Ijue Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016: Uchambuzi wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari


Tanganyika Law Society

IJUE SHERIA YA HUDUMA ZA VYOMBO VYA HABARI YA 2016

UCHAMBUZI WA SHERIA YA HUDUMA ZA VYOMBO VYA HABARI


FEBRUARY 2019


UTANGULIZI


Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanzania Bara) ni chama pekee cha mawakili Tanzania Bara kilichoanzishwa kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1954 sura namba 307. Pamoja na mambo mengine, chama cha mawakili kinawajibu wa kuisadia mahakama, serikali na wananchi katika masuala yote yanayohusu sheria.

Kutokana na jukumu lake hilo la kuisaidia serikali, mahakama na wananchi katika mambo yanayohusu sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika kilishiriki kikamilfu kama mdau wa sheria katika utungwaji wa Sheria ya Huduma za Habari. Ni vyema ikafahamika kuwa Chama cha Mawakili hushiriki katika utungwaji wa sheria mbalimbali kwa kutoa maoni yake ya kitaalamu yanayotoka kwa wanachama wake ambao ni wabobevu kwenye eneo husika.

Chama cha Mawakili kilipokea mwaliko wa kutoa maoni yake kwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari tarehe 26 Oktoba 2016 na baada ya uratibu wa kukusanya maoni ya wanachama waliobobea kwenye tasnia ya habari, chama kiliwasilisha maoni yake mnamo tarehe 29 Oktoba 2016. Ikumbukwe chama kiliwahi kutoa maoni yake mwaka 2015 wakati muswada huu ulipopelekwa Bungeni na kupingwa na wadau kwa kuwa na mapungufu mengi.

Kutokana na unyeti wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Chama cha Mawakili kimeandaa toleo hili la sheria hiyo kwa lugha rahisi kwa lengo la kuhakikisha umma na wadau wote wa habari wanaifahamu vizuri sheria hii.



SURA YA KWANZA: MCHAKATO WA KUANZISHA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI


Uundwaji wa Sheria ya Vyombo vya Habari ni mchakato ambao umechukua muda mrefu na mvutano wa hali ya juu nchini Tanzania toka miaka ya mwanzoni mwaka 1980 na 1990. Mvutano huu awali ulianza ukiwa na sura ya vyombo vya habari na wadau wa habari ikiwemo wanasheria, kudai sheria ya haki ya kupata taarifa.

Mnamo mwaka 2015 Serikali ilipeleka muswada wa Sheria ya Kupata Taarifa na muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari chini ya hati ya dharura. Kutokana na mapungufu makubwa yaliyobainishwa katika miswada hiyo na muda mdogo wa wadau kutoa maoni, wadau wa habari wakiongozwa na CORI­Coalition on the Right to Information walisusia miswada hiyo na kuliomba Bunge kutokujadili na kupitisha miswada hiyo mpaka pale wadau watakapopewa muda mpana wakuijadili na serikali kuondoa vifungu kandamizi katika miswada hiyo.

Serikali ilikubali ombi hilo la wadau na hivyo waliondoa miswada hiyo. Mwaka 2016, Serikali iliurudisha muswada wa Sheria ya Vyombo vya habari Bungeni ambapo tarehe 16/09/2016 muswada huo uliwasilishwa Bungeni rasmi bila hati ya dharura na ukasomwa kwa mara ya kwanza. Tarehe 4/10/2016 muswada ulisomwa kwa mara ya pili kisha ukajadiliwa na kupitishwa tarehe 5/10/2016. Baada ya Kupitishwa na Bunge Sheria hii ilisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli tarehe 16/10/2016.

SURA YA PILI: MALENGO YA KUTUNGA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Kupitia sheria hii, serikali inamalengo yafuatayo;

  • Kuweka utaratibu wa kisheria katika tasnia ya habari,

  • Kuunda bodi ya ithibati ya wanahabari,

  • Kuunda baraza huru la wanahabari,

  • Kushughulikia masuala ya kashfa na

  • Kushughulikia makosa yanayohusiana na utangazaji.

Kupitia kitabu hiki, chama cha wanasheria kitachambua pamoja na mambo mengine jinsi malengo hayo ya serikali kupitia sheria hii yamefikiwa.

