ZIARA YA JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. PRO. IBRAHIM HAMIS
JUMA KATIKA KANDA YA BUKOBA

TAREHE 30 - 31 AGOSTI, 2021

KIKAO CHA WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA BUKOBA

 1.     UTANGULIZI

Awali ya yote, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kukutana leo hii hapa Bukoba na kunipa fursa ya kukutana na kuongea na watumishi wa Mahakama Kanda ya Bukoba.

Pili, nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 1.     SHUKRANI

Naomba niwashukuru sana watumishi wa Kanda ya Bukoba chini ya uongozi Mhe. Jaji Dkt. Ntemi Kilekamajenga, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwa kunikaribisha mimi, pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Rufani-Jacobs Mwambegele, Rehema Kerefu na Penterine Kente. Tumeweza kukamilisha kikao cha Mahakama ya Rufani kwa ufanisi mkubwa.

Nawashukuru pia Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu-Angaza Mwipopo, Emmanuel Loitare Ngigwana na Ayub Yusuf Mwenda.

Nawashukuru sana watumishi wote ambao wamechangia sana kuhakikisha kuwa mimi, na pia Waheshimiwa Majaji wa Rufani, tunahudumiwa vizuri hapa Bukoba na pia katika Wilaya za Muleba, Biharamulo na Ngara nilizotembelea jana tarehe 30 Agosti 2021.

3. MADHUMUNI YAZIARA

Madhumini yalikuwa: Kikao cha Mahakama ya Rufani (Tarehe 09 hadi 26 Agosti, 2021); kukutana na viongozi wa Mahakama katika Kanda na kupokea Taarifa; Kukutana na nyinyi watumishi; Kukutana na Viongozi wa Mkoa na Wilaya; Kutembelea miradi ya Mahakama inayoendelea na kuona changamoto za ujenzi (kwa mfano changamoto ya miamba migumu ardhini, katika Mahakama ya Mwanzo Kabanga). Jambo muhimu hapa ni kuwa, nimewasikiliza na nimejifunza.

A-KIKAO CHA MAHAKAMA YA RUFANI:

Katika kikao cha Mahakama ya Rufani jumla ya mashauri 40 yalipangwa kusikilizwa. Hata hivyo kwa sababu ambazo hazikuwa za mahakama, ni mashauri 36 sawa na asilimia themanini na saba nukta tano (87. 5%) ya mashuri yote arobaini yaliyopangwa kusikilizwa ndio yalisikilizwa.

Nawashukuru watumishi wote pamoja na wadau wote waliowezesha kikao hiki kusikiliza asilimia 87. 5% ya mashauri yaliyopangwa ambayo ni kiasi kikubwa sana. Aidha, natoa wito kwenu watumishi na wadau wote kuendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa vikao vijavyo vinafikia malengo ya kusikiliza mashauri yaliyopangwa kwa asilimia 100% ama zaidi ili kuondoa milundikano na pia kutimiza dira ya Mahakama ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.

Naomba nichukue nafasi kuwakumbusha Waheshimiwa Mahakimu, Naibu Wasajili, na Majaji; tusome maamuzi ya Mahakama ya Rufani ili kupata tafsiri sahihi za maswala mbali mbali ya kisheria na kupunguza dosari/mapungufu ambayo Waheshimiwa Majaji wa

Rufani wameyataja katika maamuzi yao. Hata Majaji wa Rufani wana kawaida ya kujisomea ten ana tena maamuzi yao, na maamuzi ya majopo mengine ili kujifunza na pia kuhakikisha kuwa siku zijazo hawatoi maamuzi yanayokinzana. Maamuzi ya Majaji wa Rufani na pia za Majaji wa Mahakama Kuu zinahifadhiwa na kupatikana katika mfumo wa mtandao wa TANZLIL

Katika kikao cha Mahakama ya Rufani kilichokamilika wiki iliyopita hapa Bukoba, mimi, Majaji wa Rufani, Msajili wa Mahakama ya Rufani (Mhe. Kelvin Mhina) na Naibu Msajili Mahakama ya Rufani (Mhe. Flora Mtarania) wote tulijifunza mambo mengi sana kutokana na mashauri haya. Kwa kusoma rekodi nzima ya mienendo ya mashauri, tumejifunza changamoto zinazowakabili. Tumegundua maeneo ya Sheria na Kanuni ambayo yanahitaji kuboreshwa zaidi ili kuondokana adha ya kuondosha rufani kwa sababu za kiufundi. Rai yangu kwa Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na Waendesha Mashtaka-mnatakiwa kuwa na umakini mkubwa ili dosari za kiufundi zisizuie rufani au maombi kusikilizwa na Mahakama ya Rufani.

