Kanuni za Matumizi ya Miundombinu ya Reli kwa Watoa Huduma binafsi, za Mwaka 2024

Government Notice 214 of 2024

Kanuni za Matumizi ya Miundombinu ya Reli kwa Watoa Huduma binafsi, za Mwaka 2024
Ask AI
Ask questions and understand this document faster using AI.

Tanzania
Railways Act, 2002

Kanuni za Matumizi ya Miundombinu ya Reli kwa Watoa Huduma binafsi, za Mwaka 2024

Tangazo la Serikali 214 ya 2024

[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 95(2)(n)]

Sehemu ya kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Matumizi ya Miundombinu ya Reli kwa Watoa Huduma binafsi, za Mwaka 2024.

2. Matumizi

Kanuni hizi zitatumika kwa ajili ya kuweka utaratibu wa matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma binafsi.

3. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—"mkataba wa matumizi" maana yake ni mkataba wa matumizi kati ya Msimamizi wa Miundombinu na mtoa huduma na inajumuisha viambatisho na vielelezo husika;haki ya matumizi ya miundombinu” maana yake ni haki ya kutumia miundombinu ya reli ikiwemo mapito ya reli, kama ilivyoombwa na mtoa huduma;"ada ya matumizi ya miundombinu" maana yake ni ada inayoamuliwa kwa mujibu wa mkataba wa matumizi inayolipwa na mtoa huduma kwa Msimamizi wa Miundombinu kwa ajili ya haki ya matumizi ya miundombinu, na inajumuisha faida na tozo yoyote inayolipwa kuhusiana na ada hiyo;"Sheria" maana yake ni Sheria ya Reli;[Sura ya 170]"maombi maalumu" maana yake ni maombi ya kutumia njia ya treni kwa wakati maalumu tofauti na ratiba ya kawaida ya mchakato wa ugawaji wa njia ya reli;mpango wa utozaji” maana yake ni taratibu mahususi za utozaji zilizowekwa kwa mujibu wa Kanuni hizi, Mdhibiti wa Reli au Msimamizi wa Miundombinu kadiri itakavyokuwa;mfumo wa utozaji” maana yake ni mfumo ulioanzishwa na Msimamizi wa Miundombinu ili kubainisha ada ya matumizi ya miundombinu;Msimamizi wa Miundombinu” maana yake ni Shirika lililoanzishwa kwa mujibu wa Sheria;[Sura ya 170]leseni” maana yake ni leseni ya matumizi ya reli inayotolewa na Mdhibiti;Waziri” itakuwa na maana sawa na iliyoainishwa katika Sheria;[Sura ya 170]Maelezo ya mtandao wa reli” maana yake ni maelezo kuhusu masharti ya jumla, miongozo, taratibu na vigezo vya upangaji wa ada kwaajili ya matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma binafsi;matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma binafsi” itakuwa na maana sawa na iliyoainishwa katika Sheria"mtoa huduma" maana yake ni mtu ambaye amepewa leseni kutoa huduma za reli kupitia taratibu za matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma binafsi;kibali” maana yake ni kibali cha matumizi ya reli kinachotolewa na Msimamizi wa Miundombinu; na"Mdhibiti" itakuwa na maana sawa na iliyoainishwa katika Sheria.[Sura ya 170]

Sehemu ya pili – Maombi ya kibali na leseni

4. Maombi ya kibali

(1)Mtu anayekusudia kutoa huduma za usafiri wa reli kwa utaratibu wa matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma binafsi atapaswa kuomba kibali kwa Msimamizi wa Miundombinu kwa kutumia Fomu A iliyoainishwa kwenye Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi.
(2)Maombi chini ya kanuni ndogo ya (1) yataambatishwa na taarifa zifuatazo:
(a)hesabu ya fedha iliyokaguliwa ya hivi karibuni;
(b)uthibitisho wa wafanyakazi wenye taaluma ya uendeshaji wa reli;
(c)cheti cha tathmini ya athari za kimazingira;
(d)maombi yanayobainisha aina na kiwango cha uwezo unaohitajika katika mtandao wa reli;
(e)vigezo vya usanifu wa vitendea kazi vitakavyotumika katika uendeshaji;
(f)mpango wa biashara;
(g)mkataba wa bima;
(h)mfumo wa usimamizi wa usalama;
(i)mpango wa matengenezo na miongozo ya uendeshaji;
(j)nakala ya cheti cha usajili wa kampuni; na
(k)taratibu za uthibitishaji wa madereva wa treni na moduli za mafunzo;
(3)Msimamizi wa Miundombinu atatathmini maombi na kutoa kibali ndani ya siku tisini tangu kupokea maombi hayo.
(4)Msimamizi wa Miundombinu anaweza, baada ya kufanya tathmini, kukataa kutoa kibali kwa mwombaji na kumtaarifu mwombaji kwa maandishi sababu za kukataa.
(5)Mwombaji ambaye maombi yake yamekataliwa anaweza, ndani ya siku kumi na nne tangu kupokea taarifa ya kukataliwa, kurekebisha na kuwasilisha tena maombi.
(6)Mwombaji atakayeshindwa kuwasilisha maombi ndani ya muda ulioainishwa katika kanuni ndogo ya (5) atatakiwa kuwasilisha maombi upya.

5. Ada za kibali

Mwombaji wa kibali atalipa kwa Msimamizi wa Miundombinu ada ya maombi kama ilivyoainishwa katika Jedwali la Pili ambapo, ada hizo zinaweza kubadilishwa na Mdhibiti mara kwa mara kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii.