SURA YA TATU: MAMBO YA MSINGI KATIKA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI


Ufutwaji wa Sheria ya Machapisho Sura ya 229 na Sheria ya Wakala wa Habari, Sura ya 149.

Kwa miaka mingi, Sheria ya Machapisho imeliliwa na wanahabari pamoja na wadau wa habari kuwa kandamizi na kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia Sheria hiyo pamoja na ile ya Wakala wa Habari, zilitajwa kama moja wapo ya sheria mbaya na kandamizi katika ripoti ya Tume ya Nyalali ya 1994.

Kwa kuzifuta sheria hizo, Sheria hii imeviondolea mbali vifungu kandamizi vilivyokuwa vikitumika kuminya wanahabari na vyombo vya habari. Hata hivyo, baadhi ya vifungu kandamizi vilivyokuwa kwenye sheria hizo mbili vimechukuliwa na kuwekwa kwenye sheria hii ya Vyombo vya Habari ya 2016 jambo ambalo sio jema kabisa. Miongoni mwa vifungu hivyo vilivyochukuliwa ni pamoja na mamlaka wa Waziri wa Masuala ya Habari kuweza kufungia chombo cha habari au kukataza uingizaji nchini wa jarida au gazeti kwa maslahi ya umma.

Uondoaji wa Hati ya Dharura ya Kupitisha Sheria

Baada ya kilio cha wanahabari, CORI, Baraza la Habari la Tanzania- MCT na wadau wa habari, Serikali na Bunge chini ya Spika Anna Makinda liliondoa muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa 2015 ambao uliwasilishwa Bunge kwa hati ya dharura na hivyo kuwanyima wanahabari, wadau na hata wabunge fursa ya mjadala mpana juu ya muswada huo na madhara yake. Kwa kuuondoa muswada na kuurudisha baadae bila hati ya dharura, wanahabari na wadau wa habari walipata muda mzuri wa kuujadili muswada na kuishauri Serikali na Bunge kuufanyia marekebisho. Uondoaji wa muswada na hati ya dharura ni jambo adhimu kuwahi kutokea na hivyo linapaswa kuungwa mkono na kuigwa na serikali au mabunge mengine hapa nchini na kwingineko.

Uondoaji wa Baadhi ya Vifungu Kandamizi Kwenye Muswada

Baada ya kuuondoa muswada wa 2015, serikali iliwasilisha muswada mwingine Bungeni mwaka 2016 ambao kwa kiasi Fulani ulikuwa na mabadiliko kadhaa ambayo yafuata ushauri wa wadau. Kwa mfano, muswada wa 2016 ulichukua mapendekezo 12 kama yalivyopendekezwa na CORI na kuzingatia sehemu ya mapendekezo 15 ya CORI. Japo mapendekezo 35 ya CORI hayakuzingatiwa kabisa, ni jambo jema kuona kuwa serikali ilijali na kufuata ushauri wa wadau.

Kuanzishwa kwa Baraza la Habari Lenye Uwakilishi wa Wanahabari

Kifungu cha 24 cha Sheria ya Vyombo vya Habari ya 2016 inaanzisha Baraza Huru la Habari. Kwa jina lake, Sheria hii inalitambua na kulitaka Baraza hilo kuwa huru kitu ambacho ni jambo jema kwa maendeleo na ukuaji wa tasnia ya habari. Licha ya kutaja na kulitaka Baraza hilo kuwa Huru, Sheria hii imeweka muundo wa Baraza kuwa na wajumbe wanne ambao wote wanachaguliwa na wanahabari waliosajiliwa. Muundo huu unalipa Baraza hili uhuru stahiki tofauti na endapo kama wajumbe wa Baraza hili wangeteuliwa na Waziri au kutokea serikali au kuwa watumishi wa serikali.

Hata hivyo, pamoja na kuwa Baraza la Wanahabari linaundwa na wanahabari wenyewe na wajumbe wa Baraza wanachaguliwa na wanahabari wenyewe, idadi ya wajumbe wanne kuunda Baraza ni udhaifu mkubwa ambao unalidhoofisha Baraza kwa kulikosesha uwakilishi mpana na pia kuifanya akidi yake kuwa ndogo sana (wajumbe watatu) na hivyo kulisababishia baraza kukosa mawazo kinzani ambayo ni tija kwa makuzi na mustakabali wa taasisi yoyote ya kijamii.

