Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka, 2025

Government Notice 431 of 2025

Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka, 2025
This is the latest version of this Government Notice.
Ask AI
Ask questions and understand this document faster using AI.

Tanzania
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024

Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka, 2025

Tangazo la Serikali 431 ya 2025

  • Imechapishwa katika Subsidiary Legislation Supplement kwa 11 Julai 2025
  • Imeidhinishwa tarehe 10 Julai 2025
  • Ilianza tarehe 11 Julai 2025
  • [Hili ni toleo la hati hii katika 25 Oktoba 2025.]
  • [Note: This legislation was revised and consolidated as at 31 July 2002 and 30 November 2019 by the Attorney General's Office, in compliance with the Laws Revision Act No. 7 of 1994, the Revised Laws and Annual Revision Act (Chapter 356 (R.L.)), and the Interpretation of Laws and General Clauses Act No. 30 of 1972. All subsequent amendments have been researched and applied by Laws.Africa for TANZLII.]
  1. [Iliyorekebishwa na Kanuni za Marekebisho ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025 (Tangazo la Serikali 610 ya 2025) hadi 17 Oktoba 2025]
[Zimetengenezwa chini ya kifungu cha 146(1)][TS. Na. 431 la 2025; 610 la 2025]

Sehemu ya kwanza – Masharti ya utangulizi

1. Jina

Kanuni hizi zitajulikana kama Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025.

2. Tafsiri

Katika Kanuni hizi, isipokuwa kama muktadha utahitaji vinginevyo—mahakama” maana yake ni Mahakama Kuu ya Tanzania au Mahakama Kuu ya Zanzibar, kadri inavyowezakuwa;mtendaji wa uchaguzi” maana yake ni kama ilivyotafsiriwa na Sheria;msajili” maana yake ni msajili au mrajisi wa mahakama, kaimu msajili au kaimu mrajisi, naibu msajili au kaimu naibu msajili; naSheria” maana yake ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.[Sura ya 343]

Sehemu ya pili – Uwasilishaji wa shauri la uchaguzina dhamana ya gharama za shauri

3. Kupinga uchaguzi

Uchaguzi wa Mbunge utapingwa kwa njia ya shauri la uchaguzi.

4. Anayeweza kufungua shauri la uchaguzi

Shauri la uchaguzi linaweza kuwasilishwa na mtu yeyote aliyebainishwa chini ya kifungu cha 140(1) cha Sheria.

5. Muundo na maudhui ya hati ya shauri

(1)Kila hati ya shauri itakuwa na jina linaloshabihiana na Fomu A iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi na itaainisha:
(a)maelezo binafsi ya mlalamikaji ikiwemo jina, mahali anapoishi, anwani ya barua pepe, namba ya nukushi, namba ya simu na msimbo wa posta iwapo unapatikana;
(b)maelezo binafsi ya mlalamikiwa ikiwemo jina, mahali anapoishi, anwani ya barua pepe, namba ya nukushi, namba ya simu na msimbo wa posta, endapo vinafahamika;
(c)sababu za kuleta shauri; na
(d)nafuu zinazoombwa.
(2)Kila hati ya shauri itakuwa katika aya zenye namba zinazofuatana, na kila aya, kwa kadri inavyowezekana, itajikita katika maudhui tofauti.

6. Wahusika katika shauri

(1)Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa miongoni mwa walalamikiwa katika kila shauri, isipokuwa kwa shauri alilowasilisha mwenyewe.
(2)Endapo shauri lina madai yanayohusu mwenendo mbaya au ukiukwaji wa masharti yoyote ya Sheria au masharti ya sheria nyingine yoyote uliofanywa na mgombea aliyeshinda au na mtu yeyote anayemwakilisha au kwa niaba ya mgombea aliyeshinda, mgombea aliyeshinda ataunganishwa kama mhusika katika shauri pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
(3)Endapo shauri lina madai ya mwenendo mbaya au ukiukwaji wa masharti yoyote ya Sheria au sheria nyingine yoyote uliofanywa na mtendaji wa uchaguzi, mtendaji huyo wa uchaguzi ataunganishwa kama mhusika katika shauri pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
(4)Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza kuwaunganisha kama walalamikiwa watu wote ambao wanaweza kuathirika endapo nafuu anayoiomba katika shauri aliloliwasilisha itatolewa.