6. Maombi ya leseni

(1)Mtu anayetarajia kutoa huduma za usafiri wa reli atalazimika kuomba leseni kwa Mdhibiti kwa kutumia Fomu B iliyoainishwa kwenye Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi.
(2)Maombi ya leseni chini ya kanuni ndogo ya (1) yataambatishwa na taarifa zifuatazo:
(a)katiba ya kampuni ya mwombaji;
(b)ripoti inayojumuisha maelezo ya wigo wa huduma zinazotarajiwa kutolewa;
(c)mpango wa usalama;
(d)cheti cha tathmini ya athari za kimazingira;
(e)tozo zinazopendekezwa;
(f)muundo wa shirika unaojumuisha idadi ya wafanyakazi, uzoefu katika masuala ya reli na mchanganuo wa vitengo vya shirika;
(g)uwezo wa kifedha wa uendeshaji wa biashara ya reli;
(h)makubaliano na Msimamizi wa Miundombinu wa utoaji wa huduma za reli;
(i)mwongozo kwa dereva wa treni;
(j)taratibu za kawaida za uendeshaji kwenye vituo vikubwa na karakana;
(k)mwongozo wa matengenezo;
(l)masharti ya ubebaji;
(m)wajibu kwa abiria na makatazo;
(n)utaratibu wa urejeshaji wa fedha inapotokea ucheleweshaji na usitishaji wa safari;
(o)taratibu za ushughulikiaji malalamiko;
(p)utaratibu wa kuwahudumia walemavu na wasiojiweza kwenye treni;
(q)nakala iliyothibitishwa ya kibali kilichotolewa na Msimamizi wa Miundombinu; na
(r)uthibitisho wa malipo ya ada ya maombi ya leseni kwa Mdhibiti;
(3)Mdhibiti atatathmini maombi na kutoa leseni ndani ya ishirini na moja tangu kupokea maombi hayo.
(4)Mdhibiti anaweza, baada ya kufanya tathmini ya maombi, kukataa kutoa leseni kwa mwombaji na kumtaarifu mwombaji kwa maandishi sababu za kukataa.
(5)Mwombaji ambaye maombi yake yamekataliwa anaweza, ndani ya siku kumi na nne tangu kupokea taarifa ya kukataliwa, kurekebisha na kuwasilisha tena maombi.
(6)Mwombaji atakayeshindwa kuwasilisha maombi ndani ya muda ulioainishwa katika kanuni ndogo ya (5) atatakiwa kuwasilisha maombi upya.

7. Ada za leseni

Baada ya Maombi ya leseni kukubaliwa, mtoa huduma atapaswa kulipa ada za leseni kama zilivyoainishwa katika Jedwali la Pili la Kanuni hizi.

8. Muda wa leseni

(1)Leseni ya utendaji kazi wa reli itakuwa halali kwa muda wa miaka kumi na tano kuanzia tarehe ya kutolewa kwake, isipokuwa kama itafutwa au kusitishwa kwa mujibu wa Kanuni hizi.
(2)Leseni ya mtoa huduma inaweza kuhuisha leseni baada ya kukidhi matakwa yaliyoainishwa katika Kanuni hizi.

Sehemu ya tatu – Upatikanaji wa miundombinu na huduma za reli

9. Haki ya matumizi ya miundombinu

Mtoa huduma ana haki sawa ya kutumia miundombinu kwa ajili ya uendeshaji wa aina yoyote ya shughuli za reli.

10. Matumizi ya vituo na bandari

(1)Kwa madhumuni ya uendeshaji wa reli, mtoa huduma anastahili kutumia njia ya reli na kutoa huduma katika vituo na bandari zilizounganishwa na mtamndao wa reli zinazohudumia au kuweza kuhudumia mtumiaji zaidi ya mmoja.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atahakikisha kwamba stahili zinazotolewa kwa mujibu wa Kanuni hizi zinaheshimiwa, na kwamba utumiaji na utoaji wa huduma unafanyika kwa njia ya uwazi na isiyobagua.

11. Upatikanaji wa huduma

(1)Mtoa huduma ana haki ya kupata huduma zinazojumuisha—
(a)kiwango cha chini cha huduma ya miundombinu kama kilivyoainishwa katika Jedwali la Tatu; na
(b)ufikiaji wa vifaa vya huduma na usambazaji wa huduma kama ilivyoainishwa katika Jedwali la Tatu.
(2)Endapo Msimamizi wa Miundombinu ambaye ombi limepelekwa kwake kuhusu utoaji wa huduma iliyorejewa katika aya ya 2 ya Jedwali la Tatu hatoi huduma hiyo, Msimamizi wa Miundombinu atatumia juhudi zote zinazofaa kuwezesha upatikanaji wa huduma hiyo.
(3)Endapo Msimamizi wa Miundombinu atajitolea kutoa huduma za ziada kwa mujibu wa Kanuni hizi na kwa kujibu maombi kutoka kwa mwombaji, atatoa huduma hizo kulingana na upatikanaji wa huduma hiyo.
(4)Mwombaji anaweza kuomba kupatiwa huduma zilizoainishwa katika aya ya 2 ya Jedwali la Tatu au huduma za ziada kutoka kwa Msimamizi wa Miundombinu:Isipokuwa kwamba, Msimamizi wa Miundombinu hatalazimika kukubali maombi hayo.
(5)Bila kuathiri ujumla wa kanuni hii, mtoa huduma ambaye amekataliwa haki aliyopewa kwa mujibu wa kanuni hii, anaweza kukata rufaa kwa Mdhibiti.

Sehemu ya nne – Usimamizi na uendeshaji wa miundombinu

12. Uhuru wa usimamizi

Mtoa huduma atadumisha hadhi ya mwendeshaji huru katika usimamizi wa shughuli zake za kutoa huduma ya reli.

13. Mpango wa biashara

(1)Msimamizi wa Miundombinu atatengeneza mpango wa biashara ambao umeundwa kwa madhumuni ya kuhakikisha—
(a)matumizi bora na thabiti ya miundombinu, na inajumuisha uendelezaji wa miundombinu; na
(b)uwezo wa kifedha.
(2)Mpango wa biashara utajumuisha maelezo ya mipango ya uwekezaji na fedha, na kutoa njia ambazo malengo yaliyowekwa yatafikiwa.
(3)Mtoa huduma atatengeneza mpango wa biashara unaojumuisha uwekezaji na mipango yake ya ufadhili, na ambao umeundwa kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwepo kwa—
(a)uwezo wa kifedha; na
(b)malengo mengine ya kiufundi, biashara na usimamizi wa fedha.
(4)Mpango wa biashara utaainisha njia za kufikia malengo yaliyowekwa katika kanuni ndogo ya (3).
(5)Msimamizi wa Miundombinu na Mtoa huduma, kila mmoja atawasilisha mpango wa biashara na ripoti kwa Mdhibiti kwa kila mwaka ambayo itaainisha matakwa ya Kanuni hizi.

