Sheria Katika Lugha Rahisi: Mambo 101 Unayohitaji Kuyafahamu Kuhusu Polisi Lakini Unagopa Kuyauliza


JUKWAA LA HAKI NA USALAMA

Jukwaa la Haki na Usalama lilianzishwa mwaka 2012. Miongoni mwa mashirika waanzilishi wa Jukwaa ni pamoja na; Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Asasi ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria (NOLA), Shirika la Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Shirika la Kimataifa la Haki za Binadama la Mataifa ya Jumuiya ya Madola (CHRI) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Baada ya kuanzishwa kwake, Jukwaa liliandaa; mkakati wa ushawishi wa maboresho ya mfumo wa haki jinai, kusajili wanachama na wabia zaidi na kumteua mratibu ambaye ni Chama cha Wanasheria Tanganyika.

Miongoni mwa mambo mengine, Jukwaa lilianzishwa kwa lengo la kuunga mkono na kuchochea maboresho ya mfumo wa haki jinai hapa nchini. Baadhi ya mambo ambayo Jukwaa limekwisha yafanya katika kufikia lengo lake ni kukusanya maoni ya wanasheria juu ya mfumo wa haki jinai ulio bora na kuyawasilisha kwa Tume ya Marekebisho ya Katiba mnamo mwaka 2012. Aidha Jukwaa limeandaa machapisho ambayo yanahamasisha ushirikishwaji wa jamii katika kudumisha ulinzi, usalama, amani na utulivu wa taifa letu. Machapisho hayo ni pamoja na;

⮚ Jeshi la Polisi na Serikali Kuu Tanzania,

⮚ Uwajibikaji Ndani ya Jeshi la Polisi,

⮚ Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya

⮚ Mambo 101 Unayohitaji Kuyafahamu Kuhusu Polisi lakini Unaogopa Kuyauliza.

Jukwaa lilichapisha jumla ya nakala elfu nane (8000) na kuzisambaza katika idara mbalimbali za serikali zikiwemo: Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, baadhi ya ofisi za Afisa Tawala za Mikoa na Wilaya, makao makuu ya Jeshi la Polisi na baadhi ya ofisi za Makamanda wa Polisi wa mikoa na wilaya, baadhi ya ofisi za Wakuu wa Magereza wa mikoa na wilaya, wanasheria, wasaidizi wa sheria, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla.


 

Wanachama wa Jukwaa hili kwa sasa ni pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika, Asasi ya Haki za Binadamu ya Jumuiya za Madola (CHRI), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Wanawake cha Msaada wa Kisheria (WLAC), Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Asasi ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria (NOLA), Asasi ya Vijana Tanzania (TYVA), Asasi ya Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), Mtandao wa Kiafrika wa Kuzuia na Kulinda Watoto dhidi ya Utelekezwaji na Unyanyaswaji (ANPPCAN), Asasi ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Wanawake (WATED), Asasi ya Wanawake katika Sheria na Maendeleo ya Afrika (WiLDAF) na Asasi ya Haki za Wanawake na Watoto Tanzania (TCWC), Forum 4 Justice na Gender Action Tanzania-GAT.

Pia Jukwaa la Haki na Usalama lina wabia mbalimbali wakiwemo wa kiserikali na wasio wa kiserikali. Miongoni mwa wabia hao ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jeshi la Polisi, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Shirika la Hanns Seidel Foundation.

Chini ya ufadhili wa Open Society Initiative For Eastern Africa (OSIEA) na ushirikiano wa kitaalamu wa CHRI na asasi mbalimbali za kiraia, Jukwaa limeazimia kuwa chachu ya maboresho kwa Jeshi la Polisi kuanzia mwaka 2016 na kuendelea.

SHUKRANI

Kukamilika kwa kitabu hiki muhimu ni zao la ushirikiano na juhudi za watu na taasisi mbalimbali.

Katika kukamilisha kitabu hiki, utafiti wa kina ulifanywa na taasisi ya Haki za Binadamu ya Jumuiya za Madola kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chini ya uratibu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.

Shukrani za dhati ziwaendee wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika maandalizi ya kitabu hiki. Aidha, shukrani za pekee ziwaendee Jeshi la Polisi, Tume ya Marekebisho ya Sheria na wanachama wote wa Jukwaa la Haki na Usalama kwa mchango wao wa kitaaluma na muda wao katika hatua zote za utafiti na uandishi wa kitabu hiki.

Kitabu hiki, utafiti wake na mijadala itakayoendeshwa chini ya kitabu hiki ni matunda ya ufadhili wa shirika la Open Society Initiative for Eastern Africa. Kwa namna ya pekee, Jukwaa la Haki na Usalama linathamini ufadhili huu.

UTANGULIZI

Unakutana na Polisi kila wakati, na unawaona wakifanya kazi nyingi na jamii, kama vile kuongoza magari, kuwalinda viongozi, kuratibu makundi ya watu, kusindikiza watuhumiwa Mahakamani, kufanya upelelezi, kutoa ushahidi Mahakamani, kupokea malalamiko, kubaini, kuzuia au kukamata wahalifu, na kazi nyinginezo. Pia umesikia na unaendelea kusikia mengi kuhusu Polisi kupitia magazeti, televisheni, redio na maneno ya watu. Aidha, kila mtu ana mtazamo wake juu ya Polisi. Hata hivyo, watu wengi bado wana shauku ya kufahamu zaidi kuhusu Polisi.

Katika nchi inayofuata misingi ya utawala bora Polisi siyo chombo cha kuwakandamiza wananchi na kuwadhibiti, bali ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ili kuwalinda raia na mali zao. Polisi wanatoa huduma muhimu ambazo kisheria zina jukumu la kumlinda na kumwangalia kila mmoja wetu kwa hiyo kwa kiwango fulani wanafanana na taasisi nyingine mathalani kikosi cha zimamoto au Mamlaka ya Kodi ya Mapato. Kwa kadiri Polisi walivyo na wajibu kwa wananchi, nao wananchi wanao wajibu kwa Polisi. Raia wema wenye kuwajibika hawapaswi kuwaogopa au kuwachukia Polisi au kuogopa kwenda kituo cha Polisi pale wanapokuwa na matatizo. Bali wananchi na Polisi wanatakiwa wafanye kazi pamoja katika kuzilinda sheria.

Hivyo basi, ni muhimu ukazielewa kazi za Polisi, jinsi wanavyozifanya na changamoto wanazokumbana nazo. Pia ni muhimu ukajua jinsi taasisi hii inavyoonekana na ukomo wa madaraka na kazi zao. Aidha, ni muhimu kwako kujua haki na wajibu wako ili pasiwepo yeyote si Polisi wala wewe raia atakayevunja sheria pasipo kuchukuliwa hatua yoyote. Na hii ndiyo maana halisi ya utawala wa sheria.

Kitabu hiki ni nyenzo katika kulifahamu Jeshi la Polisi. Ni kwa kulifahamu vizuri Jeshi la Polisi tu ndipo jamii itashirikiana nalo katika kukemea maovu yanayojitokeza katika jamii, na kwa kufanya hivyo kutajenga mahusiano mazuri kati ya jamii na polisi katika kutokomeza uhalifu.

SEHEMU YA KWANZA: JESHI LA POLISI: LENGO, MAJUKUMU NA MUUNDO

  1. PT ni nini?

PT ni kifupi cha Polisi Tanzania. Ni chombo cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachotambuliwa na Katiba na sheria ya Bunge.

  1. Kwanini kuna Jeshi la Polisi


 

Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi na wakazi wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.


 

  1. Jeshi la Polisi linapaswa kufanya nini?

Jeshi la Polisi lina kazi kuu zifuatazo: kuzuia na kudhibiti uhalifu na kubaini na kuchunguza uhalifu unapotokea. Pia hutayarisha maelezo ya shauri la kweli na lenye ushahidi ili mwendesha mashitaka aweze kuwasilisha Mahakamani. Jeshi la Polisi lina jukumu la kudumisha utulivu na utii wa sheria kwa kukusanya taarifa kuhusu kinachotokea katika jamii na kuchukua hatua kama itakavyohitajika kwa mujibu wa sheria.

  1. Je ni kazi ya Polisi kumtia hatiani mtuhumiwa?




 

Hapana. Kazi ya Polisi ni kukamata mtuhumiwa, kufanya upelelezi na kupeleka taarifa za upelelezi kwa Mwendesha Mashitaka kwa uchambuzi na uandaaji wa shitaka na hatimaye kumfikisha mtuhumiwa mahakamani pamoja na ushahidi ili mahakama iweze kufanya uchambuzi na kutoa hukumu. Polisi hawana mamlaka ya kumuadhibu au kumchukulia mtuhumiwa kama kwamba ana hatia. Kwa ujumla, hakuna mtu anayeweza kutiwa hatiani bila ya mahakama yenye mamlaka kutamka bayana.

  1. Je Polisi wana mamlaka gani?

Jeshi la Polisi lina mamlaka mbalimbali yaliyotolewa kisheria na linapaswa kutumia mamlaka hayo kulingana na taratibu zilizoainishwa katika sheria husika. Hivyo Polisi wanaweza kukamata, kufanya upekuzi, kushikilia, kumpeleleza mtuhumiwa, kumuhoji shahidi, kufanya mahojiano na mtuhumiwa, kushikilia kitu chochote kinachohusiana na kosa au kilichotumika kufanya kosa kama kielelezo, kuratibu maandamano na kuhakikisha usalama katika jamii. Aidha Jeshi la Polisi wanatakiwa kusimamia usalama barabarani, kuongoza misafara ya viongozi hufanya hivyo kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Sheria, Kanuni na Miongozo na siyo vinginevyo. Matumizi yoyote mabaya ya mamlaka au uzembe katika kazi unapelekea utovu wa nidhamu na uhalifu na afisa wa Polisi anayetenda hayo anapaswa kuchukuliwa hatua stahiki. Sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Jeshi la Polisi Na. 322 (Police Force and Auxiliary Service Act CAP 322) na Kanuni za Polisi (Police General Orders) zimeainisha mamlaka ya Polisi.

  1. Je, kuna Jeshi la Polisi moja tu nchini Tanzania?

Ndiyo, nchini Tanzania kuna Jeshi moja la Polisi lenye vikosi, idara na vitengo mbalimbali kama vile kikosi cha Kutuliza ghasia, kikosi cha Usalama barabarani, kikosi cha Wanamaji, kikosi cha Mbwa na Farasi, Kamisheni ya Upelelezi, kitengo Maalum cha Kuzuia dawa za kulevya na vingine vingi.

  1. Nani Mkuu wa Jeshi la Polisi?


 

Mkuu wa Jeshi la Polisi ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) ambae ni mmoja tu nchini na anasaidiwa na Makamishina wa Polisi. IJP anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliongoza Jeshi la Polisi.

  1. Kwa nini Inspekta Jenerali wa Polisi awajibike kwa Waziri?

Jeshi la Polisi ni moja kati ya majeshi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo husimamiwa na Waziri. Kwa sababu hiyo, Inspekta Jenerali wa Polisi huwajibika kupokea maelekezo ya kisera na kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi kwa Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi.

  1. Je Kuna vikosi vingine vya usimamizi wa utekelezaji wa sheria vyenye mamlaka sawa na Polisi?

Ndiyo, katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria kuna vyombo vingine ambavyo hufanya kazi ambazo kwa kiasi kikubwa hufanana na kazi za Polisi ikiwemo, ukamataji, upekuzi, upelelezi na kuandaa mashitaka. Vikosi hivi ni kama Idara ya Uhamiaji na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

  1. Je, mtu yeyote anaweza kuwa Polisi?

Hapana,ni lazima awe Mtanzania kwa kuzaliwa, asiyekuwa na historia ya kufanya makosa ya jinai na anayekidhi masharti na vigezo vitakavyowekwa ili kuweza kujiunga na Jeshi la Polisi.