Aidha katika baadhi ya maamuzi yetu, tumetambua mzigo mzito ambao majaji na mahakimu wanaosikiliza mashauri hubeba ya kuandika kumbukumbu na mienendo ya mashauri. Jukumu hili duniani kote linabebwa na wataalamu waliosomea kazi hiyo waitwao-Court Reporters au Court Recorders. Hawa ndio wamesomea namna ya kuandika kila kitu kinachosemwa mahakamani, na kumuacha jaji au hakimu ajikite katika kusikiliza shauri. Hili ni changamoto ambalo linatafutiwa ufumbuzi wa kiteknolojia nafuu ili mzigo wanaoubeba majaji na mahakimu ubebwe

kitaalamu zaidi.

Kama nilivyodokeza awali, Majaji wa Rufani hujifunza mengi sana wanaposoma kumbukumbu za mienendo ya mashauri kuanzia zilipoanzia ngazi za chini kabisa hadi zinapofika ngazi ya mwisho ambayo ni Mahakama ya Rufani.

Kuna jalada moja ambalo lilipitia mkononi mwetu, ambalo ni mfano mzuri sana kuhusu umuhimu wa Mahakimu wanaosikiliza Committal Proceedings, kuondoa ucheleweshwaji mkubwa unaolalamikiwa katika ngazi hiyo kwa kuwadhibiti wapelelezi na waendesha mashtaka ambao bila udhibiti huchelewesha mashauri ya mauaji katika ngazi za Mahakama za Mahakimu. Eneo la COMMITTAL linahitaji kufuatiliwa kwa makini sana na Waheshimiwa Majaji Wafawidhi kwa ni eneo ambalo majalada hukwama pasipo sababu za msingi na kuchelewesha HAKL Jalada ninalolitumia kama mfano leo:

 • Ingawa Kosa la mauaji lilitendeka mwaka 2011, historia ya jalada ni kimya kuhusu kipindi cha miaka mitano.
 • Jalada halionyeshi historia ya hatua zilizochukuliwa baada ya tukio mwaka 2011 hadi tarehe 09/07/2015, siku ambayo Mwendesha Mashtaka (PP) aliifahamisha Mahakama ya Wilaya kuwa upelelezi haujakamilika. Hakuna mantiki, miaka minne baada ya tukio, Mwendesha Mashtaka anasema upelelezi bado, na hakimu hajamuuliza PP maswali ya kutaka kujua huo upelelezi unaoendelea ni kitu gani kinatafutwa katika huo upelelezi? Ni jukumu la Hakimu kuandika undani wa huo upelelezi unaoendelea badala ya kukubali maelezo ya juu juu kutoka kwa PP. Hakimu mnatakiwa mtoe ukomo wa

lini huo upelelezi uwe umekamilika, na ikibidi mpelelezi husika alete hati ya kiapo kuonyesha nini katika upelelezi bado anautafuta.

 • Hadithi ya "upelelezi haujakamilika" au "kumbukumbu bado zinapigwa chapa (committal proceedings still being typed)" au "jalada bado linapitiwa kama kuna washtakiwa wa kuongezwa" ilidumu kila baada ya wiki mbili, hadi uamuzi wa Mahakama ya Wilaya mwaka 2017.
 • Majaji Wafawidhi wasimamie mashauri yanayokwama wakati wa Committal.

B. MIUNDOMBINU YA MAHAKAMA

Katika ziara hii nimepata fursa ya kujionea mazingira mnayofanyia kazi. Namshukuru sana Jaji Mfawidhi kwa Taarifa ya Utendaji Kazi ambayo imenisaidia kufahamu hali halisi ya miundombinu za Mahakama. Nimekumbushwa kuhusu:

 • Wilaya za Kyerwa na Misenyi hawana Mahakama za Wilaya. Wilaya ya Kyerwa inahudumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Karagwe. Wilaya ya Misenyi inahudumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Bukoba.
 • Kwa taarifa iliyopo, Wilaya za Misenyi na Kyerwa hivi karibuni zitapata majengo ya Mahakama za Wilaya ambazo zipo miongoni mwa Wilaya 25 zitakazojengewa Mahakama za Wilaya kutokana na Mkopo wa Benki ya Dunia.

Taarifa ya Mhe. Jaji Mfawidhi imeonyesha jumla ya Mahakama za Mwanzo 12 ambazo hazifanyi kazi. Katika Wilaya za Bukoba/Misenyi

Mahakama za Mwanzo zisizofanya kazi:

 1.     Mahakama ya Mwanzo Kanyigo
 2.     Mahakama ya Mwanzo Ndwanilo

Katika Wilaya Biharamulo Mahakama za Mwanzo zisizofanya kazi:

 1.     Mahakama ya Mwanzo Nyakahura
 2.     Mahakama ya Mwanzo Kalenge

Katika Wilaya ya Muleba Mahakama za Mwanzo zisizofanya kazi:

 1.     Mahakama ya Mwanzo Kimwani
 2.     Mahakama ya Mwanzo Bumbile

Nilipomtembelea jana, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. TOBA AINASON NGWILA alitukumbusha maeneo yanayohudumiwa na mahakama za Mwanzo Kimwani na Bumbile ina idadi kubwa sana ya watu, ambao sasa wanalazimika kutafuta haki mbali sana na maeneo yao.

