Sheria Katika Lugha Rahisi: Kujenga Uwezo aa Jamii Kupitia Sheria





KUJENGA UWEZO WA JAMII KUPITIA SHERIA

SHERIA KATIKA LUGHA RAHISI



KIMETOLEWA NA CHAMA CHA WANASHERIA TANZANIA BARA (TANGANYIKA LAW SOCIETY) KWA UFADHILI WA TAASISI YA LEGAL SERVICE FACILITY (LSF)

FEBRUARI, 2016

SHUKRANI

Kamati ya Msaada wa Sheria ya Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara inatoa shukrani za pekee kwa wadau mbalimbali kutoka mashirika ya kutoa msaada wa kisheria kwa ushauri wao maridhawa katika kuandaa kijarida hiki cha Kujenga uwezo wa jamii kutumia sheria.

Pili, Shukrani ziende kwa Taasisi ya Legal Service Facility (LSF) kwa ufadhili na ushauri wa kipekee katika kuandaa kijarida hiki.

Pia Kamati inatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria chini ya Rais Charles Rwechungura na Sekretariat ya Chama chini ya Kaleb Gamaya kwa rasilimali na ushirikiano waliotoa katika kukamilisha kazi hii muhimu kwa taifa letu inayolenga kukuza uelewa wa sheria miongoni mwa wananchi.

Utangulizi

Kujenga uwezo wa jamii kutumia sheria ni nyenzo muhimu ya kulinda, kutetea, kutafuta na kutekeleza haki. Wana jamii wakijengewa uwezo watafahamu kuwa sheria ni chombo cha kulinda, kutetea, kutafuta na kutekeleza haki na pia watafahamu namna ya kuitumia.

Kujenga ujuzi wa jamii kupitia sheria, kunahusisha utumiaji wa sheria kuongeza/kukuza uwezo wa watu na jamii kutawala maisha yao kupitia elimu ya sheria na hatua za kisheria. Hii ina maanisha mtu anakuwa na ujuzi na maarifa ya kutumia uelewa wa sheria alionao kubadilisha maisha yake na yale ya jamii inayomzunguka. Ujuzi na maarifa huongeza na hujenga uwezo wa mtu kisheria. Pia kupitia sheria, dhana ya utawala wa sheria inapanuliwa kuinufaisha jamii yote kwa ujumla, matajiri kwa masikini, wanaume kwa wanawake, waishio mijini na vijijini, bila kujali kuwa ni kundi la wengi au wachache.

Ujengwaji uwezo hutokea kwa mtu au kikundi cha watu pale hatua fulani zinapofanyika kukuza nafasi ya mtu au kikundi katika kufanya uchaguzi juu ya jambo fulani. Hii inahusisha kuimarisha uwezo wa mtu au jamii kufikiri na kwa makusudi kufanya uchaguzi kwa kubashiri kulingana na rasilimali walizonazo, ikiwamo mali, uwezo na mitazamo na uwezo ambao unajengwa kupitia fursa zilizoundwa katika sheria. Hivyo ujengewaji uwezo huangaliwa kama hatua na matokeo.

Sheria na kanuni zimekuwa zikitazamwa kama kikwazo katika kufikia haki. Ili kuifanya sheria imnufaishe kila mtu, sheria na kanuni zinatazamwa kama chombo kikuu cha kuwajengea uwezo watu wenye kipato cha chini. Hili si suala la haki kuimarishwa, bali kuwapa watu wenye kipato cha chini uwezo wa kutambua haki zilizopo katika mifumo ya sasa na kupambana na mifumo iliyopo inayozuia upatikanaji na utekelezaji wa haki hizo.

SEHEMU YA 1

Maana

Uelewa wa Sheria ni uwezo wa jamii fulani kujua sheria mbalimbali na uhusiano wa sheria hizo na maisha yao ya kila siku. Mara nyingi uelewa wa kisheria huwafanya wananchi kung’amua kuhusu ushiriki wao katika utungwaji wa sheria na pia utawala wa sheria.

Kwa maana pana, zaidi uelewa wa sheria utaonekana iwapo wananchi watakuwa na uwezo wa:

  • Kuchanganua sheria

  • Kufuatilia mchakato wowote wa kisheria

  • Kuangalia ni kiasi gani cha rasilimali kimewekwa Kuhakikisha kuna usimamizi na utekelezaji wa sheria

Kwa maana nyingine, jamii isiyo na uelewa wa kisheria itaona kuwa sheria hazifahamiki na watu, watu hawashiriki katika kutoa maoni wakati wa utungwaji wa sheria na pia hakuna rasilimali toshelevu kuwezesha utekelezaji wa sheria hizo.





Haki za watu ikiwemo mali na nyezo zake za kiuchumi zinaposhindwa kulindwa na sheria, mtu huyu huishi mazingira hatarishi, hukosa usalama na kuwa na uwezo mdogo katika uzalishaji. Kwa maana hiyo, ‘Uelewa wa Sheria’ unabeba maana pana zaidi kuonyesha umuhimu wake katika maendeleo na ukuaji wa kiuchumi wa mtu au kundi la watu.

Mbali na mambo mengine, kipengele muhimu sana katika kuongeza uelewa wa sheria kwa jamii ni utoaji wa elimu. Utoaji wa elimu ya kisheria ni muhimu sana kwa kuwa mbali na watu kupata elimu, pia jamii itaweza kupata taarifa muhimu kuhusu sheria. Cha muhimu ni kuhakikisha taarifa hizi zinatolewa kwa wakati na kwa usahihi.

Uelewa wa sheria kwa kundi la wanawake pia ni muhimu sana kwa kuwa kundi hili limebaguliwa na kutengwa kufikia haki nyingi. Ni jukumu la Serikali na asasi za kiraia kutoa elimu kwa makundi mbalimbali yaliyo na changamoto ili yaweze kufikia huduma za kisheria.