  1. Mtu anawezaje kujiunga na Jeshi la Polisi Tanzania?


 

Anaweza kujiunga na Jeshi la Polisi kwa kutuma maombi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kama ametoa tangazo la ajira kwa kupitia ofisi za wilaya, mkoa na taifa, au kupitia katika tovuti yao. Akishapeleka maombi yanayokidhi vigezo na masharti atachaguliwa na kufanyiwa usaili na akishinda usaili atapelekwa Chuo cha Taaluma ya Polisi kwa ajili ya mafunzo maalumu


 

  1. Je, Askari wanawake wana majukumu tofauti?


 

Hapana, hadi sasa kulingana na kanuni na sheria zilizopo Polisi wanawake wanatekeleza majukumu sawa na Polisi wanaume. Hii inawasaidia wanawake kujiamini na kuonesha uwezo wao katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ambayo awali yalionekana kuwa ni ya wanaume. Aidha wanawake wanapelekwa kwenye vituo vile vile ambavyo Polisi wanaume wanapelekwa na kutekeleza majukumu yaleyale kama vile katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kamisheni ya Upelelezi, Kikosi cha Mbwa na Farasi, Kikosi cha Wanamaji, Kikosi Maalum cha Kupambana na Madawa ya kulevya au Kikosi cha Usalama Barabarani. Hata hivyo ni askari wa kike pekee mwenye mamlaka ya kumpekua mtuhumiwa wa kike.

  1. Askari Polisi hupata mafunzo ya namna gani ?

Askari polisi hufundishwa majukumu ya msingi na wajibu wake ndani ya Jeshi la Polisi.

Kuna mafunzo juu ya kazi za polisi, usimamizi wa sheria, medani za kivita na mafunzo mengine ya uongozi kutegemea na cheo alichonacho.

Aidha, polisi wanapata mafunzo ya awali kwenye Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi au Chuo cha Polisi Zanzibar.

Kwa wakaguzi na maafisa wa Polisi wanapata mafunzo yao kwenye Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini Dar es Salaam na Kidatu Morogoro. Ikumbukwe pia mapendekezo ya mafunzo ya kozi za uongozi kama ukaguzi na kuendelea mbele yanafanywa na Tume ya Polisi na Magereza.

  1. Je, ni aina gani nyingine ya mafunzo hutolewa?

Mafunzo mengine ya polisi hutolewa baada ya mafunzo ya msingi kwa kutegemea majukumu na wajibu atakaopangiwa na idara husika. Mafunzo pia yanaweza kuzingatia mabadiliko ya sheria, taratibu, teknolojia, muda, mahali na mahitaji ya Jeshi la Polisi. Mafunzo yanaweza kuhusu mazoezi ya viungo, matumizi ya silaha, huduma ya kwanza, kudhibiti ghasia na mapambano bila kutumia silaha, mafunzo maalumu ya kupambana na makosa ya mitandao, ugaidi, dawa za kulevya, sheria ya jinai, taratibu za kazi, namna ya kufanya upelelezi, namna ya kudhibiti umati wa watu na namna ya kufanya kazi katika mazingira mbalimbali wanayokutana nayo. Mengi ya mafunzo haya hutolewa katika vipindi maalumu kupitia programu ya mafunzo kazini kwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

  1. Askari Polisi anawezaje kupandishwa cheo?

Askari Polisi anaweza kupandishwa cheo kulingana na ustadi wake kitaaluma, elimu na uzoefu, uwezo wa utendaji kazi, uadilifu na kufaulu mitihani katika programu za mafunzo ya ndani ya Jeshi la Polisi. Polisi anaweza kupandishwa cheo kwenda ngazi ya koplo, sajini na stesheni sajini kwa kupata mafunzo yanayotolewa katika Chuo cha Polisi Moshi na Zanzibar na kwa cheo cha Ukaguzi na Uafisa kwenye Chuo cha Polisi Dar es Salaam kilichopo Kurasini. Hata hivyo cheo cha Ukaguzi na Uafisa kinathibitishwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza.

  1. Je, vituo vya Polisi vina madaraja?

Ndio, vituo vya Polisi vina madaraja A, B na C kutegemeana na idadi ya maofisa, eneo la kituo, idadi ya watu na takwimu za uhalifu. Vituo hivi vipo kwenye mikoa, wilaya, tarafa, kata na sehemu nyinginezo ikiwemo vijijini, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

  1. Je, kuna Askari Polisi wa kutosha kukidhi mahitaji?

Hapana, idadi ya Polisi waliopo nchini haina uwiano na wingi wa watu na mahitaji halisi. Hata hivyo askari polisi hugawanywa katika maeneo yao ya kazi ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia hali halisi ya uhalifu, ueledi wa Polisi, vifaa na teknolojia wanayotumia Polisi na wahalifu, ukubwa wa eneo na jiografia yake na mambo mengine mengi.

  1. Je, kuna umuhimu wa kuwa na mchanganyiko wa jinsi, dini na watu wa tamaduni tofauti ndani ya Jeshi la Polisi?

Hakuna nafasi zinazotengwa maalumu kwa ajili ya kundi fulani la watu katika kuajiri watumishi wa Jeshi la Polisi. Watumishi wa Jeshi la Polisi huandikishwa nchini kote kupitia ofisi za wilaya kwa kuzingatia uhitaji, sifa, masharti na vigezo vilivyoainishwa.

Hata hivyo, ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kuwa na mchanganyiko wa wanaume na wanawake kutoka jamii tofauti. Hii itajenga ushirikishwaji wa jamii katika utendaji wa jeshi la polisi.

  1. Je, nitamtambuaje kuwa mtu huyu ni afisa wa Polisi?



 

Askari Polisi ana sare za kipekee za rangi ya khaki, kijani kikavu au bluu na (barret) au chepeo, mkanda wenye rangi za bendera ya taifa na alama ya mabegani au chini ya bega inayoonesha cheo chake na kitengo au idara aliko na kofia yenye Nembo ya Taifa. Polisi wa usalama barabarani wana sare nyeupe au za khaki kwa wanaume na kofia nyeupe na kwa wanawake wana mashati meupe, suruali za bluu na kofia nyeupe.

Askari Polisi lazima pia wawe na kibandiko kifuani kinachoonesha namba ambayo ni tofauti na Polisi wengine, lakini pia katika Jeshi la Polisi kuna Kamisheni ya upelelezi ambao huvaa kiraia kutokana na aina ya kazi yao. Pia sio kila mtu atakayevaa sare ya Polisi ni Askari Polisi, mara chache watu wasio na nia njema huweza kuvaa sare za polisi ili kuwalaghai raia na kufanya uhalifu. Kwa sababu hiyo kila Askari Polisi ana kitambulisho ambacho hukitumia wakati wa kujitambulisha sehemu yoyote pale anapohitajika kufanya hivyo.

  1. Vyeo vya Jeshi la Polisi ni vipi?

Jeshi la Polisi Tanzania lina jumla ya vyeo 16 ambavyo ni:



 


 

  1. Kila Polisi anafanya kazi yoyote ndani ya Jeshi hilo?

Hapana. Polisi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Kudumu za Polisi (Police General Orders). Askari Polisi mwenye cheo cha chini hawezi kutekeleza majukumu aliyopangiwa Askari Polisi mwenye cheo cha juu. Kwa mfano konstebo wa Polisi hawezi kutekeleza majukumu aliyopangiwa koplo. Hata hivyo, chochote kinachoweza kufanywa na Askari Polisi wa cheo cha chini kinaweza kufanywa na Askari Polisi wa cheo cha juu pia.

  1. CID ni nini? Na Wanatofautianaje na Polisi wa Kawaida?


 

CID Ni kifupisho cha maneno ya Kiingereza ambayo ni “Criminal Investigation Department.” Yakimaanisha, Kamisheni ya upelelezi wa makosa ya jinai. Katika Jeshi la Polisi, maafisa katika Kamisheni hii wanapaswa kupeleleza makosa mbalimbali ya jinai.

Aidha hakuna tofauti yoyote kati ya CID na Polisi wengine kwa ujumla. Maafisa wa upelelezi wanachaguliwa miongoni mwa Askari Polisi wa kawaida ambao wamefanya kazi za kawaida za Jeshi hilo.

  1. Je, ni nani anayetoa fedha kwa ajili ya shughuli za Polisi? Na, je, kiasi kikubwa cha bajeti hiyo kinatumika kwa shughuli zipi?

Shughuli zote za utekelezaji wa majukumu ya Polisi hugharamiwa na Serikali katika bajeti ya kila mwaka kutokana na kodi ya wananchi. Aidha Jeshi la Polisi huweza pia kuchangiwa fedha na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.

Bajeti kwa ajili ya Jeshi la Polisi hupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu ulinzi na usalama ni masuala ya Muungano. Rasimu ya kwanza ya bajeti hiyo inaandaliwa na Kamisheni ya Fedha na Lojistiki ya Jeshi la Polisi. Rasimu hii hupelekwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa ajili ya kuridhiwa. Baada ya hatua hiyo, hupelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi tayari kwa kupelekwa bungeni.

Baada ya kujadiliwa bungeni, hatimaye bajeti ya Polisi ya mwaka hupitishwa. Sehemu kubwa ya bajeti hii hutumiwa kulipa mishahara. Maeneo mengine ya matumizi ni kuimarisha mifumo ya utendaji, mafunzo, upelelezi, miundombinu, ujenzi wa nyumba n.k.

  1. Je, unawezaje kujua kuwa fedha wanazopata Polisi zinatumika vizuri?

Unaweza kujua matumizi ya Jeshi la Polisi kutokana na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye hufanya ukaguzi wa akaunti na fedha zilizotumiwa na Jeshi la Polisi kila mwaka. Taarifa za ukaguzi huu huwasilishwa Bungeni. Baada ya ukaguzi taarifa hizi pia hupatikana ndani ya Jeshi la Polisi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na katika maktaba ya Bunge.

Mtu binafsi anaweza kuomba kujua matumizi halali ya Jeshi la Polisi kwa kutumia sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka katika taasisi za Serikali. Kwa kuwa kazi za Polisi zinafanywa kwa kutumia fedha za walipa kodi ambazo ni fedha za wananchi, mwananchi ana haki ya kujua fedha zilizotengwa kwa kazi za polisi zinatumika ipasavyo.

  1. Je, Jeshi la Polisi linaongozwa na sheria gani?

Jeshi la Polisi linaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi s ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara Kanuni za Polisi (Police General Orders) na sharia zingine zinazotoa mwongozo wa ushughulikiaji wa makosa ya jinai.

  1. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Ushahidi na Kanuni za Adhabu, ni nini?

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inaeleza njia ambazo Polisi na Mahakama wanapaswa kufuata katika kuwashughulikia wahalifu na watuhumiwa wa uhalifu. Hii ni pamoja na mamlaka ya Polisi na taratibu wanazotakiwa kuzifuata wakati wa ukamataji, upekuzi, mahojiano, uandishi wa maelezo, na uendeshaji wa shauri ndani ya mahakama.

Sheria ya Ushahidi inaeleza kwa undani kinachokubalika mahakamani kama ushahidi sehemu moja ya sheria hiyo inasema kuwa ushahidi uliopatikana kwa kutumia njia zisizo halali haukubaliki.

