Kanuni za Uondoaji wa Asbestosi za Mwaka 2023

Government Notice 291 of 2023

Kanuni za Uondoaji wa Asbestosi za Mwaka 2023

Tanzania
Factories Act

Kanuni za Uondoaji wa Asbestosi za Mwaka 2023

Tangazo la Serikali 291 ya 2023

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 109]

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Uondoaji wa Asbestosi za Mwaka 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—"asbestosi" maana yake ni nyuzi za aina yoyote za madini ya silika zinazoweza kuingia kwenye mapafu kwa kupitia mfumo wa hewa na zisizoweza kuvunjwavunjwa, kumeng’enywa au kutolewa ndani ya mwili;kazi inayohusiana na asbestosi” maana yake ni kazi yoyote inayohusu kubomoa, kuondoa vitu au bidhaa zenye asbestosi;kifaa kinga cha kupumulia” maana yake ni kifaa ambacho huvaliwa angalau mdomoni na puani ili kuzuia kuvuta hewa yenye asbestosi;"kikomo cha kukumbwa na asbestosi kazini" maana yake ni kikomo cha kukumbwa na asbestosi kazini cha nyuzi 0.2 za asbestosi kwa kila mililita ya hewa;"kikomo cha muda mfupi cha kukumbwa na asbestosi " maana yake ni kiwango ambacho mfanyakazi anaweza kukumbwa na asbestosi kwa wastani wa muda usiozidi dakika kumi na tano ambacho hakipaswi kuzidishwa wakati wowote kwa siku, hata kama wastani wa kukumbwa wa masaa manne uko ndani ya kikomo cha kukumbwa kazini;"mahali penye asbestosi" inajumuisha asbestosi yoyote iliyopo katika eneo la kazi, ikijumuisha bidhaa ya saruji ya asbestosi, ufunikaji uliotumia asbestosi, nyenzo zenye asbestosi, vumbi lenye asbestosi, bidhaa zilizofunikwa kwa asbestosi, na taka za asbestosi;mamlaka ya ukaguzi wa asbestosi iliyoidhinishwa” maana yake ni mtu au mkandarasi aliyeidhinishwa na Mkaguzi Mkuu kufanya kazi za asbestosi ambaye ana elimu, ujuzi na vifaa maalumu;mtu mwenye uwezo” maana yake ni mtu mwenye ujuzi, mafunzo na uzoefu unaohitajika kuhusiana na kazi za asbestosi na anatambuliwa na Mamlaka;"Sheria" maana yake ni Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi;uzuiaji kwa kutumia asbestosi” maana yake ni bidhaa yoyote ambayo ina asbestosi kwa ajili ya kuzuia joto, sauti, umeme au madhumuni mengine ikijumuisha kuzia moto isipokuwa—(a)saruji ya asbestosi, ufunikaji kwa kutumia asbestosi;(b)bidhaa yoyote ya lami, plastiki, au mpira ambayo ina asbestosi na sifa ya kuhimili joto au sauti tofauti na madhumuni yake kuu.[Sura ya 297]

3. Matumizi

Kanuni hizi zitatumika kwa kila mwajiri, mtu aliyejiajiri na ana mfanyakazi au mtu yeyote katika eneo lenye vumbi la asbestosi.

4. Utambuzi wa uwepo wa asbestosi

Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa—
(a)vifaa vyote vya asbestosi vilivyopo mahali pa kazi vinatambuliwa na mtu mwenye ujuzi;
(b)ikiwa hakuna uhakika wa uwepo wa asbestosi katika bidhaa, kuchukua na kupeleka sampuli ya bidhaa hiyo kuhahakikiwa na kupimwa katika maabara inayotambulika na yenye uwezo;
(c)ikiwa sehemu ya mahali pa kazi haifikiki na inadhaniwa na mtu mwenye ujuzi kuwa na asbestosi; itatambuliwa kuwa eneo hilo lina asbestosi, na
(d)ikiwa hakuna asbestosi iliyotambuliwa mahali pa kazi kulingana na kanuni ya 4(a), (b) na (c) itathibitishwa kwa maandishi na mtu mwenye ujuzi kuwa halina asbestosi.

