HOTUBA YA JAJI MKUU MHE. PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA KWENYE KILELE CHA WIKI YA ELIMU NA SIKU YA SHERIA JIJINI DAR ES SALAAM, TAREHE 06 FEBRUARI, 2020

admin's picture

 

HOTUBA YA JAJI MKUU MHE. PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA KWENYE KILELE CHA WIKI YA ELIMU NA SIKU YA SHERIA JIJINI DAR ES SALAAM,

TAREHE 06 FEBRUARI, 2020

Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mhe. Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Wah. Majaji Wakuu Wastaafu,

 

Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani,

 

Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani Wastaafu,

 

Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Jaji Kiongozi,

Wah, Majaji Viongozi Wastaafu, Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu,

Wah. Majaji wa Mahakama Kuu Wastaafu,

 

Balozi Augustino Mahiga (Mb) Waziri wa Katiba na Sheria,

Mhe. Prof. Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

 

Wahe. Makamishna wa Tume ya Utumishi Mahakama

 

Wahe. Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria

Wahe. Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Wahe. Viongozi wa Dini mbalimbali na vyama vya siasa, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,

Mhe. Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania,

Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali,

Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika,

Wasajili, Naibu Wasajili wa Mahakama wa ngazi mbalimbali, Wakurugenzi na Watendaji wa Mahakama,

Mhe. Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mahakimu wa ngazi mbalimbali, Viongozi Wandamizi wa Serikali, Mawakili wa Serikali na Wa Kujitegemea,

 

Wageni wetu Maalum kutoka Mahakama ya Uingereza na Scotland:

o Lord Iain Bonomy; Jaji Nic Madge; Sir Nicholas Blake; Alison Fenney; bila kumsahau Balozi wa Uingereza Sarah Cooke.

 

1.0   UTANGULIZI

Mheshimiwa Rais, kwa unyenyekevu mkubwa ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia tena katika maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini kwa mwaka 2020. Kwa niaba yangu binafsi na Mahakama ninakushukuru wewe Mheshimiwa Rais kwa kukubali mwaliko wangu kwa mwaka wa nne mfululizo bila kujali wingi wa majukumu uliyo nayo ya ujenzi wa taifa letu. Kukubali kwako kushiriki nasi Katika sherehe hizi ni heshima kubwa kwa mhimili wa Mahakama na ni ishara ya mshikamano na ushirikiano wa mihimili hii mitatu ya dola. Nichukue fursa hii kumshukuru pia Spika wa Bunge la Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai kukubali kuja kushiriki nasi katika tukio hili muhimu kwa Mahakama.

Kipekee naomba nitumie wasaa huu kuwatakia nyote heri ya mwaka mpya 2020, uwe ni mwaka wa amani na mafanikio kwetu sote.

 

2.0      KAULI MBIU MWAKA 2020

Mheshimiwa Rais, Kauli mbiu ya Mwaka huu 2020 unahusu— Uwekezaji na biashara kwa kukukumbusha wajibu wa Mahakama na wadau katika kukuza biashara na uwekezaji. Kauli mbiu hii inashabihiana na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano, kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati, ulio shindani na unaosukumwa na viwada, inayolenga kuwa na uchumi wa kati na viwanda wenye ushindani. Mahakama kama chombo cha kikatiba chenye kauli ya mwisho katika utoaji haki, ina wajibu wa kuhakikisha kuwa inatimiza wajibu wake wa kusikiliza mashauri kwa wakati, weledi na bila upendeleo; ili nchi iwe na Amani, istawi na ifikie malengo yaliyotajwa katika DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2025 na MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2015/16 - 2020/2021.

Nafasi ya Sheria katika Ufanisi wa Biashara na Uwekezaji

Wiki na Siku ya Sheria ni muda mzuri sana kwa wananchi kukumbushana umuhimu wa Katiba na Sheria katika kutuwezesha watanzania tuishi pamoja katika nchi huru na pia namna kama nchi, tunategemea kuwa sheria zitatumika kuwezesha na kufanikisha biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Sheria ina umuhimu pia kwa kuwa, panapotokea migogoro katika mahusiano ya kibiashara, uwekezaji na uchumi, wahusika hutegemea mahakama iwasikilize, itafsiri sheria na kisha itoe maamuzi kwa haraka. Kila nchi inayoazimia kuwa na uchumi unaokua kwa kasi, imeweka malengo ya kumaliza kwa haraka migogoro inayowasilishwa Mahakamani ili wananchi watumie muda wao na rasilimali yao katika kuzalisha mali, kutoa huduma na kukuza uchumi; badala ya kupoteza muda na fedha katika kufuatilia utatuzi wa mashauri yao Mahakamani. Kauli mbiu ya— “Uwekezaji na biashara; Wajibu wa Mahakama na wadau katika kukuza uwekezaji na biashara” inatukumbusha sisi Mahakama na wadau wetu katika sekta ya sheria, tunawajibu wa kuwezesha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa kuleta amani, utulivu na kuwezesha ufanyikaji wa biashara.

