Collections
Ask AI
Ask questions and understand this document faster using AI.Kijarida Kuhusu
TARATIBU ZA KUSIMAMIA MALI ZA MTU MWENYE MATATIZO YA AFYA YA AKILI KWA MUJIBU WA SHERIA YA AFYA YA AKILI YA MWAKA 2008

Aprili, 2022
Kimeandaliwa na:
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Legal and Human Rights Centre [LHRC]
S. L. P. 75254, Dar es Salaam - Tanzania
Simu: +255 22 2773038/48; Nukushi: +255 22 2773037
Barua Pepe: lhrc@humanrights.or.tz
Tovuti: www.humanrights.or.tz
Ofisi ya Arusha
Barabara ya Olerian, Olosiva
Kitalu Na. 116/5, Sakina kwa Idd, Arumeru
S. L. P. 15243, Arusha - Tanzania
Simu: +255 27 2544187;
Barua Pepe: lhrcarusha@humanrights.or.tz
Kituo cha Msaada wa Sheria
Mtaa wa Isere - Kinondoni
S. L. P. 79633, Dar es Salaam - Tanzania
Simu/Nukushi: +255 22 2761205/6
Barua Pepe: legalaid@humanrights.or.tz
Ofisi ya Dodoma
Kitalu Na. 22 – Area D
S. L. P. 2289, Dodoma - Tanzania
Simu/Nukushi: +255 26 23500050
Barua Pepe: lhrc@humanrights.or.tz
SHUKRANI
Tunatoa shukrani za dhati kwa mwanasheria wetu Wakili Amani Erad Mkwama pamoja na wafanyakazi wote wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hususani ofisi ya Arusha kwa kukiandaa kijitabu hiki.
DIBAJI
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kina azma ya kusaidia jamii ya Watanzania kuwa na uwezo wa kufahamu sheria za nchi pamoja na kufahamu haki zao ili kuzilinda na kuzitetea pamoja na kuheshimu haki za wengine ili hatimaye tuwe na jamii yenye utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu pamoja na nchi inayoheshimu utawala wa sheria.
Tunafahamu kuwa kwa raia wa kawaida si rahisi kuzifahamu sheria zetu zote, na hata baadhi tu ya sheria zinazomgusa kutokana na mfumo tulio nao, ambao hautoi nafasi kwa watu wote kuzifahamu. Hali hii inasababisha watu wengi kujikuta katika migogoro dhidi ya sheria ambayo igeweza kuepukika kama mtu huyo angejua sheria husika. Ndiyo maana basi Kituo kimeamua kutoa chapisho hili na mengine kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa raia.
Huu ni usaidizi wa kisheria unaotoa maelezo mafupi na ya msingi ili kukusaidia ndugu msomaji uweze kupata ufahamu au maelezo ya sheria husika. Ni lengo letu kuwa, katika kijitabu hiki tunatoa usaidizi wa moja kwa moja kwako wewe pale utakapokuwa na tatizo au mmoja wa ndugu au jamaa zako wanapopata matatizo ya namna hii.
Tunachokuomba ni wewe kusoma kwa makini; na pale suala lako linapokwenda mbali zaidi ya maelezo haya, basi utafute msaada wa kisheria au uende kwa mwanasheria aliye karibu na wewe ili aweze kukusaidia zaidi.
Tunaamini utapata usaidizi huu kiurahisi zaidi na maelezo yaliyomo humu yatakusaidia kwa karibu. Umalizapo, tafadhali umsaidie na mwenzako kupata usaidizi huu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
UTAMBULISHO WA KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika binafsi la kujitolea na la hiari ambalo si la kisiasa wala kibiashara. Kituo kimeandikishwa na kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania mnamo mwezi Septemba, mwaka 1995. Kabla ya kusajiliwa kama chombo huru, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilikuwa ni mradi wa haki za binadamu wa Mfuko wa Kuendeleza Elimu ya Sheria Tanzania (TANLET). Makao makuu ya Kituo yapo Dar es Salaam. Pia Kituo kina ofisi nyingine Arusha na Dodoma na ofisi ya Msaada wa Sheria iliyopo Kinondoni, Dar es Salaaam
MAONO
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kina taamali jamii yenye haki na usawa.
TAMKO LA LENGO MAHUSUSI
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali wala kibiashara linalojibidisha kukuza uwezo wa jamii ili iweze kukuza, kuendeleza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania.
LENGO KUU
Lengo kuu la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni kukuza uelewa wa sheria na haki za binadamu kwa jamii kwa ujumla na hasa wale wanajamii ambao kwa sababu moja au nyingine wameachwa nyuma. Uelewa unakuzwa kwa njia ya elimu ya uraia na msaada wa kisheria
1. UTANGULIZI.
Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 ilitungwa kwa lengo la kuratibu namna ya kushughulika, kulinda na kuwahudumia watu wenye matatizo ya afya ya akili Tanzania bara.