14. Maelezo ya mtandao wa miundombinu

(1)Ndani ya mwezi mmoja baada ya kuanza kutumika kwa Kanuni hizi, Msimamizi wa Miundombinu atashauriana na wahusika wote na kuandaa maelezo ya mtandao wa miundombinu.
(2)Maelezo ya mtandao wa miundombinu yatakuwa na taarifa zifuatazo:
(a)sehemu inayoeleza sifa ya miundombinu ya reli ambayo inapatikana kwa waombaji na masharti ya kuipata;
(b)maelezo ya taarifa zaidi ambayo yanaweza kupatikana kuhusu sifa ya njia, na utoaji wa huduma katika vituo, bandari na vifaa vya huduma kwa mujibu wa Kanuni hizi;
(c)ufafanuzi wa mifumo ya malipo na tozo, ikiwa ni pamoja na maelezo kuhusu methodolojia ya malipo;
(d)maelezo ya gharama za utoaji wa huduma;
(e)maelezo ya kanuni na vigezo vya ugawaji wa uwezo wa miundombinu, kuweka sifa za jumla za uwezo wa miundombinu inayopatikana na vikwazo vya matumizi yake, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya uwezo wa matengenezo; na
(f)utaratibu na tarehe za mwisho katika mchakato wa ugawaji wa uwezo na vigezo maalumu vilivyotumika katika mchakato huo ambao unajumuisha—
(i)taratibu ambazo waombaji wanaweza kuomba uwezo wa miundombinu kutoka kwa Msimamizi wa Miundombinu;
(ii)taarifa itakayotolewa na waombaji;
(iii)ratiba ya maombi na mchakato wa ugawaji;
(iv)utaratibu wa utatuzi wa migogoro ulioanzishwa na Msimamizi wa Miundombinu katika kutatua migogoro inayohusu ugawaji wa uwezo wa miundombinu ya reli;
(v)maelezo kuhusu sehemu ya miundombinu ya reli ambayo imetengwa kwa matumizi maalumu ya huduma za reli;
(vi)utaratibu unaopaswa kufuatwa kwa miundombinu yenye msongamano na vigezo vyovyote vya kipaumbele vya ugawaji wa miundombinu yenye msongamano vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni hizi;
(vii)matokeo ya mpango wowote wa kukuza uwezo uliokamilishwa kwa mujibu wa Kanuni hizi;
(viii)maelezo ya makatazo juu ya matumizi ya miundombinu;
(ix)kiwango cha kizingiti kitakachotumiwa na Msimamizi wa Miundombinu katika kuhitaji njia ya treni kuirudisha;
(x)masharti yanayohusu viwango vya awali vya matumizi ya uwezo yazingatiwe na Msimamizi wa Miundombinu katika kuamua vipaumbele; na
(xi)hatua zinazochukuliwa na Msimamizi wa Miundombinu ili kuhakikisha kuwa kunatendewa haki kwa waendeshaji mtandao na katika kujibu maombi maalumu ya uwezo wa miundombinu.
(3)Mtoa huduma atampa Msimamizi wa Miundombinu taarifa kama inavyohitajika ili kuwezesha msimamizi wa miundombinu—
(a)kujumuisha maelezo juu ya hali ya upatikanaji wa njia, usambazaji wa huduma, vituo na vifaa ambavyo vinaweza kupatikana; na
(b)sasisha maelezo ya mtandao na kuirekebisha inapohitajika.
(4)Ikiwa Msimamizi wa Miundombinu hajaridhika na taarifa iliyowasilishwa na mtoa huduma, atamtaka mtoa huduma kuwasilisha tena taarifa za kutosha.
(5)Msimamizi wa Miundombinu katika kila mwaka wa fedha atatayarisha taarifa ya mtandao si chini ya miezi minne kabla ya tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ya matumizi ya miundombinu kama ilivyofafanuliwa kwenye ratiba ya maombi na hatua za ugawaji.

Sehemu ya tano – Tozo za miundombinu

15. Kuanzisha, kupanga na kukusanya tozo

(1)Msimamizi wa Miundombinu atatakiwa—
(a)kupendekeza tozo zitakazotozwa kwa ajili ya matumizi ya miundombinu zitakazozingatia mfumo wa malipo, sheria na kanuni zilizoainishwa katika Jedwali la Nne; na
(b)kukusanya tozo hizo.
(2)Mdhibiti ataamua utaratibu wa kutoza na miongozo mahususi inayosimamia maamuzi ya utozaji wa tozo hizo.
(3)Mwombaji atalipa ada atakazotozwa na Msimamizi wa Miundombinu kwa matumizi ya miundombinu ya reli.
(4)Msimamizi wa Miundombinu atawasilisha taarifa kuhusu gharama za matumizi ya miundombinu kwa Mdhibiti pale itakapohitajika.
(5)Msimamizi wa miundombinu ataheshimu usiri wa kibiashara wa taarifa zinazotolewa kwake na waombaji kuhusu uwezo wa uendeshaji.

16. Mpango wa utendaji kazi

(1)Msimamizi wa Miundombinu ataanzisha mpango wa utendaji kazi kama sehemu ya mfumo wa utozaji ili kuwahimiza watoa huduma kutoa huduma endelevu na kumwezesha Msimamizi wa Miundombinu kupunguza usumbufu kwa lengo la kuboresha utendaji wa mtandao wa reli.
(2)Mpango wa utendaji unaweza kujumuisha—
(a)adhabu kwa vitendo vinavyovuruga uendeshaji wa mtandao wa reli;
(b)fidia kwa biashara ambayo inakabiliwa na usumbufu; na
(c)malipo ya ziada kwa utendaji kazi uliovuka malengo.
(3)Misingi ya mpango wa utendaji kazi itatumika kwa njia isiyo ya kibaguzi katika mtandao wote ambao mpango huo unahusika.

17. Tozo kwa miundombinu isiyotumika

Msimamizi wa Miundombinu anaweza kutoza tozo atakazoona zinafaa kwa uwezo ulioombwa na kutotumika, na atatoa motisha kwa matumizi bora ya uwezo.