Katika Wilaya ya Ngara Mahakama za Mwanzo zisizofanya kazi:

 1.     Mahakama ya Mwanzo Mabawe
 2.     Mahakama ya Mwanzo Kirushya
 3.     Mahakama ya Mwanzo Bugarama
 4.     Mahakama ya Mwanzo Bukiriro
 5.     Mahakama ya Mwanzo Nyakisasa
 6.     Mahakama ya Mwanzo Muganza

Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu 2016/2017-2020/2021 ulioongoza mikakati ya ujenzi wa majengo mapya na ukarabati majengo machakavu ya Mahakama utakamilika

mwaka huu (2021) na tayari matayarisho wa MPANGO WA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU kwa miaka mitano ya pili (2021/2022-2026/2027) yameanza. Nawasihi viongozi wa Mahakama Kuu hakikisheni rasimu ya mapendekezo yenu huko Makao Makuu ya Mahakama yanawahusisha viongozi wa Kanda, Mikoa na Wilaya ambazo zitajengewa mahakama mpya au majengo ya Mahakama zao zimewekwa katika mpango wa ukarabati.

Aidha mnapaswa pia kuwashirikisha viongozi wa Serikali ngazi za Mkoa, Wilaya na Tarafa ili maoni na mapendekezo yao yasikilizwe kabla ya kuzindua MPANGO WA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU kwa miaka mitano ya pili (2021/2022-2026/2027). Mpango huu wa Miundombinu kwa miaka mitano ijayo isisahau kutoa majibu kwa Mahakama za Mwanzo ambazo hazifanyi kazi.

 1. 0 UPIMAJI WA WAZI NA UTENDAJI KAZI KUPITIA

OPRAS NA JOPRA

Sina budi kuendelea kutoa pongezi kubwa sana kwenu kwa kumaliza mashauri mengi zaidi ya yale yaliyofunguliwa katika mahakama zenu. Mnapomaliza mashauri Zaidi ya yale yaliyofunguliwa ni kwamba mnapunguza milundikano. Nawapongeza kwa kufikia hatua ya mashauri mengi kufunguliwa kwa njia ya mtandao, ambayo ni dalili kuwa safari ya kufikia Mahakama Mtandao imeanza. Ni dhahiri kuwa mafaniko haya yanatokana na jitihada za kila mmoja wenu katika kada zote.

Taarifa ya Mhe. Jaji Mfawidhi imegusia upimaji wa wazi wa utendaji kazi
kupitia OPRAS (kwa watumishi wanaofanya kazi zisizo za kiuhakimu) na
JOPRAS (kwa watumishi wanaofanya kazi za kiuhakimu). Utaratiobu wa
OPRAS na JOPRAS ni kuwa, fomu zinajazwa na kuwasilishwa kwa
7

mamlaka husika.

Nina uhakika kuwa upimaji wa OPRAS na JOPRAS umesaidia kupata matokeo yanayopimika; kwa mfano, kupima kuwa kwa mwaka, kila hakimu anatakiwa asikilize angalau mashauri 250 kwa mwaka; majaji mashauri 220 kwa mwaka.

4. 1 WANANCHI PIA WANATUPIMA KILASIKU

Naomba kuwakumbusha vipimo vya utendaji kupitia JOPRAS na OPRAS ni vyetu tunapimana sisi kwa sisi na ndani kwa ndani ya Mahakama. Tukumbuke, wananchi nao, wanapofuata huduma za utoaji haki kutoka kwetu; hali kadhalika wadau wa Mahakama, wanavyo vigezo vyao wanazotumia kutupima kila siku. Hawategemei vipimo vya JOPRAS au OPRAS kutupima. Kwa mfano wanapokuwa katika vibanda kusubiri zamu za kuitwa mahakamani, wanatujadili, kila mmoja wetu wanatusema-Tunapimwa kwa kiasi gani hakimu au jaji anachelewesha mashauri kwa sababu hawataki mashauri yachelewe.

Wanaposubiri kuitwa Mashakamani, huambizana, Hakimu au Jaji fulani, ni mbobezi wa kuahirisha, au kuchelewa, au anaongea kwa sauti ya chini sana na hasikiki na hasomeki! Wanatupima katika utoaji wa nakala za hukumu hapo hapo.