Kusimamia Ueledi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Habari

Kupitia kifungu cha 26(1)(a) Sheria hii inalipa Baraza Huru la Wanahabari jukumu la kuandaa kanuni za nidhamu ya wanahabari na vyombo vya habari na kuzisimamia kanuni hizo. Kwa kulipa Baraza hili la wanahabari jukumu hili, ni dhahiri kwamba, Sheria hii imelenga mambo mawili makubwa. Moja ni kuwa wanahabari walinde nidhamu yao wao wenyewe (self regulation) na pili kuwalinda wananchi na jamii dhidi ya wanahabari wasiofuata maadili mema katika jamii.

Pia kanuni hizi ambazo zitatokana na mamlaka ya Baraza chini ya Sheria hii, zitakuwa na msukumo wa kisheria na hivyo wanahabari na vyombo vyote vya habari vitapaswa kuzifuata.

Kuwataka Wamiliki wa Vyombo vya Habari kuwakatia Wanahabari Bima na Kuwalipia Hifadhi ya Jamii

Kazi ya uanahabari ni kazi ambayo kwa wakati mwingine kufanywa katika mazingira ya hatari ambayo yanaweza kuhatarisha uhai, afya na hata vitendea kazi vya mwanahabari. Licha ya kuwa ni kazi ambayo huweza kufavywa kwenye mazingira magumu pia ni kazi ambayo inaweza kumsababishia mwanahabari uadui miongoni mwa wanajamii anaoishi nao au anaoweza kukutana nao miaka mingi baadae hata baada ya kuacha kazi za uanahabari. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kazi ya uanahabari hugusa maslahi na maisha ya watu wakati wote na mara nyingi kwa ubaya na hivyo ni kazi inayojenga maadui dhidi ya mwanahabari.

Kwa kulitambua hilo, kupitia kifungu cha 62(1) Sheria hii imewataka wamiliki wa vyombo vya habari na waajiri wa wanahabari kuhakikisha kuwa wanawawekea bima dhidi ya hatari za kikazi wanahabari waliowajiri pamoja na kuwalipia pesa ya kinua mgongo katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa manufaa yao ya baadae.

Pia sheria inawataka wanahabari wa kujitegemea kukata bima zao za hatari kazini ili pia nao wajilinde dhidi ya hatari au madhara yanayotokana na kazi ya uanahabari.

Sharti hili linaweza kuonekana kama linaongeza gharama za uendeshaji wa vyombo vya habari lakini ukweli ni kuwa linatengeneza mazingira bora ya kazi kwa wanahabari na hivyo kuuhakikishia umma habari bora zaidi na endelevu kwani wanahabari watafanya kazi kwenye mazingira bora bila woga huku wakiwa na uhakika wa maisha yao ya baadae wakati wakiwa hawana nguvu za kufanya kazi (uzeeni)

Kuwatambua Wanahabari Huru/Binafsi

Kupitia kifungu cha 3 cha Sheria hii ambacho hutoa tafsiri ya maneno mbalimbali yaliyotumiwa, Sheria hii inamtambua mwanahabari ni pamoja na mwanahabari huru au binafsi ambaye hufungwi na chombo kimoja cha habari au huhudumia vyombo mbalimbali vya habari.

Hatua hii ya kutambua wanahabari huru ni nzuri nay a kuungwa mkono kwani kinapanua wigo wa taaluma au tasnia ya habari na kuongeza fursa za kujiajiri katika jamii na hivyo kuondoa dhana na kuajiriwa na badala yake kushawishi wanahabari kujiajiri.

Kuwatambua wanahabari huru au binafsi ni muendelezo wa taaluma na tasnia mbalimbali kutambua kada hiyo muhimu. Kwa upande wa taaluma/tasnia nyingine kama uanasheria na uhasibu, wapo wanasheria binafsi na wakujitegemea na wale wa kuajiriwa na pia wapo wa kuajiriwa. Vile vile kwa wahasibu, wapo walioajiriwa na wapo waliojiari na wote wanatambuliwa na sheria zinazoongoza taaluma au tasnia zao.