5. Orodha ya asbestosi iliyotambuliwa

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba asbestosi iliyotambuliwa au kudhaniwa kuwa ipo mahali pa kazi na mtu mwenye ujuzi kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 4, inaingizwa katika orodha ya asbestosi ambayo itatunzwa mahali pa kazi.
(2)Orodha ya asbestosi iliyopo mahali pa kazi inatakiwa kuwa na taarifa zifuatazo:
(a)tarehe ambayo kitu chenye asbestosi kimetambuliwa;
(b)maelezo ya kitu chenye asbestosi, idadi na hali ya uchakavu;
(c)ramani yenye maelezo ya kina kuhusu maeneo yenye asbestosi;
(d)uthibitisho wa kuwepo lebo na ishara kama iilivyoainishwa katika kanuni ya 19;
(e)uainishaji wa hatari ya uwezekano wa kukumbwa na asbestosi kama ilivyofafanuliwa katika kanuni ya 6(3); na
(f)maelezo ya kazi za baadae na matukio yanayohusiana na uwezekano wa kukumbwa.
(3)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba mtu mwenye ujuzi anapitia na ikibidi kurekebisha orodha ya asbestosi zilizopo mahali pa kazi kwa kipindi kisichozidi miezi ishirini na nne.
(4)Orodha ya asbestosi zilizopo mahali pa kazi itarekebishwa ikiwa—
(a)vitu zaidi vyenye asbestosi vimetambuliwa; na
(b)kitu chenye asbestosi kimechakaa kwa kiasi kikubwa, kimeondolewa, kimeharibika, kimefungiwa au kufunikwa.
(5)Pale ambapo kuondolewa au ukarabati wa asbestosi umepangwa, taarifa ya kina ya orodha ya vitu venye asbestosi vilivyopo mahali pa kazi, itafafanuliwa vya kutosha kuhusiana na kazi itakayofanywa.
(6)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba nakala ya orodha ya vitu vyenye asbestosi vilivyopo katika mahali pa kazi—
(a)vinatolewa kwa mkandarasi wa asbestosi aliyesajiliwa kabla ya kuanza kuondoa au kukarabati asbestosi;
(b)vitapatikana kwa urahisi kwa wafanyakazi na mkaguzi katika mahali pa kazi; na
(c)ikiwa umiliki utabadilika, apatiwe mmiliki mpya wa majengo.
(7)Mkandarasi wa asbestosi aliyesajiliwa ambaye anafanya kazi ya kuondoa au kukarabati asbestosi mahali pa kazi atahakikisha kuwa, kama kiambata kinachodhaniwa kuwepo ni asbestosi
(a)anapata nakala ya orodha ya asbestosi kutoka kwa mwajiri au mtu aliyejiajiri; na
(b)ikiwa inadhaniwa kuwa asbestosi ipo kwenye jengo au mtambo, amjulishe mwajiri au mtu aliyejiajiri ambaye atawajibika kuhakikisha kwamba mtu mwenye ujuzi atathibitisha.
(8)Kwa kazi zote zinazofanyika mahali pa kazi ambapo kuna uwezekano wa kukumbwa na asbestosi inayopeperuka hewani—
(a)mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba mtu anayeidhinisha kazi husika anapewa nakala ya orodha ya asbestosi zilizopo mahali pa kazi;
(b)mtu anayeidhinisha kazi iliyotajwa katika aya (a), atathibitisha kutoka kwenye orodha ya asbestosi zilizopo, kama kazi zijazo na matukio yanayohusiana na uwezekano wa kukumbwa na asbestosi upo, ikijumuisha kutambua vidhibiti vinavyopendekezwa; na
(c)mwajiri au mtu aliyejiajiri atalazimika kuhakikisha kwamba vidhibiti vinavyopendekezwa vinatekelezwa kuhusiana na kazi hiyo.
(9)Asbestosi zote zilizoorodheshwa katika orodha ya asbestosi kama inavyotakiwa na kanuni hii zitawekwa lebo, alama au ishara za wazi kwa mujibu wa kanuni ya 19.

6. Tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na asbestosi

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na asbestosi katika eneo la kazi inafanyika na Mamlaka iliyoidhinishwa ili kubaini kama mtu yeyote anaweza kuwa katika hatari ya kukumbwa; na
(b)taarifa ya tathmini iliyofanywa katika aya ya (a) itawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu.
(2)Mwajiri kabla ya kufanya tathmini, lazima ashauriane na kamati ya afya na usalama ili kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya uwezekano wa kukumbwa na asbestosi.
(3)Matokeo ya tathmini yatakuwa na uainishaji wa hatari kulingana na uwezekano wa kukumbwa kwa kila kitu chenye asbestosi, kutokana na—
(a)athari za kiafya za asbestosi;
(b)idadi ya watu wanaoweza kukumbwa katika mahali pa kazi;
(c)muda wa kuwepo katika eneo lenye asbestosi;
(d)hali ya uharibifu wa bidhaa zenye asbestosi mahali pa kazi ikijumuisha, shughuli za matengenezo, matukio yanayoweza kutokea na shughuli za kawaida mahali pa kazi; na
(e)hali ya bidhaa yenye asbestosi, ikijumuisha uchakavu.
(4)Uainishaji wa hatari unaokusudiwa katika kanuni ndogo ya (3) utatumika kubainisha iwapo kuna sababu ya kuendelea kutumia, kurekebisha au kuondolewa kwa bidhaa yenye asbestosi.
(5)Tathmini ya uwezekano wa kukumbwa, unaotokana na kazi ya kurekebisha bidhaa zenye asbestosi kama inavyotakiwa katika kanuni ndogo ya (1), (2) na (3) itajumuisha—
(a)kufafanua kila hatua ya kazi ya urekebishaji;
(b)tathmini ya hatari ya kukumbwa na asbestosi, inayohusiana na kila hatua ya kazi; na
(c)vidhibiti vinavyohitajika ili kupunguza kiwango cha hatari ya kukumbwa na asbestosi.
(6)Tathmini ya uwezekano wa kukumbwa, unaotokana na kazi ya kuondoa bidhaa zenye asbestosi kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 16, itazingatia—
(a)vipengele vilivyofafanuliwa katika kanuni ndogo ya (5);
(b)tathmini ya hatari iliyofanywa;
(c)uwezekano wa kukumbwa kwa watu wengine ambao si wafanyakazi;
(d)uwezekano wa uchafuzi wa hewa, ardhi na maji;
(e)kuwaepusha au kuwakinga na asbetosi wafanyakazi na mahali pa kazi;
(f)usafirishaji wa bidhaa za asbestosi na taka za asbestosi; na
(g)matukio ya dharura.
(7)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atapeleka orodha ya bidhaa zenye asbestosi na tathmini ya uwezekano wa kukumbwa katika mamlaka ya ukaguzi kwa ajili ya kupitiwa na kuidhinishwa, isipokuwa kwamba mapitio na uidhinishaji hautahitajika ikiwa kazi hiyo ilifanyika na Mamlaka ya ukaguzi.

7. Mpango wa usimamizi wa asbestosi

(1)Pale ambapo bidhaa zenye asbestosi zinatambuliwa kama inavyotakiwa katika kanuni ya 4, mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa mpango wa usimamizi wa asbestosi mahali pa kazi unaandaliwa na mtaalamu wa asbestosi.
(2)Mpango wa usimamizi wa asbestosi utajumuisha—
(a)taratibu zinazohusiana na—
(i)utekelezaji wa kanuni ya 4, 5, 6 na 9 mahali pa kazi;
(ii)ukarabati, uondoaji na usimamizi wa bidhaa zenye asbstosi; na
(iii)utekelezaji wa Kanuni za kupiga marufuku matumizi;
(b)utaratibu mahususi wa kupunguza hatari ya kukumbwa kwa wafanyakazi pamoja na kuathiriwa na asbestosi kwa hali zifuatazo—
(i)matukio;
(ii)dharura;
(iii)kazi ya uondoaji; na
(c)sera, utaratibu na mpango wa utekelezaji wa kuondoa bidhaa zilizopo zenye asbestosi mahali pa kazi, ambazo zinazingatia—
(i)kanuni ambayo inatekelezeka ipasavyo, na
(ii)sababu za maamuzi.

8. Taarifa na mafunzo

(1)Mwajiri yoyote anayejihusisha na kazi zinazohusiana na asbestosi au kutumia bidhaa zenye asbestosi baada ya kushauriana na Kamati ya Afya na Usalama iliyoundwa, atalazimika kuwapa wafanyakazi taarifa na mafunzo kuhusiana na—
(a)vyanzo vya kukumbwa na asbestosi;
(b)hatari ya kiafya inayoweza kusababishwa na kukumbwa na asbestosi, ikijumuisha hatari za kiafya kwa familia za wafanyakazi na wengine, ambao wanaweza kuathirika kutokana na vifaa au nguo zilizotumika kazini kupelekwa nyumbani;
(c)tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na mfanyakazi kumkinga dhidi ya vihatarishi vya kiafya vinavyotokana na kukumbwa na asbestosi, ambazo zinajumuisha kuvaa na kutumia vifaa kinga;
(d)umuhimu, matumizi sahihi, matunzo na uwezo wa vifaa kinga, vifaa na hatua za udhibiti wa uhandisi zinazotolewa;
(e)tathmini ya kukumbwa na asbestosi, madhumuni ya kuchukua sampuli za hewa, umuhimu wa ufuatiliaji wa afya za wafanyakazi na faida za muda mrefu za kufanyiwa ufuatiliaji wa kiafya;
(f)muda wa kazi na kiwango cha ukomo wa kukumbwa na asbestosi;
(g)taratibu salama za ufanyaji kazi kuhusu utumiaji, utunzaji, usindikaji, uhifadhi na utupaji wa kitu au bidhaa yoyote iliyo na asbetosi, ili kupunguza uenezaji wa asbestosi nje ya eneo la kazi; na
(h)taratibu zinazopaswa kufuatwa katika tukio la kusambaa au dharura nyingine yoyote.
(2)Mafunzo ya rejea yatatolewa juu ya masuala yanayokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1) angalau kila mwaka au mkaguzi atakavyoelekeza.
(3)Mafunzo yatatolewa na mtu ambaye ana weledi na anayetambuliwa na Mamlaka kutoa mafunzo hayo.
(4)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba anatoa taarifa na maelekezo yanayohusiana na kukumbwa na madhara ya asbestosi kwa mtu yeyote katika eneo lake la kazi.
(5)Mwajiri atatoa maelekezo kwa maandishi ya taratibu zinazokusudiwa katika kanuni ndogo ya (1)(h) kwa madereva wa magari yanayobeba asbestosi au bidhaa zenye asbestosi ambayo yana uwezekano wa kusababisha uchafuzi wa mazingira au kuleta athari kwa watu.
(6)Mwajiri atatoa taarifa kwa mtu ambae anaweza kukumbwa na asbestosi katika eneo la kazi—
(a)kupitia mafunzo ya awali pale tu anapoanza ajira; na
(b)pale ambapo orodha ya bidhaa zenye asbestosi inapitiwa.

