiwa ndani ya jengokisizidi 4000 ppm ikiwa njeMuda wowote
naitrojeni dayoksaidi40ppm8
salfa dayoksaidikisizidi 1ppm8
Unyevu wa kwenye hewa ndani ya jengokiwe kati ya 30% na 70%Muda wowote
Mzuguko wa hewakisipungue 0.5m/s na kisizidi 2m/sMuda wowote
ozonikisizidi 78ppm8
formaldehydekisizidi 0.5ppm8
oksijeniKisipungue 19% na kisizidi 23% 
Chembe chembe kuanzia 2.5μm (PM2.5)
Aina ya chembe chembeKipimo katika μmUkomo katika ppm
ukomo wa chiniukomo wa juukiasi cha kuvumilika
silica2.55.00.05
vumbi la mbao ngumu2.55.01.0
vumbi la mkaa2.55.03.0
vumbi la mbao laini2.55.05.0
vumbi la pamba2.55.01.0
vumbi la katani2.55.01.0
vumbi la muwa2.55.01.0
vumbi lolote2.55.05.0

Jedwali la sita (Limetengenezwa chini ya kanuni 11(3)(a))

Ukomo wa kuvumilia mtetemo wa mwili mzima

Ukomo wa kukumbwa kila sikuKiwango cha juu cha kukumbwa kila sikuKiwango cha kuchukua hatua ya kukumbwa
saa 81.15 m/s20.5 m/s2
Ukomo wa kuvumilia mtetemo wa mkono
Ukomo wa kukumbwa kila sikuKiwango cha juu cha kukumbwa kila sikuKiwango cha kuchukua hatua ya kukumbwa
saa 85 m/s22.5 m/s2
▲ To the top

History of this document

07 April 2023 this version