Faida za Uelewa wa Sheria kwa jamii

Uelewa wa sheria kwa jamii una faida kubwa zifuatazo:

  • Kujenga uwezo wa jamii kujiamini na kudai haki za kisheria pale zinapokiukwa

  • Kuimarisha uwajibikaji wa taasisi na vyombo mbalimbali

  • Husaidia kutolewa kwa fidia halisi katika ngazi zote

  • Wananchi kufahamu wajibu wao, kisheria, na kuuheshimu

  • Kupunguza kuwepo kwa mgongano kati ya wananchi na sheria

  • Wananchi kujenga imani na vyombo vya utoaji haki

Kuandaa Programu ya kujenga Uelewa wa Sheria

Ziko njia mbalimbali zinazoweza kutumika kuandaa Programu ya kujenga uelewa wa sheria kwa jamii:

  1. Kuandaa programu ya sheria kwa kuzingatia mahitaji ya jamii. Mfano kama programu inahusu wanawake au watu wanaoishi na ulemavu, basi mahitaji yao ndio yatakayoangaliwa zaidi. Kama wengi wa wanajamii hawajui kusoma na kuandika ni muhimu kuandaa programu kwa kutumia vipindi vya radio au vikundi vya uhamasishaji.

  2. Kuhakikisha sheria husika zinatafsiriwa kwa lugha nyepesi na inayoeleweka na kusambazwa kwa jamii.

  3. Ni muhimu kuhakikisha ushirikishwaji wa jamii husika katika programu iliyoandaliwa. Ushirikishwaji wa jamii utasaidia kujenga jamii inayobeba jukumu la kuwa wanamabadiliko na si kutegemea mabadiliko yanaletwa na mtu au kundi la watu wengine.

  4. Makundi mbalimbali ya jamii yashirikishwe katika program ya uelewa wa sheria bila kusahaulika. Mfano ni

  • umuhimu wa kushirikisha vijana wa kike na kiume, wazee, wanawake

  • kushirikisha makundi katika nyanja zote kama wasaidizi wa kisheria, wafanyabiashara, watoa huduma, wasanii, viongozi wa dini,wanahabari, wazee wa mila, shule n.k

  1. Kuandaa taarifa zingine muhimu kwa lugha nyepesi na lugha inayofahamika na makundi yote na kisha kuisambaza kwa jamii. Kuandaa taarifa kwa maandishi au kusambaza taarifa kwa njia mbadala. Mfano taarifa juu ya njia ya kutafuta na kupata haki bila msaada wa mwanasheria, njia ya kujieleza mahakamani, njia ya kusuluhisha migogoro, wajibu wa jamii katika kuheshimu sheria nk.

  2. Serikali katika ngazi zote kukubali na kushiriki kusaidia utekelezaji wa programu ya uelewa wa sheria. Mfano kushirikisha wasimamizi wa utekelezaji wa sheria katika mafunzo au kama wakufunzi Mfano polisi, mahakama, mabaraza ya kata, kamati maalum katika ngazi zote.

  3. Mara nyingi kuongezeka kwa uelewa wa sheria husababisha baadhi ya watu kuibua matatizo ya sheria yaliyowapata na hivyo kuhitaji huduma ya msaada wa sheria. Ni vema kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa kutoa taarifa juu ya taasisi zinazotoa huduma hizi au andaa mazingira maalum kuhakikisha wananchi hao wanapata msaada zaidi wa sheria.

Njia za kujenga Uelewa wa Kisheria kwa jamii

Ziko njia mbalimbali zinazoweza kutumika kutoa uelewa wa sheria kwa jamii.

B
aadhi ya njia hizo ni:

  • Kuandaa matamasha ya utoaji elimu

  • Uzinduzi wa kampeni

  • Kufanya mhadhara

  • Kuandaa warsha shirikishi

  • Kufanya maonyesho ya wazi

  • Kuandaa vipindi vya radio na luninga

  • Kuandaa mabango na vipeperushi

  • Kuweka michoro ya ukuta maeneo ya shule, biashara au barabarani

  • Kuandaa maonyesho ya picha

  • Kuandaa michoro ya vibonzo

  • Kutumia ubao wa matangazo kuweka taarifa muhimu hasa kwenye majengo au ofisi za serikali

Kubainisha vipingamizi katika kufikia Uelewa wa Sheria

Kwa kuwa lengo la kujenga uelewa wa sheria kwa jamii hulenga pia kuleta mabadiliko kuhusu mwenendo wa watu na taasisi husika basi vipingamizi huweza kutokea.

Ni vizuri kubainisha vipingamizi na kuwa na mikakati ya kuvishughulikia. Uzoefu unaonyesha vipingamizi vyaweza kusababishwa na elimu duni kwa jamii, umaskini au vikwazo vya kiuchumi, lugha, misimamo inayotokana na mila, desturi na tamaduni, imani na itikadi zinazoleta mitazamo tofauti, hali ya kisiasa na mwamko duni wa jamii kwa ujumla.

Mafanikio ya kuwepo kwa uelewa wa sheria

Ni vizuri kutathmini kama kuna matokeo chanya kwa jamii iliyolengwa kufikiwa katika kupata uelewa wa sheria. La muhimu ni je, watu kwa kuitumia mfumo wa sheria, wanaweza kujiongoza wenyewe na kuelewa kwa umakini kila hatua wanayoichukua?. Kama jibu kwa swali hili litakuwa ni ‘Ndiyo’ basi hii ni dalili nzuri ya kuwepo kwa uelewa wa kutosha wa sheria.

Kipimo cha kuwepo kwa mafanikio ya uelewa wa sheria ni iwapo jamii:

  • Inatambua haki na wajibu katika sheria

  • Ina uwezo wa kutambua tatizo la kisheria linapotokea na jinsi ya kulishughulikia

  • Inachukua hatua muafaka kushughulikia tatizo

  • Inafahamu mahali sahihi pa kupata taarifa kuhusu sheria na kuzipata inafahamu muda muafaka na mahali sahihi pa kupata msaada wa kisheria

  • Ina imani na mfumo wa sheria katika kutoa haki

  • Ina uelewa wa mchakato wote wa kufikia haki na kuona haki inafikiwa

Mbinu zilizooonyesha mfanikio


  1. Mafunzo ya wawezeshaji

Kuandaa mafunzo ya wawezeshaji kwa wanajamii kupitia warsha kutasaidia kujenga timu ya wawezeshaji wenye ujuzi. iwapo watachaguliwa toka katika vikundi mbalimbali vya jamii basi wataweza kupeleka elimu na ujuzi katika vikundi vyao na pia kwa jamii wanayoshirikiana nayo. Baada ya kukamilisha mafunzo ni vizuri wawezeshaji wakaandaa mpango kazi utakaotumika kueneza uelewa wa sheria kwa jamii husika. Pale inapowezekana, ufanyike uchambuzi wa mahitaji muhimu kama vifaa vinavyohitajika kufanikisha shughuli zao.