Sheria ya Kanuni ya adhabu (Penal Code) inatoa ufafanuzi wa makosa, viini vya makosa, utetezi na adhabu stahiki zinazoweza kutolewa na Mahakama.

Kuna Sheria Nyingine ambazo Jeshi la Polisi Huzitumia Katika Kupambana na Uhalifu. Ni jukumu la Jeshi la Polisi kupambana na Ugaidi, madawa ya kulevya na Makosa ya Mitandao kwa kuwakamata wahalifu mara moja wanapopata malalamiko au taarifa za kiintelijensia kutoka kwa wananchi na kuwafikisha Mahakamani wahalifu hao kwa kufuata taratibu za kisheria kama ilivyoelezwa kwenye sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

  1. Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi (Sura ya 322) inahusu nini?

Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi inaeleza kuhusu uanzishwaji wa Jeshi la Polisi, usimamizi na uendeshaji, uteuzi na huduma; mamlaka na majukumu ya maofisa wa Polisi; nidhamu; Mfuko wa tuzo na tozo; viinua mgongo na mafao ya maofisa wasiokuwa katika pensheni; mamlaka na kazi za Polisi na Polisi Wasaidizi na mambo mengine yanayolihusu Jeshi hilo. Inaeleza kwa kina njia mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa katika kuhakikisha sheria na kanuni za nchi zinatekelezwa katika haki na kwa uwazi.

SEHEMU YA PILI: HAKI NA WAJIBU WA RAIA NA POLISI

  1. Askari Polisi wanafanya kazi hatarishi. Je, wana bima?

Askari Polisi wa Tanzania hawana bima ya maisha ila wana bima ya afya ambayo haikidhi haja kulingana na hatari anazoweza kuzipata akiwa kazini. Familia ya Askari Polisi aliyeuwawa au kufariki kazini inapewa fidia,na Askari aliyeumia kazini anaweza akalipwa fidia au posho kulingana na Kanuni ya Fidia kwa Polisi ya mwaka 2013.

  1. Je, haki za Polisi ni zipi?

Polisi wana haki sawa na raia wengine isipokuwa kwenye mambo machache. Kama wananchi wengine Polisi wanapaswa kuheshimiwa utu wao na kupewa haki zote za kibinadamu, Hata hivyo Polisi hawaruhusiwi kujiunga na vyama vya siasa na wafanyakazi. Ni kosa la jinai kumvamia au kumdhuru polisi akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

  1. Je, Askari Polisi anatakiwa kukubali kila amri aliyopewa na mkuu wake wa kazi ndani ya Jeshi la Polisi?


 

Ndiyo, kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazoliongoza Jeshi la Polisi, kila Askari analo jukumu la kutekeleza kila amri anayopewa na Askari aliyemzidi cheo. Ikiwa kuna hoja kuhusiana na uhalali wa amri hiyo, Askari aliyeamriwa anapaswa kuwasilisha hoja za kutotekeleza amri kwa askari/afisa aliyempa amri na asiposikilizwa atazipeleka kwa askari wa cheo cha juu. Hata hivyo, ikiwa Askari Polisi atatekeleza amri ambayo inakiuka sheria hataweza kujitetea baadae kuwa alitenda kosa kwa sababu alikuwa anatekeleza amri aliyopewa na Askari/ afisa wa cheo cha juu na atawajibishwa.

  1. Je, Askari Polisi anatakiwa kukubali kila amri aliyopewa na Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, n.k?

Hapana. Askari Polisi lazima atii amri ikiwa tu haikinzani na sheria. Atawajibika kwa chochote kibaya atakachokifanya. Hawezi kujitetea kwa kusema kuwa mwenye mamlaka alimuamuru kutenda jambo baya na lililo kinyume cha sheria.

  1. Je, Askari Polisi yuko kazini muda wote?

Ndiyo. Kulingana na sheria ya Polisi na kanuni zake Askari Polisi yupo kazini muda wote na ana mamlaka kama Polisi aliye kazini. Lakini hiyo haina maana kuwa haruhusiwi kupumzika. Hii ina maana kuwa popote alipo, akivaa au kuvua sare zake, lazima ajihusishe kulinda sheria. Hawezi kusema “sipo kazini” kama anashuhudia uhalifu unatendeka au anasikia mtu anaomba msaada.

  1. Je Askari Polisi wa usalama barabarani anaweza kumkamata mtu kwa kosa lisilohusiana na usalama barabarani?

Ndiyo. Kimsingi Polisi wa usalama barabarani ni Polisi wa kawaida waliopewa majukumu ya usalama barabarani. Akimuona mtu anafanya uhalifu wowote anaweza kumkamata kama Polisi mwingine yeyote anavyopaswa kukamata. Kama akimkamata kwa tuhuma za uhalifu ni lazima amfikishe mara moja katika kituo cha polisi kilicho karibu.

Aidha ikumbukwe kuwa idara na vitengo vya polisi ni mgawanyo wa majukumu ya kikazi tu, askari polisi yeyote ana wajibu wa kuzuia utendekaji wa kosa la aina yoyote bila kujali idara au kitengo anachofanyia kazi.

  1. Je, naweza kupata ulinzi wa Polisi kwa ajili ya shughuli zangu binafsi?

Ndiyo, mtu binafsi, taasisi binafsi au ya umma inaweza kuomba ulinzi wa Askari Polisi kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa makubaliano maalumu na watagharamiwa na aliyefanya maombi.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kufanya chochote atakacho?


 

Hapana, Askari Polisi anapaswa kufanya yale yanayokubaliwa na sheria tu. Ifahamike kuwa, Askari wote wanaongozwa na sheria na kanuni za nchi. Kwa mfano hairuhusiwi Polisi kukutukana au kukudhalilisha. Hata hivyo, ikiwa Askari Polisi hatii sheria hizo, anaweza kulalamikiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Kitengo cha Sheria na Uadilifu ndani ya Jeshi la Polisi au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora au mahakamani kulingana na uzito wa suala lenyewe. Ni vizuri kupeleka malalamiko kwa maandishi na kupata uthibitisho wa maandishi kuwa malalamiko yamepokelewa.

  1. Nini wajibu wa Polisi katika “Utawala wa Sheria”

Polisi wana wajibu wa kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia utawala wa sheria. Ina maana kuwa kila tendo linalofanywa na Askari Polisi lifanywe kulingana na sheria; na iwapo hatafanya hivyo Askari Polisi huyo atawajibika mbele ya sheria.

Katika utawala wa Sheria, watu wote ni sawa mbele ya sheria; mkubwa au mdogo, tajiri au masikini, mwanaume au mwanamke, hata serikali na jamii nzima kwa ujumla, ni vyema kutii sheria na lazima kuishi kwa mujibu wa masharti ya Katiba na sheria za nchi. Hivyo basi, hakuna aliye juu ya sheria.

  1. Je, Askari Polisi wanayo ruhusa ya kupata huduma bure?


 

Hapana, hata hivyo kutokana na upungufu wa vitendea kazi na mahusiano mazuri na raia askari polisi wamekuwa wakipata huduma mbalimbali zinazowasaidia katika utekelezaji wa kazi zao au kupambana na changamoto za kazi zao.

  1. Je, natakiwa kuzingatia kila agizo la Askari Polisi?

Ndiyo, kama ni amri halali inayohusiana na kazi yake mfano wakati wa kuzuia uhalifu. Katika kutimiza majukumu yake Askari Polisi anapaswa kujitambulisha akitaja jina, cheo na kituo anakotoka. Hata hivyo, jamii ina wajibu wa kumsaidia Askari Polisi katika kutekeleza kazi zake; hasa iwapo Polisi anajaribu kutuliza ghasia, kusimamisha mapigano, kuzuia uhalifu au ikiwa anajaribu kumzuia mtu kutoroka katika ulinzi wake.

  1. Je, endapo Askari Polisi atatoa amri ya kuambatana na mtu kwenda mahali anapohitaji ni lazima kutii amri hiyo?

Ni vizuri kutii amri hiyo na kuambatana naye hususan kwenda kituo cha Polisi au sehemu ambayo askari polisi anahitaji ili ukawe shahidi wa kitu anachokifanya kama sehemu ya kazi yake, kama vile kumkamata mtu, kutwaa mali, au kuchunguza eneo la uhalifu. Kwa kawaida katika kufanya hivyo anaweza kuitwa kama shahidi anayeweza kuieleza mahakama alichokiona bila kuegemea upande wowote.

  1. Je, ni lazima kujibu maswali yote anayouliza Askari Polisi?

Ni vizuri kujibu maswali yote kwa ukweli na uwazi na kuwaeleza Askari Polisi mambo yote yaliyotendeka kuhusiana na tukio husika. Iwapo anayehojiwa hajui chochote, Askari Polisi hawezi kumlazimisha kutoa maelezo. Daima ni vizuri kuambatana na wakili, ndugu au mtu mwingine wakati wa mahojiano.

Pia, anayehojiwa ana haki ya kukaa kimya na kuacha kujibu maswali kama jibu litamsababisha ajitie hatiani.

  1. Je, Askari Polisi ana wajibu wa kumsadia mtu wakati wa dharura na akiwa anahitaji msaada wake?

Ndiyo. Askari Polisi anatakiwa kutoa msaada kwa mtu aliyeathirika kwa uhalifu au mshukiwa kwa uhalifu na bila kujali hali yake ya kimaisha au nafasi ya mtu katika jamii. Kulingana na kanuni za maadili kazi kubwa ya Polisi ni kutoa ulinzi kwa jamii bila woga au upendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma na kuwa na uhusiano mwema na jamii. Askari akishindwa kutimiza haya atakuwa amekiuka kanuni za maadili za jeshi la polisi.

  1. Je, mtu anaweza kumwomba Askari Polisi kumsaidia katika matatizo ya kifamilia?


 

Inategemea aina ya tatizo ikiwa lina asili ya kijinai. Iwapo kinachotokea ni uhalifu kama wa kufanya vurugu katika familia, kumpiga mwanamke au mtoto, au wanandugu kujamiiana, kuvamia eneo la mtu mwingine kwa jinai, Polisi atalazimika kuingilia kati. Katika migogoro ya kifamilia isiyo na asili ya jinai askari polisi hawezi kuingilia

  1. Je, kuna utaratibu maalum wa kuwashikilia watoto waliokinzana na sheria?

Ndiyo. Kila kituo cha Polisi nchini ni lazima kiwe na dawati la jinsia lenye kusimamiwa na Askari Polisi waliopata mafunzo maalumu kuhusu kuwashikilia wanawake na watoto. Hali kadhalika, watoto waliokinzana na sheria hawachangamani na mahabusu watu wazima. Polisi watakuwa na wajibu wa kuwatunza na kuangalia ustawi wa watoto walioshikiliwa. Hata hivyo, Watoto wanaokamatwa wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa masharti yaliyoko katika Sheria ya Mtoto.

Sheria ya Mtoto inasema kuwa endapo mtoto atakamatwa na Askari Polisi, ni jukumu la lazima kwa askari huyo kumtaarifu mzazi au mlezi wa mtoto huyo wakati huo huo pasipokuchelewa. Taarifa hiyo itaeleza kuhusu kukamatwa kwa mtoto huyo na pili kuhusu sababu za kukamatwa kwake. Pia ni lazima kuharakisha taratibu za kumfikisha mtoto huyo katika mahakama ya Watoto ndani ya saa ishirini na nne. Ikiwa mtoto atafikishwa mahakamani, na kama kesi haihusu mauaji au adhabu inayozidi miaka saba itakuwa ni jukumu la Askari anayehusika kumuachia mtoto huyo kwa dhamana ya mzazi au mlezi isipokuwa tu pale ambapo kwa maslahi bora zaidi ya mtoto husika itaonekana kuwa ni vibaya kwa mtoto huyo kuchangamana na watu wasiofaa au kwamba kumwachia mtoto huyo kutaathiri upatikanaji wa haki.

