Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi
Legal and Human Rights Center Tanzania

This booklet is published in partnership with the LHRC. The LHRC empowers the public and promotes, reinforces and safeguards human rights and good governance in Tanzania.

Collections

Kijarida Kuhusu

SHERIA YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI



Aprili, 2022

Kimeandaliwa na:


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Legal and Human Rights Centre [LHRC]

S. L. P. 75254, Dar es Salaam - Tanzania

Simu: +255 22 2773038/48; Nukushi: +255 22 2773037

Barua Pepe: lhrc@humanrights.or.tz

Tovuti: www.humanrights.or.tz


Ofisi ya Arusha

Barabara ya Olerian, Olosiva

Kitalu Na. 116/5, Sakina kwa Idd, Arumeru

S. L. P. 15243, Arusha - Tanzania

Simu: +255 27 2544187;

Barua Pepe: lhrcarusha@humanrights.or.tz


Kituo cha Msaada wa Sheria

Mtaa wa Isere - Kinondoni

S. L. P. 79633, Dar es Salaam - Tanzania

Simu/Nukushi: +255 22 2761205/6

Barua Pepe: legalaid@humanrights.or.tz


Ofisi ya Dodoma

Kitalu Na. 22 – Area D

S. L. P. 2289, Dodoma - Tanzania

Simu/Nukushi: +255 26 23500050

Barua Pepe: lhrc@humanrights.or.tz




SHUKRANI

Tunatoa shukrani za dhati kwa mwanasheria wetu Fredrick Lyimo na Fransisca Lengeju (wakili) pamoja na wafanyakazi wote wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hususani ofisi ya Arusha kwa kukiandaa kijitabu hiki.

DIBAJI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kina azma ya kusaidia jamii ya Watanzania kuwa na uwezo wa kufahamu sheria za nchi pamoja na kufahamu haki zao ili kuzilinda na kuzitetea pamoja na kuheshimu haki za wengine ili hatimaye tuwe na jamii yenye utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu pamoja na nchi inayoheshimu utawala wa sheria.


Tunafahamu kuwa kwa raia wa kawaida si rahisi kuzifahamu sheria zetu zote, na hata baadhi tu ya sheria zinazomgusa kutokana na mfumo tulio nao, ambao hautoi nafasi kwa watu wote kuzifahamu. Hali hii inasababisha watu wengi kujikuta katika migogoro dhidi ya kisheria ambayo igeweza kuepukika kama mtu huyo angejua sheria husika. Ndiyo maana basi Kituo kimeamua kutoa chapisho hili na mengine, kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa raia.


Huu ni usaidizi wa kisheria unaotoa maelezo mafupi na ya msingi ili kukusaidia ndugu msomaji uweze kupata ufahamu au maelezo ya sheria husika. Ni lengo letu kuwa, katika kijitabu hiki tunatoa usaidizi wa moja kwa moja kwako wewe pale utakapokuwa na tatizo au mmoja wa ndugu au jamaa zako wanapopata matatizo ya namna hii.


Tunachokuomba ni wewe kusoma kwa makini; na pale suala lako linapokwenda mbali zaidi ya maelezo haya, basi utafute msaada wa kisheria au uende kwa mwanasheria aliye karibu na wewe ili aweze kukusaidia zaidi.


Tunaamini utapata usaidizi huu kiurahisi zaidi na maelezo yaliyomo humu yatakusaidia kwa karibu. Umalizapo, tafadhali umsaidie na mwenzako kupata usaidizi huu.


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.


UTAMBULISHO WA KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika binafsi la kujitolea na la hiari ambalo si la kisiasa wala kibiashara. Kituo kimeandikishwa na kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania mnamo mwezi Septemba, mwaka 1995. Kabla ya kusajiliwa kama chombo huru, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilikuwa ni mradi wa haki za binadamu wa Mfuko wa Kuendeleza Elimu ya Sheria Tanzania (TANLET). Makao makuu ya Kituo yapo Dar es Salaam. Pia Kituo kina ofisi nyingine Arusha na Dodoma.


MAONO

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kina taamali jamii yenye haki na usawa.


TAMKO LA LENGO MAHUSUSI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali wala kibiashara linalojibidisha kukuza uwezo wa jamii ili iweze kukuza, kuendeleza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania.


LENGO KUU

Lengo kuu la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni kukuza uelewa wa sheria na haki za binadamu kwa jamii kwa ujumla na hasa wale wanajamii ambao kwa sababu moja au nyingine wameachwa nyuma. Uelewa unakuzwa kwa njia ya elimu ya uraia na msaada wa kisheria.