9. Uanishaji wa kazi za asbestosi

(1)Kazi ya asbestosi daraja A—
(a)inahusisha upakaji wa saruji za asbestosi kwa namna ambayo hauhitaji maandalizi ya kwenye sakafu, na haiwezi kusababisha kusambaa kwa nyuzi za asbestosi;
(b)inahusisha uondoaji wa saruji za asbestosi isiyozidi mita kumi za mraba au mabomba yenye asbestosi au ubao pinzani wenye asbestosi; na
(c)haihitaji mkandarasi maalum wa asbestosi aliyesajiliwa.
(2)Kazi ya asbestosi daraja B—
(a)inahusisha ukarabati au ufunikaji wa bidhaa za saruji za asbestosi kwa namna ambayo hauhitaji maandalizi ya sakafuni;
(b)inahusisha kuondolewa kwa bidhaa za saruji za asbestosi au ubao pinzani wenye asbestosi; na
(c)inahitaji mkandarasi maalum wa asbestosi aliyesajiliwa.
(3)Kazi ya Asbestosi daraja C—
(a)inahusisha uondoaji, ukarabati au uwekaji wa asbestosi na bidhaa yenye asbestosi yeyote; na
(b)inahitaji mkandarasi maalum wa asbestosi aliyesajiliwa.

10. Wajibu wa watu wanaoweza kukumbwa na asbestosi

(1)Mtu ambaye anaweza kukumbwa na asbestosi atatakiwa—
(a)kutii maagizo yanayohusu afya na usalama kazini yanayotolewa na au kwa niaba ya mwajiri;
(b)kuhudhuria mafunzo ya uelewa wa asbestosi juu ya orodha ya asbestosi zilizopo kwenye jengo; na
(c)kutoa taarifa ya bidhaa yoyote yenye asbestosi iliyoharibika kwa mwajiri au mwakilishi wa afya na usalama mahali pa kazi.
(2)Mtu ambaye anafanya matengenezo yasiyohusika na kazi za asbestosi, na ambaye anaweza kukumbwa na asbestosi atatakiwa—
(a)kupewa nakala ya orodha ya bidhaa zenye asbestosi zilizopo mahali pa kazi panapohusika ambapo matengenezo yasiyohusika na asbestosi yatafanyika;
(b)kuzuia uharibifu wa, au kusababisha usambaaji wa asbestosi mahali pakazi; na
(c)kuacha kazi mara moja na kutoa taarifa kwa mwajiri au mwakilishi wa afya na usalama mahali; pa kazi, iwapo uharibifu au usambaaji wa asbestosi utatokea.
(3)Mtu anayefanya kazi ya asbestosi ya daraja “A” atatakiwa—
(a)kupata nakala ya orodha ya bidhaa zenye asbestosi zilizopo mahali pa kazi;
(b)kuweka mipaka ya eneo linalodhibitiwa lenye asbestosi kama inavyotakiwa katika kanuni ya 18;
(c)kutumia njia ya kuweka maji wakati wa kuondoa bidhaa zenye asbestosi;
(d)kutumia zana na vifaa vinavyofaa ili kupunguza kusambaa vumbi la asbestosi;
(e)kuhakikisha kifaa kimesafishwa baada ya kufanya kazi za asbestosi;
(f)kuhifadhi, kuweka lebo na kuondoa taka za asbestosi kwa mujibu wa kanuni ya 19; na
(g)kutumia vifaa kinga pamoja na vifaa kinga vya kupumulia vya kutupwa, na vitaondolewa kama taka za asbestosi.
(4)Mtu yeyote ambaye anahusika katika kazi ya asbestosi ya daraja B na C na ambaye anaweza kukumbwa na asbestosi mahali pa kazi, atatii maagizo yote halali yanayohusu afya na usalama mahali pa kazi, yatakayotolewa na au kwa niaba ya mwajiri au mtu aliyejiajiri, kuhusu—
(a)kutekeleza mahitaji ya mpango kazi wa asbestosi ambao umeidhinishwa kwa kazi hiyo maalum ya asbestosi, kwa mujibu wa kanuni ya 15;
(b)kutumia njia za kuweka maji wakati wa kuondoa bidhaa zenye asbestosi;
(c)kuzuia vumbi la asbestosi kusambaa kwenye hewa;
(d)aina na matumizi sahihi ya vifaa kinga;
(d)uvaaji wa kifaa cha ufuatiliaji ili kupima kiwango cha mtu kukumbwa na asbestosi;
(e)kusafisha na kuondoa taka za asbestosi;
(f)usafishaji wa mabaki ya vumbi la asbestosi linalotokana na kazi;
(g)mpangilio katika mahali pa kazi, usafi binafsi, tamaduni nzuri za mazingira, afya na usalama ikiwa ni pamoja na kula, kunywa na kuvuta sigara katika maeneo maalum yaliyotengwa;
(h)taarifa na mafunzo yaliyotolewa kama ilivyokusudiwa katika kanuni ya 8; na
(j)kuzingatia taratibu sahihi za kusafisha kama ilivyoainishwa katika mpango kazi asbestosi ulioidhinishwa.[Please note: numbering as in original]

