TAARIFA KWA UMMA: HATUA NA TAHADHARI MBALIMBALI ZINAZOCHUKULIWA NA MAHAKAMA KATIKA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA KIMAHAKAMA WAKATI HUU WA TAHADHARI YA JANGA LA COVID - 19 (KORONA)

Attachment | Size |
---|---|
![]() | 239.96 KB |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAHAKAMA YA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA: HATUA NA TAHADHARI
MBALIMBALI ZINAZOCHUKULIWA NA MAHAKAMA
KATIKA UENDESHAJI WA
SHUGHULI ZA KIMAHAKAMA WAKATI HUU WA
TAHADHARI YA JANGA LA COVID - 19 (KORONA)
Wananchi na waandishi wa habari wote mnafahamu kuwa Jana tarehe 23 Machi, 2020 Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania akiwa katika vikao vya Mahakama ya Rufani vinavyoendelea katika Kanda ya Mahakama Kuu Mwanza alitoa taarifa kwa umma kupitia
vyombo vya habari akiwa Jijini Mwanza kuhusiana na UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA KIMAHAKAMA WAKATI HUU WA TAHADHARI YA JANGA LA COVID -19 (KORONA) na akaeleza kuwa Taarifa ya kina zaidi kuhusu nini hasa kinafanyika itatolewa na viongozi wa Mahakama waliopo Dar es Salaam siku ya leo.
Wote mnafahamu kuwa jukumu la Mahakama ya Tanzania chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ni kutoa haki kwa kutoa maamuzi katika mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria. Katika kufanya hivyo Mahakama hushirikiana na wadau mbalimbali kama polisi, Magereza Mawakili wa Serekali na wa kujitegemea, wadau wa mashauri ya jinai na madai.
Hivyo ni dhahiri Mahakama zetu zinakuwa na muingiliano na mkusanyiko mkubwa wa watu mbalimbali hivyo endapo maelekezo na tahadhari yaliyotolewa na Serikali ya Tanzania kupitia kwa Mhe. Rais, Mhe. Waziri Mkuu, Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na pia Mhe. Jaji Mkuu hayatazingatiwa ipasavyo shughuli zetu zinaweza kusababisha au kuchangia kwa kiasi kikubwa kusambaa kwa haraka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Hivyo basi, kama alivyoahidi Mhe. Jaji Mkuu naomba kuwajuza hatua na tahadhari ambazo Mahakama imeshazichukua hadi sasa na jinsi ilivyojipanga kuepukana na kuepusha kutokea kwa maambukizi ya virus vya Corona wakati wa uendeshaji wa shughuli za Mahakama pamoja na huduma zingine za utoaji haki hapa nchini.
Hatua hizo ni kama zifuatazo:
1. Kuongeza na kushawishi matumizi zaidi ya TEHAMA katika utoaji na upatikanaji wa huduma za kimahakama. Kama mnavyofahamu, kuanzia mwaka 2015 Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa kipindi cha miaka mitano (2015/2016 - 20/2021) pamoja mradi wa uboreshaji wa huduma za kimahakama, imekuwa ikitekeleza maboresho ya huduma za utoaji haki ambapo moja ya mikakati yake ni utoaji wa huduma kwa kutumia TEHAMA. Tayari hivi sasa mahakama ina mifumo mbalimbali ambayo inaruhusu utoaji wa huduma zinazohitajika bila ya wadaawa au mwananchi kufika Mahakamani. Kutaja kwa uchache ni pamoja na:
- Mfumo wa kielektroniki wa kusajili na kuratibu Mashauri (JSDS2) ambao umeunganishwa na mfumo wa malipo Serikalini (Government Electronic Payment Gateway);
- Mfumo wa kusimamia na kuwatambua Mawakili halali (TAMS)-tams.judiciary.go.tz;
- Mfumo wa usikilizaji wa mashauri kwa njia ya “Video Conferencing”.
