Kanuni za Vifaa Kinga za Mwaka 2023

Government Notice 292 of 2023

Kanuni za Vifaa Kinga za Mwaka 2023

Tanzania
Factories Act

Kanuni za Vifaa Kinga za Mwaka 2023

Tangazo la Serikali 292 ya 2023

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 109]

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Vifaa Kinga za Mwaka 2023.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—egonomia” maana yake ni muingiliano sahihi unaozingatia mahitaji ya kimaumbile na kiutambuzi ya mtu na mazingira anayoishi au kufanyia kazi;kifaa kinga” maana yake ni kifaa chochote kilichotengenezwa kwa ajili ya kuvaliwa au kutumika na mtu kwa ajili ya kumlinda dhidi ya kihatarishi kimoja au zaidi cha afya na usalama, ambacho—
(a)kimetengenezwa na vitu kadhaa ambavyo vimeunganishwa kikamilifu na mtengenezaji kwa ajili ya kumlinda mtu dhidi ya hatari moja au zaidi zinazoweza kutokea kwa wakati mmoja;
(b)kinaweza kuvaliwa chenyewe au kuvaliwa pamoja na visivyo vifaa kinga kwa ajili ya kufanya kazi fulani; na
(c)kinaweza kuwa na kitu au sehemu ambayo inaweza kubadilishwa kwa ajili ya ufanisi wa kifaa hicho;
Mamlaka” maana ni Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

3. Matumizi

(1)Kanuni hizi zitatumika katika maeneo yote ya kazi kama ilivyoelezwa katika Sheria.
(2)Kanuni ya 4 hadi ya 12 hazitatumika kuhusiana na vifaa kinga ambavyo ni—
(a)nguo za kawaida na sare ambazo hazilindi afya na usalama wa mvaaji;
(b)vifaa vinavyobebeka vya kugundua na kuashiria hatari; na
(c)vifaa vinavyotumika wakati wa michezo.
(3)Kifaa kinga chochote cha kichwa kinachotolewa kwa mujibu wa Kanuni hizi kitazingatia Sheria au amri nyingine yoyote ambayo inatekeleza masharti yoyote ya usanifu au utengenezaji kuhusiana na afya au usalama katika sekta husika.

4. Utoaji wa vifaa kinga

(1)Kila mwajiri atahakikisha anawapatia vifaa kinga stahiki wafanyakazi ambao wanaweza kuwa katika hatari za kiafya na kiusalama kazini isipokuwa pale ambapo hatari hiyo imedhibitiwa vya kutosha kwa njia nyinginezo.
(2)Mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa anatumia kifaa kinga sahihi akiwa katika hatari ya kiafya au kiusalama kazini isipokuwa pale ambapo hatari hiyo imedhibitiwa vya kutosha kwa njia nyinginezo.
(3)Bila kuathiri masharti ya kanuni ndogo ya (1) na (2) kifaa kinga hakitakuwa sahihi isipokuwa kama kinafaa kutumika kujikinga na hatari zilizopo katika eneo la kazi na hali hatarishi ambayo wafanyakazi wanaweza kukumbana nayo ikiwa—
(a)kinazingatia mahitaji ya egonomia na hali ya afya ya mtu au watu ambao watakitumia;
(b)kina uwezo wa kumtosha mtumiaji kwa usahihi, kama kuna ulazima wakufanya marekebisho, yazingatie wigo wa uhitaji kulingana na muundo wa kifaa;
(c)kwa kadri inavyowezekana, kinaufanisi wa kuzuia au kudhibiti hatari bila kuongeza hatari zaidi; na
(d)kinazingatia sheria yoyote ambayo inatekelezwa chini ya masharti ya muundo au utengenezaji kulingana na afya au usalama wa kifaa kinga.