Sehemu ya sita – Mgawanyo wa matumizi ya miundombinu ya reli

18. Maombi ya mgao wa miundombinu

(1)Mtoa huduma anaweza kuwasilisha kwa Msimamizi wa Miundombinu maombi ya mgao wa matumizi ya miundombinu.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atakuwa na wajibu wa kuweka kanuni mahususi za mgawanyo kwa madhumuni ya ugawaji wa miundombinu kulingana na uwezo.
(3)Msimamizi wa Miundombinu atashughulikia maombi ya mgao wa matumizi ya miundombinu ndani ya siku kumi na nne za kazi tangu maombi hayo kuwasilishwa.
(4)Msimamizi wa Miundombinu hatagawa matumizi ya miundombinu kwa njia mahususi za treni kwa kipindi chochote kinachozidi muda wa ratiba ya kazi.
(5)Mkataba au aina yoyote ya makubaliano yanayoweka haki na wajibu wa wahusika, yatatakiwa kuingiwa kati ya Msimamizi wa Miundombinu na mwombaji yeyote ambaye ameruhusiwa kutumia miundombinu ya reli kabla hajaanza kutumia miundombinu hiyo.
(6)Msimamizi wa Miundombinu atazingatia nafasi iliyowekwa na mtoa huduma katika kuhifadhi mgao wa matumizi ya miundombinu kwa madhumuni ya matengenezo ya njia yaliyopangwa.

19. Ratiba ya uendeshaji

(1)Msimamizi wa Miundombinu ataandaa ratiba ya uendeshaji mara moja kwa kila mwaka.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atashauriana na wahusika kuhusu rasimu ya ratiba ya uendeshaji na kutoa muda wa angalau mwezi mmoja kwa wahusika kuwasilisha maoni yao.
(3)Ratiba ya uendeshaji iliyorejewa chini ya kanuni ndogo ya (1) inaweza kupitiwa upya mara kwa mara kadiri itakavyohitajika au pale Msimamizi wa Miundombinu atakapoona inafaa.

20. Kutohamishika

(1)Mwombaji ambaye amepewa mgao wa matumizi ya miundombinu na Msimamizi wa Miundombinu hatabadilisha nafasi hiyo na mwombaji mwingine au kuihamisha kwa mtoa huduma mwingine, iwe nafasi hiyo ni ya—
(a)makubaliano yaliyofanywa kwa mujibu wa Kanuni hizi; au
(b)uwezo maalumu wa miundombinu katika mfumo wa njia ya treni.
(2)Mtu anayekiuka masharti ya kanuni ndogo ya (1) hataruhusiwa kuomba mgao wa matumizi ya miundombinu kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kosa kuthibitika.

21. Mgao usio na upendeleo

Msimamizi wa Miundombinu atahakikisha kwamba mgao wa matumizi ya miundombinu unatolewa kwa misingi ya haki na isiyo ya upendeleo, na mkataba unaoingiwa ni wa uwazi na kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni hizi.

22. Kupanga na kuratibu

(1)Msimamizi wa Miundombinu atashughulikia maombi yote ya mgao wa matumizi ya miundombinu na kuzingatia vikwazo vyote kwa waombaji, ikiwa ni pamoja na athari za kiuchumi kwenye biashara zao.
(2)Msimamizi wa Miundombinu anaweza kutoa kipaumbele kwa huduma mahususi ndani ya mchakato wa kuratibu kwa mujibu wa masharti ya Kanuni hizi.
(3)Endapo kuna mgongano kati ya maombi tofauti ya uwezo wa miundombinu, Msimamizi wa Miundombinu kwa kushauriana na waombaji husika, na kupitia uratibu wa maombi, atapendekeza mgao mbadala wa matumizi ya miundombinu kutoka katika ule ulioombwa ili kutatua mgogoro huo.
(4)Msimamizi wa Miundombinu atawezesha uanzishaji na uendeshaji wa mfumo wa ndani wa utatuzi wa migogoro ili kutatua migogoro ya mgao wa matumizi ya miundombinu.
(5)Msimamizi wa Miundombinu atachukua hatua zinazofaa ili kushughulikia masuala yote yanayohusu mchakato wa mgao wa matumizi ya miundombinu uliotolewa na wahusika wenye nia.
(6)Kwa madhumuni ya kanuni hii “wahusika wenye nia” ni pamoja na—
(a)waombaji wote wa mgao wa matumizi ya miundombinu kama sehemu ya mchakato maalumu wa ugawaji ambao rasimu ya ratiba ya uendeshaji inahusiana; na
(b)wadau ambao wameonesha kwa Mdhibiti nia yao ya kujadili rasimu ya ratiba ya uendeshaji.

23. Mkataba wa matumizi ya miundombinu

(1)Mwombaji ambaye ni sehemu ya makubaliano ya mkataba wa matumizi ya miundombinu anaweza kuomba kupatiwa mgao wa matumizi ya miundombinu kwa mujibu wa masharti ya makubaliano hayo.
(2)Mkataba wa matumizi ya miundombinu hautazuia matumizi ya miundombinu ya reli kwa watoa huduma wengine.
(3)Mkataba wa matumizi ya miundombinu utakuwa na masharti yanayoruhusu marekebisho au ukomo wa masharti yoyote yaliyomo katika makubaliano hayo ili kuwezesha matumizi bora ya miundombinu ya reli.
(4)Mkataba wa matumizi ya miundombinu utaainisha adhabu zitakazotumika katika kurekebisha au kusitisha makubaliano na upande wowote.
(5)Mkataba wa matumizi ya miundombinu kwa mujibu wa Kanuni hizi hautazidi muda wa miaka mitano na unaweza kuhuishwa.
(6)Bila kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (5), mkataba wa matumizi ya miundombinu unaweza kuwa wa muda wa zaidi ya miaka mitano katika mazingira ya kipekee hasa pale ambapo kuna uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu ambapo uwekezaji huo unafungamana na masharti ya kimkataba.