11. Udhibiti wa kukumbwa na asbestosi

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kukumbwa na asbestosi mahali pa kazi kunazuiwa au ikishindikana kudhibitiwa vya kutosha, udhibiti huo utachukuliwa kuwa wa kutosha ikiwa kiwango cha asbestosi katika hewa;—
(a)kipo chini ya kikomo cha kukumbwa kazini; au
(b)kipo juu ya kikomo, lakini sababu imetambuliwa na hatua ya haraka ya kugawa vifaa kinga vya kupumulia imechukuliwa ili kupunguza kiwango hicho.
(2)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atadhibiti uwezekano wa mtu kukumbwa na asbestosi kwa—
(a)kupunguza au kudhibiti idadi ya watu wanaoweza kukumbwa na asbestosi;
(b)kupunguza muda ambao mtu atakumbwa au anaweza kukumbwa na asbestosi;
(c)kupunguza kiwango cha vumbi la asbestosi ambacho kinaweza kuingia katika mazingira ya kazi; na
(d)kuanzisha hatua za udhibiti wa kihandisi ili kupunguza kukumbwa na asbestosi kama—
(i)kutenganisha mchakato unaohusiana na asbestosi, kufungia bidhaa au eneo lenye asbestosi;
(ii)kuchanganya nyuzi za asbestosi na vitu vingine ili kuzuia kusambaa kwa vumbi la asbestosi;
(iii)kutumia njia ya kuweka maji kudhibiti vumbi la asbestosi pale itakapoonekena inafaa; na
(iv)usafishaji unafanyika kwa kutumia kifaa kinachoweza kuvuta uchafu chenye ufanisi wa kuchuja wa angalau asilimia 99 ya chembe zenye ukubwa wa maikromita moja, ili vumbi lenye asbestosi lisisambae kwenye hewa ya mahali pa kazi.
(3)Pale ambapo asbestosi imeingia kwenye maji—
(a)maji yaliyochafuliwa na asbestosi kutokana na kazi iliyofanyika yatapitishwa kwenye mfumo wa kuchuja maji kabla hayajaingia kwenye mazingira; na
(b)sehemu ya mtambo wa kuchuja maji iliyotumika kuchuja asbestosi itachukuliwa kama taka ya asbestosi.
(4)Kuanzisha taratibu salama za ufanyaji kazi za maandishi ambazo mfanyakazi atatakiwa kufuata ili kuhakikisha kuwa—
(a)bidhaa zenye asbestosi zinashikwa, kuhifadhiwa, kusafirishwa na kuondolewa kwa usalama; na
(b)usimikaji, vifaa, zana na vifaa vya kuvutia uchafu vinatumiwa, vinasafishwa na kutunzwa kwa usalama.
(5)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atatoa taarifa kwa Mkaguzi Mkuu kuhusu umwagikaji, uharibifu na usambaaji wa asbestosi ambao utakuwa ni hatarishi kwa afya za watu.

12. Kutoa taarifa ya kazi za asbestosi

(1)Mwajiri au mtu aliyejiajiri hataruhisiwa kufanya kazi ya daraja lolote la asbestosi isipokuwa mpaka pale ambapo Mkaguzi Mkuu, amejulishwa kwa maandishi kuhusu eneo, mahali na mawasiliano ya mahali ambapo kazi ya asbestosi itafanyika siku kumi na nne kabla ya kuanza kwa kazi hiyo.
(2)Bila kuathiri kanuni ndogo ya (1), Mkaguzi Mkuu anaweza kuruhusu muda mfupi zaidi wa kutoa taarifa katika hali ya dharura.
(3)Taarifa ya maandishi iandikwe kama ilivyoainishwa katika Jedwali la Pili.