Wanafahamu ni nani akisoma hukumu atakuzungusha kupata nakala kwa wiki au miezi. Wananchi wanataka mienendo ya mashauri yao ichapwe haraka na wapate nakala ili wakate rufani. Wanafahamu makarani wasiochapa kwa haraka, wanafahamu nani huwazungusha. Wengi wanatushangaa kwa nini hatujibu barua zao.

Wananchi hawataki mienendo ya mashauri yenye makosa ambayo wakati mwingine husababisha rufaa zao kuondolewa mahakamani. Wanapenda wanapokuja Mahakamani na shida, wasikilizwe na waelimishwe.

Sisi tutajipima na JOPRAS, OPRAS tutapandishana vyeo lakini wananchi wanajua nani angestahili kupandishwa cheo, nani angestahili asifanye kazi Mahakamani.

 1. 2 HUDUMA MPYA YA MREJESHO WA UBORA WA HUDUMA ZITOLEWAZO NA MAHAKAMA

Sote tunafahamu umuhimu wa wananchi, wadau na wanaotumia huduma za mahakama, kuwa na imani na Mahakama. Ni jukumu la kila mtumishi wa Mahakama ifikapo jioni baada ya kazi kujiuliza je nimewaridhisha niliowahudumia kazini siku ya leo?

Mwaka 2015, Mahakama ya Tanzania iliona umuhimu wa kujua wananchi na wanaofuata huduma za haki kutoka kwetu wanasemaje kuhusu hizo huduma. Je huduma zetu ni kwa kwa faida kujiridhisha sisi au kwa faida ya kuwaridhisha wananchi wanaofuata hizo huduma. Mahakama ya Tanzania iliamua kuwatumia taasisi isiyo ya kiserikali ya REPOA inayojihusisha kutafiti umaskini. Tuliwaomba watutafiti kwa kukusanya taarifa zetu za awali (baseline survey) kuhusu kiwango ambacho watumiaji wa huduma za Mahakama wanaridhishwa na huduma zinazotolewa katika ngazi zote za Mahakama na kufahamu maeneo ambayo yangehitaji maboresho ili kuongeza kiwango cha kuridhishwa na huduma.

Ripoti ya kitafiti ya REPOA (COURT USER SURVEY) ya mwaka 2015 iligusa maeneo ambayo yalisaidia sana Mahakama katika kutekeleza Mpango Mkakakati wa Miaka Mitano (2015/2016-2020/2021) na Programu ya Maboresho. Utekelezaji wa mikakati uliimarishwa na maoni yaliyokusanywa na REPOA kutoka kwa wananchi na wadau. REPOA ilitafiti maeneo yafuatayo ya uridhikaji na huduma zetu:

 1.   kuridhika na huduma zinazotolewa na mahakama.
 2.   kiwango cha upatikanaji na urahisi wa kupata taarifa muhimu kuhusu shauri lililo mahakamani.
 3.   Je huduma zinalenga kumridhisha mtumiaji wa huduma au zinalenga kumridhisha anayetoa huduma.
 4.   Kiwango cha weledi anauonyesha afisa wa mahakama anayetoa huduma.
 5.   Wepesi wa kupata nyaraka muhimu za kimahakama, kwa mfano hukumu, amri za kukaza hukumu, mienendo, barua kupata majibu, malalamiko kushughulikiwa haraka.
 6.   Je, tovuti ya Mahakama ina msaada wowote kwa watumiaji?
 7.   Urahisi wa kutekeleza amri za Mahakama, kwa kukaza hukumu na amri za Mahakama.

Ili kujitathmini katika miaka mitano ya maboresho, Mwaka 2019, Mahakama ya Tanzania illiomba tena REPOA ifanye tafiti wa mafanikio ya utekelezaji wa yale wadau na watumiaji huduma waliyoyaibua mwaka 2015 (COURT USERS' SATISFACTION FOLLOW-UP SURVEY 2019). Itoshe kuwakumbusha kuwa upimaji wa wazi wa Utendaji Kazi OPRAS/JOPRAS ni wetu sisi Mahakama, cha muhimu zaidi ni kwa kiwango ambacho wananchi na watumiaji wa huduma zetu wanavyoridhika ndio hujenga Imani endelevu juu ya Mahakama. Mhe. Jaji Mfawidhi, siku zote tafuta mbinu mbali mbali za kujua wanafuata

huduma zetu, na wadau wetu, wanakumbana na changamoto za aina gani. Ubora wa huduma ni muhimu kuliko hata majengo yaliyo bora, maana unaweza kuwa na jingo la kisasa kabisa lakini huduma yenye usumbufu mkubwa.