Kutambua na Kuweka Utaratibu kwa Wanahabari Toka Nje ya Tanzania

Taaluma au tasnia ya uanahabari haina mipaka ya kijiografia au utaifa, vivyo hivyo habari hazina mipaka au utaifa. Wanajamii wanapaswa na wanahaki ya kupata taarifa/habari ndani na nje ya mipaka ya taifa lao haswa pale inapokuwa habari hizo zinaweza kuathiri maisha yao kwa namna moja au nyingine.

Sheria hii kupitia Kifungu cha 19(3) inaruhusu wanahabari ambao sio watanzania au sio wakazi wakudumu wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria za uhamiaji kupewa kibali cha kufanya shughuli za uanahabari hapa nchini kwa muda usiozidi siku 90.

Hali hii ya kuwaruhusu wanahabari wan je ya nchi kufanya kazi ya uanahabari hapa nchini kuna faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni kuruhusu ulimwengu nje ya Tanzania kupata habari za Tanzania, kutoa fursa kwa wanahabari wa hapa nchini kujifunza kutoka kwa wanahabari wan je ya Tanzania ilihali wapo hapa nchini na kutoa fursa kwa tasnia ya habari hapa nchini kukua kama nchi zingine kwani wanahabari hawa wageni huja na teknolojia mpya.

Kuunda Mfuko wa Mafunzo ya Uanahabari

Kupitia Kifungu cha 22 cha Sheria hii, sheria imeunda mfuko wa mafunzo ya uanahabari na kuupa jukumu la kuwezesha utoaji mafunzo ya taaluma habari kwa wanahabari, kuwezesha uendeshaji wa tafiti mbalimbali zinazohusu uana habari na kuwawezesha mipango ya kuwajengea uwezo wanahabari wazawa. Mfuko huu uko chini ya Bodi ya Usajili wa Wanahabari na vyanzo vyake vya mapato ni pamoja na michango, ruzuku, tozo kutoka kwa vyombo vya habari na fedha zingine zozote zinazoweza kupatikana chini ya Sheria hii.

Kuundwa kwa mfuko huu na kuuwekea vyanzo vya mapato ni jambo zuri lakini vyanzo hivyo sio vya uhakika isipokuwa tozo inayotolewa na vyombo vya habari. Kutokana na ukubwa wa kazi itakayofanywa na mfuko huo ni vyema kama kungekuwa na chanzo cha mapato kinachotoka serikalini haswa kwenye bajeti ya taifa inayopitishwa na Bunge.

Ikumbukwe kuwa Serikali kuu inawajibu wa kuendeleza tasnia ya habari na hivyo kutokuweka chanzo cha mapato toka serikalini ni sawa na kukimbia wajibu wake.

Kuanzishwa kwa Orodha ya Wanahabari na Kutoa Kitambulisho cha Uanahabari

Tafsiri sahihi ya uanatasnia au uanataaluma ni watu wenye ujuzi au uelewa wa suala Fulani baada ya kufuzu mafunzo ya taaluma hiyo na kuwa na kutambulika kwa kuwepo kwenye orodha ya wanataaluma hao katika jamii Fulani. Uanahabari ni taaluma baada ya kupata mafunzo kutoka vyuo vya habari na kufuzu mafunzo hayo.

Nchini Tanzania mafunzo ya uanahabari yapo ya ngazi mbali mbali ikiwemo ni pamoja na mafunzo ya cheti, stashahada, shahada na kuendelea. Kwa bahati mbaya, tofauti na ilivyo kwa baadhi ya taaluma ambapo mtu mwenye cheti au stashahada kutokutambuliwa kama ni mwanataaluma hiyo, kwa upande wa tasnia ya habari hali bado haijawekwa sawa kwani hata mtu mwenye cheti na stashada ya habari anatambuliwa na jamii kama mwanahabari.

Kwa kuanzisha orodha ya wanahabari nchini Tanzania, Sheria hii ya Vyombo vya Habari kupitia Kifungu cha 20 na 21 kinahakikisha kuwa kunakuwa na vigezo na viwango vya mtu kufikia ili kuingizwa kwenye orodha hiyo ya wanahabari. Pia uwepo wa orodha hii ni nyenzo muhimu ya kuwatambua wanahabari waliokidhi viwango vinavyokubalika na hivyo kuhakikisha wanatoa habari zenye ubora.