  1. Mafunzo kwa Jamii

Mafunzo ya jamii ni muhimu yakaandaliwa katika ngazi ya kaya au kijiji na yakafanyika kwa kuwepo kwa makubaliano kati ya wawezeshaji na jamii. Maandalizi yazingatie muda, mahali na nyenzo sahihi zinazohitajika ili kufanikisha kuwepo kwa uelewa wa sheria.

  1. Kusaidia shughuli za utetezi na ushawishi

Mara nyingi wanajamii wanapopata uelewa wa sheria huanza kushawishi mabadiliko ya sera, kanuni au tabia toka kwa viongozi wao. Ni muhimu ukawepo utaratibu wa kusadia harakati hizo kwa kutoa ushauri sahihi, kuandaa machapisho, mafunzo na kutoa rasilimali muhimu hata kwa uchache kutia moyo jitihada zinazofanywa na vikundi.

  1. Huduma ya kujitolea

Ni vizuri kutumia fursa iliyopo kwa kukaribisha wanafunzi walio vyuoni au waliohitimu fani ya sheria katika ngazi yeyote kutoa msaada wa kitaalamu kwa mashirika, vikundi na pia kusaidia kutoa elimu kwa jamii.

Wanafunzi wa sheria wanaweza kusaidia kuandaa vijarida vya sheria vitakavyotumika kutoa elimu, kufanya tafiti katika jamii, kuwezesha semina na warsha, kuandaa nyaraka za mahakamani na kusaidia ufuatiliaji wa miradi. Mbali na wanafunzi kuwa na uwezo wa kuisadia jamii, pia watapata fursa ya kujenga uwezo wao kitaaluma. Mara nyingi kupitia shughuli za jamii wasomi huweza kuchagua kwa usahihi zaidi wapi uwe mwelekeo wao wao kitaaluma.

  1. Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli

Ili kufanikisha shughuli katika kujenga uelewa wa jamii kuhusu sheria ni vyema kufanya ufuatiliaji wa kila shughuli ili kuona kama kuna mafanikio yaliyopatikana. Kama ni mafunzo, basi kubainisha ni kwa kiwango gani washiriki wameongeza uelewa juu ya sheria tofauti na hapo awali. Mara nyingi ufuatiliaji husaidia kurekebisha upangaji na uendeshaji wa shughuli zijazo.

Tathmini kwa upande mwingine hutoa nafasi ya kuona kama kuna matokeo yaliyozaliwa kutokana na shughuli zilizofanywa.



SEHEMU YA 2: Kujenga Uwezo wa jamii kutumia Sheria



Walengwa wa kupatiwa Uwezo kupitia sheria

Walengwa wa kupatiwa uwezo wa sheria ni kila mwanajamii ambaye hana ufahamu wa umuhimu na juu ya sheria zinazomzunguka. Tofauti inaweza kuwepo kuhusu kiwango cha uhitaji na uwezo wa mtu mmoja mmoja kufikia kiwango cha uwezo wa sheria. Mara nyingi watu maskini na wale wanaoishi katika mazingira magumu au kupitia changamoto za kimaisha, wamekuwa wakipewa kipaumbele zaidi. Neno masikini, katika hali ya kawaida, huzungumzwa katika muktadha wa kipato na mali. Lakini ili kuwapa watu uwezo kisheria, uwezo unaozungumziwa ni wa mtu masikini kuweza kutawala maisha yake. Hivyo basi, masikini ataweza kutawala maisha yake si kwa kutatua ukandamizwaji wa kiuchumi pekee, bali pia ukandamizwaji wa kijamii na kisiasa.

Nguzo Nne za Kuwapa Jamii Maskini na Watu Wenye Kipato cha Chini Uwezo

Mpango wa kuwapa watu uwezo kupitia sheria unaweza kutimia tu kwa kupitia mabadiliko ya mifumo yanayolenga kuwapa watu fursa ya kutumia uwezo wao wa kiraia na kiuchumi. Nguzo hizi nne ni:

  1. Upatikanaji wa Haki na Utawala wa Sheria

  2. Haki ya Kumiliki Mali

  3. Haki za Mahali pa Kazi

  4. Haki za Biashara


Nguzo ya Kwanza: Upatikanaji wa Haki na Utawala wa Sheria



Haki ya kwanza miongoni mwa haki zote ni haki inayotoa hakikisho la kupatikana haki zingine zote: kutendewa haki na utawala wa sheria. Uwezo wa kupitia sheria hauwezi kupatikana wakati watu masikini wananyimwa mfumo bora wa kisheria, aidha kupitia sheria mbovu au kupitia haki. Haki na majukumu ya jamii yanapotekelezwa kupitia sheria bora, kunakuwa na manufaa yasiyo na kipimo kwa kila mtu, hasa wenye kipato cha chini.

Kuhakikisha upatikanaji wa haki sawa si suala rahisi. Hata kama mfumo wa sheria unatambua usawa wa watu wote katika katiba, upatikanaji wa haki sawa unaweza kufikiwa tu kupitia kujitolea kabisa kwa serikali na taasisi za umma katika utekelezaji. Kwenye nguzo hii ya kwanza, hatua za kuwapa watu uwezo kupitia sheria lazima zihakikishe mambo yafuatayo:

  • Kuhakikisha kwamba kila mtu anapata haki ya kutambuliwa kisheria kwa kuandikishwa baada ya kuzaliwa.

  • Kuondoa au kubadilisha sheria zinazokinzana na haki, maslahi, na riziki za watu masikini.

  • Kufadhili na kubuniwa kwa mashirika ya serikali na makundi ya kiraia ikiwemo makundi maalum ya kuwasaidia, kisheria, watu waliotengwa.

  • Kubuni vyombo halali vya dola vya kushinikiza utekelezaji wa sheria, kwa mfano kupitia idara ya polisi isyoegemea upande mmoja.

  • Kuhakikisha upatikanaji rahisi wa huduma za mahakama rasmi, mifumo ya usimamizi wa ardhi, na taasisi zingine husika za umma, kwa kutambua na kujumuisha sheria zisizo rasmi zinazozingatiwa na watu mashinani, ambazo watu masikini tayari wanazielewa.

  • Kuhimiza mahakama kuzingatia maslahi ya watu masikini

  • Kuunga mkono njia za mbadala za kutatua mizozo miongoni mwa watu.