13. Majukumu ya mkandarasi aliyeidhinishwa kwa kazi ya asbestosi

(1)Pale ambapo kazi ya asbestosi ya daraja B na C inahusika, mkandarasi aliyeidhinishwa wa asbestosi atatakiwa—
(a)kufanya aina ya kazi ya asbestosi ambayo ameidhinishwa na Mkaguzi mkuu;
(b)kuteua mwakilishi wa afya na usalama mahali pa kazi, kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 11 cha Sheria; na
(c)kupata nakala ya orodha ya bidhaa za asbestosi zilizopo kabla ya kazi ya asbesto kufanyika.
(2)Kabla ya kuanza kwa kazi yoyote ya asbestosi na wakati wa kazi hiyo, mkandarasi aliyeidhinishwa wa asbestosi atahakikisha tathmini ya hatari inafanywa ikiwa ni pamoja na—
(a)utambuzi wa vihatarishi ambavyo mtu anaweza kukumbwa;
(b)tathmini ya hatari inayohusiana na vihatarishi;
(c)hatua za kudhibiti vihatarishi vilivyopo ili kupunguza hatari;
(d)tathmini ya hatari itapitiwa—
(i)kwa vipindi vya kawaida;
(ii)wakati tukio limetokea; au
(iii)wakati wigo wa kazi unabadilika;
(e)kuhakikisha nakala ya tathmini ya hatari iliyohuishwa inapatikana katika eneo husika la kazi ya asbestosi.
(3)Mkandarasi wa asbestosi aliyeidhinishwa atahakikisha kwamba—
(a)mpango kazi ulioidhinishwa unawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu, angalau siku kumi na nne kabla ya kuanza kwa kazi ya asbestosi;
(b)anateua kwa maandishi msimamizi wa asbestosi kwa kila eneo la kazi la asbestosi, ambaye atahakikisha—
(i)uzingatiaji wa afya na usalama kwenye eneo ambalo asbestosi inaondolewa;
(ii)uzingatiaji taratibu za kuondoa au kukarabati asbestosi kwa usalama;
(iii)uzingatiaji wa matumizi sahihi ya vifaa kinga, na
(iv)usafishaji wa eneo la kazi na uondoaji wa taka.
(c)mbinu za ukarabati au kuondoa zinazohusiana na udhibiti zinazotolewa katika mpango kazi;
(d)kwamba kumbukumbu za afya na mafunzo ya wafanyakazi zinapatikana katika mahali pa kazi kwa ajili ya ukaguzi na uthibitisho;
(e)kuhakikisha kwamba taarifa za mfanyakazi zimehifadhiwa kwa muda usiopungua miaka thelathini kwa kuzingatia—
(i)anwani ya kila mradi wa kazi ya asbestosi;
(ii)majina na namba za utambulisho za wafanyakazi ambao wanaweza kukumbwa; na
(f)kabla ya kuanza kazi ya asbestosi vifaa vyote vimesafishwa na kutunzwa katika utaratibu mzuri wa kufanya kazi.

14. Majukumu ya mamlaka ya usimamizi wa kazi za asbestosi

Mamlaka ya usimamizi wa kazi za asbestosi itahakikisha kwamba—
(a)kazi za asbestosi za daraja B na C zinafanywa na mkandarasi wa asbestosi aliyeidhinishwa;
(b)inaidhinisha mpango kazi wa asbestosi kutoka kwa mkandarasi aliyeidhinishwa;
(c)mkandarasi wa asbestosi aliyeidhinishwa kabla ya kuanza kwa kazi za asbestosi anapeleka mpango kazi kwa Mkaguzi Mkuu kwa uthibitisho;
(d)inathibitisha kumbukumbu ya mafunzo na afya za wafanyakazi wa kazi ya asbestosi;
(e)inatoa muongozo na maagizo kwa mkandarasi aliyeidhinishwa wa asbestosi kwenye mpango kazi ulioidhinishwa;
(f)inakagua uzingatiaji wa mpango kazi ulioidhinishwa na matakwa ya kanuni hizi; na
(g)inazuia mkandarasi wa asbestosi aliyeidhinishwa kutekeleza kazi ya asbestosi ambayo inahatarisha afya na usalama kwa watu hadi wakati ambapo hatari hiyo itakuwa imedhibitiwa.