Pia utoaji wa vitambulisho vya wanahabari ni jambo zuri kwani litahakikisha kuwa taifa linaondokana na wanahabari feki au ambao hawajafuzu wanaojulikana kwa jina maarufu la “makanjanja.” Pia vitambulisho hivi vitaleta heshima na nidhamu miongoni mwa wanahabari kwani watakuwa na woga wa kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu. Orodha hii ya wanahabari itasaidia pia kupata takwimu sahihi za idadi ya wanahabari waliopo nchini, wapo eneo gani la nchi na wanaubobevu wa eneo gani la habari.

Katibu wa Baraza la Wanahabari Kuteuliwa na Baraza la Wanahabari

Kupitia Kifungu cha 31, sheria hii inaunda nafasi ya Katibu wa Baraza la Wanahabari na linaweka sharti kuwa ateuliwe na Baraza kwa utaratibu wa ushindashi. Sharti hili ni zuri kwani linampa katibu huyo uhuru wa kiutendaji na kumfanya pia awajibike kwa Baraza Huru la Wanahabari na sio serikalini au kwingineko. Uhuru huu wa Katibu wa Baraza ni muhimu haswa kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari na hivyo ni muhimu awe huru kutetea maslahi ya wanahabari pale ambapo Bodi hiyo inafanya maamuzi yanayogusa maslahi ya wanahabari. Sheria hii pia imehakikisha kuwa Katibu wa Baraza hawi Katibu wa milele kwani imeweka ukomo wa kutumikia Baraza kwa kipindi cha muhula wa miaka mitano kinachoweza kuongezwa mara moja tu. Sharti hili linahakikisha kuwa damu mpya na maarifa mapya na mbadala yanapata nafasi kuingia kwenye utumishi wa Baraza la Wanahabari.

Mitambo ya Uchapaji kutotwaliwa wakati wa Kutwaa

Kwa kawaida katika sheria za jumuiya ya madola mamlaka ya kutwaa vifaa vinavyotumika kuchapisha machapisho yanayovunja sheria ya vyombo vya habari ilihusisha hata vyombo vya uchapaji ambavyo wakati mwingine humilikiwa na watu tofauti na wamiliki wa chombo cha habari. Kupitia Kifungu cha 60(1) Sheria hii imekataza utwaaji wa vifaa hivyo mpaka pale itakapothibitika kuwa kuendelea kutumika kwa vifaa hivyo kutazuia upelelezi.



SURA YA NNE: MAPUNGUFU YA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI


Serikali kuwa na Mamlaka ya Kuelekeza Maudhui ya Vyombo Binafsi vya Habari

Kupitia kifungu cha 7 (2)(b)(iv) Sheria ya Huduma za Habari inavitaka vyombo binafsi vya habari kutoa habari zenye maslahi ya kitaifa kama Serikali itakavyo elekeza. Kifungu hiki kwa hali ya kawaida sio kibaya ila kinatoa mwanya wa kutumiwa vibaya. Pia sharti hili au mamlaka yamewekwa kwa vyombo binafsi tu na sio vile vya Serikali ambavyo ndio haswa Serikali inapaswa kuvitumia kutoa habari zenye maslahi ya taifa. Sheria ingeweza kuvitaka vyombo vya habari binafsi kutoa habari zenye maslahi ya taifa na hivyo wao wangechagua habari hizo kwa kuzingatia sera na malengo yake. Kitendo cha kutoa mamlaka kwa Serikali kutoa maelekezo juu ya maudhui ya chombo cha habari hakiendani na uhuru wa kutoa na kupokea habari au kujieleza.

Vyombo Vya Habari Kutoruhusiwa Kutoa Habari Inayofanya Serikali Kushindwa Kumudu Uchumi

Kifungu cha 7(3)(h) kinavikataza vyombo vya habari kutoa taarifa au habari ambayo itaifanya Serikali kushindwa kumudu au kusimamia uchumi wa nchi. Hiki ni kifungu kingine ambacho kwa juu juu kinaonekana ni kizuri na kinalengo zuri la kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi hautetereki kutokana na habari iliyotolewa na chombo cha habari.

Hata hivyo bila kukiwekea ufafanuzi wa ni habari ipi ambayo itaifanya Serikali ishindwe kumudu uchumi, kifungu hiki kinatoa uhuru kwa Serikali kuamua ni habari ipi itaifanya ishindwe kumudu uchumi na hivyo kuvifanya vyombo vya habari na wahariri katika wakati mgumu wa kuamua ni habari ipi inayohusu uchumi itoke na ipi isitoke.