Mhe. Rais, kauli mbiu ya mwaka huu, inatutaka sisi katika utumishi wa umma tujitathmini kama tunatumia sheria na  taratibu za kimahakama sio kwa lengo la kuwezesha biashara na uwekezaji bali tunatekeleza sheria kwa kuweka vikwazo na vizuizi dhidi ya biashara na uwekezaji. Wewe binafsi, umekuwa mara kadhaa ukionyesha kutofurahishwa namna kadhaa wanaosimamia sheria za biashara na uwekezaji wamekuwa wakijenga urasimu, vizuizi na vikwazo badala ya kuwezesha na kufanikisha. Kwa mfano, mwaka 2016 uliagiza kuwa wajasiriamali wadogo wadogo (machinga) wanayo haki ya kufanya biashara na wasibughudhiwe. Disemba mwaka 2018 alizindua vitambulisho maalum kwa lengo la kuwatambua na kuwaruhusu hawa machinga wafanye biashara zao bila bugudha. Mfano mwingine, ni pale ulipoitaka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutochelewesha vibali vya tathmini ya athari ya Mazingira kwa wawekezaji ili kuongeza kasi  ya uwekezaji katika sekta ya viwanda na kufanikisha ukuaji wa uchumi. Ikiwezekana wawekeze kwanza vibali vya NEMC vitafuata baadae.

Mhe. Rais, nchi yetu kuwa na Sheria na taratibu nyingi nzuri haitoshi kuwezesha biashara na uwekezaji kama tabia na vitendo vya watumishi wa umma kujaa vikwazo na vizuizi dhidi ya walio masikini au wasio na uwezo. RIPOTI YA KAMISHENI KUHUSU MATUMIZI YA SHERIA KUWAWEZESHA MASKINI YA SHIRIKA LA MAENEDELEO LA UMOJA WA MATAIFA YA MWAKA 2008 (United Nations Commission on Legal Empowerment of the Poor, Making the Law Work for Everyone, UNDP, 2008) inatukumbusha watumishi wa umma na watumishi wa mahakama kwamba:

  1. Sheria lazima ifanye kazi kwa manufaa ya kila mtu bila ubaguzi wala upendeleo. Kwa zaidi, Sheria na taratibu za kimahakama ziwanufaishe watu walio masikini au wasio na uwezo. Usawa ni kumpandisha daraja aliye chini ili awe katika mizani sawa ya HAKI.
  2. Mafanikio ya sheria yapimwe kwa kutathmini ni kwa kiasi gani, Sheria imefanikiwa kuwaweka maskini walio wengi katika mizani sawa na wananchi wengine wenye uwezo au uelewa wa Sheria na taratibu.
  3. Uwezo wa sheria kuwezesha wananchi walio wengi hakuwezekani pale ambapo wananchi maskini au wasio na uwezo wanakutana na vikwazo vya sheria au taratibu za kimahakama ambazo zinawazuia kufaidi mfumo wa utoaji wa haki wa kimahakama. Kuna mifano mingi ya watumishi wa umma wanaosimamia leseni, vibali, ukaguzi, ukusanyaji wa kodi, uuzwaji wa mazao, biashara na kadhalika kuwa vikwazo vya biashara na uchumi badala ya kuwa wezeshi.

Ingawa Mahakama ndio sehemu ya mwisho unapotafuta haki, uondoshaji wa vizuizi na vikwazo dhidi ya biashara na uwekezaji, uanzie tokea Sheria na taratibu zinapotungwa, zinapotekelezwa hadi migogoro inapofikishwa Mahakamani. Vikwazo na vizuizi vinaweza kusababishwa na tabia binafsi ya uvivu, kupenda rushwa, uzembe na hata uwezo hafifu wa watumishi wa umma na watumishi wa mahakama.