  1. Polisi anapaswa kuwahudumia vipi watu wenye ulemavu?


 


 

Watu mwenye ulemavu wanapaswa kuhudumiwa vizuri kulingana na aina ya ulemavu. Sheria ya Haki za Watu Wenye Ulemavu, imeweka masharti ya msingi ya jumla kuhusu wajibu wa umma na dola kuhusiana na watu wenye ulemavu. Askari anaposhughulika na mtuhumiwa au mlalamikaji ambaye ana ulemavu anapaswa kuhakikisha kuwa miundombinu, vifaa na mazingira yanakuwa rafiki kwa mtu huyo.

Mlemavu wa viungo anahitaji miundo mbinu rafiki inayofikika kwa wote: mlemavu wa macho anahitaji maandishi yaliyo katika nukta nundu, mtu mwenye ualbino hapaswi kuwekwa kwenye jua kali na pia anahitaji maandishi yaliyokuzwa na mlemavu wa kusikia anahitaji mawasiliano kwa njia ya lugha ya alama. Haya ni mahitaji ya msingi ambayo Askari Polisi anapaswa kuyazingatia anapokuwa akishughulikia malalamiko dhidi ya mtu mwemye ulemavu.

Ikumbukwe kuwa haki za msingi za binadamu haziondolewi kwa sababu ya tuhuma au mashtaka ya mtu. Heshima ya utu wa kila mtu unapaswa kulindwa. Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kuwa miundo mbinu yake yote ikiwemo ya Mahakama na Vituo vya Polisi ni rafiki kwa watu wote hasa watu wenye ulemavu.

  1. Iwapo Askari Polisi hatoi msaada au hayupo karibu, je, wananchi wanaweza kumkamata mwizi au mhalifu yeyote na kumwadhibu papo hapo?


 

Hapana, kumpiga mhalifu ni kosa la jinai. Kinachopaswa kufanywa ni kumkamata mhalifu na kumuweka chini ya ulinzi wa wananchi na kumpeleka kituo kisha kumpeleka kituo cha Polisi kilichopo karibu.

Hairuhusiwi kumpiga mhalifu au kushirikiana na kundi la watu wanaofanya hivyo. Wananchi wanayo haki ya kujilinda dhidi ya shambulio la kudhuru mwili linalofanywa na mtuhumiwa au mtu yeyote lakini kujilinda huko kuwe kwa kiasi. Haiwezi kugeuzwa kuwa ni kipigo cha upande mmoja au udhalilishaji wa kutisha na Askari Polisi anayeruhusu hilo au anayeungana na wanaofanya hivyo anaweza kukabiliwa na mashtaka ya kinidhamu au jinai. Kumbuka kuwa kumpiga mhalifu ni uhalifu pia.

  1. Je, Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu?

Katika mazingira ya kawaida Askari Polisi haruhusiwi kutumia nguvu dhidi ya mtu yeyote yule isipokuwa tu kama mtu huyo anakataa kukamatwa au anajaribu kutoroka au anahatarisha uhai wa Askari, mtu mwingine au uharibifu wa mali. Sheria inamruhusu Askari Polisi kutumia nguvu pale inapolazimu tu, na iwapo atatumia nguvu isivyohitajika atachukuliwa hatua za kinidhamu au kufunguliwa mashtaka kwa kosa la jinai.

  1. Je Askari Polisi anaweza kumsimamisha mtu yeyote mtaani na kumuuliza chochote ?

Ndiyo. Ikiwa kuna kitu anachokitilia shaka juu ya jambo fulani, Askari Polisi anaweza kumsimamisha na kumuuliza juu ya chochote. Askari Polisi wanatumia mamlaka haya mara nyingi kama njia ya kupata taarifa, kuwabaini au kuwakamata washukiwa wa uhalifu. Wananchi wanahimizwa kutoa ushirikiano.

  1. Je waathirika na watuhumiwa wa makosa ya jinai wana haki sawa?

Ndiyo. Mtuhumiwa na muathirika wa makosa ya jinai kwa pamoja wana haki sawa mbele ya sheria. Wote wanahitaji ulinzi wa sheria na haki. Tafsiri ya haki ni mtu kupata kile anachostahili. Hii ina maana kuwa, pale Mtuhumiwa anapotiwa hatiani na mahakama huadhibiwa na muathirika hufidiwa. Watu wengi wanafikiri kuwa hakuna anayewajali waathirika wa vitendo vya kihalifu. Kwa kweli nguvu zote za Serikali ni kwa ajili ya kumsaidia muathirika. Ni kwa niaba ya waathirika vyombo vya dola vinawatafuta wahalifu. Pia ni kwa niaba ya waathirika serikali inawaweka waendesha mashitaka kuwatetea mahakamani ambapo mahakama pia inaweza kumuamuru mtuhumiwa kumlipa fidia muathirika endapo Mahakama itamkuta na hatia. Vile vile ni kwa niaba ya waathirika serikali inawaadhibu wakosaji.

Adhabu anayopewa mtuhumiwa ya kumlipa fidia muathirika inahitaji iendane sambamba na madhara aliyopata muathirika hivyo ni wajibu wa muathirika na mwendesha mashitaka kutoa maombi stahiki ya fidia kwa mahakama.

SEHEMU YA TATU: TARATIBU ZA TAARIFA, UPELELEZI NA MASHTAKA

  1. Je, mtu anaweza kumwita Askari Polisi wakati wowote anapohitaji?

Ndiyo, lakini anapaswa tu kuwaita Askari Polisi kwa malalamiko au taarifa zinazohusu uhalifu. Anapaswa kuwaita Polisi kwa njia ya simu namba 112 iwapo ameona au amesikia au anatendewa kitendo cha kihalifu. Aidha ikiwa, kuna uhalifu umetokea au unatokea, au kuna uwezekano wa kutokea ghasia, watu wanapigana na kuna uwezekano wa kutokea machafuko, au iwapo ana taarifa nzito ya kuwapatia. Lakini hapaswi kuwaita Polisi kwa suala lisilohusiana na kazi za Askari Polisi. Wakati mwingine watu wanafanya utani na wanawaita Polisi hata kama hakuna jambo lolote lililotokea. Kuwaita Askari Polisi kwa mambo ya mzaha huweza kupelekea kuadhibiwa kwa mzaha huo.

  1. Ikiwa mtu anataka kuwapa Askari Polisi taarifa ya uhalifu, afanyeje?

Iwapo ni taarifa ya uhalifu kwa mfano: mauaaji, wizi, uvunjwaji wa nyumba, udhalilishaji wa kijinsia, shambulio, udhalilishaji wa watoto, ubakaji, kumchukua mtu kinguvu na kumshikilia, usafirishaji haramu wa binadamu n.k., anaweza kutoa taarifa hiyo katika kituo cha Polisi au kwa Afisa wa Polisi anayemwamini na atawajibika kutoa maelezo ya jinsi anavyolifahamu tukio analolitolea taarifa.

Pia anapaswa kufahamu kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kuwalinda watoa taarifa, Askari Polisi haruhusiwi kumtaja mtoa taarifa kwa mtu yeyote bila sababu ya msingi. Aidha ni jukumu la mtoa taarifa kuhakikisha kuwa anatoa taarifa za ukweli kwa Jeshi la Polisi na wajibu wa mpokea taarifa ni kuzifanyia kazi taarifa hizo haraka iwezekanavyo na kutunza siri za mtoa taarifa.

  1. Taarifa ya awali ni nini?

Ni maelezo ya awali ya tukio lililotokea, yanayotolewa kwa polisi na mlalamikaji muathirika, shahidi au mtu yeyote anayejua kuhusu tukio uhalifu. Kinachoelezwa kwenye taarifa hiyo ya awali kitasaidia Polisi kuanza uchunguzi kuhusu suala hilo na kukusanya ushahidi ili kujiridhisha iwapo kuna kesi inayoweza kufunguliwa au la.

Taarifa ya awali ni maelezo ya ukweli kama alivyofahamu; alivyoona au kama alivyoambiwa. Kwa maana hiyo, ni lazima atoe taarifa sahihi.

Taarifa ya awali hueleza au hujumuisha sehemu, siku au tarehe na muda wa tukio. Aidha hujumuisha taarifa juu ya wasifu na matendo au maneno ya kila mtu aliyehusika: walikuwa akina nani, walikuwa wapi, walikuwa wanafanya nini, mlolongo wa kila kilichofanyika na kila mtu, kila aina ya majeruhi au uharibifu wa mali uliofanywa, aina ya mali n.k. Endapo tukio limehusisha matumizi ya silaha basi maelezo yatajumuisha aina ya silaha na jinsi ilivyotumika. Ni vizuri kuweka kumbukumbu za ukweli na hali halisi haraka iwezekanavyo. Ikiwa maelezo ya awali yanatolewa kwa kuchelewa anapaswa kumjulisha Askari Polisi sababu za kuchelewa kwake kutoa hayo maelezo.

  1. Mtoa taarifa atajuaje kuwa Askari Polisi ameandika maelezo yake kwa usahihi a?


 

Kumbuka kuwa maelezo ya mtoa taarifa, siyo maelezo ya Polisi. Wajibu wa Askari Polisi ni kunukuu maelezo ya mtoa taarifa kwa usahihi bila kuongeza au kupunguza neno lolote . Ili kujiridhisha na hili, sheria inamhitaji Askari Polisi kumsomea mtoa taarifa au kumpa mwenyewe na kuisoma; kufanya marekebisho kwa kuongeza au kupunguza maelezo.

Pindi atakapokubaliana nayo itabidi atie sahihi. Ikiwa kama hakubaliani na maelezo hayo Polisi hana mamlaka ya kumlazimisha kutia sahihi.. Maelezo hayo pamoja na Taarifa ya awali itatunzwa na kufunguliwa jalada ambalo litapelekwa kwa Afisa wa Polisi wa cheo cha juu kwa ajili ya hatua zaidi.

  1. Je, mtu anaweza kwenda kufungua kesi kwenye kituo kidogo cha Polisi au katika kituo chochote cha Polisi?

Ndiyo, mtu anaweza kufungua kesi katika kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu nae au karibu na uhalifu ulipotendeka.Jeshi la Polisi lina Vituo vinavyohamishika [mobile police stations] vinavyohudumia wananchi katika sehemu mbalimbali nchini ambavyo vina majukumu sawa na vituo vya kudumu vya Polisi.

Ikiwa atafungua shauri lake katika Kituo Kingine cha Polisi, wataingiza taarifa zake katika kumbukumbu na kisha kuwasiliana na kituo stahiki. Askari Polisi hawawezi kukataa kupokea taarifa eti kwa sababu tu uhalifu haukutokea katika eneo ambalo wana mamlaka nalo.

  1. Askari Polisi anaweza kukataa kupokea taarifa ya uhalifu?

Hapana, Askari Polisi ni lazima apokee na kusajili taarifa inayomfikia kuhusu uhalifu. Baada ya kupokea taarifa hiyo na kuisajili, Askari Polisi kwa kufuata taratibu za kisheria na Kanuni za Polisi anaweza kukataa kushughulikia tatizo lako ila atalazimika kukupatia sababu za uamuzi huo.