Pamoja na mambo mengine, sheria ya afya ya akili imeainisha ni kwa namna gani mtu mwenye tatizo la afya ya akili atapokelewa na kupatiwa matibabu iwe kwa hiari au kwa shuruti kwenye vituo vya kutolea matibabu.
Imeanisha taratibu za kushughulika na mtu mwenye tatizo la afya ya akili, imeainisha uanzishwaji wa kamati, mamlaka yenye majukumu ya kushughulika na matatizo ya afya ya akili nchini. Pia imeainisha taratibu za kusimamia mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili.
Utimamu wa afya ya akili kwa tafsiri nyepesi ni hali ya mtu kuwa sawa kiakili na kisaikolojia au kutokuwepo kabisa kwa usumbufu wa akili ya mtu.
Ni hali ya kuwa na mawazo chanya, kuwa sawa kijamii na kisaikolojia na kuweza kuchangia katika utendaji wa mtu huyo wa kila siku na uwezo wa kuridhisha wa kimawazo au kitabia.
Uwezo wa mtu kuwa timamu kiakili huhusisha kuweza kutatua matatizo mbalimbali yanayomkabili yahusishayo msongo wa mawazo katika maisha, shuguli za uzalishaji na mchango wa mtu husika katika jamii.
Afya ya akili huhusisha ustawi wa akili, kujitambua kwa ufanisi, uhuru, umahiri, utegemezi wa ulimwengu na kujitambua kwa uwezo wa kiakili na kimhemko dhidi ya wengine.
Sababu za ugonjwa wa akili mara nyingi hazieleweki na kwa kawaida ugonjwa wa akili unaweza kuchangiwa na jinsi mtu anavyohemka, anavyotenda, anavyowaza na anavyohisi watu wengine, vitu na matukio mbalimbali.
2. MATIBABU KWA MTU MWENYE MATATIZO YA AFYA YA AKILI
Matibabu ya mtu mwenye matatizo ya afya ya akili ni matibabu yenye utaratibu wa kipekee kidogo hasa kwa kuzingatia aina ya tatizo lenyewe na madhara ya tatizo hilo kwa mgonjwa na jamii inayomzunguka kwa ujumla.
Matibabu kwa mtu mwenye matatizo ya afya ya akili yanategemea sana hali halisi ya mgonjwa na madhara anayoweza kupata au kuleta kwa jamii hasa kwa kuzingatia kuwa suala la utimamu wa akili ndio msingi wa maisha ya mtu kwa ujumla.
Matibabu kwa mtu mwenye matatizo ya afya ya akili yamegawanyika mara mbili kwa kuzingatia hali halisi ya mgonjwa kama inavyoainishwa hapa chini:
1. Matibabu kwa hiari: Matibabu haya hufanywa na mtu mwenyewe kwa hiari yake na mara nyingi huhusisha matatizo ya afya ya akili ambayo hayajaathiri utimamu wa akili kwa kiwango cha kushindwa kuratibu uwezo wa akili kufanya maamuzi sahihi.
2. Matibabu kwa shuruti: na haya hufanywa chini ya maagizo ya mahakama kwa kuzingatia hali halisi ya mgonjwa hasa pale matatizo ya akili yanapopelekea mgonjwa kuhatarisha maisha yake pamoja na maisha ya watu wengine.
3. TARATIBU ZA KURATIBU NA KUSIMAMIA MALI ZA MTU MWENYE MATATIZO YA AFYA YA AKILI
Mtu anapopatwa na matatizo ya afya ya akili kwa kiwango cha kushindwa kuratibu na kusimamia matumizi ya mali zake alizochuma kabla ya kupata matatizo hayo, sheria imetoa nafasi kwa mtu mwingine kufuata taratibu na kuweza kusimamia mali za mtu huyo.
Taratibu hizo ni kama ifuatavyo:
3.1 Mtu yoyote mwenye nia ya kutaka kusimamia mali za mtu aliyepata matatizo ya afya ya akili kwa kiwango kikubwa anapaswa kufanya maombi rasmi katika mahakama yenye mamlaka ya kupokea na kusikiliza maombi hayo.
3.2 Maombi ya usimamizi yanapaswa kuwasilishwa katika Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi yenye mamlaka katika eneo ambalo mtu mwenye matatizo ya afya ya akili alikuwa akiishi kabla ya kupata matatizo.
3.3 Maombi ya usimamizi wa mali yanaweza kufikishwa mahakamani na mzazi, mtoto ambaye ametimiza umri wa miaka 18, mtu wa karibu, ndugu au mtu yeyote mwenye mahusiano na ambaye amekuwa muangalizi wa karibu wa mgonjwa.
3.4 Pale ambapo maombi yatawasilishwa yakihusisha mtu ambaye amekwisha wasilishwa kwenye hospitali kwa ajili ya matibabu, maombi ni lazima yaambatanishwe na cheti chenye kuthibitisha uwepo wa mgonjwa katika hospitali husika akipatiwa matibabu.