7. Kuongeza au kubadilisha wahusika katika shauri

Endapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mhusika pekee katika shauri na kwa madhumuni ya kuamua masuala husika mahakama inaona inafaa au ni muhimu mgombea aliyeshindwa au mtu mwingine yeyote aunganishwe kuwa mhusika katika shauri, mahakama inaweza kutoa amri ya kumuunganisha mgombea aliyeshindwa au mtu huyo mwingine kuwa mhusika katika shauri, na amri hiyo itakapotolewa, shauri litaahirishwa hadi wakati ambapo mtu ambaye anapaswa kuunganishwa katika shauri amepewa nakala ya hati ya shauri.

8. Kuwasilisha hati ya shauri

(1)Hati ya shauri itawasilishwa ndani ya siku thelathini tangu tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi kwa kuiwasilisha kwa msajili na kwa kulipa ada iliyoainishwa.
(2)Shauri litafunguliwa katika masjala ya mahakama iliyopo katika jimbo ambalo uchaguzi wake unakusudiwa kupingwa.
(3)Shauri linaweza kuwasilishwa na mlalamikaji au wakili wake.

9. Kukataliwa au kurekebishwa kwa hati ya shauri wakati wa uwasilishaji

(1)Endapo hati ya shauri haijaandaliwa kwa namna iliyoainishwa katika kanuni ya 8, inaweza kukataliwa na kurudishwa kwa mlalamikaji kwa madhumuni ya kurekebishwa ndani ya muda utakaopangwa na msajili.
(2)Endapo msajili atakataa hati ya shauri lolote, ataandika sababu za kufanya hivyo na kuandika tarehe ya kuwasilishwa na kukataliwa kwa hati hiyo.
(3)Mtu yeyote asiyeridhika na uamuzi wa msajili chini ya kanuni hii, anaweza kupeleka maombi ya masahihisho kwa Jaji kwa uamuzi wa upande mmoja utakaotolewa ndani ya siku nne za kuwasilishwa kwa maombi ya masahihisho na uamuzi wa Jaji utakuwa wa mwisho.
(4)Maombi chini ya kanuni hii yanaweza kuwasilishwa kwa maandishi ndani ya siku tano za uamuzi.
(5)Endapo uamuzi wa msajili utabadilishwa na Jaji, mlalamikaji anaweza kuwasilisha tena hati ya shauri lake na muda uliotumika tangu alipowasilisha shauri lililokataliwa hadi uamuzi wa Jaji katika maombi ya masahihisho ulipotolewa hautajumuishwa katika kuhesabu muda wa ukomo wa kufungua shauri chini ya kifungu cha 144(1) cha Sheria.
[T.S. Na. 610 la 2025 k.2]

10. Kupeleka hati ya shauri na kuwasilisha majibu

(1)Endapo hati ya shauri imewasilishwa na haijakataliwa au kurudishwa kwa mlalamikaji, msajili ndani ya siku tano:
(a)atatuma kwa mtendaji wa uchaguzi nakala ya hati ya shauri pamoja na notisi iliyoainishwa katika Fomu B iliyopo katika Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi;
(b)ataagiza kila mlalamikiwa kupelekewa nakala ya hati ya shauri pamoja na notisi iliyoainishwa katika Fomu C iliyopo katika Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi; na
(c)atabandika katika ubao wa matangazo wa mahakama nakala ya hati ya shauri iliyothibitishwa.
(2)Upelekaji wa nyaraka zilizotajwa katika kanuni ndogo hii utakuwa kwa njia ya makabidhiano binafsi.
(3)Endapo mahakama imeridhika kwamba—
(a)mlalamikiwa hawezi kupatikana;
(b)mlalamikiwa amekataa kupokea nyaraka;
(c)makabidhiano binafsi hayawezi kufanyika bila kucheleweshwa au bila gharama kubwa; au
(d)ni vyema kufanya hivyo, inaweza kuelekeza upelekaji wa nyaraka ufanyike kwa njia mbadala kwa namna ambayo mahakama inaweza kuelekeza.
(4)Mara baada ya kupokea nakala ya hati ya shauri, mjibu maombi atawasilisha mahakamani majibu yake ndani ya siku kumi na nne tangu tarehe ya kupokea hati hiyo, isipokuwa kama hana nia ya kupinga shauri.