  1. Nini kifanyike endapo askari polisi atakataa kupokea malalamiko yanayohusu kosa la jinai.

Kwa mujibu wa sheria, malalamiko yoyote yatakayofikishwa katika Kituo cha Polisi yanapaswa kusajiliwa. Endapo Askari Polisi amekataa kupokea na kusajili malalamiko ya jinai anapaswa kumjulisha mkuu wa kituo endapo hajasaidiwa amjulishe Kamanda wa Polisi wa wilaya na ikiwa bado hajapata msaada amjulishe Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Kitengo cha Malalamiko ndani ya Jeshi la Polisi au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora au mahakamani kulingana na uzito wa suala lenyewe.

  1. Nini kitakachofuata baada ya kutoa taarifa ya awali?

Baada ya kupokelewa kwa taarifa ya awali, Askari Polisi atapanga na kuanzisha uchunguzi. Katika uchunguzi huo Polisi wanaweza kuongea na waathirika na mashahidi, kuchukua maelezo na vielelezo kwa kadiri itavyohitajika.


 

  1. Je, nini kinafuata baada ya uchunguzikukamilika?


 


 

Baada ya uchunguzi kukamilika Askari Polisi aliye na madaraka atayaangalia maelezo yaliyotolewa na kuamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha wa kuonesha kuwa uhalifu ulitendeka na kumfungulia mashitaka ya jinai mtu mtuhumiwa. Polisi ataandaa taarifa ya mwisho kwa ajili ya mwendesha mashitaka, ambayo kwa maoni ya afisa wa upelelezi itaonesha kuwa kuna ushahidi na taarifa za kutosha kwa mahakama kulisikiliza shauri. Hivyo mtuhumiwa atashtakiwa mbele ya mahakama kwa uhalifu, ambapo ushahidi utatolewa na mtoa taarifa anaweza akaitwa kuwa shahidi wa upande wa mashitaka kisha mahakama itaamua kama mtuhumiwa ana hatia au la.

  1. Kwa nini mara nyingi baada ya Mtu kufikishwa Mahakamani, Polisi au Waendesha Mashitaka hudai kuwa Upelelezi haujakamilika?

Hii huweza kutokea kutokana na mazingira ya tuhuma, ushahidi na taarifa za ziada ambazo huweza kupatikana baada ya kesi kufunguliwa.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Polisi, endapo vipengele vyote vya uhalifu havikukamilika itakuwa ni upotezaji wa muda kumshtaki mtu na kumpeleka mbele ya mahakama. Waendesha Mashitaka na mahakama wataichunguza hati ya mashtaka wenyewe ili kuona uwezekano wa uhalifu kuwa umetendeka. Pia shauri la jinai likikaa mahakamani kwa muda wa siku sitini (60) bila ushahidi kukamilika, mahakama italitupilia mbali shauri hilo na mtuhumiwa kuachiwa huru.

  1. Je, Askari Polisi anatakiwa kumkamata kila mmoja aliyetajwa ndani ya taarifa ya awali?

Hapana,mtu kutajwa katika taarifa ya awali siyo sababu inayojitosheleza ya kukamatwa kwake. Ni pale tu kutakapokuwa na sababu za kutosha za kuonesha kuwa mtu huyo amehusika katika kufanya uhalifu ndipo Askari Polisi wanaweza kumkamata.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kufunga malalamiko bila kuchukua hatua zaidi?


 


 

Ndiyo. Polisi wanaweza kuamua kufunga malalamiko na wana wajibu wa kutoa sababu za kufikia uamuzi huo.

Sababu hizo zinaweza kuwa ni kukosekana kwa taarifa za kiuchunguzi juu ya ukweli unaosaidia kuonesha kuwa uhalifu ulitendeka, au iwapo hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa kuna ukweli katika tuhuma zilizotolewa au kuthibitisha kuwa uhalifu umefanyika, lakini watu waliofanya uhalifu huo hawajulikani. Hata hivyo polisi hupaswa kutoa taarifa ya uamuzi huo.

Baada ya kufahamishwa kwamba malalamiko yamefungwa,kuna nafasi ya kupinga kufungwa kwa malalamiko hayo kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Kitengo cha Malalamiko ndani ya Jeshi la Polisi au Tume ya Haki za Binadamu

na Utawala Bora au Mahakamani kulingana na uzito wa suala lenyewe.

  1. Je, mtu anaweza kuendelea kupewa taarifa ya maendeleo ya kesi inayotokana na taarifa yake?

Hakuna kipengele maalumu katika sheria kinachomtaka Askari Polisi kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya kesi iliyopelekwa mahakamani. Hii ni kwa sababu kesi inayohusu uhalifu husimamiwa na kuendeshwa na serikali. Hivyo, ni jukumu la mtoa taarifa kufuatilia taarifa za uendeshwaji wa kesi mahakamani.

  1. nini kifanyike iwapo Askari Polisi hawalichunguzi jambo langu au wanafanya pole pole au wanakataa kuchunguza masuala yaliyo wazi katika mkondo wa uchunguzi?

Kuna kanuni muhimu katika Sheria kuwa hakuna mtu awezaye kuingilia upelelezi wa Polisi. Hivyo iwapo Polisi wanakataa kuendelea na upelelezi au wanafanya hivyo pole pole sana au kwa makusudi wakapuuza masuala muhimu katika mkondo wa upelelezi hakika kuna uwezekano wa kulalamika kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya (OC/CID); Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO); Kamanda wa Polisi wa Mkoa; au Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mashitaka (DPP)

  1. Je, Askari Polisi anaweza kuingia kwenye nyumba ya mtu na kufanya upekuzi bila kukaribishwa?

Ndiyo, endapo ruhusa ya kuingia haitapatikana au endapo nyumba itakuwa imefungwa, Askari Polisi anayo mamlaka ya kuvunja mlango, dirisha au kutumia mbinu zozote zinazoruhusiwa na sheria kuweza kuingia na kupekua na kuchukua kitu au mtu aliyehusika katika uhalifu. Hata hivyo, kabla ya kuchukua hatua hizo Askari anapaswa kuwajumuisha na uongozi wa eneo husika.

Ikiwa Askari Polisi atachukua kitu chochote ndani ya nyumba lazima atoe hati ya kushikilia mali (Certificate of Seizure) ya kukubali kuhodhi mali hizo, ikiwa na sahihi ya mmiliki, au mkazi wa makazi hayo au ndugu yake wa karibu na sahihi ya mashahidi walioshuhudia upekuzi huo kama wapo.

  1. Nini maana ya Amri na Hati ya upekuzi?

     


 

Amri ya Upekuzi (Search Order) ni Kibali kinachotolewa na Mkuu Wa Kituo cha Polisi wakati Hati ya Upekuzi (Search Warrant) ni kibali kinachotolewa na Mahakama. Vyote vinatoa ruhusa kwa Askari Polisi kupekua sehemu yenye uwezekano wa kuwepo ushahidi unaohusiana na kosa lililofanyika au ushahidi kuhusu kosa linalodhaniwa kuwa litatendeka.

Mamlaka yoyote haiwezi kuingia na kupekua nyumba na ofisi za watu bila sababu za msingi kwa kuwa ni maeneo ya faragha. Hivyo Sheria inamtaka yeyote anayehitaji kuingia katika maeneo binafsi kueleza kwa nini anaona kuwa ni muhimu kuingilia haki ya mtu ya faragha.

Aidha, Askari Polisi wanaweza kufanya upekuzi wa dharura bila ya uwepo wa amri ya kimaandishi au hati ya upekuzi pale wanapoona tukio la kijinai linafanyika. Iwapo kuna uwezekano wa mtuhumiwa kukimbia na Askari Polisi anazo sababu zinazomfanya aamini hivyo au iwapo kuna uwezekano wa ushahidi kuharibika, au ikiwa mtuhumiwa, mhalifu au kitu kinatakiwa kipatikane bila kuchelewa na kuna hofu kitapotea iwapo hakitatwaliwa wakati huo, basi Askari Polisi wanaweza kuingia kwenye nyumba ya mtu bila hati ya upekuzi na kuchuchua chochote kitakacho shukiwa kuhusika na uhalifu.

  1. Je, Polisi wanapataje amri au hati ya upekuzi?

Mkuu wa kituo cha Polisi anaweza kutoa amri ya upekuzi kwa sababu zilizotajwa hapo juu, lakini atafanya hivyo tu iwapo ataridhika kuwa ucheleweshwaji wowote utakaotokana na kuomba kibali cha upekuzi Mahakamani kutasababisha kuondolewa au kuharibiwa kwa ushahidi, au kutahatarisha uhai au mali. Askari Polisi lazima pia atoe taarifa ya utolewaji wa hati ya upekuzi kwa hakimu aliyepo eneo la karibu, akieleza kwa nini alitoa hati ya upekuzi na mali zilizoonekana kutokana na upekuzi uliofanyika.

Askari Polisi wanatakiwa waende mbele ya Hakimu na kueleza sababu zinazowafanya wafikiri kuwa kuna mali, nyaraka au watu waliofichwa kwenye nyumba husika ambapo kukamatwa kwao kutasaidia kuleta suluhisho la uhalifu. Iwapo hakimu atashawishika kuwa kuna sababu za msingi za kufanya upekuzi wa majengo hayo, atatoa kibali. Kibali hicho kina mipaka na kinatoa jina na cheo cha Askari Polisi anayeruhusiwa kuingia ndani ya jengo husika na kinatolewa chini ya sahihi ya Hakimu na muhuri wa Mahakama.

Askari Polisi wanaweza kusimamisha na kupekua chombo chochote cha usafiri iwapo wataamini kuwa ndani yake kuna mali za wizi, vitu vilivyotumika au vitakavyotumika katika uhalifu, au silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria. Hii ni tofauti na kupekua nyumba.

  1. Utaratibu gani unatumika katika Upekuzi?


 

Hati ya upekuzi iwepo au isiwepo bado kuna utaratibu unaotakiwa kufuatwa. Upekuzi lazima ufanyike mmiliki akiwepo. Mmiliki hatakiwi kuondolewa wakati upekuzi unaendelea. Polisi wanatakiwa kuorodhesha vitu wanavyovichukua.

Mashahidi, Askari Polisi na mmiliki wa nyumba au ofisi lazima watie sahihi kuthibitisha vitu vilivyochukuliwa. Lazima nakala iliyosainiwa na wote iachwe kwa mmiliki. Iwapo ndani ya nyumba kuna mwanamke, ambaye hatakiwi kukamatwa, na ambaye kwa mujibu wa mila hatakiwi kutoka nje, Askari Polisi anatakiwa atoe taarifa kwa mwanamke huyo ya kumtaka aondoke ndani ya nyumba hiyo na atoe muda wa kutosha wa mwanamke huyo kuondoka.

Iwapo wanawake wanatakiwa kupekuliwa, upekuzi huo lazima ufanyike na Askari wa kike kwa uangalifu na heshima ya hali ya juu. Upekuzi lazima ufanywe kati ya muda wa jua kuchomoza na kabla ya jua kuzama na lazima awepo kiongozi wa serikali za mitaa au mtu ambae ni jirani wa mtuhumiwa au ndugu yake isipokuwa iwapo Mahakama imeamuru vinginevyo.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kutumia bunduki na risasi za moto katika kupambana na uhalifu?