 1. 0 SAFARI KUELEKEA MAHAKAMA MTANDAO

Wote mnafahamu kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Mahakama ya Tanzania imefanya uwekezaji na maboresho makubwa katika mifumo ya TEHAMA, na matumizi ya TEHAMA. Lengo la maboresho ni kubadili tabia na mienendo yetu katika utoaji haki na uendeshaji wa mashauri. Uwekezaji mkubwa hautakuwa endelevu endapo tabia zetu na mitizamo yetu ya utoaji huduma itabaki ile ya kizamani. Ni matumaini yangu maeneo yafuatayo ambayo Mahakama ya Tanzania imewekeza matumizi ya TEHAMA, imebadilisha mitazamo yetu, tabia zetu na imetujengea ufanisi binafsi, kutufanya kuwa na uwazi na imetuongezea uwajibikaji:

 1.           Je JSDS2 imetubadili? Je tunaitumia JSDS2 kikamilifu? -Huu ni mfumo unaotuwezesha kusajili mashauri kwa masaa 24; kuwapangia waheshimiwa mahakimu na majaji mashauri ya kusikiliza; kufuatilia mmenendo wa mashauri; kutoa taarifa kwa njia ya sms; kutoa bili za malipo; kufanya malipo; kuonyesha taarifa fupi za mashauri na takwimu kwa kupitia case dashboard. JSDS2 itaunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
 2.           Je tunajaza taarifa muhimu na kuitumia JMAP kutusaidia kufanya maamuzi? -Mfumo huu huonyesha taarifa mbalimbali za kila ngazi ya mahakama, kwa mfano hali ya majengo, umbali, sehemu ilipo n. k. ili kuwezesha kufanya maamuzi mbali mbali bila kulazimika kwendakatika Mahakama husika.
 1.   Je TAMS imetusaidia? -Mfumo wa kusajili Mawakili wa kujitegemea, kuhifadhi taarifa zote za mawakili hawa, elimu zao, na uhai wa leseni zao za kutoa huduma za uwakili.
 2.   E-LIBRARY-Je tunajisomea na kujiongeza kupitia Maktaba Mtandao? Maktaba Mtandao 'ni mfumo uliotengenezwa kutusaidia kuhifadhi nyaraka mbali mbali ikiwemo maamuzi, sheria, kanuni, vitabu mtandao na Makala. Aidha, mfumo huu umerunganishwa na maktaba mtandao mbali mbali duniani. Je unatusaidia kuboresha kazi zetu? Au imebaki ni pambio tu?
 3.   TANZLII-Kanzidata ya maamuzi/hukumu za Mahakama KUU na RUFANI. Mahakama ya Tanzania imejizolea sifa nyingi duniani kutokana TANZLIL Wanasheria wengi duniani wamesifu msaada wa TANZLII. Je sisi wenye TANZLII tunapandisha hukumu zetu? Je tunautumia huu mfumo ambao umepunguza makali ya kutafuta maamuzi ya zamani?
 4.   Je tunapata taarifa mbali mbali kutoka TOVUTI ya Mahakama-mfumo huu unawaezesha watumishi wa Mahakama na wananchi kwa ujumla kupata taarifa na nyaraka muhimu za mahakama. Moja ya Malengo muhimu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni Tanzania kuwa taifa la watu walioelimika vyema na wanaojifunza. Zama za leo Mahakama ina mambo mengi ambayo watumishi wanatakiwa wao wenyewe wajifunze. TOVUTI ya Mahakama imesheheni mambo mengi ya kujifunza. Kwa mfano leo hii, TOVUTI ilionyesha kusheheni maandiko yenye kutoa mafunzo-Mahakama inayotembea (Mobile Court); Taratibu za Rufaa na Mapitio Mahakama za Wilaya; Taratibu za Ufunguzi wa Mashauri kwa Njia ya Elektroniki; Utaratibu wa Mapitio, Masahihisho na Marejeo Katika Mahakama ya Rufani; Haki Bulletin; N. K. Katika karne hii ya TEHAMA hakuna hata siku moja utaletewa

mezani taarifa kwa mfano: Tangazo la Serikali Namba637 la tarehe 27/08/2021 kuhusu Kanuni Mpya za uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao [Remote Proceedings and Eiectronic Recording Rules, GN 637 of 2021] au Mamlaka ya Mahakama ya Mwanzo Temeke itakayosimamia mashauri yay a ndoa, mirathi [Tangazo la Serikali Namba 639 ya tarehe 27/08/2021]—Watumishi wa Mahakama katika Mapinduzi ya Nne ya viwanda, wanajisomea na kuiongeza wao wenyewe.

 1.          VIDEO CONFERENCE—Mfumo wa kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusisha vikao kwa njia ya video bila wahusika kukutana. Teknolojia hii imetumika kusikiliza mashauri na mafunzo mbali mbali.
 2.          AUDIO VISUAL RECORDING—mfumo wa kuchukua Ushahidi kwa sauti na video. Mfumo huu unahifadhi Ushahidi na mwenendo wa shauri kwa njia ya sauti na video, hivyo kusaidia kufanya rejea wakati wa kuandika hukumu.
 3.          JUDICIARY MOBILE TZ-Kumuwezesha mwananchi kutoa mrejesho wa ubora wa huduma za mahakama kupitia simu janja (SMART PHONE).