5. Tathmini ya kifaa kinga

(1)Kila Mwajiri atahakikisha kuwa, endapo kuna hatari zaidi ya moja kwa afya au usalama, mfanyakazi wake anavaa au kutumia kwa wakati mmoja kifaa kinga zaidi ya kimoja, na kuhakikisha kuwa kifaa hicho kinaendana na kinaendelea kuwa na ufanisi dhidi ya hatari zinazohusika.
(2)Kila mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa, endapo kuna hatari zaidi ya moja kwa afya au usalama, anavaa au kutumia kwa wakati mmoja zaidi ya kifaa kinga kimoja, na atahakikisha kifaa hicho kinaendana na kinaendelea kuwa na ufanisi dhidi ya hatari zinazohusika.

6. Tathmini ya kifaa kinga

(1)Kabla ya kuchagua kifaa kinga chochote kwa mujibu wa kanuni ya 4, mwajiri atahakikisha kwamba mapendekezo muhimu ya mwakilishi wa afya na usalama au kamati ya afya na usalama na afisa usalama yanazingatiwa.
(2)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kuwa tathmini inafanywa ili kubaini kama kifaa kinga kinafaa.
(3)Tathmini inayotakiwa na kanuni ndogo ya (2) itajumuisha—
(a)tathmini ya hatari yoyote au hatari kwa afya au usalama ambayo haiepukiki kwa njia nyingine;
(b)ufafanuzi wa sifa ambazo lazima kifaa kinga kiwe nazo ili kiwe na ufanisi dhidi ya hatari zilizotajwa katika kanuni ndogo ya 3(a), na kwa kuzingatia hatari zozote ambazo kifaa chenyewe kinaweza kusababisha; na
(c)ulinganisho wa sifa za vifaa kinga vilivyopo na sifa zilizotajwa katika kanuni ndogo ya (3)(b).
(4)Kila mwajiri au mtu aliyejiajiri anayetajwa na kanuni ndogo ya (1) atahakikisha tathmini inafanywa, inapitiwa na mabadiliko yanazingatiwa iwapo—
(a)kuna sababu ya kudhaniwa kuwa hakifai; au
(b)kumekuwa na mabadiliko makubwa katika kazi ambayo kinahusiana nayo.

7. Utunzaji na ubadilishaji wa kifaa kinga

(1)Kila mwajiri atahakikisha kwamba kifaa chochote cha kujikinga kinachotolewa kwa wafanyakazi wake kinatunzwa, kinabadilishwa, kinakarabatiwa au kusafishwa ili kifanye kazi iliyokusudiwa kwa ufanisi.
(2)Kila mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kifaa chochote cha kujikinga anachokitumia anakitunza, anakibadilisha, anakikarabati au anakisafisha ili kifanye kazi iliyokusudiwa kwa ufanisi.
(3)Kila mwajiri au mtu aliyejiajiri atahakikisha kwamba kifaa kinga chochote ambacho kimethibitika kuwa hakiwezi kutunzwa, kukarabatiwa au kusafishwa hakitumiki.

8. Uhifadhi wa kifaa kinga

Pale ambapo mwajiri au mtu aliyejiajiri anahitajika, kwa mujibu wa kanuni ya 4, atahakikisha anatoa au anatumia vifaa kinga, pia atahakikisha uhifadhi unaofaa wa vifaa hivyo wakati havitumiki.

9. Taarifa, maelekezo na mafunzo

(1)Pale ambapo mwajiri anatakiwa kuhakikisha vifaa kinga vinatolewa kwa mwajiriwa, atahakikisha kwamba mfanyakazi anapewa taarifa, maelekezo na mafunzo ambayo yatajumuisha—
(a)hatari ambazo kifaa kinga kitaepusha au kupunguza na mipaka ya matumizi;
(b)wafanyakazi wanaelekezwa na kufunzwa jinsi ya kuvitumia, kuvisafisha na kuvitunza;
(c)madhumuni na namna ambayo kifaa kinga kitatumika; na
(d)hatua za kuchukuliwa na mfanyakazi ili kuhakikisha kuwa kifaa kinabaki katika hali ya ufanisi na kufanya kazi iliyokusudiwa kama inavyoelekezwa na kanuni ya 7(1).
(2)Bila kuathiri masharti ya kanuni ndogo ya (1), taarifa na maelekezo yanayotolewa kwa mujibu wa kanuni hiyo hayatatosheleza na kufaa isipokuwa kama yataeleweka kwa watu waliokusudiwa.