 

3.0   MATUMIZI YA TEHAMA

Mhe. Rais, dhana kwamba Mahakama na Taasisi za Umma zitumie sheria pamoja na taratibu za kimahakama kama nyenzo za kuwezesha na kufanikisha uchumi, biashara na uwekezaji; imetumiwa na Mahakama ya Tanzania kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo Mahakama ya Tanzania imeamua kuitumia. Uwezeshaji na ufanisi wa biashara na uwekezaji utakuwepo pale ambapo Sheria na taratibu zinafuata misingi ya uwazi, uwajibikaji na ufanisi. Kwa

Mahakama ya Tanzania, matumizi ya TEHAMA yameendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwezesha utoaji haki kwa wakati na kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.

Mheshimiwa Rais, Mfumo wa Kielekitroniki wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS II) uliouzindua mwaka jana umeendelea kuwa msaada mkubwa katika kurahisisha shughuli za uendeshaji wa mashauri. Mfumo huu ambao unatoa taarifa kwa wadau kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi na barua pepe, umeunganishwa pia na wa malipo ya serikali (Government Electronic Payment Gateway (GEPG)) na Mfumo wa Kusimamia Mawakili (TAMS). Kuunganishwa Mfumo wa JSDS2 na mfumo wa malipo ya Serikali umeiwezesha Mahakama kudhibiti ukusanyaji wa Tozo na Ada. Udhibiti huu umewezesha ongezeko la maduhuli toka shillini billion 1.6 mwaka 2017 mpaka shililing billion 2.5.

Pia katika kipindi cha mwaka jana jumla ya mashauri 2435 yalifunguliwa kwa kielektroniki. Lengo la Mahakama ni kuendelea kuboresha mfumo kwa kutumia wataalamu wa ndani.

Aidha katika kuhakikisha maamuzi yanakuwa na ubora na kutolewa kwa wakati, maamuzi mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani yamewekwa katika tovuti ya Mahakama kupitia kanzidata ya TanzLii kuwezesha ufanyikaji wa rejea na utafiti kwa Majaji na Mahakimu na wadau wote.

Mheshimiwa Rais, Mahakama inatambua kuwa bajeti yake inatokana katika kodi za wananchi, kwa hiyo ni wajibu wetu kuendelea kubuni na kutumia mikakati ambayo inapunguza gharama na muda wa kuendesha wa mashauri ili wananchi wapate muda mwingi zaidi katika uzalishaji mali na kutoa huduma. Ninayo furaha kukutaarifu kwamba tumesimika vifaa vya  mawasiliano kwa njia ya video (Video Conferencing) katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, Bukoba na Mbeya. Pia vifaa hivyo vimefungwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Mashauri 60 ya Mahakama ya Rufani yamesikilizwa kwa kutumia mfumo huu. Mfumo huu umetumika pia kuwasikiliza mashahidi waliokuwa katika nchi za Uingereza, Marekani, China na Nairobi. Njia hii ya usikilizaji wa mashauri inapunguza gharama na muda wa wadaawa na wa Mahakama. Kwa mwezi Januari, 2020 pekee, mashauri 27 yamesikilizwa kwa njia ya Video Conference kati ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko hivyo kuokoa gharama za ulinzi na usafirishaji wa mahabusu. Ni malengo ya Mahakama kuendelea kusimika vifaa hivi katika maeneo husika ili kupunguza gharama na muda na kuwawezesha wadau na wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kwa manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

 

4.0   MAENDELEO YA WATUMISHI

Mheshimiwa Rais, mahitaji ya watumishi ni makubwa, hii ni kutokana na ukweli kwamba sio tu shughuli za Mahakama zimesambaa kila kona nchini, bali zimeongezeka sana baada ya uzinduzi wa mahakama nyingi hivi karibuni. Uchambuzi unaonesha kwamba, ili mahakama zote nchini zifanye kazi kwa ufanisi kwa upande wa rasilimali watu, inahitaji kuwa na watumishi 10,351. Hata hivyo watumishi waliokuwepo mpaka sasa ni watumishi 5,947 tu ikiwa ni pungufu ya watumishi 4,404 .

Mheshimiwa Rais, pamoja na upungufu uliopo, idadi ya watumishi wa Mahakama imeendelea kupungua siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali. Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2019, jumla ya watumishi 258 wameondoka kazini kati yao 192 kwa kustaafu, 39 kwa kufariki, na 27 kuacha kazi. Watumishi wengine 2 waliondolewa kazini kutokana na sababu za kimaadili.