- Mfumo wa kuhifadhi Maamuzi ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (TANZLII)-tanzlii.org
■ Mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa majengo, watumishi na mahitaji ya Mahakama (Court Mapping - JMAP) unapatikana kupitia jmap.judiciary.go.tz;
■ tovuti ya Mahakama, tanzaniajudiciary.blogspot.com na SMS notification) na barua pepe Mifumo hii ya Tehama ambayo ni matunda/matokeo ya utekelezaji wa maboresho yanayoendelea Mahakamani imetoa fursa zaidi za upatikanaji wa huduma za kimahakama katika kuharakisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama na kuzisogeza karibu na mwananchi. Hii ni pamoja na fursa za usajili wa mashauri kielektroniki, usikilizaji wa mashauri kupitia Mahakama mtandao (video conferencing), upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kimahakama kwa kupitia njia ya simu(SMS notification) na barua pepe pamoja na kupata taarifa na huduma mbali mbali kupitia tovuti ya Mahakama. Fursa hizi zinaruhusu mwananchi au mdaawa wa shauri kupata huduma hizi bila kumlazimu kufika katika Mahakama zetu hivyo kutoa fursa kwao kutumia muda huo katika shughuli za uzalishaji na utoaji huduma.
Hivyo kwa kutumia mifumo hii ya TEHAMA, Mahakama itaweza kukabiliana na janga la Korona kwa kuwa inatoa fursa ya usajili wa mashauri
kielektroniki, usikilizaji wa mashauri kupitia Mahakama mtandao (video conferencing).
Hadi hivi sasa Mahakama imeweka mifumo ya “Video Confrencing” kwenye:- Mahakama Kuu Masijala Kuu - DSM:- Mahakama Kuu Mbeya:- Mahakama Kuu Bukoba, Kituo cha Mafunzo Kisutu:- Chuo Cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto, Magereza ya Keko na Segerea.
Kupitia mifumo hii Mahakama ilishanza kusikiliza mashauri bila ya ulazima wa wadaawa kufika Mahakamani hata kabla ya kutokea kwa janga hili la COVID-19.
Hivyo basi, katika kipindi hiki cha kupambana na kukabiliana na maambukizi ya virusi vya COVID 19.
- Mahakama imeongeza kasi ya matumizi ya mifumo hii kwa kanda nyingine nje ya Dar es salaam ambapo kwa sasa mashauri yote ya jinai yanayoahirishwa kutokana na sababu mbalimbali kwa watuhumiwa au mahabusu waliopo katika gereza la Keko na Segerea bila ya kuwalazimiki kufikishwa Mahakamani, badala yake mashauri hayo yanaendelea kuahirishwa kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference) ili kuepuka msongamano na mkusanyiko wa mahabusu na wafungwa Mahakamani;
- Kwa Kanda ya Mbeya na Bukoba zenye vifaa vya Mahakama mtandao, utaratibu unakamilishwa kwa uwekaji wa vifaa hivyo katika Magereza yaliyopo katika Kanda hizo ili huduma kama inayotolewa katika kanda ya DSM pia iweze kutolewa katika kanda hizo hivi mara moja. Juhudi za kuweka vifaa hivyo kwa kanda zingine zilizosalia zinaendelea na baada ya muda mfupi huduma kama hizo zitatolewa;
- Utumiaji wa mfumo wa usajili wa mashauri kwa njia “E-FILING”. Mahakama inaimarisha na kuwasisitiza wadau wote (wananchi, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea) kusajili mashauri kwa njia hii ya mitandao (online case registration) ili kupunguza msongamano na mchanganyiko wa watu katika maeneo ya Mahakama;
- Mahakama itaongeza wigo wa matumizi ya TEHAMA kwa njia ya barua pepe na simu za mkononi kwa kutumia mfumo wa SMS notification na USSD katika usambazaji na upatikanaji wa taarifa za mashauri ambao hautawalazimu wadaawa kufika Mahakamani kupata taarifa hizo.
- Mahakama itaendelea mfululizo na programu ya elimu ya namna ya kusajili mashauri, kupata taarifa pamoja na kutoa msaada wa usajili wa mashauri kwa njia ya kielektroniki kwa kuanza na Mahakama zenye mashauri mengi ambazo zinaweza kusababisha mkusanyiko wa watu wengi.