  • Kubuni taasisi za kuwasaidia watu kupata huduma za kisheria, ili watu wenye kipato cha chini wawe na ufahamu wa sheria na wazitumie kwa manufaa yao.

  • Kuunga mkono hatua madhubuti za kuwapa uwezo, kupitia sheria, wanawake, jamii za watu walio wachache, wakimbizi, watu waliopoteza makazi yao na jamii za kijadi.



Shirika: Women Legal Aid Centre (WLAC)

Mradi: Kampeni ya TUNAWEZA

Lengo: Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia katika jamii

Shughuli:

  1. Msaada wa Kisheria

  2. Elimu ya uelewa wa sheria kwa wanawake wenye migogoro ya kisheria



Huduma ya msaada wa kisheria na elimu ilitolewa kwa Aisha K. (miaka 52) aliyesaidiwa kufungua shauri la mirathi Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2009. Mbali na kupewa huduma ya msaada wa sheria WLAC Aisha alipokea elimu ya mirathi na haki za kisheria kupitia mafunzo yanayotolewa kwa wateja siku za huduma. Elimu hiyo imempa uwezo wa kujiamini. Aisha aliamua kutoa elimu aliyopata kwa wanawake wengine katika eneo la Manzese anakoishi. Mara kadhaa Aisha amewaleta wanawake wenye uhitaji wa kisheria kupata ushauri WLAC na wengine wameweza kufungua kesi kutokana na matatizo waliyokuwa nayo. Aisha huwasindikiza wanawake mpaka WLAC na kuhakikisha wamehudumiwa ipasavyo.

Mafanikio:

Maisha ya Aisha yamebadilika kabisa, kwani amekuwa mwanamabadiliko katika jamii yake kwa kujituma kusaidia wanawake wanaopitia changamoto za kisheria. Umri wa miaka 52 alionao si kikwazo cha kuendeleza harakati zake kwa jamii. Wanawake zaidi wananufaika kupitia kwake.

Nguzo ya Pili: Haki ya Kumiliki Mali

Kumiliki mali mtu binafsi au kwa vikundi ni haki ya binadamu. Mfumo halisi wa kusimamia umiliki wa mali unajumuisha vyombo vinne:

  • Sheria zinazoeleza haki na wajibu kati ya watu na mali,

  • Mfumo wa utawala

  • Soko la kubadilishana mali linalofanya kazi;

  • Chombo cha sera za kijamii.



Kila moja ya vyombo hivi, kinaweza kukosa kuwafaidisha watu wenye kipato cha chini au hata kuwakandamiza. Mfumo unapofanya kazi vizuri, unakuwa chombo cha kuwajumuisha watu wenye kipato cha chini katika uchumi rasmi, na wanapata njia ya kujiimarisha kijamii. Ikiwa mfumo mzima unashindwa kufanya kazi au hata mojawapo wa vyombo tanzi, watu wenye kipato cha chini wananyimwa fursa na kubaguliwa.

Ili mali ziweze kutumika kuleta faida, zinahitaji kutambuliwa rasmi katika mfumo unaojumuisha haki za mtu binafsi au makundi ya watu kumiliki mali. Hii inajumuisha:

  • kutambua haki za jamii katika ngazi za chini

  • Kuhifadhi kumbukumbuku ya haki hizi, stakabadhi na mikataba kulingana na sheria kunahakikisha usalama wa mali kwa familia na biashara.

  • Watu waondolewe kwa nguvu kwenye mali zao ikiwa tu kuna hatari ya usalama wa maisha au mali, au makubaliano ya mkataba yamekiukwa au chini ya taratibu za haki za utawala. Fursa ya mhusika kukata rufani lazima iwepo, na mhusika alipwe gharama za kuhamishwa kulingana na utaratibu.

  • Kutambulika kwa mali kuwape watu fursa ya kujiendeleza kupitia mikopo iliyodhaminiwa na mali zao.

  • Kumbukumbu ya taarifa za umiliki wa mali zinapohifadhiwa, mipango iliyofanyika katika nyakati na sehemu tofauti inakuwa chini ya mfumo mmoja wa sheria na kuleta uwiano. Hii inasaidia kuleta pamoja masoko ya kijamii, na kuwezesha biashara kupanuka zaidi pamoja na kuziweka chini ya mipango ya sheria inayotambulika rasmi na hivyo kulindwa na sheria iliyopo.


Shirika: Morogoro Paralegal Centre (MPCL)

Jina la mradi: Mama Ardhi

Lengo la mradi: Kujengea jamii uelewa kuhusu sheria za ardhi na umiliki wa ardhi kwa jamii hususani wanawake.

Mfadhili: Action Aid Tanzania

Eneo la mradi:

Mradi ulipangwa kutekelezwa katika vijiji 10 vya mkoa wa Morogoro ambavyo ni Mvuha, Dalla, Lukulunge, Kikundi, Kiloka, Kiziwa, Kibangile, Mtamba, Kongwa na Tawa. Wakati wa utekelezaji wa mradi kijiji cha Tawa kiliachwa kutokana na kugawanywa kuwa vijiji viwili.

Yaliyofanyika:

  1. Elimu kwa jamii kuhusu sheria za ardhi, katika kutoa elimu hiyo makundi yafuatayo yalifikiwa

  1. Halmashauri ya Kijiji

  2. Wajumbe wa mabaraza ya ardhi vijiji na kata

  3. Madiwani

  4. Wananchi katika maeneo ya mradi

  1. Kupima vijiji. Vijiji vipatavyo 9 viliweza kupimwa

  2. Kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi

  3. Kujenga majengo ya masijala katika vijiji 9

  4. Kununua vifaa vya Masijala

  5. Kuandikisha watu kwa ajili ya hati miliki za kimila

Mafanikio

  1. Mradi ulifanikiwa kufikia vijiji 9 kati ya 10, kwa maana hiyo mradi ulifanikiwa kwa asilimia 90. Wanainchi wenyewe kwa sehemu kubwa ndio waolifanikisha mradi huu.

  2. Wanajamii walijitokeza na kujiandikisha kupata hatimiliki za kimila, hati zipatazo 710 zilitolewa, ambapo 450 zilitolewa kwa wanaume, 200 wanawake na 60 umiliki wa pamoja.

  3. Viongozi ambao walikiuka sheria kwa kugawa ardhi bila kufuata taratibu kuwajibishwa.( mwenyekiti kijiji cha Dalla)

  4. Diwani kijiji cha Mtamba alichangia mabati20 kuongeza ukubwa wa masijala ambapo wasaidizi wa kisheria wamepatiwa ofisi.