1. UTANGULIZI


Katika dunia ya sasa yenye maendeleo makubwa ya viwanda na sayansi, wafanyakazi wanafanya shughuli nyingi na hatari pia imeongezeka kutokana na shughuli hizo. Kwa kutambua kuwa wafanyakazi ni kundi muhimu sana ambalo linahitaji ulinzi wa kisheria kutokana na kazi wanazofanya, na kwamba hakukuwa na sheria inayoelekeza mfumo mzima wa fidia kazini, mwaka 2008 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya Fidia ya Wafanyakazi.


Sheria hii imekuja kuleta muongozo wa fidia kutokana na kuumia kwa mfanyakazi, kifo cha mfanyakazi au madhara anayopata kutokana na kazi.

2. MALENGO YA SHERIA HII


Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ilitungwa mwaka 2008 na imeanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwaka (na kufanyiwa marejeo mwaka 2015), ikiwa na malengo makuu yafuatayo:

  • Kuainisha kiwango cha madhara kwa wafanyakazi na kutoa fidia stahiki kwa wafanyakazi wanaopata ajali au ugonjwa kazini au kufariki wakiwa kazini.

  • Uanishaji wa viwango vya madhara, kutoa fidia stahiki kwa wafanyakazi wanaopata ajali, ugonjwa kazini au kufariki wakiwa kazini.

  • Kusaidia kurudisha hali ya awali ya wafanyakazi waliopata ajali kazini au ugonjwa unaotokana na kazi.

  • Kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa ajili ya wafanyakazi.

  • Kuanzisha mfumo wa kusaidia kuzuia ajali na magonjwa yanayotokana na mahali pa kazi.

3. MATUMIZI YA SHERIA

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inaelezea haki na wajibu wa makundi yafuatayo.

  • Waajiri na wafanyakazi wote wa sekta binafsi na umma.

  • Kwa wafanyakazi: -

    • Ambao wameajiriwa katika ndege au meli za Tanzania.

    • Ambao wameajiriwa nje ya Tanzania lakini wamepata madhara wakiwa Tanzania na mwajiri alikuwa akiwalipa kwenye Mfuko wa Fidia kwa mujibu wa Sheria.

    • Ambao wameumia au kupata magonjwa kutokana na kazi zao nje ya Tanzania ikiwa Mwajiri anaendesha shughuli zake kuu ndani ya Tanzania.



4. MAMBO MUHIMU YALIYOAINISHIWA KWENYE SHERIA YA FIDIA YA WAFANYAKAZI

Sheria hii imeainisha mambo kadhaa ya msingi ambayo mwajiri na mfanyakazi wanapaswa kuyafahamu. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:


4.1 Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi

Sheria imeanzisha mfuko maalum wa Fidia ya Wafanyakazi kuweza kutoa fidia kwa ugonjwa au madhara ya ajali iliyotokana na majukumu ya kazi. Mfuko huu unatoa viwango ambavyo mwajiri anapaswa kuchangia, faini endapo mwajiri atachelewa kuchangia, na usajili wa waajiri wanaochangia mfuko huo. Mfuko huu ni kwa mujibu wa sheria na ni lazima kwa waajiri wote kuchangia kama ilivyo mifuko mingine ya hifadhi ya jamii mfano NSSF na PSSSF. Hivyo waajiri wote wanapaswa kuchangia mfuko huu.

Kutokana na Kanuni za Fidia ya Wafanyakazi, waajiri wa Taasisi za Umma watachangia kiasi cha 0.5% ya mshahara wa mfanyakazi na Mwajiri sekta binafsi atachangia kiasi cha 1% ya mshahara wa mfanyakazi.


ANGALIZO

Ikumbukuwe kiasi hiki hakipaswi kukatwa kwenye mshahara wa mfanyakazi bali ni kiwango kinachochangiwa na mwajiri mwenyewe.



4.2 Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi

Sheria hii pia imeunda na kuanzisha Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Bodi ndio chombo chenye madaraka ya juu cha Mfuko wa Fidia. Kazi za bodi ni kuratibu shughuli za mfuko, kutengeneza sera na kusimamia utekelezaji wake, kumshauri waziri anayehusika na masuala ya kazi.


4.3 Haki ya Fidia na Ulinzi

Sheria hii pia imeelezea haki ya mfanyakazi kulipwa fidia pindi akipata ajali au ugonjwa. Sheria hii pia inatamka juu ya haki ya wategemezi kupata fidia endapo mfanyakazi atafariki kutokana na sababu ya kazi yake.


4.4 Utaratibu wa Madai ya Fidia

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi imeeleza na kuweka utaratibu unaotakiwa kufuatwa na mfanyakazi ili kudai fidia kwenye Mfuko wa Fidia. Ambazo ni;


  • Mfanyakazi anapaswa kutoa taarifa kwa mwajiri juu ya ajali aliyopata akiwa katika majukumu ya kazi, taarifa hii inaweza kuwa ya mdomo au maandishi.