11. Dhamana ya gharama za shauri

(1)Ndani ya siku kumi na nne baada ya kufungua shauri, mlalamikaji atapeleka maombi kwa ajili uamuzi wa kiwango kinachopaswa kulipwa kama dhamana ya gharama za shauri.
(2)Utaratibu wa kuweka dhamana ya gharama za shauri utakuwa kama ulivyoainishwa chini ya kifungu cha 140 cha Sheria.
(3)Endapo mlalamikaji ana uwezo wa kifedha na yuko tayari kuweka kiwango cha juu cha dhamana ya gharama za shauri kilichoainishwa chini ya kifungu cha 140(2) cha Sheria, hatahitajika kupeleka maombi kwa ajili ya uamuzi wa kiwango kinachopaswa kulipwa kama dhamana ya gharama za shauri, isipokuwa ataweka kiwango hicho ndani ya siku kumi na nne tangu kufungua shauri.
(4)Hakuna dhamana ya gharama za shauri itakayowekwa na mlalamikaji ambaye amepewa msaada wa kisheria chini ya Sheria ya Msaada wa Kisheria.[Sura ya 21]

Sehemu ya tatu – Orodha ya kura zinazopingwa na malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi katika kituo cha uchaguzi

12. Orodha ya kura zinazopingwa

(1)Endapo mlalamikaji au mlalamikiwa anaomba uchunguzi wa kura chini ya kifungu cha 45(1)(d) cha Sheria, atawasilisha kwa msajili orodha ya kura anazokusudia kuzipinga na pingamizi kwa kila kura ndani ya siku zisizopungua sita kabla ya siku iliyopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri, na hakuna ushahidi utakaotolewa wakati wa usikilizwaji wa shauri dhidi ya uhalali wa kura yoyote au kuunga mkono pingamizi lolote ambalo halijaainishwa kwenye orodha hiyo, isipokuwa kwa ruhusa ya mahakama na kwa masharti ambayo mahakama inaweza kutoa.
(2)Nakala ya orodha chini ya kanuni hii itatumwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi na kwa kila mhusika katika shauri.

13. Malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi katika kituo cha uchaguzi

(1)Endapo mlalamikaji anadai kuwa mgombea mwingine yeyote tofauti na mlalamikiwa alichaguliwa kihalali, atawasilisha kwa msajili orodha ya matokeo ya uchaguzi ya kituo cha kupigia kura anayokusudia kuitumia ndani ya siku zisizopungua sita kabla ya siku iliyopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri.
(2)Nakala ya orodha chini ya kanuni hii itatumwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi na kwa kila mhusika katika shauri.
(3)Mlalamikaji hatasikilizwa juu ya sababu yoyote ya malalamiko ambayo haijaainishwa katika orodha inayotakiwa kuwasilishwa chini ya kanuni hii, isipokuwa kwa ruhusa ya mahakama na kwa masharti ambayo mahakama inaweza kutoa.