  5. Diwani kutoka Konde, kijiji ambacho hakikuwa kwenye mradi amehamasika kufanyiwa mchakato na tayari ameshatoa mabati 10 kujenga masijala na MPLC tumeanzisha kituo kidogo cha wasaidizi wa kisheria.

Changamoto

  1. Mradi ulipokwisha MPLC inaendelea kuhamasisha jamii.

  2. Ukosefu wa rasilimali fedha ni kikwazo kikubwa.

  3. Viongozi kubadilishwa hususani wale wa kiserikali wenye dhamana kisheria na kupelekea ugumu katika kuhamasisha upatikanaji wa hati miliki za kimila.

  4. Mchango wa rasilimali fedha toka serikalini ulikuwa mdogo.

Hatua za Kuwapa watu uwezo kupitia sheria ya haki za kumiliki mali lazima izingatie mambo yafuatayo:

  1. Kuhimiza usimamizi bora wa mali zinazomilikiwa na watu binafsi au makundi ya watu ili kuleta pamoja shughuli za kiuchumi zisizotambulika rasmi kisheria, na zile zinazotambulika katika sheria iliyopo, pamoja na kuhakikisha usawa.

  2. Kuhakikisha kwamba mali inayomilikiwa inatambulika na kulindwa kisheria na kwamba wamiliki wote wanapata haki sawa.

  3. Kuhakikisha kwamba kuna soko au taasisi za kubadilishana mali kwa watu wote lenye uwazi na uwajibikaji.

  4. Kuongeza wigo wa haki za kumiliki mali, kujumuisha upatikanaji wa kibali cha kumiliki, kupitia mipango ya kijamii au mipango mingine ya umma kama vile upatikanaji wa nyumba, mikopo yenye viwango vya chini vya riba, na ugavi wa ardhi ya umma.

  5. Kuhimiza mfumo wa wa haki za kumiliki mali, unaotambua mali zilizonunuliwa na wanaume zinamilikiwa kwa pamoja na wake zao.

Nguzo ya Tatu: Haki za Mahali pa Kazi

Watu masikini hutumia muda mwingi mahali pa kazi huku kipato bado hakitoshi kumudu maisha. Uhalali au kukubalika kwa uchumi kunategemea haki za msingi za ajira, sawa na uwezo wa kufanya kazi unaohitajika ili uchumi kukua. Pia kuimarika kwa haki za kazi na za kijamii, kunategema soko la kiuchumi lenye ufanisi na linalofanya kazi vizuri. Hii inaendana na kubadili mtindo wa siku zote wa uzalishaji duni, mapato ya chini na kuhatarisha maisha kazini na nafasi yake kuchukuliwa na utekelezaji wa kanuni za kimsingi za haki mahali pa kazi pamoja na ajenda ya mazingira bora ya kazi na mkakati wa kuhakikisha usalama na fursa kwa wafanyakazi katika biashara zisizotambulika rasmi.

Hili linawezekana kwa njia zifuatazo:

  • Kuheshimu, kuhimiza na kutambua uhuru wa watu kujiunga na makundi au vyama ili kuimarisha sauti ya uwakilishi wa wafanyakazi maskini katika midahalo ya kijamii na kisiasa kuhusu mabadiliko na miundo yake;

  • Kuimarisha taratibu za kusimamia maswala ya ajira na namna taasisi za kuyasimamia zinavyofanya kazi, na kuleta ulinganifu kati ya usalama, uzalishaji kwa watu masikini;

  • Kuhakikisha utekelezaji wa kisheria wa haki za wafanyakazi na wenye biashara ndogondogo zisizotambulika rasmi.

Sera na Haki za Kimsingi Kazini

  1. Kuongeza upatikanaji wa ajira katika uchumi unaokuwa, kujumuisha watu wote kwa usawa (wanawake, wanaume, vijana, wazee, walemavu, makundi ya watu wachache n.k).

  2. Kuimarisha mipango ya usalama wa mapato ya watu masikini kazini wakati kunapokuwa na mtikisiko wa kiuchumi au mabadiliko kazini;

  3. Kuimarisha hatua za upatikanaji wa matibabu, bima ya afya na mafao ya uzeeni.

  4. Kuhakikisha kwamba hatua za kuwapa watu uwezo kupitia sheria, zinazingatia viwango vya shirika la kazi duniani ambalo linalenga kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake na kutoa nafasi za kazi, kwa usawa, kwa wanawake, ambao ni nguzo muhimu katika kuangamiza umaskini.

Nguzo ya Nne: Haki za Kupata Kipato/Biashara

Watu wenye kipato cha chini wanapaswa kupata haki za mahali pa kazi na vile vile haki ya kuendeleza biashara zao wao wenyewe. Hii inajumuisha haki zifuatazo kwa mjasiria mali:

  1. Upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu wanaotaka kuanzisha biashara

  2. Usalama wa mali

  3. Uwezo wa kuwa na mikataba

  4. Kufanya makubaliano ya kibiashara

  5. Kujenga mitaji kupitia ununuzi wa hisa

  6. Kuhakikisha sheria ya usajili wa biashara inalinda riziki ya mwenye biashara wakati hasara inapotokea.

  7. Uwezekano wa vizazi vingine kurithi biashara.

Haki hizi ni lazima zipatikane kwa wenye biashara ndogondogo katika nchi inayostawi kama Tanzania, ambako biashara nyingi kama hizi zinaendeshwa na wanawake na zinaajiri sehemu kubwa ya nguvukazi. Mara nyingi kufanikiwa au kushindwa kwa sekta hii ya biashara ndogondogo kunaleta tofauti kati ya ufanisi na mdororo wa kiuchumi; nafasi nyingi za kazi na ukosefu wa ajira; kubuniwa kwa vyama vya wafanyabiashara na ukosefu wa usawa katika biashara.

Mhusika: Equality for Growth (EfG)

Mradi: Sauti ya Mwanamke sokoni (2012-2014)

Malengo: Kujenga sauti na uchumi wa wanawake wafanyabiashara sokoni ili waweze kudai uwajibikaji na utawala bora katika eneo la biashara

Eneo la mradi: Masoko 18 ya Dar-es-Salaam



Yaliyofanyika:

  1. Kuanzisha huduma ya wasaidizi wa kisheria ambao ni wafanyabiashara wenyewe.

  2. Kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) kama vikundi vya kiuchumi na kupokea elimu na ujuzi wa kisheria.

