Kanuni za Matumizi ya Mafao ya Mwanachama kama Dhamana ya Mkopo wa Nyumba za Mwaka 2024

Government Notice 149 of 2024

Kanuni za Matumizi ya Mafao ya Mwanachama kama Dhamana ya Mkopo wa Nyumba za Mwaka 2024

Tanzania
Social Security (Regulatory Authority) Act, 2008

Kanuni za Matumizi ya Mafao ya Mwanachama kama Dhamana ya Mkopo wa Nyumba za Mwaka 2024

Tangazo la Serikali 149 ya 2024

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 38]

Sehemu ya kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Matumizi ya Mafao ya Mwanachama kama Dhamana ya Mkopo wa Nyumba za Mwaka 2024.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—Bodi” maana yake ni Bodi ya Wadhamini ya Mfuko;Divisheni” maana yake ni Divisheni inayohusika na masuala ya hifadhi ya jamii iliyopo ndani ya Wizara yenye dhamana na masuala ya hifadhi ya jamii;Mfuko” ina maana iliyotolewa kwenye sheria ya mfuko husika;michango” maana yake ni michango inayolipwa kwenye Mfuko kama ilivyoainishwa kwenye sheria za mifuko ya pensheni;mwanachama” maana yake ni mwajiriwa au mfanyakazi aliyesajiliwa katika skimu na inajumuisha mwanachama anayestahili, au anayepokea, mafao chini ya skimu;mwanachama anayestahili” maana yake ni mwanachama ambaye amechangia kwa kipindi kisichopungua miezi mia moja themanini ambapo kati ya miezi hiyo, michango ya miezi kumi na mbili ni lazima iwe imechangwa mfululizo kabla ya tarehe ya kutolewa kwa dhamana;mwongozo wa uendeshaji” maana yake ni nyaraka ya ndani ya Mfuko inayoelekeza namna ya utekelezaji na utoaji wa dhamana za mikopo chini ya Kanuni hizi;mkopo wa nyumba” maana yake ni mkopo unaotolewa kwa mwanachama anayestahili kwa malengo ya kununua, kujenga au kuboresha nyumba ya makazi ambayo imedhaminiwa na nyumba yenyewe kama dhamana ya kwanza;Sheria” maana yake ni Sheria ya Hifadhi ya Jamii;[Sura ya 135]taasisi” maana yake ni mabenki na taasisi nyingine za fedha zilizosajiliwa na kupata leseni chini ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha.[Sura ya 342]

Sehemu ya pili – Dhamana

3. Matumizi ya mafao kama dhamana

(1)Mwanachama anaweza kuruhusu sehemu ya stahili ya mafao yake kutoka kwenye Mfuko itumike kama dhamana kwa ajili ya kupata mkopo wa nyumba kutoka kwenye taasisi za fedha ili kumwezesha—
(a)kujenga nyumba ya makazi kwenye kiwanja anachomiliki kisheria;
(b)kununua nyumba ya makazi; au
(c)kuboresha, kubadilisha au kufanya ukarabati wa nyumba ambayo mwanachama anamiliki kisheria.
(2)Mfuko hautatoa dhamana zaidi ya moja kwa mwanachama anayestahili.
(3)Mfuko utatoa dhamana kwa mwanachama baada ya kuwasilisha maombi rasmi kama ilivyoainishwa kwenye mwongozo wa uendeshaji wa Mfuko.
(4)Mfuko utahakiki maombi ya mwanachama kwa ajili ya kubaini sifa za mwombaji na mwanachana atajulishwa matokeo ya uhakiki huo.

4. Kiwango cha mafao kwa ajili ya dhamana

(1)Kiwango cha mafao kitakachotolewa kama dhamana ya mkopo wa nyumba kitakuwa—
(a)si zaidi ya asilimia hamsini ya kiwango cha mafao anachostahili mwanachama wakati wa maombi; au
(b)kiwango cha thamani ya soko ya nyumba hiyo,
ambapo kiwango cha chini kati ya viwango vilivyotajwa katika aya (a) na (b) kitachukuliwa.
(2)Pale ambapo ununuzi wa nyumba haujakamilika na bei ya ununuzi imekubaliwa na pande zote mbili, thamani ya nyumba hiyo haitakuwa kwa kiwango cha juu kuliko bei ya ununuzi iliyoainishwa na wahusika kwa madhumuni ya ushuru wa stempu.
(3)Iwapo lengo la mkopo ni kuboresha, kubadilisha au kukarabati nyumba ya makazi, makadirio ya bei ya soko ya nyumba hayatazidi gharama za maboresho, mabadiliko au ukarabati.

Sehemu ya tatu – Masharti ya dhamana

5. Masharti ya dhamana kwa mwanachama

Mwanachama atakuwa na sifa ya kupata dhamana ya Mfuko kama amekidhi masharti yafuatayo:
(a)awe ni raia wa Tanzania;
(b)awe mwanachama anayestahili; na
(c)uhai wa dhamana hauzidi umri wa kustaafu wa lazima wa mwanachama.

6. Masharti ya dhamana kwa taasisi

Taasisi itakayohitaji dhamana ya Mfuko kwa ajili ya mkopo kwa mwanachama itapaswa—
(a)kupata idhini ya Divisheni;
(b)kuwa na miongozo toshelezi na mifumo ya udhibiti wa ndani kwa lengo la kusimamia na kuendesha utaratibu wa mikopo;
(c)kutunza na kuhuisha taarifa sahihi kuhusu mwenendo wa akaunti ya mkopo ya mwanachama; na
(d)kutoa taarifa kadiri itakavyohitajika na Mfuko.