- Kwa usimamizi wa Waheshimiwa Majaji Wafawidhi Mahakama kwa kufuata sheria na nyaraka na miongozo mbalimbali iliyopo kuhakikisha mashauri ambayo yanapaswa kusikilizwa ,Mahakama zitakuwa zikitoa ratiba za usikilizaji wa mashauri hayo kwa muda maalumu na ikibidi pia njia
itakayotumika wakati wa usikilizaji kwa kila shauri ili kutosababisha wadaawa kuwepo Mahakamani katika wakati mmoja. Hivyo wadaawa wa mashauri wanashauriwa kuwa makini na kuzingatia muda wanaopangiwa kufika
Mahakamani pamoja na kuhakikisha namba zao za mawasiliano ziko kwenye fomu ya kufungulia kesi au hati za kesi.
- Mawakili na maafisa wa mahakama wanaoandaa hati za ki-mahakama wahakikishe wanaweka majina yao kama yanavyotambulika kwenye ofisi zao pamoja na kuwa na sahihi za ki-electonic (electronic signatures) ili kurahisisha uthibitisho pale utakapohitajika.
- Kesi zote za mahakama za mwanzo zifunguliwe baada ya mlalamikaji kuwaandaa mashahidi wake na mahakama kujiridhisha kwamba mshtakiwa yupo na apewe fursa ya kuita wadhamini.
- Katika mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi kesi za jinai zifunguliwe kwa kuzingatia matakwa ya Tangazo la Serikali Na. 296 la 2012 linatoa mwongozo kwa kesi nyingi isipokuwa zile zinazohusisha makosa makubwa kufunguliwa baada ya kukamilishwa kwa upelelezi ili kuepusha kuongeza mlundikano usio wa lazima magerezani.
- Kuongeza matumizi ya huduma za Mahakama inayotembea (Mobile Court) kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza.
Kwa utekelezaji wa hatua hizi za awali na wakati Mahakama inaendelea kujipanga zaidi juu ya hatua zingine za uwezeshaji wa usikilizaji wa mashauri na upatikanaji wa huduma zingine za kimahakama, maelekezo kwa Wasajili, Mahakimu wafawidhi na Watendaji wa Mahakama ni:-
- Kwa kushirikiana na Watendaji wa Mahakama kuzuia watu wasio na ulazima kufika na kuingia kwenye kumbi za mahakama.
- Kuhakikisha mashauri yanasajiliwa kwa njia ya kielektroniki na yanahudumiwa mara tu yanapofika kwenye mfumo wetu na taarifa zimrudie mteja wetu ndani ya muda mfupi iwezekanavyo.
- Kwa kusaidiana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri na TEHAMA kuhakikisha Majaji na Mahakimu wote wana sahihi za kielektroniki (electronic signatures). Pia kuhakikisha kuna timu itakayotoa msaada na ushauri wa ki-ufundi kwa masaa yote ishirini na nne;
- Kuhakikisha mashauri yote yanayosajiliwa kwenye mfumo mara tu yanapopata sifa za kusajiliwa na kuwa na taarifa zote muhimu za waadawa ili kurahisha mawasiliano yote kwa njia ya TEHAMA.
- Kuhakikisha mfumo unahuishwa (updates) kwa wakati ili taarifa za tarehe za kesi ziwafikie wateja wetu bila kuwalazimisha kuja kuulizia tarehe za kesi zao mahakamani.
- Kuwataka wananchi kufuatilia maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Mahakama zetu na pia kutoa taarifa pale ambapo huduma hazitolewi ipasavyo.
MWISHO
Ni wito kwa watumishi wa Mahakama, wadaawa pamoja na wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuwezesha matumizi zaidi ya TEHAMA ili kuendeleza mapambano ya kujikinga na ugojwa wa Corona na kuwezesha haki inapatikana kwa wakati.
Ni Imani ya Mahakama kwamba kwa kutumia mifumo ya TEHAMA iliyopo Mahakamani mifumo hiyo itasaidia sana wananchi katika kupunguza maambukizi ya virus vya COVID 19 vilevile kuepusha gharama na usumbufu wa kusafiri kuja Mahamakani na kutumia muda huo katika shughuli zingine za uzalishaji wa uchumi na za kijamii.
Aidha, jitihada hizi zitawaepusha watumishi 5,841 wa Mahakama kubaki na afya njema ya kutoa huduma kwa watanzania katika kupata haki zao.
Nawashukuru sana, ahsanteni kwa kunisikiliza.
JAJIKIONGOZI
24.03.2020