Ndiyo, Askari Polisi anaweza kutumia bunduki na risasi za moto ikiwa njia nyingine zote za udhibiti zimejaribiwa na kushindikana. Kwa mfano inaruhusiwa kutumia bunduki na risasi za moto dhidi ya mtu anayetoroka; anayefanya jaribio la kutoroka toka kizuizini au kwa ajili ya mtu anayetoroka na ili akamatwe, silaha hizo zinatumika kumpunguzia mwendo pasipo kumuua. Izingatiwe kwamba, silaha zinatumika pale tu Askari Polisi anapokuwa na sababu za msingi za kuamini kuwa hawezi kuzuia utoro huo kwa njia nyingine na ametoa onyo kwa mtu huyo kuwa yuko karibu kutumia bunduki, na mtu huyo hakujali onyo lililotolewa.

Pia Askari Polisi anaweza kutumia bunduki dhidi ya mtu ambaye anatumia nguvu kumwondoa mtu mwingine kutoka katika kizuizi halali au kuzuia ukamatwaji halali wa mtu mwingine. Hata hivyo, katika suala hili, Askari Polisi anaweza tu kutumia bunduki kwa kuzingatia sheria na kanuni za matumizi ya silaha iwapo hakuna njia nyingine ya kumzuia mtu huyo na iwapo Askari Polisi ana sababu za msingi za kuamini kuwa mtu mwingine, au Askari Polisi wenyewe, wako hatarini kuumizwa.

  1. Je, Askari Polisi afanye nini kama watu ni wakaidi na wanarusha mawe au kuhaharibu mali?

Askari Polisi wana wajibu wa kulinda uhai na mali za watu lakini kuna utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika utekelezaji wa jukumu hilo. Kwanza polisi wanawajibu wa kutoa onyo mara tatu ya kuwataka watu watawanyike, kwa mdomo na kwa maandishi na wanapaswa kutoa muda wa utekelezaji wa

amri hiyo.Kama bado hawatawanyiki nguvu ya kadiri inaweza kutumika. Aina ya nguvu hizo ni matumizi ya maji ya kuwasha, mabomu ya machozi, virungu na mbwa, silaha zinaweza kutumika pia kama vile risasi za mpira.

Polisi wakati wote lazima wajitahidi kutumia njia yenye madhara kidogo na kutumia njia nyingine kama ile imeshindikana. Iwapo Polisi watatumia risasi za moto wafanye hivyo kama njia ya kujihami, na lazima pawepo na maonyo ya wazi kuwa risasi zitatumika. Hapa pia kanuni ni kutumia nguvu kiasi, mara kundi hilo linapoonyesha dalili ya kutawanyika upigaji wa risasi lazima usimamishwe. Majeruhi lazima wasaidiwe kwa kupelekwa hospitali mara moja. Hata hivyo kila Askari Polisi anawajibika kuandika taarifa ya uhusika wake kwa ajili ya kumbukumbu. Lakini njia iliyo bora ni ile ya kushauriana kwa mazungumzo na waandamanaji.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kumkamata mtu bila kutoa sababu?


 

Hapana. Ni wajibu wa Askari Polisi kujitambulisha na kueleza kosa Lililofanyika kabla ya ukamataji . Mathalani, kama mtu amekamatwa akifanya uhalifu, mazingira yote ya uchunguzi yanaonyesha kumtuhumu mtu huyo au mtu huyo anaonekana akimsadia mtu mwingine kufanya uhalifu kabla, wakati au baada ya tukio kutokea, anaweza kukamatwa. Ni lazima kuwe na sababu za msingi za kumkamata mtu.

  1. Je, Askari Polisi anahitaji kuwa na kibali ili aweze kumkamata mtuhumiwa?


 

Inategemea aina ya kosa. Kuna makosa maalumu yaliyoorodheshwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai yenye kuruhusu Askari Polisi kumkamata mtu bila kibali. Kwa mfano, Uvunjifu wa amani, kumzuia Askari kufanya kazi yake, kudharau Bendera au Wimbo wa taifa, n.k. Hata hivyo makosa mengine yote yanamtaka Askari Polisi kupata hati ya kukamata kutoka kwa Hakimu. Endapo Askari Polisi watamkamata mtu bila ya kuwa na kibali, ni lazima watoe taarifa mahakamani kuhusu ukamataji huo. Pamoja na hayo, mtu aliyekamatwa kwa kibali au pasipo kibali, anayo haki ya kuongea na mwanasheria na mwanafamilia au rafiki wakati anapokuwa amekamatwa.

  1. Je, kuna kanuni maalum za kuwakamata na kuwahudumia wanawake walioko kizuizini?

Ndiyo. Upekuzi wowote wa mwanamke lazima ufanywe na Askari Polisi mwanamke, kwa kuzingatia heshima ya mwanamke anayepekuliwa. Zaidi ya hayo, kila Kituo cha Polisi nchini ni lazima kiwe na Dawati la Jinsia lenye kusimamiwa na Askari Polisi waliopata mafunzo maalumu kuwahudumia wanawake na watoto. Mahabusu wanawake hawachanganywi katika chumba kimoja na mahabusu wanaume.

  1. Je, Askari Polisi wanaruhusiwa kumkamata mtuhumiwa na kumshikilia kwa muda wowote wanaopenda?

Hairuhusiwi. Ikiwa amekamatwa na Polisi na kuwekwa mahabusu bila kibali au wakiwa na kibali, basi Askari Polisi ni lazima wampeleke mtu huyo mahakamani ndani ya saa ishirini na nne. Hata hivyo, iwapo amekamatwa kwa kibali kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifo Polisi lazima wampeleke mbele ya Mahakama mapema iwezekanavyo, kama hawajampeleka mahakamani ndani ya saa 24 ana haki ya kuwataka wampeleke mahakamani haraka iwezekanavyo au anaweza kuwasiliana na ndugu/rafiki au mwanasheria apeleke maombi mahakama Kuu ya kuamrisha Jeshi la Polisi limpeleke mahakamani. Ikiwa hajakamatwa, lakini ameletwa kituo cha polisi kwa ajili ya kuhojiwa, basi Askari Polisi lazima waandike taarifa hiyoliweke suala hilo katika kumbukumbu zao pia.

  1. Polisi wanaweza kukamata familia ya mtu anayetuhumiwa kutenda kosa la jinai?

Hapana, hawana mamlaka hayo. Hakuna hatia ya kufungamanishwa. Mtu kuwa na hatia au kukosa hatia lazima kuamuliwe kwa kuangalia vitendo vya mtu binafsi na siyo kwa sababu mtu huyo yupo karibu na au anahusiana na mtu fulani ambaye ni mtuhumiwa. Uhuru wa mtu yeyote hauwezi ukatwaliwa isipokuwa kwa sababu maalum za sheria.

Askari Polisi hawaruhusiwi kuwatisha wanafamilia au marafiki au kuwafungia mahabusu kama njia ya kumbana mhalifu akiri kosa au kama amekimbia ajisalimishe Polisi. Njia hii ya kuteka na kuwashikilia mateka watu wa karibu wa mtuhumiwa ni kinyume cha sheria na ni kosa kubwa. Hivyo, Polisi wakifanya hivyo aliyekamatwa ana haki ya kuwashtaki Mahakamani au kupeleka malalamiko Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Haijalishi kesi wanayoishughulikia ni ngumu kiasi gani, Polisi hawawezi kutumia njia zisizo halali ili kumlazimisha mtuhumiwa kujisalimisha au kukiri kosa. Watu pekee wanaoweza kukamatwa ni wale ambao kuna sababu za msingi dhidi yao za kufikiriwa kuwa wamefanya uhalifu.

  1. Je, Polisi anaweza kumshikilia mtu mafichoni bila kutoa taarifa?

Hapana. Jeshi la Polisi likikushikilia mafichoni ni kinyume cha sheria. Mara Askari Polisi wanapomuweka mtuhumiwa mahabusu ni jukumu lao kuangalia afya yake na kuzilinda haki zake. Iwapo atapata madhara yoyote au haki zake hazitaheshimiwa na zikavunjwa kwa namna yoyote ile Jeshi la Polisi litawajibika. Hili ni jambo muhimu la kisheria na ni vizuri kulikumbuka.

Askari Polisi wana wajibu wa kuandika taarifa za watu wote wanaofika kituoni kwenye kitabu cha taarifa za kumbukumbu za mahabusu za kila siku, kitaonesha muda mtuhumiwa alioletwa kituoni kwa mahojiano na wakati gani alikamatwa. Kumbuka kuwa mtuhumiwa anayo haki ya kuwa na mwanasheria wake wakati wa mahojiano. Hivyo, sehemu ya mahabusu lazima ijulikane na iweze kufikiwa na mwanasheria wake, marafiki, familia au jamaa.

  1. ni halali mtu kukakukamatwa siku ya Ijumaa jioni na kuwekwa mahabusu mpaka Jumatatu?


 


 

Haitakiwi kuwa hivyo. Inapokuwa haiwezekani kumpeleka mtu aliyekamatwa mahakamani ndani ya saa 24 kuanzia alipowekwa mahabusu, afisa msimamizi wa Kituo cha Polisi ambako mtuhumiwa ameshikiliwa anaweza kuichunguza kesi na anaweza kumwachia mtu huyo baada ya kuweka dhamana isipokuwa kama kosa linaonekana na afisa huyo kuwa ni kubwa. Dhamana itatolewa kwa kiasi cha fedha kinachohitajika, akiwa na wadhamini au bila ya wadhamini na itamtaka kwenda katika Kituo cha Polisi katika muda na mahali palipotajwa kwenye dhamana ili apelekwe mbele ya mahakama ikiwa hati ya mashitaka itakuwa imekwishaandaliwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali.

  1. Je, kuna utaratibu wa kuwajulisha ndugu wa mtuhumiwa endapo atakamatwa?

Sheria inampa haki mtuhumiwa kutoa taarifa kwa familia, mwanasheria au rafiki juu ya kukamatwa kwake. Polisi lazima wamfahamishe mtuhumiwa kuhusu haki hii. Pia lazima wahakikishe anafahamu na anaweza kuongea na mwanasheria au mtoa huduma za kisheria. Vitu hivi vyote vimewekwa kisheria kupunguza uwezekano wa Askari Polisi kutumia madaraka yao vibaya. Iwapo Askari Polisi hawafuati taratibu hizi, mtuhumiwa atatakiwa kutoa malalamiko na polisi watatakiwa kujibu malalamiko mbele ya Mahakama.

  1. Je, Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu wakati wa kumkamata mtuhumiwa?

Hapana, katika mazingira ya kawaida, endapo mtuhumiwa atatoa ushirikiano kwa Polisi wakati wa kukamatwa au kuhojiwa, Polisi hawaruhusiwi kutumia nguvu. Hata hivyo kama mtuhumiwa atakataa kukamatwa na akatumia nguvu kujitoa chini ya ulinzi, Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu kwa kiasi kile tu kinachohitajika kumuwekachini ya ulinzi.

  1. Polisi wanatunzaje kumbukumbu za mali wanazohodhi kutoka kwa mtuhumiwa?

Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinaloliongoza Jeshi la Polisi, mtuhumiwa anapokamatwa mali yake huchukuliwa na Jeshi la Polisi. Mtuhumiwa hupaswa kutoa maelezo ya kina kuhusu vifaa hivyo. Aidha anapaswa kueleza aina ya mali, idadi yake, hali yake, na thamani yake iwekwe wazi. Hii husaidia kuondoa usumbufu au uwezekano wa kuchanganywa na vifaa vya mtu mwingine hali ambayo huweza kusababisha kubadilishana kwa mali au upotevu wa mali.