24. Maombi ya dharura

(1)Mtoa huduma anaweza kuwasilisha kwa Msimamizi wa Miundombinu, maombi ya dharura ya uwezo wa miundombinu katika mfumo wa njia za treni.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atajibu maombi hayo ndani ya siku tano za kazi kuanzia tarehe ya kupokea maombi hayo.
(3)Msimamizi wa Miundombinu atahakikisha kwamba taarifa juu ya mtandao wa reli wa akiba zinapatikana kwa watoa huduma wote.
(4)Msimamizi wa Miundombinu atahakikisha uwepo wa uwezo wa akiba utakaowekwa wakati wa ratiba ya mwisho ya kazi ili kumuwezesha kujibu haraka kwa kile kinachotarajiwa.

25. Tamko la miundombinu maalumu

Msimamizi wa Miundombinu anaweza kutenga sehemu fulani za miundombinu kwa ajili ya matumizi ya aina maalumu za huduma ya reli na, mara tu miundombinu itakapotengwa, anaweza kutoa kipaumbele kwa aina hiyo maalumu ya huduma ya reli katika mgao wa miundombinu.

26. Msongamano katika miundombinu

(1)Endapo itashindikana kukidhi maombi ya uwezo, baada ya kushauriana na waombaji, msimamizi wa Miuondombinu atatoa tamko kwanini maombi hayo hayawezi kutekelezwa.
(2)Katika utayarishaji wa ratiba ya kazi, Msimamizi wa Miundombinu akiona viashiria vya miundombinu kusongamana katika kipindi kinachohusiana na ratiba ya kazi, atatoa tamko juu ya viashiria hivyo.
(3)Wakati miundombinu imetangazwa kuwa na msongamano chini ya masharti ya kanuni hii Msimamizi wa Miundombinu atawajulisha—
(a)watumiaji waliopo;
(b)waombaji wapya; na
(c)Mdhibiti.
(4)Miundombinu inapotangazwa kuwa na msongamano, Msimamizi wa Miundombinu atafanya uchambuzi wa uwezo wa miundombinu yenye msongamano, isipokuwa kama mpango wa uimarishaji uwezo uko katika mchakato wa kutekelezwa.
(5)Ikiwa tamko la miundombinu iliyosongamana limetolewa, lakini tatizo la msongamano likatatuliwa kabla ya uchambuzi wa uwezo wa miundombinu kukamilika, Msimamizi wa Miundombinu anaweza kubatilisha tamko la msongamano lililotolewa chini ya kanuni hii na kuwajulisha watumiaji waliopo, waombaji wapya na Mdhibiti wa reli.

27. Uchambuzi wa uwezo wa miundombinu

(1)Pale ambapo kuna msongamano, Msimamizi wa Miundombinu atafanya uchambuzi wa uwezo wa miundombinu iliyosongamana ili kubaini sababu za msongamano huo na hatua za kuchukua ili kutatua msongamano huo.
(2)Katika kufanya uchambuzi wa uwezo wa miundombinu, Msimamizi wa Miundombinu atazingatia—
(a)sifa za miundombinu iliyosongamana;
(b)taratibu za uendeshaji zinazotumika kwenye miundombinu hiyo; na
(c)sifa za huduma mbalimbali za reli zilizopewa uwezo wa kufanya kazi kwenye miundombinu hiyo.
(3)Wakati wa kutatua msongamano, Msimamizi wa Miundombinu atazingatia—
(a)upangaji upya wa huduma;
(b)kupanga upya muda wa huduma;
(c)mabadiliko ya mwendokasi; na
(d)uboreshaji wa miundombinu.
(4)Msimamizi wa Miundombinu atakamilisha uchambuzi wa uwezo wa miundombinu ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe ambayo miundombinu imetangazwa kuwa na msongamano na kutoa matokeo ya uchambuzi huo kwa watoa huduma waliopo, waombaji wapya na Mdhibiti.

28. Mpango wa kuimarisha uwezo wa miundombinu

(1)Msimamizi wa Miundombinu, atatayarisha mpango wa kuimarisha uwezo wa miundombinu ndani ya mwezi mmoja baada ya kukamilisha uchambuzi.
(2)Katika kuandaa mpango wa kuimarisha uwezo wa miundombinu, Msimamizi wa Miundombinu atashauriana na wadau wakiwemo watoa huduma waliopo, waombaji wapya na Mdhibiti.
(3)Mpango wa kuimarisha uwezo wa miundombinju utajumuisha—
(a)uwezekano wa ukuaji wa usafirishaji kwa siku zijazo;
(b)vikwazo katika maendeleo ya miundombinu;
(c)chaguo na gharama za kuongeza uwezo wa miundombinu, pamoja na athari zinazoweza kujitokeza;
(d)maelezo ya hatua zitakazochukuliwa ili kuimarisha uwezo wa miundombinu yenye msongamano kwa kuzingatia uchambuzi wa faida na gharama; na
(e)ratiba ya kukamilisha hatua za kina zilizoainishwa kwa mujibu wa aya ya (d).
(4)Mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa uwezo wa miundombinu, Msimamizi wa Miundombinu atawapa wahusika alioshauriana nao chini ya kanuni ndogo ya (2), nakala ya mpango na ratiba ya kukamilisha hatua zilizoainishwa ili kutatua msongamano.

29. Matumizi ya njia za treni

(1)Pale ambapo miundombinu imetangazwa kuwa na msongamano, Msimamizi wa Miundombinu atamtaka mtoa huduma ambaye, kwa kipindi cha angalau mwezi mmoja, ametumia njia ya treni mara chache kuliko kiwango kilichoainishwa katika taarifa ya mtandao, kusalimisha njia hiyo ya treni.
(2)Masharti ya kanuni ndogo (1) hayatatumika endapo kwa mujibu wa Msimamizi wa Miundombinu itaonekana kuwa mtoa huduma ameshindwa kutumia njia ya reli kwa kiwango kilichoainishwa katika taarifa ya mtandao kutokana na sababu zisizo za kiuchumi ambazo ziko nje ya uwezo wa mtoa huduma.
(3)Msimamizi wa Miundombinu anaweza, katika taarifa ya mtandao kubainisha masharti ambayo viwango vya awali vya matumizi ya uwezo wa miundombinu vitazingatiwa ili kuonesha vipaumbele wakati wa kufanya maamuzi kuhusu ugawaji.