14. Kupanga tarehe ya kusikiliza shauri

(1)Kwa kuzingatia Kanuni hizi, baada ya kukamilika kwa uwasilishwaji wa nyaraka za shauri, msajili atawapangia, mapema iwezekanavyo, wahusika wote au mawakili wao kufika mbele yake kwa madhumuni ya kupanga tarehe ya kusikilizwa kwa shauri.
(2)Endapo mhusika yeyote katika shauri atashindwa kufika mbele ya msajili baada ya kutakiwa kufanya hivyo, msajili ataendelea kupanga tarehe ya usikilizaji bila uwepo wa mhusika huyo na atamtaarifu mhusika huyo kwa maandishi tarehe ya usikilizaji iliyopangwa.
(3)Bila kujali masharti mengine yoyote ya Kanuni hizi, kufuatia maombi ya mhusika katika shauri, mahakama inaweza kuelekeza kwamba mwenendo wa shauri unaweza kuendeshwa kwa njia ya mtandao kwa kuzingatia masharti ya Kanuni za Uendeshaji wa Mashauri kwa Njia ya Mtandao na Kurekodi Mwenendo Kielektroniki za Mwaka 2021.[TS Na. 637 la 2021]
[TS Na. 610 la 2025 k. 3]

Sehemu ya nne – Utaratibu wa kusikiliza mashauri ya uchaguzi

15. Mahali na muda wa usikilizwaji wa shauri

(1)Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 139 cha Sheria, usikilizwaji wa shauri utafanyika katika muda na mahali kadri msajili anavyoweza kuamua.
(2)Msajili anaweza, na atapaswa kama ataelekezwa na mahakama kufanya hivyo, kutoa notisi ya siku, muda na mahali ambapo shauri litasikilizwa kwa kila mhusika katika shauri na kubandika notisi hiyo kwenye ubao wa matangazo wa mahakama au kutangaza katika magazeti kama anavyoweza kuona inafaa au kama mahakama inavyoweza kuelekeza.
(3)Kila shauri litasikilizwa katika mahakama ya wazi.

16. Kuunganisha mashauri

Endapo mashauri mawili au zaidi yamewasilishwa kuhusiana na uchaguzi mmoja, mahakama inaweza kuelekeza kwamba baadhi au mashauri hayo yote yaunganishwe na kusikilizwa kama shauri moja.

17. Shauri kusikilizwa na Jaji zaidi ya mmoja

(1)Jaji Mkuu anaweza kuelekeza kuwa shauri lolote lisikilizwe na Jaji zaidi ya mmoja endapo kwa maoni yake, ataona kuwa shauri hilo linaweza kuibua hoja ngumu za kisheria au zisizo za kisheria au zote kwa pamoja.
(2)Pale shauri linaposikilizwa na Jaji zaidi ya mmoja, litaamuliwa kulingana na maamuzi ya majaji walio wengi.

18. Utoaji wa nyaraka

Wahusika katika shauri au mawakili wao watawasilisha, kabla au wakati wa usikilizaji wa awali, nyaraka zote wanazokusudia kuzitoa kama ushahidi wakati wa usikilizaji wa shauri ambazo hazikuambatishwa kwenye hati ya shauri au kwa namna yoyote ile hazijawasilishwa mahakamani, na nyaraka ambazo mahakama imeamuru ziwasilishwe.[TS Na. 610 la 2025 k. 4]

19. Usikilizwaji wa awali

(1)Mara baada ya kukamilika kwa uwasilishwaji wa nyaraka za shauri, mahakama itafanya usikilizaji wa awali mbele ya wahusika au mawakili wao ili kuainisha masuala yasiyobishaniwa kati ya wahusika wa shauri na yatakayowezesha usikilizwaji wa shauri kwa haki na haraka.
(2)Mahakama itajiridhisha kutoka kwa wahusika na kupitia nyaraka za shauri, masuala ya kisheria au yasiyo ya kisheria yasiyobishaniwa.
(3)Mwishoni mwa usikilizaji wa awali chini ya kanuni hii, mahakama itaandaa hati ya masuala yasiyobishaniwa na hati hiyo itasomwa na kufafanuliwa kwa wahusika wa shauri au mawakili wao.
(4)Hati iliyoandaliwa chini ya kanuni hii itasainiwa na wahusika wa shauri au mawakili wao pamoja na Jaji.
(5)Suala lolote au nyaraka yoyote iliyokubaliwa na kuainishwa katika hati iliyoandaliwa chini ya kanuni hii, itachukuliwa kuwa imethibitishwa.
(6)Bila kujali masharti ya kanuni ndogo ya (5), endapo wakati wa usikilizwaji wa shauri mahakama ina maoni kwamba maslahi ya haki yanahitaji hivyo, mahakama inaweza kuelekeza kwamba suala lililokubaliwa au nyaraka iliyopokelewa katika hati iliyoandaliwa chini ya kanuni hii vithibitishwe rasmi.