Ombi langu, tutumie uwekezaji huo kikamilifu kwa sababu ni maandalizi ya MAHAKAMA MTANDAO. Nawapongea wote kwa kuendelea kuunga mkono safari ya Mahakama ya Tanzania kuelekea kuwa mahakama isiyotumia karatasi (paperless courf).

Taarifa ya Mhe. Jaji Mfawidhi inaonesha kuwa katika kanda hii kuanzia Januari, 2021 mashauri yapatayo 2,167 yalifunguliwa na kati ya hayo mashauri 2, 052 yalifunguliwa kwa njia ya mtandao. Aidha ni mashauri 775 tu hayakufunguliwa kwa njia ya mtandao kwa kanda nzima. Ni

jambo la kujipongeza kuwa tunatumia vizuri uwekezaji wetu katika TEHAMA.

TEHAMA ni muhimu kwa kuwa inaiwezesha Mahakama kuboresha ufanisi, inasaidia kujenga uwajibikaji na kuweka uwazi katika kazi za ngazi za utoaji haki. TEHAMA inaiweezesha Mahakama kuweka mazingira rafiki kwa wanaotafuta huduma za utoaji haki. TEHAMA inabadili tafsiri ya "huduma za kimahakama" kutegemea kusafiri hadi katika jengo. Kwa mfano, unaweza kufungua shauri ukiwa huko ulipo bila kusafiri hadi katika jengo la Mahakama.

5. 1 SAFARI KUFIKIA MAHAKAMA MTANDAO INATEGEMEA USHIRIKI WA WADAU

Leo nitaongelea wadau wa Mahakama ambao tutawategemea sana kufanikisha safari ya Mahakama Mtandao. Nianze na wadau ambao husambaza nishati ya umeme kwa kusisitiza umuhimu wa Mahakama zetu za Mwanzo ziunganishwe katika miundombinu ya Nishati ya umeme ili zijiunge na safari ya Mahakama Mtandao.

Taarifa ya Mhe. Jaji Mfawidhi imeonyesha maeneo ya ujenzi wa Mahakama ambayo imepata Hati za Viwanja vya Mahakama. Nakuomba Jaji Mfawidhi, hakikisha Mtendaji anafuatilia mipango ya mdau anayesambaza nishati ya umeme vijijini [WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)], ili afikishe nguzo zenye umeme katika Mahakama za Mwanzo ambazo zimepata hati. Mahakama hizi za Mwanzo ni-Kalenge (Biharamulo), Nyakahula (Biharamulo), Katoro (Bukoba) na Nyakibimbili (Bukoba). Nishati ya umeme ni muhimu sana katika kufanikisha Mahakama Mtandao tunakoelekea.

Safari ya kufikia Mahakama Mtandao inategemea sana uwekezaji ambao unafanywa na MHIMILI WA SERIKALI kupitia Wizara ya Mawsiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ndiye msimamizi wa barabara itakayotumiwa na Mahakama ya Tanzania kufikia Mahakama Mtandao. Viongozi wa Mahakama katika ngazi zote, fuatilieni sera, mikakati na mipango yote inayotolewa na Wizara ya Mawsiliano na Teknolojia ya Habari kwa sababu inagusa safari yetu ya Mahakama Mtandao ifikapo 2025.

Alipowasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha Kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, Waziri Mawsiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile (Mb) alitaja mambo ambayo ni muhimu sana kwa safari ya Mahakama Mtandao. Hivyo basi ni lazima viongozi wa Mahakama tufuatilie kwa ukaribu. Nitatoa mifano michache: -

 • Sisi Mahakama, ni wadau wakubwa sana wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano au National ICT Back Bone (NICTBB)Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya sio tu zimeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia Shirika La Mawasiliano Tanzania (TTCL) bali pia zinatumia. Mafanikio au changamoto yoyote itakayogusa Mkongo wa Mawasiliano itatugusa sisi Mahakama.
 • Maandalizi ya kuanzisha chombo huru cha kusimamia, kuendesha na kuendeleza Mkongo wa Taifa yanaendelea, hatua inayofuata ni kupata vibali kutoka mamlaka husika. Mahakama ni mtumiaji mkubwa wa huduma kutoka Mkongo wa Mawasiliano, hivyo tutafuatilia hiki chombo huru, na

tuhakikisha kuwa chombo hiki kiwe wezeshi kwa Mahakama Mtandao.