Mheshimiwa Rais, Naishukuru Serikali kutoa vibali vya ajira kwa watumishi 137 waliajiriwa mwaka 2019. Hata hivyo kupitia kwako tunaomba tukubaliwe kuajiri watumishi 268 kwa ajili ya Mahakama mpya zinazoanzishwa, zikiwemo Mahakama Kuu ya Kigoma na Musoma ambazo zitazinduliwa hivi karibuni.

Aidha, tumewasilisha nafasi za ajira mbadala 358 ambazo maombi yake yaliwasilishwa kwenye mamlaka husika. Bado tunasubiri majibu.

 

5.0   RUSHWA NA MAADILI SEHEMU YA KAZI

Mheshimiwa Rais, ili Mahakama ya Tanzania ifanikiwe katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kutoa haki kwa wakati kwa mujibu wa ibara ya 107A (1), ni lazima watumishi watekeleze majukumu yao kwa weledi, nidhamu na maadili. Hili linafanyika kupitia MPANGO WA KUPAMBANA NA RUSHWA ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kupambana na Rushwa Nchini (NACSAP III).

Mpango huu na mikakati mingine ambayo Mahakama imejiwekea ya kupambana na vitendo vya rushwa, kwa mfano kupitia mabango na namba za simu za kutoa taarifa. Juhudi hizi zimepunguza idadi ya watumishi ambao walishtakiwa kwa masuala na kinidhamu.

 

6.0   KAMATI ZA MAADILI

Mheshimiwa Rais, Katika kusimamia nidhamu na maadili Tume ya Utumishi wa Mahakama hushirikiana na Kamati za Kamati za maadili za Mikoa na Wilaya ambazo zinaongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Kamati hizi zinaundwa chini ya kifungu 36 cha SHERIA YA UENDESHAJI WA MAHAKAMA,

SHERIA NA.4/2011 ndio ni jicho la Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kusimamia na kuimarisha nidhamu na maadili ya Mahakimu. Tathmini iliyofanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu utendaji wa Kamati za Maadili hizi ilibaini kuwepo kwa mapungufu ya wajumbe wa Kamati za Mikoa na Wilaya kutofahamu vyema majukumu na mamlaka waliyopewa na sheria, kuchelewa kwa chunguzi zinazofikishwa kwenye Kamati; na Kamati hizo kushindwa kukutana kama Sheria inavyozitaka kukutana angalau mara moja kila mara baada ya miezi tatu.

Mheshimiwa Rais, kutokana na mapungufu hayo, athari zinazojitokeza ni pamoja na kuchochea malalamiko kutoka kwa wananchi hivyo kupunguza imani ya wananchi juu ya Mahakama kwa vile malalamiko dhidi ya mahakimu hayashughulikiwi kwa wakati. Mapungufu katika utendaji wa Kamati huchangia pia kumomonyoka kwa maadili kwa baadhi ya Mahakimu ambao wanahisi kuwa hakuna chombo madhubuti katika ngazi za mikoa na wilaya kuweza kushughulikia utovu wao wa nidhamu. Wakati mwingine wenye viti wa Kamati za Maadili ya Mikoa na Wilaya huvuka mipaka ya mamlaka zao kwa mujibu wa sheria na kuingilia kazi za kimahakama za utoaji haki.

Mheshimiwa Rais, ili kukabiliana na changamoto hizo, Tume imeandaa muongozo wa Maadili ya Maafisa wa Mahakama unaokidhi mahitaji ya SHERIA YA UENDESHAJI WA MAHAKAMA NA.4/2011 na maboresho ya Mahakama yanayoendelea. Muongozo huu wa uendeshaji wa Kamati ambazo wenyeviti wake huwa ni wakuu wa Mikoa na Wilaya unakusudia kutolewa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili. Miongozo hii iliyotayarishwa kusaidia utendaji wa Kamati za Maadili ya Mikoa na Wilaya itazinduliwa na Dkt. Augustine Philip Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria huko Dodoma mnamo tarehe 11 Februari 2020.

Mheshimiwa Rais, kwa kuwa wakuu wa Wilaya na Mikoa wako chini ya Ofisi yako (TAMISEMI), tunaomba Wizara ya TAMISEMI ihakikishe kuwa wakuu wa Wilaya na Mikoa wanawezeshwa kibajeti ili hizi Kamati za Maadili za Wilaya na Mikoa zifanye kazi kama ambavyo viongozi hawa wa mikoa na wilaya husimamia huduma za sekta nyingine kwa mfano afya, elimu, barabara, kilimo n.k

Ni matumaini yangu na ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa, Wajumbe wa Kamati za Maadili za Mahakimu katika ngazi za Mikoa na Wilaya watazingatia vema taratibu kama ambavyo zimefafanuliwa kwenye hii Miongozo itakayozinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria.