  • Mwajiri pia anapaswa kutoa taarifa ya tukio la ajali linalomuhusu mfanyakazi wake ndani ya siku 7 tangu kupata taarifa, taarifa hii itatolewa kwenye fomu maalumu na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia.




4.5 Mchakato wa Uamuzi wa Kiasi na Aina ya Fidia

Sheria ya Fidia pia imeelezea mchakato wa kisheria wa namna ya kuhakiki kama ugonjwa au ajali husika iliyotolewa taarifa inakidhi vigezo vya kulipwa fidia. Sheria imeweka umakini huu ili kuondoa namna zote za udanganyifu zinazoweza kujitokeza katika zoezi zima la ulipaji wa fidia.



4.6 Fidia ya Matibabu na Ushauri

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi imeenda mbali zaidi kwa ajili ya kutoa nafuu ya matibabu na ushauri wa kimatibabu wa wafanyakazi waliopata madhara ya ajali au ugonjwa unaotokana na majukumu ya kazi. Mfano mfanyakazi ambaye amepata matibabu, mfuko utakuwa unawajibika kumlipia gharama za matibabu kwa kipindi cha miaka 2 mfululizo akiwa hospitali au akiwa anapata matibabu nyumbani kwa maelekezo ya wataalam wa afya.


4.7 Wajibu wa Waajiri

Kwa mujibu wa sheria hii mwajiri ana wajibu kama ifuatavyo;


  • Kutoa taarifa kuhusiana na shughuli anazofanya na juu ya wafanyakazi wake.

  • Kutunza kumbu kumbu za mishahara ya wafanyakazi na endapo atahitajika kutoa nyaraka hizo kwa ukaguzi anatakiwa afanye hivyo.

  • Endapo mwajiri atashindwa kutekeleza masharti ya wajibu wake basi anaweza kulipa faini isiyozidi Milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka 5.

4.8 Utatuzi wa Migogoro ya Fidia

Sheria pia imeweka utaratibu wa utatuzi wa migogoro inayotokana na ulipwaji wa fidia. Katika mchakato wa ulipaji fidia inawezekana upande wa mfanyakazi usiridhike, sheria imeweka utaratibu wa kusikiliza malalamiko ambapo mkurugenzi mkuu wa mfuko atafanya uamuzi na pindi akiona bado hajaridhika anaweza kukata rufaa kwa waziri kisha Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.


5. UTARATIBU WA KUFUATA ILI KUDAI FIDIA

5.1 Fidia ya Kifo

Mtu yeyote kwa niaba ya familia ya marehemu atatoa taarifa ya kifo kwa mwajiri haraka iwezekanavyo, pia anaweza kutoa taarifa kwa kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko haraka iwezekanavyo katika kipindi kisichozidi miezi 12 baada ya kifo cha mwajiriwa kilichotokana na ajali au ugonjwa uliotokana na kazi.


Mwajiri atatakiwa kutoa taarifa ya kifo kwa mkurugenzi mkuu ndani ya miezi 12 baada ya kifo cha mwajiriwa kilichotokana na ajali au ugonjwa uliotokana na kazi kwa kutumia fomu WCN-1, ambazo zitakuwa katika nakala halisi 3;

ambapo nakala ya kwanza itabaki kwa mwajiri, nakala ya pili atapatiwa mwakilishi wa familia ya marehemu na nakala ya tatu itawasilishwa kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko ndani ya miezi 12 ikiwa imeambatanishwa na: -



  • Nakala ya mkataba wa kazi au barua ya ajira;

  • Nakala ya kitambulisho cha kazi au barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri; na

  • Ripoti ya mwajiri kuhusu taarifa ya ajali.



Baada ya kutoa taarifa ya kifo cha mwajiriwa kwa mkurugenzi mkuu, mwakilishi wa familia ya marehemu atatakiwa kujaza taarifa za wategeemzi kwa kutumia fomu WCP-7 ambayo itathibitishwa na mahakama.


Mwajiri au mwakilishi wa familia ya marehemu atawasilisha madai ya fidia kwa mkurugenzi mkuu kwa kutumia Fomu WCC-1 na taarifa za wategemezi zilizopo katika fomu WCP- 7 pamoja na vielelezo vfuatavyo:

  • Cheti cha Kifo;

  • Kibali cha Mazishi;

  • Ripoti za Polisi hii ni (Taarifa ya udhibitisho ambayo hutolewa na askari endapo ajali imetokea barabarani angani au majini au taarifa ya upepeplezi wa kifo);

  • Muhtasari wa kikao cha familia ulioidhinishwa na mahakama husika ambapo shauri la mirathi limefunguliwa;

  • Kiapo cha msimamizi wa mirathi;

  • Hukumu ya mahakama kuhusiana na mirathi husika;

  • Taarifa za kibenki za wategemezi (Akaunti za Benki za Wategemezi);

  • Cheti cha ndoa kama marehemu ameacha mjane/mgane au kiapo cha ndoa kwa mwenza kutoka mahakamani;

  • Nakala za vyeti vya kuzaliwa vya watoto kama marehemu ameacha watoto chini ya umri wa miaka kumi na nane.