30. Hatua maalum za kuchukua wakati wa dharura

(1)Msimamizi wa Miundombinu atachukua hatua zinazohitajika ili kurejesha utendaji kazi wa kawaida wa mtandao wa reli baada ya kutokea hitilafu kwenye njia ya treni iliyosababishwa na tatizo la kiufundi au ajali.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atakuwa na mpango wa dharura wa kushughulikia usumbufu mkubwa wa usafiri wa treni, mpango huo utaonyesha wadau wakuu ambao wanatakiwa kufahamishwa kuhusu tukio hilo.
(3)Pale inapotokea dharura itakayosababisha kufungwa kwa muda sehemu ya miundombinu, Msimamizi wa Miundombinu anaweza, bila taarifa kusitisha njia za reli zilizotengwa kwa muda ili kukarabati miundombinu iliyoathirika.
(4)Msimamizi wa Miundombinu anaweza kuhitaji watoa huduma kutumia rasilimali ambazo zinafaa kurejesha utendaji kazi wa kawaida wa mtandao.
(5)Pale ambapo mkataba wa matumizi ya miundombinu kati ya mtoa huduma na Msimamizi wa Miundombinu unajumuisha masharti kuhusu hatua maalumu zinazopaswa kuchukuliwa endapo kutatokea usumbufu, rasilimali zinazohitajika na Msimamizi wa Miundombinu chini ya kanuni ndogo ya (4) zitazingatia masharti hayo.

Sehemu ya saba – Udhibiti na rufaa

31. Mamlaka ya udhibiti

(1)Upatikanaji na usimamizi wa miundombinu ya reli utakuwa chini ya uangalizi wa Mdhibiti.
(2)Msimamizi wa Miundombinu atahakikisha kwamba tozo za matumizi ya miundombinu ya reli zinazingatia matakwa ya kanuni hizi.
(3)Msimamizi wa Miundombinu atawasilisha kwa Mdhibiti taarifa ya mtandao reli kwa ajili ya kuidhinishwa, mpango wa ugawaji wa uwezo, utaratibu na mfumo wa tozo, muundo wa ada za miundombinu na ukokotoaji utakaofanywa ili kufikia mapendekezo ya ada na mipango mingine yoyote kuhusiana na haki ya upatikanaji iliyotolewa.

32. Uwasilishaji wa malalamiko kwa Mdhibiti

(1)Endapo mtoa huduma anaamini kuwa hajatendewa haki, kubaguliwa au kutokuridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na Msimamizi wa Miundombinu, anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Mdhibiti.
(2)Taratibu za kushughulikia malalamiko kama zilivyoainishwa na Mdhibiti zitatumiwa na watoa huduma pamoja na wahusika kuwasilisha malalamiko dhidi ya Msimamizi wa Miundombinu.
(3)Baada ya kupokea malalamiko Mdhibiti anaweza—
(a)kuthibitisha uamuzi wa msimamizi wa miundombinu; au
(b)kubadilisha maamuzi kwa kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Msimamizi wa Miundombinu.

33. Masuala ya ushindani

Mdhibiti atawajibika kukuza ushindani wa haki katika huduma za reli na kuzuia vitendo vinavyokiuka misingi ya ushindani katika soko la huduma za reli.

34. Uwezo wa kupata taarifa

Mdhibiti atakuwa na uwezo wa kupata taarifa zinazohusiana na majukumu na kazi zake kutoka kwa Msimamizi wa Miundombinu, watoa huduma na wadau wengine.

Sehemu ya nane – Masharti ya jumla

35. Masharti ya leseni

Kwa kuzingatia Kanuni hizi, mtoa huduma atahakikisha—
(a)hakuna mabadiliko ya shughuli au udhibiti bila ridhaa ya maandishi ya Mdhibiti;
(b)kuna matengenezo sahihi ya mfumo wa taarifa za usimamizi ili kufuatilia utendaji na maendeleo ya huduma za reli;
(c)taarifa zinazotolewa katika mfumo wa taarifa za usimamizi zinawasilishwa kila mwezi au kwa vipindi vingine vilivyoainishwa na Mdhibiti mara kwa mara;
(d)sehemu ya uhasibu katika mfumo wa taarifa za usimamizi haikinzani na sheria za Jamhuri ya Muungano; na
(e)ndani ya miezi sita ya kila mwaka wa fedha kuwasilisha kwa Mdhibiti taarifa ya utendaji kazi na hali ya kifedha kutoka kwa mkaguzi huru.

36. Uchunguzi na uchambuzi wa ajali

(1)Ajali inapotokea, uchunguzi na uchambuzi utafanywa na Msimamizi wa Miundombinu na mtoa huduma kwa pamoja.
(2)Ili kuzuia kutokea kwa ajali, Msimamizi wa Miundombinu na mtoa huduma wataridhia kwa pamoja maazimio ya ripoti ya ajali.
(3)Pale ambapo chanzo cha ajali hakijathibitishwa na wahusika au pale ambapo maafikiano hayajafikiwa kati ya mtoa huduma na Msimamizi wa Miundombinu kuhusu chanzo cha ajali, Mdhibiti atachunguza ajali hiyo na taarifa yake itakuwa ni maamuzi ya mwisho kuhusu chanzo cha ajali.

37. Uwajibikaji

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, aliyesababisha ajali atawajibika kulipa fidia ndani ya siku sitini kuanzia tarehe ya kukamilika kwa uchunguzi.

38. Shughuli za uokoaji

Katika tukio la ajali inayohusisha treni ya mtoa huduma, kazi za uokoaji ili kurejesha shughuli za uendeshaji zitafanywa na Msimamizi wa Miundombinu kwa mujibu wa mipango ya dharura na itakuwa katika gharama za ziada.