 

7.0   MASLAHI YA WATUMISHI

Mheshimiwa Rais, ulipokuja kuungana nasi kama mgeni rasmi kwenye kilele cha Siku ya Sheria tarehe 6 Februari, 2019, ulisikia kilio cha watumishi wa ngazi mbalimbali za Mahakama kuhusiana na maslahi mbalimbali ya kikazi. Hili ni kutokana na hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ya kimahakama ambayo hutofautiana sana na Taasisi nyingi za Umma. Sihitaji kueleza hapa zaidi ya ulichoahidi wakati ukifungua Bunge jipya tarehe 20/11/2015 kwamba utalipa uzito swala la uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.

Mheshimiwa Rais, Tume ya Utumishi wa Mahakama tayari imeshatekeleza wajibu wake kwa kukushauri juu ya maslahi na mishahara ya watumishi wa Mahakama chini ya Ibara ya 113 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria Na. 4 (2011) kifungu cha 31(1) na (2) na 32 cha Sheria hiyo. Naomba kuchukua fursa kukukumbusha juu ya mapendekezo yetu kwako kuhusu maslahi na mishahara ya watumishi wa Mahakama. Ni matumaini yetu kwamba maombi yetu hayo madogo kwako yatapata baraka zako tele na watumishi wa mahakama wataendelea kuchapa kazi kwa ari zaidi na uadilifu zaidi. Najua unafahamu sana maana kila mara umekuwa ukiniambia kuwa unafahamu hali halisi ya maslahi ya watumishi wa Mahakama.

8.0   USIKILIZAJI WA MASHAURI

Mheshimiwa Rais, kupitia mashauri mbali mbali Mahakama ya Tanzania inatekeleza wajibu wake wa kikatiba, ambao ni kutoa  haki sawa kwa wote na kwa wakati. Tuna imani kwamba katika kutoa haki kwa weledi na wakati tunaimarisha uchumi. Kupitia utoaji haki, amani, utulivu, utawala wa sheria na ustawi wa nchi upatikana na hivyo kuwapa nafasi kwa wananchi  kufanya shughuli za kiuchumi na kuweka mazingira wezeshi ya ufanyikaji wa biashara. Wafanyabiashara na wawekezaji  watavutiwa kuwekeza katika nchi yetu iwapo kutakuwa na misingi imara ya utoaji haki iliyo bora inayotoa haki bila upendeleo na kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni.

Mheshimiwa Rais, Kwa kuzingatia elekezo la kikatiba linaloilazimu Mahakama kuzingatia takwa la kutochelewesha haki bila sababu za msingi, Mahakama imejiwekea sera ya kuhakikisha kuwa mashauri yanapofunguliwa Mahakamani yanakuwa na muda maalum wa kukamilika katika ngazi husika ya Mahakama. Sambasamba na hili, kama unavyofahamu kila Jaji na Hakimu ana malengo ya kumaliza idadi ya mashauri kwa mwaka. Pamoja na kubeba mzigo mzito wa mashauri, Majaji, Wasajili, Mahakimu, watendaji na watumishi wengine, wamejitahidi na kuweza kuvuka malengo waliyojiwekea.

Kwa mwaka jana 2019 Mahakamani iliweza kumaliza mashauri kwa idadi sawa na idadi ya mashauri yaliyofunguliwa mwaka huo wa 2019 (100% clearance rate) na kutozalisha mlundikano wa mashauri. Mahakama katika ngazi zote ilianza mwaka 2019 ikiwa na mashauri 67,881 yaliyobaki kutoka mwaka 2018. Mashauri 272,326 yalifunguliwa kati ya Januari mosi na tarehe 31 Disemba 2019 hivyo kuwa na jumla ya mashauri 340,137 kwa mwaka 2019. Jumla ya Mashauri 271,214 yalisikilizwa mwaka 2019 na kubakiwa na mashauri 68,648 tu kati ya mashauri hayo, ni mashauri 3,677 tu ndiyo yenye zaidi ya miaka miwili Mahakamani sawa na 5% ya mashauri yote yaliyobakia. Ninapenda kukutaarifu kwamba Mahakama za Mwanzo ambazo ndio zinatumiwa zaidi na wanachi zilimaliza mwaka kwa kubakiza mashauri 4 tu yenye zaidi ya miezi 6 Mahakamani na baadhi ya Mahakama za Mwanzo hazikubakisha shauri lolote lenye umri Zaidi ya miezi sita tangu kusajiliwa. Mashauri hayo 4 niliyoyataja yapo katika mahakama za juu kwa ajili ya rufaa na mapitio. Lengo letu ni kuendelea kupunguza mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama. Takwimu zinathibitisha kuwa Mahakama ya Tanzania inachapa kazi na kiwango cha uchapa kazi wa kila mtumishi kinapimwa ki-takwimu.