 • Waziri Dkt Ndugulile aliieleza Bunge kuwa, "Maandalizi ya mradi wa Tanzania ya Kidijitali yamekamilika na unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22. Mradi huu unalenga kuleta mabadiliko ya kidijitali kwa kuwezesha maunganisho ya kijiditali ya kikanda na kimataifa na hatimaye kukuza Uchumi. " Tanzania inapoelekea kuwa ya Kidijitali Mahakama haiwezi kuruhusiwa kubaki nyuma. Mahakama inausubiri kwa hamu mradi huu kwa sababu tayari Mahakama imetayarisha Andiko la hatua katika safari ya kufikia MAHAKAMA MTANDAO ifikapo 2025. Mradi huo wa Wizara kuhusu TANZANIA YA KIDIJITALI itasaidia SAFARI YA MAHAKAMA MTANDAO.
 • Waziri Ndungulile alielezea pia kuhusu-Mkakati wa Taifa wa Mtandao wenye Kasi (National Broadband Strategy 2021-2026) umeandaliwa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha uwepo wa intaneti yenye kasi kubwa, ubora wenye viwango vya juu na gharama nafuu za huduma za mitandao, maudhui, programu za kompyuta, usalama wa mitandao na watumiaji. Hii ni Habari njema sana kwa Mahakama. Mkakati utaondoa malalamiko yaliyopo ya kasi ndogo ya Internet hasa wakati wa kusikiliza mashauri kwa njia ya VIDEO CONFERENCE. Mahakama itapenda kutumia mfumo wa INTERNET wenye kasi. Kwa hiyo mkikumbana na kasi ndogo ya Internet, msikate tamaa na kuacha matumizi ya TEHAMA Mahakamani kwa sababu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatafuta ufumbuzi wa kudumu.

• Mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ambao uko chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inayosimamiwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile. Waziri alilijulisha Bunge kuwa, "Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ni Mradi unaotoa taarifa sahihi ya anapopatikana mwananchi na utambuiisho wa matumizi ya eneo husika. Taarifa hizo zinarahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma za Serikali na kijamii mahali alipo mwananchi sambamba na kuwezesha biashara mtandao (e-Commerce). " Huu mradi ni muhimu sana kwa Mahakama. Kesi zinapofunguliwa Mahakama husajili majina ya washtakiwa, wadaawa na baadaye hata Mashahidi. Anuani za makazi za watu hawa ni muhimu sana katika ubora wa huduma za Mahakama, hasa inayosajili mashauri kwa njia ya Mtandao. Mahakama inapenda kuwa kila Mtanzania ambaye anayo kadi ya uraia, aweze kujidhamini pale anaposhtakiwa kwa makosa yanayodhaminika. Mahakama haitaweza kutoa dhamana pale kadi ya uraia haiambatani na uthibitisho wa anuani ya Makazi ya muhusika.

Nawaomba watumishi wote wa Mahakama watambue kuwa kila mmoja wenu ana mchango wa kuhakikisha tunasafiri kwa pamoja kwenda katika Mahakama Mtandao. Kila mmoja wetu ni lazima afahamu kilichomo katika hilo ANDIKO LA SAFARI KUELEKEA MAHAKAMA MTANDAO. Maboresho endelevu ni yale ambayo yanafahamika na kila mtumishi wa Mahakama. Safari hii sio ya Kurugenzi ya TEHAMA peke yake, au ya viongozi wa Mahakama peke yao, KILA MMOJA WETU NISEHEMU YA UENDELEVU WA

MABORESHO.

 1. MAFUNZO KATIKA KARNE YA 21 Nl KUPITIA TEHAMA

Mwandishi mmoja maarufu wa maswala ya MAHAKAMA MTANDAO (E-JUDICIARY) aitwaye RICHARD SUSSKIND aliandika kitabu kiitwacho HATIMA YA MAHAKAMA MTANDAO NA HATIMA YA UTOAJI HAKI ["ONLINE COURTS AND THE FUTURE OF JUSTICE, 2019"] Alitamka bila kupepesa macho kuwa, mifumo ya kisheria, kimahakama na hata taaluma ya sheria duniani kote bado ni ile ya karne za 19 na 20, wakati mabadiliko makubwa yamefikiwa kulingana na karne ya 21: "... in truth, despite all manner of reform initiatives around the world, today's court systems-along with our legal professions and our law schools—remain fundamentally 19th and 20th Century institutions. They are out of place and inadequate in the 21st Century. It is time for radical change. " Ameongeza pia kuwa, wakati wafanya biashara na mabenki haraka haraka walitambua hayo mabadiliko ya Karne ya 21 na wameacha mifumo ya kizamani, mifumo ya kisheria na ya kimahakama bado imeganda kwenye zama za karne ya 19 na 20.