39. Kusitishwa na kufutwa kwa kibali

(1)Msimamizi wa Miundombinu anaweza kumuamuru mtoa huduma kurekebisha mapungufu ya kiutendaji na masharti yoyote ambayo yamekiukwa katika kibali.
(2)Msimamizi wa Miundombinu anaweza kusitisha kibali cha mtoa huduma kwa muda usiozidi miezi kumi na mbili kwa sababu zifuatazo iwapo mtoa huduma:
(a)ataacha kutoa huduma za reli kwa mujibu wa masharti ya kibali kwa muda wa wiki nne bila taarifa rasmi;
(b)hakidhi viwango vya uendeshaji vinavyohitajika au uwezo wa kufanya kazi;
(c)yupo katika hatua za kufunga biashara kutokana na kushindwa kulipa madeni ya kisheria na mengineyo; au
(d)amekiuka masharti ya leseni mara kwa mara.
(3)Baada ya kuisha kwa kipindi cha usitishwaji, mtoa huduma ataendelea kutoa huduma za reli kwa kuzingatia masharti yaliyotolewa na Msimamizi wa Miundombinu.
(4)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (3), iwapo mtoa huduma atashindwa kukidhi matakwa au masharti yaliyotolewa na Msimamizi wa Miundombinu baada ya kipindi cha usitishwaji kumalizika, Msimamizi wa Miundombinu anaweza kufuta kibali na kumpatia taarifa mtoa huduma na Mdhibiti.

40. Kusitishwa na kufutwa kwa leseni

(1)Mdhibiti anaweza kumuamuru mtoa huduma kurekebisha mapungufu ya kiutendaji na masharti yoyote ambayo yamekiukwa kuhusu leseni.
(2)Kwa kuzingatia kanuni ndogo ya (1), iwapo mtoa huduma atashindwa kurekebisha hitilafu au ukiukwaji wa masharti yoyote, Mdhibiti atasitisha au kufuta leseni baada ya kutoa notisi ya miezi miwili iwapo—
(a)mtoa huduma ameshindwa kuanza kutoa huduma za reli ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe iliyoainishwa leseni kuanza kutumika;
(b)mtoa huduma amebainika kutoa taarifa za uongo katika maombi yake ya leseni;
(c)mtoa huduma ameshindwa kutimiza amri yoyote inayomtaka kurekebisha masharti ya leseni;
(d)Msimamizi wa Miundombinu amefuta kibali cha mtoa huduma;
(e)kuna mabadiliko ya biashara au umiliki wa mtoa huduma bila kutoa notisi kwa Mdhibiti; au
(f)mtoa huduma amepewa ya kusitisha mkataba na Msimamizi wa Miundombinu.
(3)Baada ya kuisha kwa kipindi cha usitishwaji, mtoa huduma ataendelea kutoa huduma za reli kwa kuzingatia masharti yaliyotolewa na Mdhibiti.
(4)Endapo leseni itafutwa, mtoa huduma atatakiwa kuwasilisha maombi mapya baada ya muda wa miezi kumi na mbili kumalizika tangu tarehe ya kusitishwa kwa leseni.

41. Matumizi na uhifadhi wa kibali au leseni

(1)Mtu hataruhusiwa—
(a)kutumia leseni yoyote, cheti, kibali au idhini au hati nyingine iliyotolewa au inayohitajika chini ya Kanuni hizi ambayo imeghushiwa, kubadilishwa, kubatilishwa, kusimamishwa au ambayo mtu huyo hastahili;
(b)kughushi au kubadilisha leseni, kibali, idhini au hati nyingine yoyote iliyotolewa au kuhitajika chini ya Kanuni hizi;
(c)kuazimisha leseni, kibali, idhini au hati nyingine yoyote iliyotolewa au inayohitajika chini ya Kanuni hizi kwa mtu mwingine; au
(d)kulaghai kwa madhumuni ya kujipatia leseni, kibali, idhini au hati nyingine yoyote.
(2)Mtu hatatoa leseni yoyote, kibali au idhini au hati nyingine yoyote kwa madhumuni ya Kanuni hizi isipokuwa kama ameidhinishwa kufanya hivyo chini ya Kanuni hizi.

42. Taarifa ya ukiukwaji

(1)Mtu mwenye taarifa ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni au amri yoyote iliyotolewa chini yake, atamtaarifu Mdhibiti.
(2)Mdhibiti ataamua aina ya uchunguzi wa ziada au hatua zitakazochukuliwa.

43. Ukaguzi wa kibali au leseni

Mdhibiti au mtu mwingine yeyote aliyeidhinishwa na Mdhibiti anaweza kuamuru mtu mwenye leseni, kibali au idhini chini ya Kanuni hizi kuwasilisha kwa ajili ya ukaguzi.

Sehemu ya tisa – Makosa na adhabu

44. Makosa na adhabu

(1)Mtu anayekiuka masharti ya Kanuni hizi anatenda kosa na endapo atatiwa hatiani, atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tano na isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo kisichopungua miaka miwili jela na kisichozidi miaka mitano jela au vyote kwa pamoja.
(2)Ikiwa ukiukwaji wa sheria au kanuni utaendelea, kila siku ya uvunjaji huo itakuwa ni kosa tofauti na atatozwa faini ya ziada isiyopungua shilingi milioni tano kwa kila siku kosa lilipoendelea kutendeka.
(3)Iwapo itathibitika kwamba kitendo au kutotendwa kwa jambo fulani na mtu yeyote, jambo ambalo lingekuwa ni ukiukwaji wa masharti ya kanuni, amri au notisi iliyotolewa chini yake kulitokana na sababu yoyote isiyoepukika kutachukuliwa kuwa si ukiukwaji wa masharti hayo.

Jedwali la Kwanza (Linietengenezwa chini ya kanuni ya 4(1) na 6(1))

Fomu

[Ujumbe wa uhariri: Fomu hazijatolewa tena. Tafadhali rejelea hati ya uchapishaji.]