  3. Kutoa elimu ya haki za binadamu na sheria kwa wanawake na viongozi katika masoko.

  4. Kusambaza taarifa na machapisho juu ya haki na sheria za soko.

  5. Kusaidia hatua za kuleta mabadiliko masokoni ili kuimarisha uwajibikaji na kuongeza nafasi za wanawake katika uongozi. Mradi ulilenga kujenga uwezo wa wafanyabiashara kuelewa haki zao za kiuchumi na uwezo wao kama raia katika kuleta mabadiliko katika masoko. Elimu ya sheria ilitolewa kwa wanachama wa VICOBA vilivyoanzishwa na viongozi kupitia Kamati za soko.

Mafanikio:

  1. Ongezeko la wanawake katika kugombea uongozi kwa asilimia 50 ikilinganishwa na wale wa awali wa asilimia 30 wakichaguliwa kama viongozi katika masoko.

  2. Kuongezeka kwa idadi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za wanawake na wafanyabiashara yanayoripotiwa katika vyombo vya utekelezaji wa sheria. Wanafanyabiashara

  3. kuchukua hatua kufatilia haki zao.

  4. Kubadilika kwa mitazamo na tabia kandamizi kwa baadhi ya viongozi wa masoko.

  5. Kuongezeka kwa uwezo wa kiuchumi kwa wanawake ikiwemo kipato na kuendesha biashara mbadala kutokana na kupungua kwa matukio ya bughudha za kijinsia kwa wanawake. Hii imesaidia pia kujenga hali ya kujiamini kwa wanawake na kufanya kazi kwa umoja, ili sauti zao zisikike.

  6. Viongozi wa siasa kushughulikia kero za wanawake walio sokoni.



Changamoto:

  1. Bajeti ya fedha inayotengwa na Manispaa kuhudumia masoko ni ndogo.

  2. Kukosekana kwa usimamizi mzuri wa sheria zilizopo na mapungufu yake.

  3. Kuendelea kwa mfumo dume unaolenga kuwakandamiza wanawake, ikiwemo kuwanyima madaraka.

  4. Usimamizi duni wa ukusanyaji wa ushuru na mapato ya soko unaodumaza ufanisi wa masoko.

Hatua za kuwapa watu uwezo, kisheria, kupitia nguzo hii ya upatikanaji wa haki za kibiashara ni lazima:

  1. Zitoe hakikisho la upatikanaji wa haki za kibiashara, ikiwa ni pamoja na haki ya kuchuuza, kuwa na sehemu ya kufanyia biashara na mahitaji mengine, kama vile vibanda umeme, maji na usafi;

  2. Kuimarisha usimamizi bora wa kiuchumi unaorahisisha uwezekano wa kuanzisha na kuendesha biashara, uwezekano wa kupata wanunuzi na uwezo wa kuacha biashara hiyo panapo haja ya kufanya hivyo;

  3. Kuhakikisha usajili wa biashara unatambua tofauti kati ya biashara hiyo na mali za mtu binafsi, ili kuhakikisha usalama wa mali kama hizo endapo biashara itakumbwa na matatizo kisheria.

  4. Kuhakikisha wajasiriamali wanapata huduma muhimu za kifedha, kama vile benki za kuweka akiba, mikopo, bima, malipo ya uzeeni na mbinu nyingine za usalama wa biashara;

  5. Kuongeza nafasi za biashara, kupitia mipango maalum ya kuwahamasisha wajasiriamali kuhusu masoko yanayoibuka, na kuwasaidia kufuata taratibu zinazohitajika na pia mipango inayojenga uhusiano kati ya biashara ndogondogo na biashara kubwa.



Mifano ya Sheria Ambazo Zinawapa Watu Uwezo Kisheria

Zipo sheria nyingi Tanzania ambazo zinaweza kuleta tofauti katika kuwapa watu uwezo. Baadhi zinawalenga watu wanaokandamizwa pekee na baadhi zinalenga makundi yote ya watu. Sheria hizi zimeongelewa katika mada tofauti za kitabu hiki. Baadhi ya mifano ya sheria zenye matokeo ya kuwapa watu uwezo ni:

  1. Katika Mali

  • Sheria zinazopanua upatikanaji wa mikopo kwa dhamana ya mali isiyohamishika au mali ambayo dhahiri.

  • Sheria zinazorahisisha usajili, kwa mfano, usajili wa ardhi

  • Sheria zinazoongoza usajili na zinazorahisha matumizi ya mali zinazohamishika katika dhamana

  • Sheria zinazotoa haki ya kumiliki mali pasipo vizuizi visivyo vya lazima katika masharti, vibali, na taratibu.

  • Sheria zinazozuia utwaaji wa mali binafsi kwa manufaa ya umma pasipo fidia kamili na ya haraka.

  • Sheria zinazotoa haki ya kumiliki mali pasipo vizuizi visivyo vya lazima katika masharti, vibali na taratibu.

  • Sheria zinazozuia utwaaji wa mali binafsi kwa manufaa ya umma pasipo fidia kamili na ya haraka.

  • Sheria zinazoruhusu watu wasio na makazi rasmi kupata haki katika ardhi waliyotwaa na kutumia kwa amana.

  • Sheria zinazoweka utaratibu mzuri, kisheria, kwa watuamiaji wa ardhi, aidha rasmi ama siyo rasmi, ambao wapo katika hatari ya kufukuzwa au kunyang’anywa ardhi hiyo.

  • Sheria zinazozuia ubaguzi dhidi ya makundi yaliyo pembezoni.

  1. Katika Biashara

  • Sheria zinazounda utaratibu kwa ajili ya kutoa ushauri na kuzitegemeza biashara ndogo na mpya zikue.

  • Sheria zinazotengeneza fursa kwa biashara ndogo na kuanzisha mpya kupitia miradi na mikataba ya serikali.

  • Sheria za manunuzi ya bidhaa na huduma ambazo zinatoa fursa ya ushindani kwa wafanyabiashara wadogo na manufaa kwa wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo.

  • Sheria zinazotoa nafuu ya gharama za upatikanaji wa leseni za biashara na kuondoa vigezo vya viwango vya ubora ambavyo ni vya kibaguzi.

  • Sheria za mashirika na makampuni zinazolinda haki za wanahisa.

  • Sheria zinazoweka taratibu fasaha za kusitisha mkataba wa ajira dhidi ya mfanyakazi.