15. Mahitaji ya mpango kazi wa asbestosi

Mpango kazi wa asbestosi unapaswa kuwa na—
(a)jina, mawasiliano na majukumu ya mkandarasi aliyeidhinishwa wa asbestosi, kusafirisha na kutupa taka za asbestosi;
(b)jina na mawasiliano ya msimamizi wa uondoaji wa asbestosi katika eneo husika;
(c)taarifa za asbestosi inayotakiwa kuondolewa, na eneo husika, aina, kiwango na hali ya asbestosi;
(d)orodha ya majina ya wafanyakazi na namba za utambulisho na uthibitishaji wa kupatiwa mafunzo ya asbestosi na kumbukumbu za uchunguzi wa afya katika eneo la kazi ya asbestosi;
(e)tarehe ya kuanza na kukamilika kwa kazi;
(f)njia ya ufuatiliaji wa hewa inayotumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 17;
(g)taarifa za kina za kuondoa asbestosi, vifaa na mbinu zitakazotumika na vifaa kinga sahihi vitakavyotumiwa;
(h)maelezo ya uwekaji mipaka;
(i)utaratibu wa kusafisha eneo la kazi;
(j)taratibu za dharura katika tukio la kusambaa kwa asbestosi; na
(k)njia za uondoaji taka za asbestosi.

16. Eneo la asbestosi lililodhibitiwa

Mwajiri au mtu aliyejiajiri ambaye anafanya kazi yoyote ya asbestosi
(a)ataweka mipaka ya wazi na kutambua eneo husika; na
(b)atahakikisha kuwa hakuna mtu anayeingia au kubaki katika eneo linalodhibitiwa la asbestosi isipokuwa awe amevaa vifaa kinga vya kupumulia stahiki kama ilivyoainishwa katika kanuni ya 18.

17. Ufuatiliaji wa afya

(1)Kila mkandarasi wa kazi ya asbestosi aliyeidhinishwa atahakikisha wafanyakazi wote wanaohusika katika kazi ya asbestosi na ambao wana uwezekano wa kukumbwa na vumbi la asbestosi, wako chini ya uangalizi wa afya na mkaguzi wa afya aliyeidhinishwa na Mkaguzi Mkuu.
(2)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (1), mkandarasi wa asbestosi aliyeidhinishwa atahakikisha kwamba mpango wa uchunguzi wa afya ulioandaliwa unatayarishwa kama masharti ya ajira, ambayo yatajumuisha—
(a)tathmini ya awali ya afya, inayofanywa na daktari aliyeidhinishwa mara tu au ndani ya siku kumi na nne baada ya mtu kuanza ajira, ambayo itajumuisha—
(i)tathmini ya historia ya afya na taaluma ya mfanyakazi;
(ii)uchunguzi wa kimwili unaofaa;
(iii)uchunguzi wa ziada ambao unapaswa kujumuisha upimaji wa utendaji kazi wa mapafu; na
(iv)uchunguzi mwingine wowote muhimu wa afya kama vile picha ya mionzi ya kifua ambayo, kwa maoni ya daktari wa afya wa mahali pa kazi aliyeidhinishwa ni muhimu ili kumwezesha daktari huyo kufanya tathmini inayofaa kwa afya.
(3)Mwajiri hataruhusu mfanyakazi ambaye amethibitishwa kuwa hatakiwi kufanya kazi za asbestosi na mkaguzi wa afya mahali pa kazi, kufanya kazi ya asbestosi:Isipokuwa kwamba, mfanyakazi husika anaweza kuruhusiwa kurudi kazini ikiwa imeidhinishwa kwa maandishi na mkaguzi wa afya kuwa anaweza kufanya kazi hiyo.
(4)Endapo imethibitishwa kuwa mfanyakazi hatakiwi kufanya kazi ya asbestosi kama ilivyoainishwa katika kanuni ndogo ya (4) kutokana na kuathiriwa na asbestosi, mwajiri atafanya uchunguzi wa tukio hilo.
(5)Kutoa taarifa ya matukio na ugonjwa kwa Mkaguzi Mkuu na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kunazingatiwa kama ilivyoainishwa.

18. Vifaa kinga

(1)Pale ambapo vifaa kinga vya kupumulia vimetolewa, mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba—
(a)kifaa husika kina uwezo wa kuweka kiwango cha kukumbwa na asbestosi chini ya kikomo cha kukumbwa mahali pa kazi;
(b)kifaa husika kinatumika, kinahifadhiwa na kutunzwa kwa usahihi na ipasavyo;
(c)taarifa, maelekezo, mafunzo na usimamizi ambao ni muhimu kuhusiana na matumizi ya kifaa kinga, yanatolewa kwa watu; na
(d)kifaa kinawekwa katika hali nzuri na utaratibu mzuri wa kufanya kazi.
(2)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atatakiwa—
(a)kutotoa kinga kwa mtu, isipokuwa pale ambapo kifaa hicho kimesafishwa na kimetakaswa; na
(b)kuwa na sehemu ya kuhifadhia vifaa kinga wakati ambapo havitumiki.
(3)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba, vifaa kinga vyote vilivyochafuliwa na vumbi la asbestosi vinasafishwa kwa uangalifu na—
(a)endapo vifaa kinga vinasafishwa kwenye eneo la kazi, tahadhari zitachukuliwa ili kuzuia uchafuzi wa eneo wakati wa kusafisha;
(b)maji ambayo yametumika kusafisha eneo la kazi yanaondolewa kwa njia ya kuzuia uchafuzi wa mazingira; na
(c)maji ambayo yametumika kusafisha vifaa yatachujwa kwa mujibu wa kanuni ya 11(3) kabla ya kutolewa kwenye mfumo wowote wa maji.
(4)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (3)(a), mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba hakuna mtu anatoa vifaa kinga vichafu kutoka mahali pa kazi.