10. Matumizi ya kifaa kinga

(1)Mwajiri atachukua hatua zote zinazofaa ili kuhakikisha kifaa kinga kinachotolewa kwa wafanyakazi wake kwa mujibu wa kanuni ya 4(1) kinatumika ipasavyo.
(2)Mfanyakazi atatumia kifaa kinga chochote alichopewa kwa mujibu wa kanuni hizi kulingana na mafunzo na maelekezo ya matumizi ya kifaa kinga alichopatiwa kwa mujibu wa kanuni ya 9.
(3)Mtu aliyejiajiri atatumia kikamilifu na ipasavyo kifaa kinga chochote kwa mujibu wa kanuni ya 4(2).
(4)Mfanyakazi na mtu aliyejiajiri ambaye amepewa kifaa kinga kwa mujibu wa kanuni ya 4 atachukua hatua zote zinazofaa ili kuhakikisha kinarejeshwa mahali maalum pa kuhifadhia baada ya matumizi.
(5)Kazi ambayo inachukua muda mfupi au mfanyakazi ana uzoefu nayo kwa muda mrefu na haijawahi kusababisha ajali haitazuia matumizi ya vifaa kinga.
(6)Mwajiri au mtu aliyejiajiri atatumia vifaa kinga kama suluhisho la mwisho la kinga dhidi ya hatari.

11. Utoaji wa taarifa ya upotevu au uharibifu

Mfanyakazi ambaye amepewa kifaa kinga kwa mujibu wa kanuni ya 4(1) atatoa taarifa ya upotevu au uharibifu wa kifaa hicho mara moja kwa mwajiri wake mara baada ya kupotea au kuharibika.

12. Uthibitisho wa ubora wa vifaa kinga

(1)Itakuwa ni wajibu wa kila mtu ambaye, anasanifu, anatengeneza, anaingiza au anasambaza vifaa kinga, kukusanya taarifa na kuwasilisha nyaraka za kitaalamu kwa mamlaka husika kuhusu matumizi ya kifaa yaliyokusudiwa, kujaribiwa na kuidhinishwa na kuhusu hali yoyote ya muhimu ili kuhakikisha matumizi sahihi kwa ajili ya kulinda usalama wa wafanyakazi.
(2)Uwasilishaji wa nyaraka za kitaalamu kama ilivyo katika kanuni ndogo ya (1) hautahitajika kwa mazingira ya aina ya kifaa kinga chenye usanifu rahisi ambapo msanifu anadhani mtumiaji atatathmini viwango vya uzuiaji wa hatari ndogo ambapo madhara yake yanaweza kutambuliwa na mtumiaji kadiri ya muda.

13. Vifaa kinga dhidi ya kemikali na visababishi vya muwasho

Itakuwa ni wajibu wa mwajiri kuwapatia wafanyakazi—
(a)vifaa kinga vya kupumulia vinavyofunika mwili mzima kwa ajili ya kumlinda mfanyakazi dhidi ya mazingira ya kazi yenye viambata vya sumu;
(b)vifaa kinga vya kupumulia vinavyofunika mwili mzima kwa ajili ya kumlinda mfanyakazi dhidi ya mazingira ya kazi yenye viambata vya sumu;
(c)vifaa kinga vinavyomlinda mfanyakazi dhidi ya madhara ya kemikali au mionzi ayonishi; na
(d)vifaa kinga vya dharura kwa ajili ya matumizi katika mazingira ya joto la juu ambalo madhara yake yanalinganishwa na yale ya joto la hewa la 100oC au zaidi na ambalo linaweza kuwa au lisiwe na sifa ya kuwepo kwa mionzi isiyo ayonisha, miale ya moto au kumwagika kwa kiasi kikubwa cha vitu vinavyoyeyuka.
▲ To the top

History of this document

07 April 2023 this version
03 April 2023
Assented to