Mheshimwa Rais, pamoja na wewe binafsi kuteuwa Majaji 11 wa Mahakama ya Rufani na 39 wa Mahakama Kuu, bado mzigo wa kazi ni mkubwa kupita malengo ambayo tumejiwekea. Mathalani Mahakama ya Rufani ina mzigo wa kazi wa mashauri 847 kwa idadi wa majaji ambao wapo sasa 17 na ifikapo mwezi Julai mwaka huu majaji wa Rufani watapungua hadi 16. Mahakama Kuu kabla ya uteuzi ulioufanya mwishoni mwa mwaka jana mzigo wa kazi ulikuwa ni mashauri 585 kwa kila Jaji. Ongezeko la majaji 12 limepunguza kidogo mzigo wa kazi kuwa mashauri 513 kwa kila Jaji.

Kwa mwaka 2019, jumla ya Majaji watano (5) walistaafu, na mwaka huu 2020 Majaji wanne (4) watastaafu. Tume ya Utumishi ya Mahakama itatapendekeza kwako hivi karibuni, uteuwe Majaji na pia kuongeza ajira kwa Mahakimu ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutoa haki kwa wakati.

 

9.0   MKAKATI WA KUONDOA MLUNDIKANO WA MASHAURI Mheshimiwa Rais, Mahakama katika kuondokana na mlundikano wa        mashauri    imekuwa    ikitumia    mbinu    kadhaa,    ikiwemo kuwatumia   Mahakimu  wenye   Mahakama   za   ziada   (Extended Jurisdiction)   kusaidia   mashauri   katika   Mahakama   Kuu   na tumekuwa kukiendesha mipango maalum ya umalizikaji wa mashauri ya mlundikano.

Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya sheria, aliwapa Mahakimu takribani 195 mamlaka ya ziada ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu. Ningependa kuchukua fursa hii, kukutaarifu kwamba Mahakimu 98 wenye mamlaka ya ziada wameweza kumaliza mashauri 1,132 ya Mahakama Kuu kwa kipindi cha mwaka jana.

 

10.0 MASHAURI YA KIPAUMBELE

Mheshimiwa Rais, kwa kuelewa dira ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda Mahakama imeyapa kipaumbele na kutambua mashauri ambayo moja kwa moja yanahusiana dira hiyo yakiwemo mashauri ya kibiashara, yanayohusiana na miradi, rushwa na uhujumu uchumi na mashauri ya ardhi.

Uanzishwaji wa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na kuanzishwa kitengo mahususi kwa ajili ya usuluhishi Dar es Salaam ilikuwa ni kwa lengo la kuhakikisha mashauri haya yanayolenga uchumi yanasikilizwa kwa haraka.

Tangu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilivyoanzishwa Julai 2016 jumla ya mashauri 391 yanayohusu maombi ya kawaida na maombi dhamana yamesajiliwana mashauri 385  yamemalizika  na  kubaki  mashauri  tu.  Mashauri  119 ya uhujumu uchumi yamesajiliwa na mashauri 89 yamemalizika ikiwa ni asilimia 74 ya idadi ya mashauri. Katika mashauri hayo faini ya kiasi cha billion 13.6 na fidia ya kiasi cha shilingi billion 30.6 zimetolewa.

Idadi ya mashauri ya maombi ya dhamana katika Divisheni hii ni kiashiria cha wingi wa mashauri ya uhujumu uchumi ambayo yatashughulikiwa na pindi upelelezi wa mashauri hayo utakapokamilika. Mahakama imejipanga kuhakikisha mashauri yote yanayosajiliwa yanasikilizwa ndani ya miezi tisa kama inavyolekezwa katika Kanuni za Divisheni ya Uhujumu Uchumi. Takwimu kutoka Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya mashauri ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi bado zimekwama katika hatua za awali kusubiri upelelezi kukamilika kabla ya kuwasilishwa katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kusikilizwa.