  1. Je, ni utaratibu gani unatumika kurejesha mali zilizochukuliwa na Polisi kama vielelezo?

Ikiwa suala limeishia katika Kituo cha Polisi mtuhumiwa ana haki ya kurudishiwa mali anayomiliki kihalali, endapo mali hiyo haihusiani na shauri la jinai alilotuhumiwa nalo. Katika mazingira ambayo mali ya mtuhumiwa inahusika na kesi inayoendelea mahakamani mahali hiyo itaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kama kielelezo cha kesi husika mpaka itakapotolewa mahakamani.

Iwapo shauri limeishia mahakamani na mali haikuhusika katika uhalifu; mtuhumiwa ana haki ya kuiomba Mahakama itoe amri ya kurudishiwa mali yake mara kabla au baada ya hukumu. Ikiwa vifaa hivyo vilitumika katika uhalifu mahakama inayo haki ya kuamuru vitaifishwe au virudishwe kwa mmiliki wake halali kwa kutegemea na uhalali wa mali yenyewe.

Endapo mtuhumiwa hajarudishiwa mali zake, na suala limeishia Polisi na mali zinamilikiwa kwa halali na havikutumika katika uhalifu na siyo sehemu ya ushahidi, anapaswa kuwasilisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Kituo, kama hajasaidiwa ataenda kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya au Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Kitengo cha Malalamiko ndani ya Jeshi la Polisi au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora au mahakamani kulingana na uzito wa suala lenyewe.

Vilevile, asiporudishiwa mali yake na shauri limeishia mahakamani ni jukumu lake kuwasilisha maombi kwa njia ya maandishi katika mahakama iliyotoa hukumu hiyo au mahakama ya ngazi ya juu kuomba apewe mali zake zilizotumika kama kielelezo.

  1. Je, Askari Polisi ana haki ya kumpiga mtuhumiwa aliyepo mahabusu?

Hapana. Hana haki ya kumpiga, kumtisha au kumtia hofu. Kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi. Askari Polisi anayefanya hayo anaweza kuadhibiwa kwa kosa hilo.

Sheria inasema kuwa mtu akiwa kizuizini, atatakiwa kutendewa kiubinadamu na kuheshimiwa na hatapaswa kutendewa ukatili, kinyume na ubinadamu au kudhalilishwa. Aidha mtuhumiwa aliyepo katika mahabusu ana haki ya kuomba kupatiwa matibabu au ushauri kuhusiana na ugonjwa au majeraha aliyonayo.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kumlazimisha mtuhumiwa kukiri kosa?


 

Hapana. Askari Polisi anayo haki na wajibu wa kumhoji mtuhumiwa baada ya kumueleza haki zake. Hata hivyo polisi hana mamlaka ya kumlazimisha mtuhumiwa kuongea kitu chochote ambacho hataki kusema au kukiri makosa ambayo hakufanya. Ikiwa mtuhumiwa amekataa kuongea ni wajibu wa Polisi kumfikisha Mahakamani ndani ya saa 24. Kukiri kwa kosa linalotokana na kuteswa linalofanywa mbele ya Askari Polisi kwa namna yoyote ile halitakubalika mahakamani kama ushahidi.

  1. Je Polisi Wanalazimika Kuandika Mahojiano wanayoyafanya kwa mtuhumiwa wanayemkamata?

Askari Polisi ni lazima aandike mahojiano yote atakayofanya na mtuhumiwa baada ya kumkamata. Askari Polisi anapaswa kutoa tahadhari kabla ya kufanya mahojiano na mtuhumiwa kwamba taarifa yoyote atakayoitoa na chochote atakachofanya kinaweza kutumika dhidi yake kwa ushahidi mahakamani.

  1. Je, mtuhumiwa anayeshikiliwa kituo cha Polisi anaweza kupata dhamana?

Inategemea amekamatwa kwa kosa gani, kwa mfano akikamatwa kwa makosa ya mauaji, uhaini, makosa ya kutakatisha pesa, wizi wa kutumia silaha, kufanya biashara ya dawa za kulevya au ugaidi ni miongoni mwa makosa ambayo mtuhumiwa hawezi kupata dhamana. Ikiwa amekamatwa kwa tuhuma za makosa mengine ni lazima Polisi wamjulishe kuwa anayo haki ya kupata dhamana kwa mujibu wa sheria. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inaeleza kuwa mtuhumiwa ana haki ya kupata dhamana ya Polisi kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:-

  • Akubali kwa maandishi kufika katika Kituo cha Polisi, siku, tarehe na muda utakapohitajika;

  • Akubali kwa maandishi kuzingatia masharti yatakayotajwa katika hati ya dhamana;

  • Mtu mwingine anayekubalika na Polisi akiri kwa maandishi kwamba anakufahamu na ana ahidi kumfikisha mtuhumiwa katika Kituo cha

  • Polisi au kuhakikisha kuwa anafika mahakamani tarehe na muda wowote atakapohitajika; na

  • Mtuhumiwa au mtu mwingine anayekubalika na Polisi, anaweka ahadi ya maandishi ya kulipa kiasi fulani cha fedha kama dhamana iwapo atashindwa kufika katika Kituo cha Polisi wakati atakapohitajika.

Vilevile, Askari Polisi msimamizi wa kituo cha Polisi anaweza pia kumuachia mtuhumiwa kwa dhamana kama:-

  • Alikamatwa bila kibali; na baada ya uchunguzi wa kina, kwa maoni yake, anaona kuwa hakuna ushahidi unaojitosheleza kuendelea na mashitaka;

  • Kosa analoshitakiwa nalo siyo kosa kubwa; au

  • Inaonekana kwamba uchunguzi zaidi utatakiwa kufanywa na hauwezi kukamilika ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, polisi wanaweza kumnyima dhamana mtuhumiwa endapo aliwahi kufungwa kwa zaidi ya miaka mitatu au kama mtuhumiwa aliwahi kukiuka masharti ya dhamana.

  1. Je, ni kitu gani kinatokea iwapo Askari Polisi atamnyima dhamana mtuhumiwa?

Iwapo Askari Polisi atamnyima dhamana ni lazima auweke uamuzi wake katika maandishi na aeleze sababu za kumnyima dhamana. Zaidi ya hayo, lazima apelekwe mahakamani haraka iwezekanavyo ndani saa 24 au kikao cha kwanza cha mahakama. Kama mtuhumiwa yuko mahabusu akisubiri kupelekwa mahakamani anaweza kumwomba Askari Polisi kumwezesha kufika mahakamani ili aweze kuwasilisha ombi lako la dhamana kwa hakimu.

Kama Askari huyo hatekelezi hilo bado ni lazima mtuhumiwa apelekwe mbele ya hakimu ndani ya saa 24. Ikiwa mtuhumiwa hatapelekwa mahakamani ndani ya saa 24 anaweza kuomba kuwasiliana na ndugu zake kama wapo au mwanasheria wake ili wapeleke maombi Mahakama Kuu ya kuiamrisha Polisi impeleke mahakamani.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa aliye mahabusu, ana haki ya kuachiwa pasipo kuchelewa pale ambapo:-

  • Askari Polisi aliyemkamata anaamnini kuwa hakutenda kosa lolote au hana sababu za kuendelea kuwekwa chini ya ulinzi wake;

  • Askari Polisi aliyemkamata anaamini kuwa amemkamata mtu asiyehusika kwa makosa; au

  • saa ishirini na nne kupita tangu kukamatwa kwake, hakuna hati rasmi ya mashtaka iliyofunguliwa kwa ajili yake na askari polisi huyo anaamini kuwa kosa analoshukiwa nalo siyo kosa kubwa kama ilivyodhaniwa.

  1. Je mtuhumiwa aliyepo mahabusu bila kuwa na kosa la jinai anaweza kuchukua hatua gani?

Pale ambapo hakuna lalamiko la kosa la jinai, lakini polisi wanaendelea kumshikilia mtuhumiwa ni ukiukwaji wa sharia.

Hivyo basi mtuhumiwa, familia yake au rafiki zake wanaweza kulalamika dhidi ya Askari Polisi huyo kwa mkubwa wake kimadaraka au kwa cheo au malalamiko yake yanaweza kupelekwa katika kitengo cha malalamiko kilichopo makao makuu ya Jeshi la Polisi au kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Kumbuka kuwa, kupitia mwanasheria wake, familia, ndugu au rafiki yake, anaweza pia kwenda moja kwa moja Mahakama Kuu kuomba kutolewa kwa amri ya kufikishwa mahakamani (Habeas Corpus) kuangalia uhalali wa kushikiliwa kwake ili aweze kuachiliwa.

  1. Je, ni vigezo vipi Askari Polisi anatumia ili kuamua mtuhumiwa apewe dhamana ya ahadi ya maandishi au ya kiasi cha fedha?

Mkuu wa wa kituo cha polisi lazima aangalie matakwa ya dhamana kwa mujibu wa sheria kabla ya kutoa dhamana kwakujiridhisha kuwa mtuhumiwa atahudhuria mahakamani au polisi wakati wowote atakapohitajika kutokana na majukumu yake katika jamii ajira au mahali anapoishi. Pili, hali halisi ya mazingira; asili na uzito wa tuhuma zinazomkabili; uzito wa ushahidi dhidi yake; uwezekano wake wa kutoroka; muda au kipindi atakachokaaa mahabusu ikiwa dhamana itakataliwa; usalama wake endapo atakuwa nje ya ulinzi wa polisi; na uwezekano wa kuvuruga ushahidi endapo atapewa dhamana.

SEHEMU YA NNE: POLISI, DEMOKRASIA, UTAWALA BORA NA UWAJIBIKAJI

  1. Je, Polisi anaweza kumkamata Polisi mwenzake kwa tuhuma za uhalifu?


 


 

Ndiyo. Jina zuri la Jeshi la Polisi na sifa njema ya watumishi wake inategemea sana uadilifu na uaminifu wa kila Polisi. Kila tendo la uhalifu linalofanywa na Askari Polisi katika utekelezaji wa shughuli zake linatoa sifa mbaya kwa Jeshi la Polisi. Hivyo, kila Polisi anayefahamu kuwa Polisi mwenzake anajihusisha na vitendo vya kijinai halafu akashindwa kuchukua hatua yoyote ile atakuwa anafanya makosa. Vilevile, Polisi mwenye cheo cha chini anaweza kumkamata Polisi mwenye cheo cha juu ikiwa Polisi huyo atatenda kosa la jinai mbele yake.

Hata hivyo, kabla ya kumkamata Askari Polisi mwenye cheo cha juu, atawajibika kutoa taarifa kwa Polisi mwenye cheo kikubwa. Wote waliopo kwenye mamlaka ambao watashindwa kutoa taarifa ya kuwepo au kuhisi dalili za uhalifu wanajiweka kwenye nafasi ya kuhisiwa kushiriki.

  1. Askari Polisi anaweza kuadhibiwa akifanya makosa?

Ndiyo. Ikiwa Askari Polisi atavunja sheria anaweza kuadhibiwa kama mtu yeyote yule. Kwa kuwa yeye ni mtu aliyepewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria anatakiwa kupewa adhabu stahiki kwa kuvunja sheria.

  1. Askari Polisi anaadhibiwaje?

Kuna njia nyingi za kuwaadhibu Askari Polisi waliofanya makosa. Kama ametenda kosa la jinai anaweza kushtakiwa Mahakamani na akahukumiwa kama mtu mwingine yeyote au akapelekwa kitengo maalum kinacho shugulikia makosa ya kinidhamu yanayotendwa na Askari Polisi kutegemeana na ukubwa wa kosa linalomkabili. Iwapo amekiuka miiko na maadili ya Jeshi la Polisi au hakutekeleza majukumu yake inavyotakiwa, ataadhibiwa kulingana na taratibu na kanuni za Jeshi hilo, ikiwemo ni pamoja na, kupewa onyo, kutozwa faini, kushushwa cheo au kufukuzwa kazi.