 1. FURSA ZA MAFUNZO KWA NJIA YA MTANDAO KUPITIA CHUO

CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO (IJA)

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kiko katika mstari wa mbele katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama. Mkuu wa Chuo hiki, Dkt Faustine Kihwelo, JA amenijulisha kuwa wapo waheshimiwa majaji na Mahakimu wengi, wameitikia wito na wametumia vyema sana fursa za mafunzo kupitia TEHAMA zinazoratibia na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Mkuu wa Chuo amenidokeza kuwa, Kanzidata ya Chuo inaonyesha kuwa kutika Kanda ya Bukoba, Mahakimu ambao wanashiriki sana na kwa ufanisi-Hakimu Mkazi Mwandamizi FLORA B. NDALE (Hakimu Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Biharamulo); FERDINAND HILALI KIWONDE na FLORA ERHAHARD HAULE. Nawasihi Waheshimiwa Majaji, tumieni nafasi za mafunzo kwa njia ya mtandao kupitia Chuo cha Mahakama Lushoto.

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kama wakala wa mafunzo na Utafiti wa Mahakama ya Tanzania na katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama vile vile kwa kutumia fursa inayoletwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kimekuja na mpango mahsusi wa kuendesha mafunzo kwa kwa njia ya mtandao kupitia jukwaa la Virtual Court ya Mahakama ya Tanzania. Katika kufanikisha hilo, Chuo kiliandaa programu ya mafunzo kuanzia mwezi wa Julai mpaka Disemba mwaka huu 2021 katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kutatua changamoto za Mahakama ya Tanzania za sasa na za baadae kupitia kuwajengea uwezo watumishi wote.

Kuanzia mwezi wa Julai mpaka kufikia leo tarehe 31 Agosti 2021 Chuo kimeendesha mafunzo yafuatayo kwa majaji pamoja na mahakimu:

 1. Mafunzo ya Namna Bora ya Utoaji wa Adhabu (Sentencing Practice and Procedures).
 2.      Mafunzo ya Utekelezaji wa Amri na Tuzo za Mahakama (Execution of Court Decrees and Orders).
 3.      Mafunzo ya Sheria ya Miliki Ubunifu (Virtual Training on Intellectual Property Rights).
 4.      Mafunzo ya Kubadilishana Uzoefu wa Namna ya Kuendesha Mashauri katika Mahakama za Mwanzo (Experience Sharing: Practice and Procedures in Primary Courts).
 5.      Mafunzo ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (Trafficking in Person).
 6.      Mafunzo ya Sheria ya Usuluhishi (New York Convention Roadshow for Tanzania).
 7.      Mafunzo kwa Mahakimu wenye Mamlaka ya Ziada ya Usikilizaji wa Mashauri (Training for Magistrates with Extended Jurisdiction).

5. 3. 1 MAFUNZO YANAYOTARAJIWA KUSIMAMIWA NA CHUO SIKU ZA HIVI KARIBUNI

Pamoja na mafunzo hayo yaliyotolewa na Chuo, Chuo bado kinajipanga kufanya mafunzo mengine kwa njia ya mtandao kama vile Kubadilishana Uzoefu katika maeneo yafuatayo:

 1.           Utekelezaji Wosia na Usimamizi wa Mirathi (Experience Sharing in Probate and Administration of Estates);
 2.           Sheria ya Usuluhishi Tanzania (Arbitration Law in Tanzania);
 3.           Sheria ya Ushindani (Competition Law);
 1.         Sheria ya Wakimbizi (Refugee Law);
 2.         Nafasi ya Uongozi katika Utumishi wa Umma na Utungaji Sera (Role of Leadership in Public Service and Pubiic Policy);
 3.         Kubadilishana uzoefu katika Uendeshaji wa Mashauri ya Mtoto (Experience Sharing on How to Handle Juvenile Cases); na
 4.         Mafunzo ya namna bora ya kufanya utafiti wa kisheria kwa wasaidizi wa kisheria (Legal Research to Judges Law Assistants).

Ni Rai yangu kuwa mtatumia fursa hiyo kushiriki mafunzo yanayotolewa na Chuo kwa njia ya mtandao ili kujiongezea ujuzi binafsi na hivyo kuboresha utendaji kazi wa kila siku wa Mahakama. Natambua kuwa Chuo kwa kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kinaandaa Mpango wa Mafunzo kwa njia ya mtandao (virtual training) kwa Watendaji wa Mahakama, Maafisa Utumishi pamoja na Maafisa Tawala kwa kuanzia.

6. MWISHO

Nawashukuru sana kwa mapokezi yenu mazuri. Naomba niwasisitize kuwa kila mmoja amiliki maboresho yanayoendelea kufanyika na kuwa sehemu ya maboresho hayo.

AHSANTENIKWA KUNISIKILIZA.