3.5 Maombi ya usimamizi yatawasilishwa kwa fomu maalum yakiambatana na kiapo cha mpeleka maombi akiainisha sababu za maombi pamoja na taarifa kamili za mali husika anazoomba kuzisimamia.
3.6 Taarifa ya uwepo wa maombi hayo inapaswa kuwasilishwa kwa watu wote wa karibu na mgonjwa kwa ajili ya kuwafahamisha lakini pia kutoa nafasi endapo kuna yoyote mwenye pingamizi dhidi ya mleta maombi na mali zilizoainishwa.
3.7 Ili kuweza kujiridhisha juu hali ya utimamu wa mgonjwa wa afya ya akili, mahakama inaweza kuagiza mgonjwa wa afya ya akili kuwasilishwa kwenye eneo litakalofaa kwa ajili ya kujiridhisha juu ya utimamu wa afya yake ya akili kupitia mahakama au kupitia mtoa matibabu anayetambulika au mtu yeyote ambaye mahakama itaona anafaa kufanya uchunguzi huo.
3.8 Kwa kuzingatia uhitaji wa mgonjwa wa akili mahakama inaweza kuruhusu mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili ikauzwa na kitakachopatikana kuwasilishwa kwa mgonjwa kukidhi uhitaji wake.
4. UTHIBITISHO WA MATATIZO YA AFYA YA AKILI
Mahakama pindi itakaposikiliza maombi ya usimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili itazingatia vielelezo vitakavyoambatana na kiapo cha mfanya maombi ikiwa ni pamoja taarifa ya uchunguzi juu ya utimamu wa afya ya akili ya mtu ambaye maombi ya usimamizi wa mali zake yamewasilishwa.
Mahakama inaweza kupokea na kuzingatia pasipo ushahidi zaidi ya cheti cha matibabu au amri ya kupokelewa kwa mgonjwa katika kituo cha afya/hospitali.
Mahakama inaweza kufanya utafiti wake dhidi ya mali zinazotajwa kuwa ni za mgonjwa wa afya ya akili ili kujiridhisha zaidi juu ya uhalali wa maombi ya usimamizi wa mali hizo.
5. MAAGIZO YANAYOWEZA KUTOLEWA NA MAHAKAMA JUU YA USIMAMIZI WA MALI ZA MTU MWENYE MATATIZO YA AFYA YA AKILI
5.1 Baada ya kufanya utafiti na kujiridhisha juu ya mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili, Mahakama inaweza kuamuru uuzwaji wa mali inayohamishika isiyozidi kiasi cha shilingi za kitanzania Milioni Tatu.
5.2 Mahakama inaweza kutoa amri yoyote halali juu ya usimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji yake, familia yake inayomtegemea lakini pia ulipaji wa madeni yanayoweza kuwa yanamkabili.
5.3 Gharama zozote zitakazohusiana na uchunguzi wa mali za mtu mwenye matatizo ya akili, pamoja na maombi juu ya usimamizi wa mali zake zitalipwa na serikali au mtu aliyepeleka maombi ya usimamizi mahakamani.
5.4 Mahakama inapaswa kumchagua mtu sahihi kuwa msimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili ili kuhakikisha mali za mtu huyo zinakuwa chini ya uangalizi salama mpaka pale afya yake itakapotengamaa.
5.5 Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha mali pamoja na fedha za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili zinalindwa na inapaswa kujishughulisha kuhakikisha mtu anayepewa mamlaka ya usimamizi ni mtu sahihi kabisa.
5.6 Mahakama ina wajibu wa kuujulisha umma juu ya uteuzi wa msimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili na pale inapobidi inaweza kuruhusu mtu yeyote kuweka mapingamizi kwenye uteuzi huo.
6. WAJIBU WA MSIMAMIZI WA MALI ZA MTU MWENYE MATATIZO YA AFYA YA AKILI
6.1 Msimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili anapaswa kufuata maagizo ya mahakama na anapaswa kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia maagizo ya jumla au ya moja kwa moja atakayopewa na mahakama iliyomteua.
6.2 Msimamizi hapaswi pasipo kuwepo kwa ruhusa ya mahakama kuweka rehani, kuhamisha umiliki au kupangisha mali yoyote isiyohamishika kwa kipindi kinachozidi miaka mitano.
6.3 Msimamizi anapaswa kutekeleza maelekezo yote ya mahakama kuhusiana na mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili ikiwemo kutia saini makubaliano au nyaraka zozote kama atakavyoagizwa na mahakama.
6.4 Msimamizi anapaswa kuwasilisha mahakamani taarifa ya robo ya kipindi cha usimamizi juu ya mapato na matumizi yatokanayo na mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili.
7. HITIMISHO
Sheria ya afya ya akili imetengeneza utaratibu mzuri na mwepesi kama ilivyoainishwa na kijarida hiki juu ya namna ya uwasilishwaji wa maombi ya usimamizi wa mali za mtu mwenye matatizo ya afya ya akili na taratibu za kufuata ili kupatiwa uteuzi huo.