  1. Je, nini kifanyike endapo Askari Polisi atashindwa kumsaidia mtu au kuvunja haki zake?

Iwapo Askari Polisi hana msaada au amevunja haki ya mtu na kumsababishia madhara mtu huyo, anaweza kulalamika kuhusu jambo hilo kwa afisa wa Polisi wa ngazi ya juu kwa kupeleka malalamiko yake kwa njia ya barua au kwenda moja kwa moja kwa Polisi husika wa ngazi ya juu au katika kitengo ndani ya Jeshi la Polisi kinachoshughulikia malalamiko dhidi ya Askari Polisi. Katika hali hiyo Askari Polisi huyo anaweza kuonekana ana hatia ya kushindwa kutimiza wajibu wake. Vinginevyo mtu huyo anaweza pia kufungua shauri mahakamani au kulalamika kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kupeleka malalamiko yake kwa njia ya barua, simu, ujumbe mfupi wa maandishi, au kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Ili kutoa malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi, andika neno “Ujumbe” kwenda namba: +255 754 460 259.

  1. Askari Polisi anaweza kulalamikiwa dhidi ya mambo gani?

Anaweza kulalamika kuhusu tendo lolote lililofanywa au linaloendelea kufanywa na Askari Polisi ambalo ni kinyume cha Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu au Miongozo. Zingatia kuwa Askari Polisi ni mtumishi wa umma anayetakiwa kufanya kazi zake muda wote kwa mujibu wa sheria. Hapaswi kuvunja sheria, kuzembea au kuchelewa kufanya kazi yake.

  1. Ikitokea mtu amefungua malalamiko Kituo cha Polisi, na wakakataa kuchukua hatua dhidi ya Askari Polisi mwenzao afanye nini?

Hali hii ikitokea anatakiwa kupeleka malalamiko kwa mkuu wa kituo endapo hayatafanyiwa kazi ripoti kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya vivyo hivyo kama hakuridhika anatakiwa kutoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, na ikiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa hatochukua hatua stahiki anaweza kupeleka malalamiko katika Kitengo cha Sheria na Uadilifu kilichopo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania, au Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

  1. Je, Jeshi la Polisi linauhusiano gani na demokrasia ya vyama vingi vya siasa?

Kukua kwa demokrasia katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi kunategemea utendaji bora wa Jeshi la Polisi. Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi zimeweka bayana kuwa shughuli za kisiasa ni miongoni mwa mambo ya msingi katika jamii ya kidemokrasia. Hata hivyo, harakati za kisiasa zisipowekewa utaratibu mzuri huweza kugeuka kuwa vurugu na uvunjaji wa amani. Kwa sababu hiyo, jeshi la polisi lina jukumu la kutimiza wajibu wake pasipo upendeleo kuhakikisha kuwa shughuli zote za kisiasa zinafanyika kwa uhuru na kwa kudumisha amani na utulivu wa taifa.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kujiunga na Chama cha Siasa?

Hapana, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ni marufuku Polisi kujiunga au kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Jeshi la Polisi halipaswi kufungamana au kupendelea chama chochote cha siasa. Hata hivyo, Askari Polisi wana haki ya kupiga kura kama raia wengine.

  1. Je, Askari Polisi anaweza kumzuia mtu kushiriki maandamano au mkutano wa hadhara?

Inategemea na mazingira yaliyopo. Pale ambapo chama cha siasa au kundi fulaniwanapenda kufanya mkutano au maandamano lazima watoe taarifa ya maandishi kwa Afisa Polisi wa Wilaya wa eneo linalokusudiwa kufanyika mkutano au maandamano husika. Taarifa hiyo itaonyesha muda, mahala, wahusika, na lengo la mkutano au maandamano. Taarifa ya maandishi lazima itolewe Polisi muda wowote kabla ya saa 48 kufanyika kwa mkusanyiko au maandamano. Jeshi la Polisi lina wajibu wa kutoa ulinzi na kuhakikisha kuwa mkutano au maandamano hayo yanafanyika kwa amani na bila kuathiri haki ya kuishi na mali za washiriki au watu wengine. Afisa wa Polisi wa Wilaya anaweza akasitisha mkutano au maandamano endapo atahisi dalili za uvunjifu wa amani na usalama au kama taaratibu za utoaji taarifa hazikufuatwa.

Inapojitokeza kuwa Afisa Polisi wa Wilaya amezuia kufanyika kwa mkutano au maandamano ya amani, mwombaji anaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na hatimaye kufungua kesi mahakamani endapo kama mwombaji hataridhika na majibu ya Waziri.

Iwapo maandamano yameruhusiwa na katika kufanyika yakageuka kuwa fujo/ machafuko, Polisi wanaweza kuamuru yasitishwe na kuwataka wananchi watawanyike kwa amani. Wananchi wasipotawanyika hatua ya kuwatawanya itachukuliwa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

  1. Je, Polisi wanaweza kutumia nguvu kuvunja mkutano au maandamano?


 

Ndiyo, lakini hutumika tu kama njia ya mwisho baada ya njia zingine za amani kushindikana. Kama nguvu italazimika kutumika basi iwe ya kiasi, inayoendana na mazingira ya hatari inayoweza kujitokeza. Hivyo, Polisi hawapo kwa lengo la kuadhibu watu, bali kuhakikisha usalama na kulindwa kwa sheria.

  1. Je, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ina jukumu la kusimamia Jeshi la Polisi?

Ndiyo. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni taasisi huru ya kikatiba ya taifa iliyoundwa mahususi kuwa kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora Tanzania.

THBUB imeanzishwa chini ya ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 1977 na kuanza kazi yake tarehe 1 Julai, 2001 baada ya kuanzishwa sheria ya Tume Na. 7 ya 2001. Ibara ya 130 ya Katiba na kifungu 6(1) cha sheria ya Tume imeipa Tume mamlaka ya kupokea na kuchunguza malalamiko dhidi ya Askari Polisi juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo kwa mamlaka husika. Iwapo mapendekezo hayo hayakutekelezwa na mamlaka husika ndani ya miezi mitatu tangu kutolewa, Tume inaweza kupeleka masuala hayo mahakamani. Aidha, Tume hutoa ushauri kuhusu uboreshaji au urekebishaji wa sheria, kanuni au utaratibu wa kiutawala ili kukuza masuala ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

  1. Jeshi la Polisi linawajibika vipi katika kupambana na rushwa na makosa ya uhujumu uchumi?

Miongoni mwa vitendo vya kihalifu vyenye athari kubwa zaidi za kiuchumi katika taifa ni rushwa na uhujumu uchumi. Tangu miaka ya mwanzo ya 1980 taifa letu limechukua hatua mbalimbali kali za kisheria kupambana na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi. Makosa ya Rushwa hushughulikiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Miaka ya mwanzo ya 2000 Serikali iliongeza wigo wa kupambana na makosa ya ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya na utakatishaji wa fedha haramu. Ijapokuwa makosa yote haya yana viashiria tofauti, yote kwa umoja wake yanahatarisha uchumi wa nchi au hata usalama wa taifa hivyo Jeshi la polisi huchukua hatua.

Mwaka 2016 Bunge lilitunga sheria inayoanzisha Mahakama Kuu kitengo cha kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi na uhalifu unaohatarisha usalama kwa taifa. Jeshi la Polisi kama taasisi kuu ya kulinda raia na mali zao, linalo jukumu kubwa zaidi la kitaifa kwa kushirikiana na raia wema kunga’mua, kupeleleza, kukamata na kuchukua hatua zote za kisheria ili kuhakikisha kuwa juhudi za taifa za kupambana na rushwa na uhujumu uchumi zinafanikiwa.

  1. Je, Jeshi la Polisi hutilia maanani maadili na kushiriki katika michezo na utamaduni?

Kanuni za Jeshi la Polisi zinamtaka Askari kudumisha maadili mema na kuwa kiongozi wa mfano mzuri katika jamii akidumisha utamaduni wa Mtanzania na kuonesha ukakamavu unaostahili. Kwa sababu hiyo Jeshi la Polisi haliko nyuma katika shughuli za Michezo na mikakati ya kitaifa ya kudumisha utamaduni na heshima ya mtanzania. Jeshi la Polisi linazo timu za michezo mbalimbali hapa nchini. Jeshi lina vikundi vya ngoma na bendi ambavyo kwa ujumla huburudisha na kutoa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali ya ulinzi wa maisha na mali za Watanzania.

  1. Je, dhana ya Polisi Ushirikishwaji Jamii ni nini?

Katika kupambana na uhalifu, mbinu endelevu ni pamoja na kuishirikisha jamii katika kuzuia uhalifu. Dhana nzima ya Ushirikishwaji Jamii inajumuisha juhudi za pamoja na ushirika kati ya Jeshi la Polisi na raia katika kupambana na uhalifu. Inapaswa kufahamika kuwa nchi nyingi, ikiwemo Tanzania bado hazijaweza kuwa na idadi ya kutosha ya Askari Polisi kwa ajili ya kulinda raia na mali zao. Uchache wa Askari Polisi ni moja ya changamoto zilizotatuliwa kwa kuanzishwa UshirikishwajiJamii ambao licha ya changamoto zake imesaidia kukabiliana na uhalifu nchini.

Katika kuiwezesha jamii kushirikiana na jeshi la polisi katika kuimarisha ulinzi, usalama, amani na utulivu nchini, jeshi la polisi limeanzisha Kamisheni ya ushirikishwaji jamii. Kamisheni ya Ushirikishwaji wa jamii inayoongozwa na Kamishina inawawezesha wananchi kuwa karibu na polisi na kutoa taarifa kwa wakati za uhalifu na wahalifu.

Mfumo wa Polisi jamii sio tu huweka wajibu kwa wananchi kutoa taarifa kwa polisi juu ya matendo ya kihalifu bali pia kuhusisha kuweka mazingira mazuri ya mahusiano ya kupambana na makosa ya jinai kati ya polisi na wananchi. Hili linawezekana kwa kuondoa mtazamo hasi miongoni mwa wananchi kuwa polisi ni wakatili, walarushwa na wapo kwa lengo la kulinda maslahi ya serikali huku wakikiuka haki za wananchi. Polisi na wananchi wanapaswa kushirikiana kulinda taifa na sio kulinda maslahi ya watu wachache. Kuwe na mazingira mazuri ya kila mmoja kufurahia maisha yake katika nchini.

  1. Mtu atawezaje kujua haki zake akiwa chini ya ulinzi wa polisi?

Kisheria, wakati anapokamatwa na Askari Polisi anatakiwa kujulishwa haki zake zote. Pia kuna taasisi nyingi ambazo zinaweza kumsaidia mtuhumiwa kujua haki zake, kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Aidha Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha Idara Maalum kwa ajili ya Kuujulisha Umma kuhusu Haki zao na kupokea malalamiko ya masuala mbalimbali ya kisheria yanayowakabili wananchi. Vilevile kuna taasisi zinazotoa msaada wa huduma za kisheria pia zinaweza kumsaidia iwapo hajui haki zake za kisheria.


 

KWA MAWASILIANO YA DHARURA

TARIFA YA UHALIFU:

(POLISI: 112)

MALALAMIKO DHIDI YA POLISI +255 754 460 259 (TUME YA HAKI YA BINADAMU)


 

▲ To the top