20. Uainishaji wa hoja bishaniwa

Baada ya usikilizaji wa awali kukamilika, mahakama itaainisha masuala ambayo wahusika wa shauri wanabishania na kuandika hoja bishaniwa ambazo uamuzi sahihi wa shauri unaonekana kuzitegemea.

21. Usikilizwaji wa Shauri

(1)Usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi utakuwa kwa njia ya maelezo ya maandishi ya mashahidi badala ya ushahidi wa msingi wa kuhojiwa.
(2)Baada ya usikilizaji wa awali, na ndani ya saa zisizopungua arobaini na nane kabla ya muda uliopangwa na mahakama kusikiliza shauri la uchaguzi, mlalamikaji atawasilisha kwa msajili maelezo ya maandishi ya kila shahidi ambaye anakusudia kumuita wakati wa usikilizaji yakielezea msingi wa ushahidi wake.
(3)Ndani ya saa arobaini na nane za kufungwa kwa shauri la upande wa mlalamikaji, mlalamikiwa atawasilisha kwa msajili maelezo ya maandishi ya kila shahidi anayekusudia kumuita wakati wa utetezi, yakielezea msingi wa ushahidi wake.
(4)Maelezo ya maandishi ya shahidi chini ya kanuni hii—
(a)yatabainisha jina, umri, anwani na kazi ya shahidi;
(b)kwa kadri inavyowezekana, yatakuwa katika maneno ya shahidi aliyekusudiwa;
(c)yatatambua kikamilifu nyaraka yoyote inayorejewa katika maelezo bila kurudia yaliyomo isipokuwa kama ni muhimu ili kuitambua nyaraka husika;
(d)hayatajumuisha masuala ya kutaarifiwa au imani ambayo hayawezi kupokelewa kama ushahidi na endapo yanaweza kupokelewa, yataelezea chanzo cha taarifa au imani;
(e)hayatakuwa na nukuu ndefu kutoka kwenye nyaraka au kujikita katika hoja za kisheria au nyinginezo;
(f)yatajumuisha tamko la shahidi aliyekusudiwa kwamba anaamini kilichoelezwa katika maelezo hayo ni cha kweli;
(g)yatakuwa na tarehe, saini au kuthibitishwa vinginevyo na shahidi aliyekusudiwa;
(h)yatakuwa katika aya zilizo na namba; na
(i)yatakuwa katika lugha ya mahakama.
(5)Ikiwa shahidi haelewi lugha ya mahakama vizuri, lakini anaweza kujieleza na kueleweka na anaweza kuelewa lugha ya mahakama iliyo katika maandishi, maelezo yake yanaweza yasiwe katika maneno yake mwenyewe:Isipokuwa kwamba, suala hilo litapaswa kubainishwa katika maelezo husika na kuandikwa ili kuelezea kwa usahihi iwezekanavyo msingi wa ushahidi wake.
(6)Maelezo ya maandishi ya shahidi yatashabihiana na Fomu D iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi.
[TS Na. 610 la 2025 k. 5]