Pia Kifungu hiki kinaipa Serikali urahisi wa kufungia au kuadhibu chombo cha habari pale inapotaka kufanya hivyo kwa uonevu kwani habari yoyote ya kukosoa inayohusu uchumi inaweza kuchukuliwa kuwa inaifanya serikali ishindwe kumudu uchumi.

Waziri Kuteua Wanabodi wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari


Kwa mujibu wa kifungu cha 12(1) Waziri atateua wajumbe 7 kuwa wanabodi ya ithibati ya tasnia ya habari. Japo Bodi hii inauwakilishi wa wadau mbalimbali wengi wakitokea kwenye tasnia ya habari, wanabodi hao wote watateuliwa na Waziri. Ingekuwa vyema kama Sheria ingesema kuwa watu hao watachaguliwa na makundi wanayoyawakilisha. Kwa mfano, mwakilishi wa wahadhiri wa vyuo vya tasnia ya habari wangepaswa kuchaguliwa na wahadhiri wenyewe, vilevile, wawakilishi wa wanahabari pia wanapaswa kuchaguliwa na wanahabari wenyewe.

Mfumo huu wa kuchagua wawakilishi ndio bora zaidi na unaendana na demokrasia na utawala bora huku ukihakikisha kuwa maslahi ya kundi Fulani yanalindwa na hoja zao kufika bila kupindishwa. Mfumo wa wawakilishi kuteuliwa na wakilishwaji wenyewe umetumika kwenye sheria nyingi hapa nchini na hivyo ni vyema sheria hii ikarekebisha ili kuleta uwakilishi thabiti na kamili.

Ikumbukwe kuwa tasnia ya habari ni tasnia nyeti inayohitaji uhuru na ueledi wa hali ya juu hivyo uwakilishi wa moja kwamoja wa makundi yote ya tasnia hii kwenye bodi ya ithibati ni muhali.

Kuunda Makosa Yenye Wigo Mpana Unaoweza Kuminya Uhuru wa Habari

Ni dhahiri kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuwekewa misingi ambayo itahakikisha kuwa havitumiwi vibaya. Pamoja na uhitaji huo, misingi hiyo inapaswa kuwekwa umakini na kwa lugha inayoeleweka na isiyowacha tashwishi au mwanya wa kutumiwa vibaya kuminya uhuru wa habari kama unavyolindwa na Katiba.

Kifungu cha 50(1)(c) ni kifungu kimojawapo kinachotengeneza makosa ambayo yana wigo mpana na ni rahisi kutumiwa vibaya. Kifungu hiko kinaunda kosa la kutoa tamko ambalo linamaudhui ambayo yatahatarisha ulinzi, usalama, utulivu, amani na maslahi ya kiuchumi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maadili au masuala ya afya ya jamii kupitia chombo cha habari.

Kwa kuwa Sheria hii haijafafanua ni nini kinachoweza kuhatarisha ulinzi, usalama, utulivu, amani na maslahi ya kiuchumi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maadili au masuala ya afya ya jamii ni dhahiri kuwa atakacho kiona Waziri kuwa ni hatari kwa ulinzi au uchumi wa taifa sio sawa na atakavyoona mwanahabari.

Pia maadili ya watanzania sio kitu ambacho kimekubaliwa na watanzania wote kutokana na utofauti wa makabila, dini na hata hali ya hewa hivyo jambo linaloweza kuonekana ni tabia mbaya pwani huenda ikawa ni mila na desturi za watu wa kanda ya ziwa. Kwa kifupi ni rahisi kutumia kifungu hiki kwa nia ovu kuminya uhuru wa habari na kujieleza.

Mamlaka ya Waziri Kufuta au Kuadhibu Chombo cha Habari kinachohatarisha Usalama wa Taifa na Jamii

Kupitia vifungu mbalimbali hususan kifungu cha 59, Sheria imempa mamlaka Waziri kutoa adhabu kwa chombo cha habari kitakachotoa habari yenye maudhui yanayohatarisha usalama wa taifa na jamii. Hata hivyo, bila kuweka tafsiri ya maneno “usalama wa Taifa na Jamii” bayana kwenye sehemu ya tafsiri ya maneno mbalimbali, ni rahisi vifungu hivi kutumika vibaya kuviadhibu vyombo vya habari.