Sheria kuhusu Rufaa za Kodi inamruhusu mlipa kodi ambaye hakubaliani na uamuzi wa mwisho wa makadirio uliyofanywa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kupeleka rufaa yake ya awali mbele ya Bodi (Tax Revenue Appeals Board). Na endapo Mamlaka ya Mapato au mlipa kodi hajaridhika na uamuzi wa Bodi ya Rufaa za Kodi hukata rufaa katika Baraza la Kodi (Tax Revenue Appeals Tribunal). Bodi na Baraza la Kodi ipo chini ya Wizara ya

Fedha. Mahakama ya Rufaa imepewa jukumu la kusikiliza Rufaa ya mwisho kutokana na maamuzi ya Baraza la Kodi.

Kwa kipindi cha mwaka jana Mahakama ya Rufani ilisikiliza jumla ya mashauri 21 yenye kubishaniwa kodi ya kiasi cha Tanzania shililingi billioni 41.7. Vilevile yapo jumla ya Mashauri 20 yenye kubishaniwa kodi kiasi cha dola za kimarekani million 247 na shillingi za kitanzania billioni 24.3 yapo yamebaki na yanategemewa kusikilizwa katika vikao vya mwaka huu. Mashauri haya yote hayana zaidi ya miaka 2.

 

11.0 KANUNI NA MIONGOZO YA UENDESHAJI WA MASHAURI Kwa kutumia mamlaka ambayo Jaji Mkuu amepewa kupitia Sheria zilizotungwa na Bunge, katika mwaka 2019 nimetoa Kanuni na Miongozo mbalimbali zenye lengo la kuharakisha na kurahisisha usikilizaji wa mashauri Mahakamani. Kwa mfano Marekebisho ya Kanuni za Mahakama ya Rufani (Tangazo la Serikali Namba 344 ya mwaka 2019) iliweka utaratibu wa kusajili rufani Mahakama ya Rufani  kwa   njia        ya             elektroniki. Marekebisho       ya       Kanuni za Uendeshaji wa Kesi za Madai (Tangazo la Serikali Namba 381 ya mwaka 2019) ilipunguza hatua ambazo kesi za madai hupitia. Kupitia Tangazo la Serikali Namba 158 ya mwaka 2019 Jaji Mkuu aliamuru     kuwa Mahakama      za             Mwanzo  nazo   ziwe         Mahakama zinazoweza kusikiliza kesi za watoto (Juvenile Courts). Na kupitia Tangazo la Serikali Namba 107 ya mwaka 2019, Jaji Mkuu alitunga Kanuni za Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kuwapa Wasajili wa Mahakama ya Biashara kusikiliza mashauri ya upatanishi (Mediation) kwa lengo lakuwapunguzia Majaji mzigo wa mashauri.

Aidha Mahakama ya Tanzania, Wadau katika Sekta ya Sheria walishirikiana na Ubalozi wa Uingereza na kuandaa Mwongozo wa Utoaji Adhabu (Sentencing Guidelines) ambao utawaongoza Mahakimu katika utoaji wa adhabu sahihi kwa mujibu  wa sheria za Tanzania. Muongozo huu utaondoa tofauti zilizokuwepo katika utoaji wa adhabu, utaimarisha misingi ya mamlaka ya utoaji adhabu na itapunguza ucheleweshaji wa mashauri Mahakamani kwani watuhumiwa wataelewa ukomo wa adhabu watakayopewa kulingana mazingira ya kosa. Mwongozo huu utazinduliwa hivi karibuni. Namshukuru sana Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mheshimiwa Sarah Cooke na wataalum wake Bi. Claire Harris, Bw. Andy Stephens na Lilian Mkama kwa kuwezesha kupatikana kwa Mwongozo wa Utoaji Adhabu. Kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru wadau, watumishi wa Mahakama ambao wamewezesha kupatikana kwa Mwongozo huu.

 

12.0 MIUNDOMBINU YA MAJENGO

Mheshimiwa Rais, mahakama inaendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo mapya ikiongozwa na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu wa mwaka 2016/17 – 2020/21. Lengo kuu ni kumuwezesha mwananchi kupata huduma kwa haraka kwa kumpunguzia umbali na gharama.