22. Utaratibu wa kusikiliza shauri

(1)Mhusika wa shauri ambaye kwa niaba yake maelezo ya maandishi ya shahidi yamewasilishwa atahakikisha kuwa shahidi wake anahudhuria wakati wa usikilizaji kwa madhumuni ya kutoa rasmi maelezo yake na kuwasilisha vielelezo, kama vipo.
(2)Shahidi aliyehudhuria kwa ajili ya utoaji rasmi wa maelezo yake na uwasilishaji wa vielelezo ataapishwa kwa namna iliyoainishwa na sheria inayotumika katika kuapisha mashahidi.
(3)Mara baada ya maelezo ya maandishi ya shahidi kutolewa rasmi mahakamani, yatakuwa sehemu ya kumbukumbu ya usikilizwaji wa shauri na yatasomwa kwa sauti kubwa na, au kwa niaba ya, shahidi.
(4)Shahidi ambaye maelezo yake yametolewa rasmi anaweza kuhojiwa na upande wa pili wa shauri na kuhojiwa tena na upande uliomuita kutoa ushahidi.
(5)Shahidi ambaye maelezo yake hayajatolewa chini ya kanuni ndogo ya (3) au (4) hataruhusiwa kutoa ushahidi bila idhini ya mahakama, na mahakama haitatoa idhini hiyo isipokuwa kama ameonesha sababu za msingi za kushindwa huko.
(6)Endapo itathibitika mbele ya mahakama kwamba shahidi ametoa maelezo ambayo ni ya uongo, shahidi huyo atawajibika kwa adhabu ya kutoa ushahidi wa uongo kwa mujibu wa Kanuni za Adhabu.[Sura ya 16]
[TS Na. 610 la 2025 k. 6]

23. Shahidi wa mahakama

(1)Wakati wa usikilizwaji wa shauri la uchaguzi, mahakama inaweza kutoa amri ya kumtaka mtu yeyote ambaye inaona kuwa amehusika katika uchaguzi unaohusiana na shauri kuhudhuria kama shahidi.
(2)Mahakama inaweza kumhoji shahidi yeyote aliyetakiwa kuhudhuria chini ya kanuni hii na baada ya kumhoji, shahidi huyo anaweza kuhojiwa na au kwa niaba ya mlalamikaji, mlalamikiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali au mwakilishi wake, ikiwa yupo, au yeyote kati yao.
(3)Mtu yeyote atakayekataa kutii amri ya mahakama chini ya kanuni hii atakuwa ametenda kosa la kuidharau mahakama chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu na Sheria ya Adhabu.[Sura ya 16 na Sheria Na. 6 ya 2018 ya Zanzibar]
(4)Masharti ya kanuni ya 21 na 22 ya Kanuni hizi hayatatumika kwa shahidi aliyeitwa na mahakama chini ya kanuni hii.
[TS Na. 610 la 2025 k. 7]

24. Matumizi ya Sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai Sura ya 33 na Sura ya 8 ya Zanzibar

Kwa kuzingatia masharti ya Sheria na Kanuni hizi, usikilizaji, utaratibu na mwenendo wa shauri utatumia, kwa kuzingatia maboresho muhimu kwa kadri yatakavyohitajika, kanuni zinazosimamia utaratibu na mwenendo wa mashauri ya madai kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai na Amri ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.

25. Sababu ambazo hazikuainishwa kwenye hati ya shauri

Mlalamikaji hataleta hoja au kusikilizwa kuhusiana na sababu yoyote ambayo haikuainishwa katika hati ya shauri, isipokuwa kwa ruhusa ya mahakama.

26. Kuahirishwa kwa usikilizwaji wa shauri

(1)Mahakama, kwa maamuzi yake yenyewe au kufuatia maombi ya mhusika katika shauri yaliyoungwa mkono na hati ya kiapo, na baada ya notisi kwa wahusika, inaweza kuahirisha kuanza kwa usikilizwaji wa shauri mpaka siku ambayo inaweza kuelekeza.
(2)Mahakama itatuma nakala ya notisi na amri ya kuahirisha iliyotolewa chini ya kanuni hii kwa kila mhusika katika shauri na kubandika nakala nyingine kwenye ubao wa matangazo wa mahakama.
(3)Endapo usikilizaji wa shauri hauwezi kuanza au endapo umeanza, hauwezi kuendelea kwa siku iliyopangwa kutokana na kutokuwepo kwa Jaji, usikilizwaji wa shauri hilo utaahirishwa hadi siku inayofuata, au tarehe yoyote inayofaa kwa mahakama hadi hapo Jaji atakapopatikana kusikiliza shauri hilo.
(4)Endapo kuanza kwa usikilizaji wa shauri kumeahirishwa chini ya masharti ya kanuni hii na hakuna uwezekano kuwa Jaji aliyepangiwa shauri hilo atapatikana ndani ya siku thelathini zijazo, Jaji mwingine atapangiwa kuendelea na usikilizaji huo.