7. Maombi ya idhini

(1)Taasisi yoyote itakayotaka kutoa mkopo chini ya Kanuni hizi itapaswa kuwasilisha maombi kwa maandishi kwenye Divisheni kwa ajili ya kupata kibali cha kutoa mikopo hiyo.
(2)Maombi yatakayowasilishwa chini ya kanuni ndogo ya (1) yatapaswa kuambatishwa na nyaraka zifuatazo:
(a)nakala ya hati ya usajili wa kampuni;
(b)nyaraka za uendeshaji wa kampuni;
(c)nakala ya cheti cha usajili kutoka Benki Kuu ya Tanzania;
(d)nakala ya leseni halali ya biashara;
(e)taarifa za fedha zilizokaguliwa;
(f)maelezo na wasifu wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa juu wa mwombaji;
(g)maelezo kuhusu uzoefu wa mwombaji katika utoaji wa huduma zinazohusiana na mkopo wa nyumba; na
(h)idhini nyingine yoyote kutoka katika mamlaka husika itakayohitajika kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(3)Divisheni itashughulikia maombi na kutoa idhini kwa maandishi ndani ya siku thelathini tangu tarehe ya kupokea maombi, na endapo itakataa kutoa idhini, itamtaarifu mwombaji kwa maandishi ikieleza sababu za kukataa maombi yake.

8. Masharti ya utoaji wa mikopo

(1)Mfuko utaingia mkataba na taasisi kwa lengo la kuainisha utaratibu wa utoaji wa mikopo kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni hizi.
(2)Taasisi haitapaswa kutoa mkopo kwa mwanachama isipokuwa kama masharti ya Kanuni hizi yamezingatiwa.

Sehemu ya nne – Kiwango cha dhamana

9. Kiwango cha dhamana

Kiwango cha dhamana ya mkopo wa nyumba chini ya Kanuni hizi hakitazidi asilimia hamsini ya mafao anayostahili mwanachama wakati wa kufanya maombi.

10. Dhamana ya mkopo

(1)Mfuko hautatoa dhamana ya mkopo wa nyumba chini ya Kanuni hizi isipokuwa kama mkopo huo umetolewa kwa masharti yafuatayo:
(a)nyumba ya mkopo ndiyo imewekwa kuwa ni dhamana ya kwanza kwenye mkopo huo; na
(b)mwanachama ametoa ridhaa kwa Mfuko kuidhinisha kiwango cha mafao ambayo anastahili kutumia kama dhamana chini ya Kanuni hizi.
(2)Kabla ya kuidhinisha kiwango cha dhamana, taasisi itapaswa kuuhakikishia Mfuko kwamba mkopo na mali inayotumika kama dhamana ya kwanza imekatiwa bima katika taasisi ya bima inayokubalika kisheria.

Sehemu ya tano – Uhai wa dhamana

11. Uhai wa dhamana

Dhamana iliyotolewa chini ya Kanuni hizi itakuwa hai hadi yatakopotokea yafuatayo:
(a)kukoma kwa uanachama wa mwanachama husika wa Mfuko kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko;
(b)mwanachama anapokuwa amemaliza kulipa deni la mkopo na kupata uthibitisho kutoka kwenye taasisi husika;
(c)mwanachama na taasisi wamejihusisha katika makubaliano yanayokiuka masharti ya Kanuni hizi.

12. Kutumika kwa dhamana

(1)Dhamana iliyotolewa chini ya Kanuni hizi itaweza kutumika iwapo mwanachama atakuwa ameshindwa kulipa mkopo na taasisi imewasilisha kwenye Mfuko ushahidi kwamba njia zote za kurejesha mkopo huo, ikiwa ni pamoja na kutumia dhamana ya kwanza kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa kwenye mkataba, zimetumika kwa ukamilifu.
(2)Malipo yoyote yatokanayo na matumizi ya dhamana yatakayolipwa na Mfuko kwenye taasisi kwa mujibu wa masharti ya Kanuni hizi yatakatwa kutoka kwenye mafao ya mwanachama.
(3)Kiasi kitakacholipwa na Mfuko kutokana na matumizi ya dhamana hakitazidi kiasi cha dhamana iliyowekwa.

13. Usuluhishi wa migogoro

(1)Iwapo kutatokea mgogoro baina ya mwanachama na taasisi kuhusu utekelezaji wa suala lolote chini ya Kanuni hizi, Mfuko utakuwa msuluhishi wa mgogoro huo.
(2)Iwapo kutatokea mgogoro baina ya Mfuko na taasisi kuhusu utekelezaji wa suala lolote chini ya Kanuni hizi, Divisheni itakuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

14. Taarifa

Mfuko utapaswa kuwasilisha taarifa kwenye Divisheni kwa kila robo mwaka ikionesha kiwango na idadi ya dhamana zilizotolewa, pamoja na maelezo ya malipo ya mikopo na dhamana zilizotumika na zilizoisha muda wake.

Sehemu ya sita – Kuhama kwa mwanachama kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine

15. Uhamisho kwenda kwenye mifuko

Uhamisho wa mwanachama kutoka Mfuko mmoja kwenda mwingine hautaathiri dhamana iliyotolewa chini ya Kanuni hizi.

16. Ujumuishwaji

Mwanachama yeyote ambaye amechangia kwenye Mfuko zaidi ya mmoja, kwa madhumuni ya Kanuni hizi, atakuwa na haki ya kujumuisha vipindi vya uchangiaji wake kwa mujibu wa mwongozo wa ujumuishaji uliotolewa na Divisheni.
▲ To the top

History of this document

08 March 2024 this version
06 February 2024
Assented to