  1. Familia

  • Sheria zinazoimarisha haki za wanawake, hasa wajane na watalakiwa pamoja na watoto wa kike katika umiliki wa mali

  • Sheria zinazowalinda yatima dhidi ya unyang’anyi wa mali unaofanywa na walezi na wanafamilia

  1. Haki za Kisiasa

  • Sheria zinazoongeza uhuru wa watu kukusanyika kwa madhumuni ya kisiasa

  • Sheria zinazopanua haki ya kupiga kura na kuondoa vikwazo vya upigaji kura

  • Sheria zinazoruhusu wananchi kuwawajibisha viongozi waliowachagua

  • Sheria zinazowapa fursa wananchi kuchangia maoni katika kuandaa bajeti ya serikali za mitaa

  1. Utekelezaji wa Sheria

  • Sheria zinazokuza njia mbadala za utatuzi wa migogoro, aidha za kisiasa au za kitamaduni na kutambua makubaliano yanayoafikiwa.



Mwelekeo wa Kuwapa Watu Uwezo Kupitia Sheria

Ni muhimu kuelewa kwa kina na mapana kuwa katika kufanikisha lengo la kuwapa watu uwezo, kisheria, ni muhimu umasikini uangaliwe kama ukandamizwaji katika uwezo na fursa. Kwa mantiki hiyo, umasikini husababisha uwezo na fursa za mtu kufurahia na kuchangia upatikanaji wa haki zake za msingi unazuiliwa na sababu zilizo nje ya uwezo wake.

  1. Mwelekeo wa Kiuchumi

Ili kuwajengea uwezo watu, hasa katika uwezo wa kufanya biashara, uanzishaji na utekelezaji wa haki za umiliki wa mali na za wafanyakazi ni muhimu sana. Tokeo la kuwa na mfumo imara wa umiliki na uhifadhi wa mali na kuchangia kukuwa kwa pato la mwananchi hauchangiwi na uwepo wa sheria bora pekee, bali pia utaratibu mzuri wa namna gani ya kushawishi tabia ya mtu mmoja mmoja na ushirika.

Mabadiliko ya sheria pekee hayawezi kukagua kukua kwa biashara au kuhakikisha ulinzi na uhifadhi wa mali ambayo ni muhimu katika uwekezaji na uzalishaji.

Jitahada za kuanzisha biashara hufeli kwa sababu:

  • Gharama kubwa za uanzishaji na muda mrefu unaohitajika

  • Gharama kubwa na mlolongo mrefu wa kupata leseni za biashara

  • Rushwa

  1. Umiliki na Uhifadhi wa Mali

Haki ya kumiliki na kuhamisha mali, aidha kwa kuuza au kukodisha, ni sifa muhimu katika kumjengea uwezo mtu yeyote. Umiliki pekee hautoshi, bali mifumo ya kisheria na ya kijamii inabidi itambue umiliki na uhifadhi wa mali ili mwenye nayo aweze kuitumia kibiashara.

Hoja hii ni muhimu kwa sababu endapo mtu ana umiliki wa mali, lakini mifumo ya kisheria na kijamii haitambui umiliki huo, basi matokeo matatu yanaweza kumkabili:

  1. Kutumia muda na nguvu/jitihada kubwa kutetea mali hiyo dhidi ya wengine.

  2. Ni vigumu au siwezekane kabisa kutumia mali hiyo kibiashara

  3. Mali hiyo itakuwa na thamani ndogo na kama akiitumia kibiashara, basi hatafaidika nayo vile anavyostahili.



Kwa hiyo utambuzi wa haki ya umiliki na uhifadhi wa mali ni muhimu katika kumjengea mtu uwezo, na katika biashara, thamani ya mali inaendana na utambuzi na uhifadhi kisheria.

Ni muhimu pia, kufahamu kwamba nchini Tanzania, kuna mahusiano ya kibiashara katika mazingira mengi ambayo hayaongozwi au kuidhinishwa na sheria, bali hufanyika kwa amani kwa sababu jamii inatambua mahusiano hayo.

Mazingira haya pengine ni rahisi zaidi kukua baina ya watu wenye kipato cha chini hasa kwa lengo la makusudi la kukwepa mifumo rasmi ya uchumi ambayo hutizamwa na kundi hili kama kandamivu. Hivyo utambuzi wa mali kisheria na utumiaji wa kibiashara unahitaji kukubalika katika jamii ili mfumo huo rasmi ufanikiwe.

Kwa watu wenye kipato kidogo, ardhi ni rasilimali muhimu katika kuwajengea uwezo kiuchumi. Lakini pia, utambuzi wa mali nyingine zinazoweza kumilikiwa na kundi hili ni muhimu pia. Kwa mfano mazao yanayotarajiwa baada ya kuvuna yanaweza kutumika kama kigezo cha kupata mikopo endapo mfumo wa kisheria ukitambua.



  1. Faida Utambuzi na Uhifadhi wa Haki ya Kumiliki Mali

  1. Thamani kubwa ya mali

  2. Gharama ndogo kwa mmiliki katika kuhifadhi mali yake

  3. Nafasi au uwezo mkubwa wa kuwekeza

  4. Kunufaika na mipango, miradi na huduma za serikali kupitia umiliki wa mali hiyo, mfano ruzuku katika pembejeo za kilimo.

  5. Upatikanaji wa mikopo kwa kutumia mali kama dhamana

  6. Uwezo mkubwa wa kutumia mali kibiashara

  7. Uwezo mkubwa wa kuhamisha mali kwa faida kubwa kwa namna mbalimbali, kwa mfano kuuza, kupangisha, dhamana/ rehani au kuhamisha katika ushirika wa wafanyabiashara (trust)

  1. Mwelekeo wa Kijamii

Katika kuwapa uwezo wa kisheria, mwelekeo wa kijamii unaangalia uwezo wa mtu wa kipato cha chini kudai au kufanyia kazi haki alizonazo kisheria. Mwelekeo wa Kijamii katika kuwapa watu uwezo unajuimsha:

  1. Sheria na Utaratibu

Uwepo wa chombo/vyombo madhubuti, kama vile serikali ya mtaa, polisi, ambavyo vinahakikisha kuwa usalama wa maisha na mali za watu vinalindwa kwa ajili ya kuwapa fursa za maendeleo. Uhalifu, vurugu na migogoro hugharimu maisha ya watu ambao ndio nguvu kazi, lakini pia huathiri shughuli za kiuchumi na uwezo wa watu kudai na kulinda haki zao kwa umoja pasi hofu.