SURA YA TANO: MAKOSA NA ADHABU

Baadhi ya makosa yanayohusu vyombo vya habari yaliyomo kwenye sheria hii na adhabu zake ni kama ifuatavyo;

KOSA

ADHABU YA KIFUNGO

ADHABU YA FAINI

1. Kutumia chombo cha habari kwa madhumini ya kutangaza;

  1. Kwa makusudi au kwa uzembe habari uongo zitakazohatarisha maslahi ya taifa au ya mtu binafsi

  2. Taarifa yenye nia ovu au ya kutungwa

  3. Tamko lolote lenye maudhui ambayo yanahatarisha maslahi ya taifa au mtu binafsi

  4. Kuwasilisha tamko la uongo kama la kweli

  5. Kusambaza taarifa zilizokatazwa

Kisichopungua miaka 3 na kisichozidi miaka 5

Isiyopungua shilingi milioni 5 na isiyozidi shilingi milioni 20

2. Kuchapisha, kuingiza nchini, kuuza, kusambaza machapisho au sehemu ya chapisho ambalo limepigwa marufuku.

1. Kwa kosa la mara ya kwanza, Kisichopungua miaka 3 na kisichozidi miaka 5

2. Kwa makosa yanayofuatia, kifungo kisichopungua miaka 5 na kischozidi miaka 10

1. Kwa kosa la kwanza faini isiyopungua shilingi milioni 5 na isiyozidi shilingi milioni 10

2. Kwa makosa yanayofuatia faini isiyopungua shilingi milioni 8 na isiyozidi 20

3. Mtu yeyote ambaye kwa nia ya kuchochea uasi atafanya yafuatayo;

  1. Atatenda, atakula njama, atakusudia kutenda jambo lolote

  2. Atatamka maneno yoyote kwa nia ya kuchochea uasi

  3. Atachapisha, kutangaza, atauza, atasambaza chapisho lolote

  4. Ataingiza nchini chapisho

1. Kwa kosa la kwanza, kifungo kisichopungua miaka 3 na kisichozidi miaka 5

2. Kwa makosa yanayofuatia

  1. Kwa kosa la kwanza, faini isiyopungua shilingi milioni 5 isiyozidi shilingi milioni 10

  2. Kwa makosa yanayofuata, faini isiyopungua shilingi milioni 7 na isiyozidi shilingi milioni 20.

3. Kumiliki au kuwa na chapisho linalochochea uasi bila sababu za msingi

  1. Kwa kosa la kwanza, kifungo kisichopungua miaka 2 na kisichozidi miaka 5

  2. Kwa makosa yanafuata, kifungo kisichopungua miaka 3 na kisichozidi miaka 10

  1. Kwa kosa la kwanza, faini isiyopungua shilingi milioni 2 na isiyozidi shilingi milioni 5

  2. Kwa makosa yanayofuatia, faini isiyopungua shilingi milioni 3 na isiyozidi shilingi milioni 10

  3. Kushikiliwa kwa muda au Kutaifisha mitambo ya kuchapisho chapisho lenye uchochezi bila kujali mmiliki wa chapisho ni mmiliki wa mitambo

  4. Kufungia uchapaji wa chapisho kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka 3

4.Mtu aliyekutwa na kosa la kuchapa chapisho lenye uchochezi akiendelea kuchapa chapisho

kifungo kisichopungua miaka 3 na kischozidi miaka 5

Faini isiyopungua shilingi milioni 5 na isiyozidi shilingi milioni 10

5.Mtu anayechapa chapisho linaloleta hofu, mshituko au kuharibu utulivu wa jamii

kifungo kisichopungua miaka 4 na kischozidi miaka 6

Faini isiyopungua shilingi milioni 10 na isiyozidi shilingi milioni 20

6.Kosa chini ya Sheria hii linalotendwa na Shirika, Kampuni, Chama au muungano wa watu wengi

Kiongozi wa Kampuni au Chama au muungano ataadhibiwa kwa adhabu ya kosa lililotendwa chini ya sheria hii

Kampuni au Shirika au Muungano utatozwa faini isiyopungua shilingi milioni 15 na isiyozidi shilingi milioni 25.