Jedwali la Pili (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 5 na 7)

Ada za maombi

A. Ada ya maombi ya kibali

[Zimetengenezwa chini ya kanuni ya 5]
Aina ya hudumaAda ya maombiAda ya kibali
HUDUMA YA ABIRIAUS$....(au sawa na TZS)US$....(au sawa na TZS)
HUDUMA YA MIZIGOUS$....(au sawa na TZS)US$....(au sawa na TZS)
HUDUMA ZA TRENI ZA MJINIUS$......(au sawa na TZS)US$....(au sawa na TZS)

B. Ada ya maombi ya leseni

[Zimetengenezwa chini ya kanuni ya 7]
Aina ya hudumaAda ya maombiAda ya leseni
HUDUMA YA ABIRIAUS $ 100 $ (au sawa na TZS)US $ 2000 $ (au sawa na TZS)
HUDUMA YA MIZIGOUS $ 100 $ (au sawa na TZS)US $ 4000 $ (au sawa na TZS)
HUDUMA ZA TRENI ZA MJINIUS $100$ (au sawa na TZS)US $ 1000 $ (au sawa na TZS)

Jedwali la Tatu (Limetengenezwa chini ya Kanuni ya 11(1))

Stahiki za mtoa huduma

[Zimetengenezwa chini ya kanuni ya 11(1)]
1.kiwango cha chini cha huduma ya miundombinu kinachorejewa katika kanuni ya 10(1) kitajumuisha haki ya kutumia miundombinu kama ilivyotolewa na hasa—
(a)haki ya kutumia sehemu za vigeuza njia na makutano kama inavyohitajika kutumia uwezo wa njia husika;
(b)udhibiti wa treni, ikijumuisha ishara na mawasiliano na utoaji wa taarifa juu ya mwenendo wa treni; na
(c)taarifa nyingine zote kama zitakavyohitajika katika kutekeleza au kuendesha huduma ambayo
uwezo umetolewa.
2.Uwezo wa kufika kwenye vituo vya huduma na usambazaji zilizorejewa katika kanuni ya 10(1) na (4) itajumuisha pamoja na—
(a)matumizi ya vifaa vya usambazaji wa umeme;
(b)vituo vya kujazia mafuta
(c)vituo vya abiria, ikiwa ni pamoja na majengo na vifaa vingine;
(d)vituo vya kusafirisha mizigo;
(e)eneo la kupanga treni;
(f)njia za mchepuko; na
(g)Sehemu za matengenezo na vifaa vingine vya kiufundi
3.Huduma za ziada zinazorejewa katika kanuni ya 10 (4) zitajumuisha—
(a)umeme;
(b)usambazaji wa mafuta, kupanga behewa na huduma zingine zote zinazotolewa katika vifaa vya huduma za ufikiaji zilizorejewa katika aya ya (2);
(c)mikataba midogomidogo kwa ajili ya—
i.udhibiti wa usafirishaji wa bidhaa hatari; na
ii.Usaidizi katika kuendesha treni zisizo za kawaida.
4.Huduma za ziada zinazorejewa katika kanuni ya 10(4) zinaweza kujumuisha:
(a)upatikanaji wa mtandao wa mawasiliano;
(b)utoaji wa taarifa za ziada; na
(c)ukaguzi wa kiufundi wa vitembea reli.

Jedwali la Nne (Limetengenezwa chini ya Kanuni ya 15(1)(a))

Tozo za miundombinu

[Zimetengenezwa chini ya kanuni ya 15(1)(a)]
1.Misingi ya malipo ya utoaji huduma
(1)Msimamizi wa miundombinu atahakikisha kwamba matumizi ya mpango wa tozo—
(i)yanazingatia taratibu zilizowekwa katika taarifa ya mtandao iliyoandaliwa kwa mujibu wa kanuni ya 13; na
(ii)ni sawa kwa shughuli tofauti za reli zinazotoa huduma sawa katika sehemu sawa ya soko.
(2)ukokotoaji wa ada utazingatia umbali, muundo wa treni na mahitaji yoyote maalum kulingana na mwendo kasi, ekseli na kiwango au muda wa matumizi ya miundombinu.
(3)isipokuwa pale ambapo mipango mahususi inafanywa, msimamizi wa miundombinu atahakikisha kwamba mlumo wa utozaji unaotumika unatokana na kanuni sawa katika mtandao wake wote.
(4)tozo ya mindombinu iliyoainishwa katika aya ndogo ya (1) na (2) ya aya ya 1 Jedwali hili zitazingatia ghrama za moja kwa moja zilizoingiwa katika uendeshaji wa treni.
(5)katika kupangilia mfumo wa tozo wa utoaji wa huduma zilizorejewa katika aya ya 5, msimamizi wa miundombinu atazingatia hali ya ushindani wa usafiri wa reli.
(6)ada ya kutumia miundombinu inaweza kujumuisha malipo ya msongamano wa sehemu itakayokuwa imetambulika.
(7)gharama zinazorejewa katika aya ndogo ya (4) zinaweza kukadiriwa kulingana na huduma za treni, muda na gharama za miundombinu inayohusika.
2.Utofauti katika misingi ya utozaji
(1)Ili kufidia gharama zilizotumika, Mdhibiti atamuidhinisha msimamizi wa miundombinu chini ya ukaguzi wa gharama za upatikanaji kufanya marejeo ya tozo, kulingana na ufanisi, uwazi na kutokubagua, huku akihakikisha ushindani bora wa usafirishaji wa kimataifa.
(2)Bila ya kujali masharti ya aya ndogo ya (1) msimamizi wa miundombinu atajumuisha matumizi ya miundombinu ya sehemu ya soko ambayo yanaweza kulipa angalau gharama ya moja kwa moja iliyopatikana kutokana na uendeshaji wa huduma ya reli, pamoja na kiwango cha mapato ambacho soko linaweza kubeba.
3.
(1)Kwa miradi mahususi ya uwekezaji iliyokamilishwa kufuatia kuanza kutumika kwa Kanuni hizi, msimamizi wa miundombinu anaweza kuweka gharama kwa msingi wa gharama za muda mrefii za mradi.
(2)Mpangilio wa utozaji katika aya ndogo ya (1) utajumuisha makubaliano ya kugawana hatari kwa uwekezaji mpya.
4.
(1)Gharama za wastani na za ziada za msimamizi wa miundombinu kwa matumizi sawa ya miundombinu yake lazima ziwe huduma zinazoweza kulinganishwa katika sehemu ya soko moja kwa kutegemea gharama sawa.
(2)Taarifa ya mtandao inayotolewa na msimamizi wa miundombinu itaonyesha kuwa mfumo wa utozaji unakidhi mahitaji katika aya ya (1) na kufanywa bila kufichua taarifa za siri za kibiashara za mtoa huduma.
5.Ikiwa msimamizi wa miundombinu anakusudia kurekebisha vipengele muhimu vya mfumo wa tozo uliorejewa katika aya ya 2 atafanya marekebisho hayo na kuyatangaza angalau miezi mitatu kabla.

History of this document

29 March 2024 this version
20 March 2024
Assented to
To the top