  1. Ushirikishwaji

Umuhimu wa Ushirikishwaji upo hasa katika maamuzi. Wanawake hutengwa katika kufanya maamuzi yahusiyo haki zao. Kukosa taarifa na fahamu kuhusu sheria, kanuni na taratibu katika lugha nyepesi kunachangia kuwanyima wanawake fursa ya kuboresha maisha yao.

Hii husababisha kutowajibika kwa vyombo vinavyopaswa kusimamia haki hizi.

c. Elimu

Ukosefu wa elimu ya sheria, hasa kwa kutumia machapisho, unachangia sana ugumu wa watu kufahamu na kupigania haki, fursa na ulinzi wa kisheria.

d. Afya

Jamii isiyokuwa na afya nzuri, haiwezi kupigania au kutetea haki zake na kutumia fursa zilizopo. Hali halisi ni kwamba juhudi zozote za kuwajengea watu uwezo haziwezi kufanikiwa endapo hakuna upatikanaji wa huduma za afya, ulinzi wa walemavu, au juhudi za makusudi kuzuia vifo vitokanavyo na magonjwa ya mlipuko na ukosefu wa maji salama.

e. Upatikanaji wa Chakula na Malazi

Haya ni mahitaji muhimu sana kwa watu masikini ili kufanikisha usalama wa maisha yao. Mifumo duni ya ulinzi wa upatikanaji wa mahitaji haya huathiri uwezo wa watu wenye kipato cha chini kutetea haki zao na kushiriki kwenye shughuli za kisiasa. Mara nyingi mtu mwenye kipato cha chini yupo tayari kuvumilia ukandamizaji ilihali apate kile kidogo cha kumsaidia kuishi tu. Wajane ni mfano mzuri pale wanapoporwa mali na wakwe zao.

  1. Mwelekeo wa Kisiasa

Watu wenye kipato cha chini mara nyingi huwa hawashiriki au hawashirikishwi katika utungaji wa sheria na maamuzi ya kisiasa kuanzia ngazi ya chini kabisa. Demokrasia duni na elimu ndogo vinaathiri uwezo wa watu wenye kipato cha chini kupaza sauti kutetea mahitaji na haki zao. Hivyo ushirikishwaji katika nyanja ya kisiasa ni muhimu katika ujengwaji wa uwezo, kisheria, kwa watu wenye kipato cha chini.

Katika kuwapa watu uwezo kupitia sheria, mambo muhimu ambayo msaidizi wa kisheria anatakiwa ayasisitize kwa mwananchi katika

mwelekeo wa kisiasa ni mawili:

  • Haki za binadamu

  • Uwepo wa demokrasia

  1. Haki za Binadamu

Wakati watu wenye uwezo/matajiri na wenye hali hawana ushawishi na uhusiano na watu wenye nguvu, hivyo kujihakikishia ulinzi dhidi ya ukandamizwaji, watu masikini kwa upande mwingine hutegemea zaidi haki zilizobainishwa, kisheria na zinazotekelezeka. Hivyo, si utambuzi wa haki pekee unahitajika, bali pia uwezo wa kutekeleza haki hizo kwa kutumia vyombo vinavyofikika na madhubuti.

Haki za kisiasa ni kipaumbele kwa sababu ni msingi wa ushiriki wa wananchi katika utunzi wa sheria. Kukosekana kwa uhuru wa kuongea na haki ya kupata taarifa kuhusu shughuli za serikali, huwanyima watu taarifa muhimu za kuwajengea uwezo. Vile vile, kuwanyima watu haki ya kukusanyika, inaathiri ushiriki wao katika siasa. Hizi ni nyenzo muhimu kwa watu masikini katika kuwawajibisha viongozi.

  1. Uwepo wa Demokrasia

Pasipo demokrasia watu masikini hukutana na vikwazo katika kupanga jinsi ya kufikia na kutekeleza haki zao. Ili haki zilandane na mahitaji ambayo ni kipaumbele, ni muhimu sana watu masikini washiriki katika maamuzi. Hili linawezekana tu iwapo kuna demokrasia ya kweli na taasisi zilizokomaa katika demokrasia.

Demokrasia haijengwi kwa kupitia uchaguzi wa viongozi pekee, bali ni muhimu kwa watu wa vijijini kupata fursa ya kuunda vyama vya ushirika na majukwaa ya sera kwa wakulima wadogo na wafanyakazi kwa lengo la kutetea na kusimamia haki zao katika uzalishaji na biashara.

Jambo la msingi pia ni ushirikishwaji wa watu masikini katika vyombo vya utunzi wa sera, ili kukabiliana na ukosefu wa uwiano wa nguvu ambazo hujitokeza katika siasa.



KIMEANDALIWA NA

Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara (Tanganyika Law Society)

Kiwanja Na. 391, Mtaa wa Chato

Regent Estate, S.L.P 2148

Dar es Salaam, Tanzania.

Simu +255 22 2775313 / +255 22 5500002

Nukushi +255 22 2775314

Barua Pepe nfo@tls.or.tz

Tovuti www.tls.or.tz

© Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara, 2016

Waandishi

  • Kaleb Gamaya,

  • Mackphason Buberwa

  • Stephen Msechu

  • Celina Kibasa

  • John Mwang’ombola

  • Alphonce Gura

  • Judith Kapinga

Wahariri

  • Magdalena A. Mlolere,

  • Stephen Msechu

Kimeandikwa na kuhaririwa chini ya usimamizi wa;

Kamati ya Msaada wa Sheria

  • Anna Kulaya-Mwenyekiti

  • Butamo Philip

  • Daniel Lema

  • Donesta Byarugaba

  • Fulgence Massawe

  • Maria Matui

Kamati ya Utafiti na

Machapisho

  • Prof. Cyriacus Binamungu

  • Dr. Alex Makulilo

  • Dr. Lilian Mongela

  • Dr. Ally Possi

  • Madeline Kimei

  • Daniel Welwel


Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara

Kiwanja Na. 391, Mtaa wa Chato
Regent Estate, S.L.P 2148
Dar es Salaam, Tanzania.

Simu: +255 22 2775313 /+255 22 5500002

Nukushi: +255 22 2775314

Barua Pepe: info@tls.or.tz
Tovuti: www.tls.or.tz

▲ To the top