27. Katazo la kuahirisha shauri

Usikilizwaji wa shauri unapoanza, utaendelea mfululizo, isipokuwa kama mahakama itaona kuwa kuahirishwa kwa usikilizwaji zaidi ya siku inayofuata ni muhimu kwa sababu zitakazoandikwa katika mwenendo wa shauri.

28. Jaji kushindwa kuendelea na shauri

(1)Endapo Jaji alieanza kusikiliza shauri atashindwa kuhitimisha shauri kwa sababu ya ugonjwa, kifo au sababu nyingine ya msingi, Jaji mwingine anaweza kupangiwa shauri hilo ndani ya siku kumi na nne na Jaji huyo aliyepokea shauri anaweza kushughulikia ushahidi wowote au hati iliyopokelewa kama vile ushahidi huo au hati hiyo imepokelewa au kuandaliwa na yeye mwenyewe na anaweza kuendelea na shauri hilo kuanzia hatua ambayo mtangulizi wake aliishia.
(2)Jaji aliyepokea shauri ataandika sababu za kupokea shauri hilo kabla ya kuendelea na usikilizaji.

29. Mlalamikaji kushindwa kuhudhuria

(1)Endapo mlalamikaji atashindwa kufika mbele ya mahakama siku ambayo shauri limepangwa kwa kwa ajili ya usikilizaji, mahakama inaweza kutupilia mbali shauri hilo.
(2)Endapo shauri limetupiliwa mbali chini ya kanuni hii, mahakama inaweza, baada ya maombi kuletwa ndani ya siku kumi na nne tangu kutupiliwa mbali, kulirejesha shauri ikiwa mlalamikaji atairidhisha mahakama kwamba kutofika kwake siku ya usikilizaji kulitokana na sababu ya msingi.

30. Mlalamikiwa kushindwa kuhudhuria

(1)Endapo mlalamikiwa atashindwa kufika mbele ya mahakama siku ambayo shauri limepangwa kwa ajili ya usikilizaji, mahakama inaweza kuendelea kusikiliza shauri hilo bila uwepo wake.
(2)Mlalamikiwa ambaye amri au uamuzi wa upande mmoja umetolewa dhidi yake atakuwa na haki ya kuomba kutenguliwa kwa amri au uamuzi huo ndani ya siku kumi na nne tangu amri au uamuzi huo ulipotolewa.

31. Kuhudhuria kupitia wakili

Kwa madhumuni ya Kanuni hizi, kuhudhuria kwa wakili kutachukuliwa kuwa ni kuhudhuria kwa mhusika wa shauri anayewakilishwa.

32. Kuondoa shauri

(1)Mlalamikaji anaweza, kwa notisi ya maandishi, kuondoa shauri wakati wowote baada ya shauri kufunguliwa na kabla ya uamuzi kutolewa, kwa kuzingatia masharti yanayohusiana na gharama za shauri ambazo mahakama inaweza kuona inafaa kutoa.
(2)Endapo mlalamikaji ataondoa shauri, hatakuwa na haki ya kufungua shauri jipya kuhusiana na uchaguzi huo isipokuwa wakati wa kuondolewa kwa shauri hilo, mahakama inaweza kutoa amri ya kumruhusu kufungua shauri jipya kuhusiana na uchaguzi huo kwa kuzingatia sheria ya ukomo wa muda na endapo itajiridhisha kuwa uondoaji wa shauri umesababishwa na kasoro yoyote ya kiutaratibu ambayo ingesababisha shauri hilo kushindwa.
(3)Endapo kuna walalamikaji wawili au zaidi, shauri hilo halitaondolewa isipokuwa kwa maombi ya maandishi ya walalamikaji wote.