SURA YA SITA: MAPENDEKEZO NA HITIMISHO

Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 kwa mapana yake ni sheria nyeti na inayosimamia tasnia nyeti na inayopaswa kuwa huru. Kwa kiasi Fulani Sheria hii imejitahidi kuweka mazingira bora zaidi kwa wanahabari ikiwemo ni pamoja na;

  • Kutambua uhuru wa habari,

  • Kuwatambua wanahabari kama wanataaluma kwa kuwaundia Bodi ya Ithibati na orodha ya wanataaluma hao,

  • Kuundwa kwa Baraza la Wanahabari na kuweka uwakilishi wa wanahabari

  • Kuliacha jukumu la kushughulikia nidhamu ya wanahabari chini ya Bodi ya Wanahabari wenyewe,

  • Kuunda mfuko wa mafunzo ya wanahabari,

  • Kuweka sharti kwa mmiliki wa chombo cha habari kuwakatia wanahabari bima ya kazi yao pamoja na kuwalipia michango katika mfuko wa hifadhi ya jamii.

Haya na mambo mengine mengi ni mambo mazuri chini ya sheria hii yanayopaswa kuungwa mkono na kusimamiwa na wote ili yatekelezwe.

Hata hivyo, Sheria hii kama zilivyosheria zingine haijakosa mapungufu ambayo yanapaswa kurekebishwa. Miongoni mwa mambo hayo kama yalivyotajwa hapo juu ni pamoja na;

  • Kumpa waziri mamlaka mapana na anayoweza kuyatumia vibaya,

  • Kumpa Waziri mamlaka ya kuteua wawakilishi wa makundi mbali mbali katika bodi ya Wanahabari badala ya kuacha makundi hayo kuchagua wenyewe wawakilishi wao

  • Kuunda makosa yenye wigo mpana yanayoweza kutumika vibaya kuminya uhuru wa vyombo vya habari

  • Kuacha mambo ya msingi kuundiwa kanuni na Waziri badala ya kuyawekea msingi kwenye sheria mama.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki katika lugha rahisi kitamsaidia Mtanzania wa kawaida kabisa katika kuelewa maudhui ya Sheria hii, haki zilizopo, wajibu na mipaka iliyoainishwa na sheria hii.

Shape1










KIMEANDALIWA NA

Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara

Kiwanja Na. 391, Mtaa wa Chato

Regent Estate, S.L.P 2148

Dar es Salaam, Tanzania.

Simu +255 22 2775313/ +255 22 5500002

Nukushi +255 22 2775314

Barua Pepe info@tls.or.tz

Tovuti www.tls.or.tz

© Chama Cha Wanasheria Tanzania Bara, 2019

Mwandishi

Stephen Msechu

Wahariri

Mackphason Buberwa,

Mabhezya Rehani

Kaleb Lameck Gamaya

Kimeandaliwa na kuhaririwa chini ya usimamizi wa Kamati ya Masuala ya Katiba na Sheria

Mpale Mpoki

Harold Sungusia

John Seka

Stephen Mwakibolwa

Daimu Khalifani

Elizabeth Mhagama

Paul Kaunda



SHUKRANI

Shukrani za pekee ziende kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika chini ya uongozi wa Mh. Tundu Antiphas Lissu kwa kutoa dira iliyoongoza uaandaaji wa chapisho hili. Pia shukrani ziwaendee wanachama wote ambao walishiriki kutoa maoni yao ya kitaalamu licha ya uwepo wa muda mfupi wa kupitia muswada na kutoa maoni.

Aidha shukrani pia ziwaende wanakamati wa kamati ya Masuala ya Katiba na Sheria wa chama cha Mawakili Tanganyika kwa kuratibu zoezi la ukusanyaji maoni na kuyawasilisha mbele ya kamati husika ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sambamba na Kamati, shukrani ziwaendee maafisa wa Sekretariati ya Chama kwa juhudi zao za kuhakikisha malengo na majukumu ya chama yanatekelezwa.

Mwisho na kwa namna ya kipekee, Chama kinatoa shukrani kwa asasi ya Faoundation for Civil Society kwa ufadhili wao ambao ulifanikisha utoaji maoni na uchapaji wa kijarida hiki cha sheria kwa lugha rahisi.




▲ To the top