Mheshimiwa Rais, hivi karibuni Mahakama imeingia mikataba na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Mahakama Jumuishi (Integrated Justice Centres—IJCs) ambayo yatajengwa katika mikoa ya Dar es salaam (Kinondoni na Temeke), Mwanza (Ilemela), Dodoma, Morogoro na Arusha. Ndani kila jengo jumuishi kutakuwa na huduma za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Watoto. Majengo haya yatakuwa pia na ofisi za Wadau muhimu wa Mahakama (Waendesha Mashtaka, Ustawi wa Jamii na Mawakili wa Kujitegemea). Lengo la kuwa na Jengo jumuishi ni kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu katika jengo moja. Mbali na ujenzi huo, tunaendelea na maandalizi ya Ujenzi wa Mahakama (33) katika ngazi za Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo, ikiwemo Mahakama ya Wilaya ya Chamwino na Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa.

Mheshimiwa Rais, katika azma ya Makao Makuu ya Mahakama kuhamia Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma, taratibu zote za awali za maandalizi ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma yamekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni Serikali kutoa fedha ili ujenzi uanze.

13.0 BAJETI YA MWAKA 2019/20 NA MAHITAJI YA 2020/21 Mheshimiwa Rais, bajeti ya Mahakama kwa mwaka 2019/20 ni shilingi                  126,162,464,756.00      kati      ya       hizo,      shilingi 50,145,970,000.00    ni    mishahara    ya    watumishi,    shilingi 2,377,212,000.00 kwa ajili ya mishahara ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, na shilingi 51,481,382,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC). Kiasi cha shilingi 15,000,000,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo (fedha za ndani) na shilingi 7,157,900,756.00 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo (fedha za nje).

Mheshimiwa Rais, bajeti ya Matumizi Mengineyo (OC) iliongezeka kwa asilimia 1 ikilinganishwa na ile ya 2018/19, ongezeko ambalo ni kidogo sana ikilinganishwa na ongezeko la gharama za uendeshaji, na mahitaji ya msingi yaliyowasilishwa na Mahakama.

Mheshimiwa Rais, kama nilivyoeleza hapo awali, baadhi  ya maeneo yaliyokosa fedha mwaka 2019/20 yaliahirishwa kutekelezwa, lakini hata hivyo umuhimu wake ni mkubwa. Ili kukidhi mahitaji yake, Mahakama inaomba kuongezewa ukomo wa bajeti kwa mwaka 2020/21 katika maeneo yafuatayo: Programu Maalum ya Kupunguza Mlundikano wa Mashauri sh. 3,843,790,800.00; Posho za Wazee wa Baraza (Mahakama za Mwanzo) sh. 750,000,000.00; uanzishwaji wa Mahakama za Wilaya katika Wilaya 28 zisizokuwa na Mahakama hiyo— sh. 4,555,800,000,

 

14.0 MWISHO

Mheshimiwa Rais, yote niliyoyainisha hapo juu, hayajafikiwa hivi hivi tu bali ni kwa ushirikiano mkubwa wa watumishi wote wa Mahakama pamoja na wadau ikiwemo, Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Watendaji, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na wadau wengine wote. Kwa dhati ya moyo wangu nawashukuru wote na nawaombea kwa Mungu aendelee kuwapa nguvu ili tuendelee kwa pamoja kuhudumia wananchi.

Kadhalika, kipekee kabisa nakushukuru wewe Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano unaoutoa kwa Mhimili wa Mahakama. Ushirikiano ambao matunda yake yanaonekana na nimeyaelezea kwa kirefu siku ya leo. Nasema Shukran sana.

Mheshimiwa Rais, Mmoja wa Marais wa Marekani, Benjamin Franklin ambae ni mmoja wa waasisi wa Taifa hilo aliwahi kusema;

“Failing to Plan is to Plan to Fail”

Mahakama kwa kupitia Mpango Mkakati wake wenye malengo ya muda mfupi, kati na muda mrefu, itaendelea kutekeleza jukumu lake la Kikatiba la kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati na kuwezesha serikali kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya biashara na wawekezaji.

Mheshimiwa Rais, mwisho kabisa nikutakie kila kila kheri wewe Kama Kiongozi wa Nchi na pia Kiongozi wa Mhimili wa Serikali. Pia imtakie heri Kiongozi wa Mhimili wa Bunge, Mheshimiwa Spika.

Mungu Ibariki Tanzaia, Mungu Ibariki Mahakama ya Tanzania

 

“Nawashukuru Sana.”