19. Kuweka lebo na alama

(1)Asbestosi zote zilizo kwenye orodha mahali pa kazi, kama inavyotakiwa na kanuni ya 4 na 5, zitatambuliwa kwa uwazi kwa kutumia alama ya picha iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza.
(2)Taka zote za asbestosi zitawekwa lebo kama iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza.
(3)Sehemu ya ardhi iliyochafuliwa na taka za asbestosi, zitawekwa wazi na kuwekwa alama kwa kutumia lebo ya onyo iliyoainishwa katika Jedwali la Tatu.

20. Kumbukumbu

Mwajiri atatakiwa—
(a)kutunza kumbukumbu za orodha zote za asbestosi zilizopo, tathmini za uwezekano wa kukumbwa, taarifa za ufuatiliaji wa afya, na taarifa na mafunzo yaliyotolewa mahali pa kazi;
(b)kwa kuzingatia kanuni ya 20(c), kuhakikisha kumbukumbu kama ilivyoainishwa katika kanuni 20(a) apewe mkaguzi, isipokuwa kwamba kumbukumbu za afya za mtu binafsi, hatopewa bila kibali cha maandishi kutoka kwa mfanyakazi husika;
(c)kuhakikisha kumbukumbu za tathmini zote na orodha ya asbestosi zilizopo mahali pa kazi zinapatikana kwa ajili ya kusomwa na mwakilishi wa afya na usalama au kamati husika ya afya na usalama; na
(d)kutunza kumbukumbu zote zilizotajwa katika kanuni ya 20(a) kwa muda usiopungua miaka thelathini.

21. Mazuio

Mtu hataruhusiwa—
(a)kuuza, kutoa msaada, kutumia tena, kuirudisha katika matumizi asbestosi aubidhaa yenye asbestosi;
(b)kuhifadhi kwa muda asbestosi au bidhaa yenye asbestosi kwa muda zaidi ya miezi 3 kabla ya uondoaji;
(c)kuhifadhi kwa muda bidhaa yenye asbestosi iliyokusudiwa kutupwa kwa njia ambayo inaweza kuchafua ardhi au mifumo ya maji, au inaweza kusababisha kusambaa kwa vumbi la asbestosi;
(d)kutumia au kuruhusu matumizi ya hewa iliyo gandamizwa ili kuondoa vumbi la asbestosi kutoka kwenye sakafu au mtu;
(e)kutumia zana za nguvu ya umeme kukata, kusaga au kutoboa bidhaa yenye asbestosi;
(f)kuvuta sigara, kula, kunywa au kuweka chakula au vinywaji katika eneo linalodhibitiwa la asbestosi; na
(g)kusafisha au kutayarisha sakafu ya saruji yenye asbestosi kwa—
(i)kusafisha kwa maji yenye mgandamizo mkubwa;
(ii)kusafisha kwa kemikali;
(iii)kukwangua kwa maji au njia kavu;
(iv)kusugua kwa maji au njia kavu; na
(v)njia nyingine yoyote ya kusafisha au kuandaa sakafu.

Jedwali la Kwanza (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 19(1)(2))

Alama ya asbestosi

HATARI: ASBESTOSIINAWEZA KUSABABISHA SARATANIASBESTOSIHATARI INAWEZA KUSABABISHA SARATANI KWA KUVUTA PUMZIUsishughulike kufanya lolote kwenye eneo hili hadi tahadhari zote zilizoelekezwa katika Kanuni za Uondoajiwa Asbestosi na Karatasi ya Maelezo ya Usalama isomwe na kueleweka.Usivute vumbi. vaa kifaa cha kufunika uso cha kupumulia.Zingatia Kanuni za Upunguzaji wa Asbestosi zilizobainishwa katika vipengele vya kuzuia.Wakati wa kuoga, ondoa glavu na ovaroli za kutupwa kabla ya kuondoa kifaa cha kupumulia.Tupa taka za asbestosi, kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191.

Jedwali la Pili (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 12(3))

Fomu ya taarifa ya jumla ya kazi inayohusisha asbestosi

[Editorial note: The form has not been reproduced]

Jedwali la Tatu (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 19(3))

Mahitaji ya kuweka lebo kwa taka za asbestosi

A. Sampuli ya lebo ya eneo lililochafuliwa

B. Sampuli ya ishara ya onyo kwa eneo linalodhibitiwa

▲ To the top

History of this document

07 April 2023 this version
03 April 2023
Assented to