Baada ya vitu vyote hivi kukamilika na kuwasilishwa ndipo mkurugenzi mkuu atatoa maamuzi juu ya fidia ndani ya siku 30.


6. UTARATIBU WA KUFUATA BAADA YA KUPATA AJALI KAZINI


Mwathirika wa ajali kazini ambae ni mwajiriwa atapaswa kutoa taarifa ya ajali kwa mwajiri wake na kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko kwa kutumia fomu ya kutaarifu ajali WCN- 1.


Ambapo fomu WCN-1 inapaswa kujazwa katika nakala halisi tatu (3) na ziwe na muhuri wa mwajiri.Ambapo nakala moja mwajiriwa ataambatana nayo kituo cha afya au hospitali ikiwa imeambatanishwa na nakala ya kitambulisho cha kazi/barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiriwa. Nakala ya pili itabaki kwa mwajiri kwa kumbukumbu na nakala ya tatu iwasilishwe kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko ndani ya siku 7 ikiwa imeambatanishwa na:

  • Nakala ya mkataba wa kazi au barua ya ajira;

  • Nakala ya kitambulisho cha kazi au barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri;

  • Ripoti ya mwajiri kuhusu taarifa ya ajali.


Ambapo mwathirika wa ajali ambae ni mwajiriwa ataenda katika kituo cha afya au hospitali kupata matibabu na daktari anayemhudumia atapaswa kujaza fomu zifuatazo:-

  • WCC-2A fomu hii inapaswa kujazwa taarifa za awali za matibabu ndani ya siku kumi na nne;

  • WCP – 3 fomu hii itajazwa kama matibabu ya mwajiriwa yanazidi siku saba au kila wakati anapohudhuria kliniki;

  • WCP – 5 fomu hii itajazwa wakati mwajiriwa anarudi kazini kwa masharti mablimbali aliyopewa na daktari kwa mfano mapumziko ya muda wa kufanya kazi, kufanya kazi nyepesi, kubadilishiwa kazi au sharti linguine kwa kadiri daktari atakavyoona inafaa.


Baada ya kumaliza matibabu daktari anayemhudumia mwajiriwa atapaswa kujaza taarifa ya matibabu kwa kutumia fomu maalumu WCC – 2B pamoja na kumpatia cheti cha matibabu ambacho kitamuwezesha kurudi kazini WCP - 4.


Ambapo baada ya taratibu zote za utoaji taarifa na matibabu kukamilika,mwajiriwa,mwajiri au mtu yeyote kwa niaba ya mwajiriwa anaweza kuwasilisha madai ya fidia kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko kwa kutumia fomu WCC -1 ambapo baada ya kujazwa itawasilishwa kwa mkurugenzi mkuu wa mfuko katika kipindi kisichozidi miezi 12 tokea tarehe ya ajali.


Mkurugenzi mkuu atatoa maamuzi ya fidia ndani ya siku 30 baada ya kupokea madai yaliyokamilika. Ili madai yawe yamekamilika ni lazima yaambatane na vitu vifuatavyo:-

  • Nakala ya mkataba wa kazi au barua ya ajira;

  • Nakala ya kitambulisho cha kazi au barua ya utambulisho kutokakwa mwajiri;

  • Ripoti ya mwajiri kuhusu taarifa ya ajali;

  • Ripoti ya daktari ambapo itakuwa imejazwa kwenye fomu zifuatazo :-

  • (WCC-2A, WCP – 3, WCC – 2B, WCP -4, WCP-5)

  • Ripoti ya polisi ikiwa ajali hiyo inahusiana na ajali za barabarani, majini, angani au matukio ya jinai.


7. HITIMISHO


Hayo ni baadhi ya masharti na taratibu zinazotakiwa kufuatwa endapo mfanyakazi anapoumia, kufa au kupata ugonjwa kazini ili aweze kupata fidia. Hivyo ni muhimu kijarida hiki kusambazwa kwa wafanyakazi wengi zaidi kadri iwezekanavyo katika maeneo ya kazi ili waweze kujua haki zao. Kwani kuna wafanyakazi wengi wanapata ajali au magonjwa kazini lakini hawafahamu utaratibu wa kudai fidia.



▲ To the top