33. Ukomo wa shauri

(1)Shauri litakoma baada ya—
(a)kifo cha mlalamikaji aliyekuwa mhusika pekee au mlalamikaji pekee aliyekuwa amebaki hai; au
(b)kifo cha mgombea aliyeshinda.
(2)Endapo shauri litakoma kwa sababu ya kifo cha mlalamikaji aliyekuwa mhusika pekee au mlalamikaji pekee aliyekuwa amebaki hai mahakama inaweza, ikiwa itaona ni sawa na haki kufanya hivyo, kumpa mlalamikiwa au, endapo kuna walalamikiwa wawili au zaidi, kila mlalamikiwa, gharama za shauri ambazo mahakama inaweza kuona inafaa:Isipokuwa kwamba, kiwango cha gharama za shauri atakazopewa mlalamikiwa chini ya kanuni hii hakitazidi kiwango cha gharama za shauri ambacho mlalamikaji aliweka kama dhamana kwa ajili ya mlalamikiwa huyo.

34. Shauri kutotupiliwa mbali kwa sababu ya kasoro ya kiutaratibu

(1)Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika Kanuni hizi, hakuna shauri litakalotupiliwa mbali kwa sababu tu ya kutozingatia masharti yoyote ya Kanuni hizi au kasoro nyingine yoyote ya kiutaratibu isipokuwa kama mahakama ina maoni kwamba kutozingatia huko au kasoro hiyo imesababisha au inaweza kusababisha upotoshaji wa haki.
(2)Endapo masharti yoyote ya Kanuni hizi hayajazingatiwa au kumekuwa na kasoro nyingine yoyote ya kiutaratibu, mahakama inaweza kumtaka mlalamikaji kurekebisha kutozingatia huko au kasoro hiyo kwa namna ambayo inaweza kuelekeza na kwa masharti ya kulipa au kutolipa gharama kadri itakavyoamua.
(3)Endapo mahakama imetoa amri ya marekebisho chini ya kanuni hii, na mlalamikaji anashindwa kuzingatia amri hiyo ndani ya muda ulioelekezwa, mahakama inaweza kufukuza shauri hilo.

35. Ada

(1)Ada za mahakama ni kama zilivyoainishwa katika Jedwali la Pili la Kanuni hizi.
(2)Mhusika wa shauri ambaye amepewa msaada wa kisheria chini ya Sheria ya Msaada wa Kisheria hatalipa ada.
[Sura ya 21 na Sheria Na. 13 ya 2018 ya Zanzibar]

36. Kufutwa kwa Kanuni

Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Kitaifa za Mwaka 2020 zinafutwa.[TS. Na. 782 la 2020, 934 la 2020, 610 la 2025 k. 8]

Jedwali la kwanza (Limetengenezwa chini ya kanuni ya 5, 10 na 21)

Fomu A

Fomu B

Fomu C

Fomu D

Jedwali la pili (Limetengenezwa chini ya kanuniya 35(1))

Ada

1.Kufungua shauriTZS. 200,000/=
2.Kuwasilisha hati ya shauri iliyorekebishwa au kurekebisha hati ya shauriTZS. 50,000/=
3.Kuwasilisha majibu ya hati ya shauriTZS. 100,000/=
4.Kuwasilisha majibu ya hati ya shauri yaliyorekebishwaTZS. 50,000/=
5.Kuwasilisha maombi kwa ajili ya kuamua dhamana ya gharama za shauriTZS. 50,000/=
6.Kuwasilisha kiapo kinzaniTZS. 20,000/=
7.Kuwasilisha orodha chini ya kanuni ya 12(1)TZS. 50,000/=
8.Kuwasilisha orodha ya mapingamizi chini ya kanuni ya 13(1)TZS. 50,000/=
9.Kwa suala lingine loloteAda sawa na inayopaswa kulipwa kwa suala kama hilo kwenye mashauri ya madai mahakamani.

History of this document

25 October 2025 this version
Consolidation
10 July 2025
Assented to
To the top